Misimu na dhima zake katika lugha ya Kiswahili-1

Amani Njoka, Swahili Hub

Leo tutatoka kidogo kwenye mwendelezo wa mada yetu ya aina za maneno katika lugha ya Kiswahili badala yake tutajadili kwa kifupi kuhusu misimu. Misimu imekuwa na umaarufu na mchango mkubwa katika lugha hasa lugha ya Kiswahili.

Misimu ni jumla ya maneno yote ambayo siyo sanifu katika lugha yoyote mathalani Kiswahili ambayo yameibuliwa na vikundi vidogo vya watu wenye utamaduni unaofanana kwa lengo la kuwa na usemi mmoja unaolinda, mawazo na mawasiliano vya wanavikundi. Sababu ya kuitwa misimu ni kuwa maneno hayo huzuka na kupotea na mara nyingi kulingana na matukio fulani katika jamii husika.

Matukio ya kisiasa, kumekuwa na matukio mengi ambayo yametokea na yanaendelea kutokea yanayojitokeza katika jamii na kusababisha misimu mingi kuibuka. Misemo au msamiati uliyoibuka na kushika hatamu katika mzungumzo ni kama vile; soma namba, wakereketwa, mgombea mwenza n.k.

Michezo, ingawa haitajwi sana lakini na yenyewe imekuwa na misimu ambayo inapatikana na kueleweka miongoni mwa wanamichezo wenyewe. Mfano, mkata umeme, kiungo mkata shombo, mkali wa dimba na mingine ni miongoni mwa misemo ambayo ukiyatamka kwa wanamichezo hasa mpira wa miguu wanaelewa kuliko watu wengine wasio wapenzi wa mpira wa miguu.

Utani, kwa muda mrefu kumekuwa na utamaduni wa kutaniana au kuchongoana baina ya mtu na mtu, kabila au jamii fulani na jamii nyingine. Wakati mwingine utani hukuwa na hatimaye kuwa utani wa jadi. Miongoni mwa utani maarufu ni ule unaotokana na Simba na Yanga. Kupitia utani wa jadi uliopo baina ya mashabiki wa timu hizi kumeibuka msamiati kama utopolo, mikia, chura, wa matopeni, wa kimataifa n.k.

Licha ya kwamba misimu unazuka bila utaratibu maalum na kuzushwa, misimu ina umuhimu wake katika lugha au vikundi husika. Miongoni mwazo ni:

Kupamba lugha, usemaji wa misimu huleta raha katika uzungumzaji, kwa msikilizaji hata kama wakati mwingine misemo hiyo haina maana. Hata hivyo misimu hupendezesha lugha kwani huongeza mvuto kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili.

Hukuza lugha, bila shaka mismu ni maneno mapya yanayozuka, maana yake hayakuwapo katika lugha hapo kabla. Kwahiyo, misimu huongeza idadi ya msamiati katika lugha mathalani Kiswahili hasa inaposanifishwa.

Kuficha siri na kuficha ukali wa maneno, kwa kuwa huwa ni maneno yanayozushwa au kuzunumzwa a kikundi fulani cha watu, hakuna shaka kuwa huelewana wao kwa wao na hivyo kutokueleweka kwa wale wasiohusika. Mfano, watumiaji wa dawa za kulevya hutumia maneno kama ngada, pipi, kete, unga n.k ili kuficha uhalifu wao kwa vyombo vya dola au wasiohusika na kupunguza ukali wa maneno.

Kwa leo tutaishi hapa katika sababu za kutokea kwa misimu pamoja na dima zake katika lugha hasa ya Kiswahili. Wakati ujao tutaendelea na sehemu nyingine kwa kujadili aina za misimu na sifa zake.

Mwandishi ni mdau na mwalimu wa lugha na somo la Kiswahili. Maoni na ushauri: 0672395558