Mkalimani hotuba za viongozi Dodoma awaomba radhi Watanzania

Gadi Solomon, Mwananchi

Dar es Salaam. Mkalimani  Matungwa Lwamwasha amekiri kupotosha fasili ya kile ambacho kilikuwa kinazungumzwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa siku ya kuaga mwili wa Hayati John Magufuli kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Lwamasha amesema hata hivyo baada ya kutokea kwa dosari hiyo alitoa taarifa haraka kutokana na  tafsiri potofu aliyoitoa.

Akizungumza kwenye kipindi cha Leo Tena kinachorusha na kituo cha Redio Clouds, Lwamasha amesema chanzo cha tatizo ni kutokana na kutokuwepo vifaa vya kusikilizia pia kukosekana spika karibu yake, hivyo kulazimika kusikiliza sauti iliyokuwapo uwanjani hapo na wakati mwingine ilikuwa inakatakata.

 Alisema baada ya tukio hilo alipata simu na ujumbe mfupi kutoka kwa watu wengi wakihoji na kumweleza jinsi alivyopotosha umma.

“Nilishangaa kuona picha mbalimbali ambazo zilitengenezwa zikielezea mkalimani akiwa ameshika vitabu na kuibua utani mtandaoni kuhusu mkalimani,” alisema Lwamasha.

Anasema jambo hilo lilitokea ikiwa ni sehemu za changamoto za ukalimani lakini watu wengi hawabaini changamoto ya usikivu iliyomkuta.

Rais Ramaphosa katika sehemu ya hotuba yake alisema, “I felt honored because President Magufuli  was not a great traveler, he didn’t like to travel very much, he preferred to stay here at home.”

Naye Mkalimani alifasili; “Nilijisikia kuheshimiwa sana kwa sababu Mheshimiwa Magufuli alikuwa ni mtu imara, mwenye upendo ambaye alipenda pia kusikiliza na kuweza kutoa mwongozo kwa wenzake…” ( Kicheko wananchi).

Lwamasha alisema anazungumza Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kihaya, Kinyambo na Kisukuma hivyo ana umahiri wa kuzungumza lugha hizo kwa ufasaha isipokuwa jambo hilo lilitokea kama changamoto ya kazi ya ukalimani.

Kwa taaluma Lwamasha ni mwalimu wa Chuo cha Bahari, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akifundisha mabaharia na manahodha wa meli.

Amesema alishtuka baada ya kicheko kilichotoka kwa wananchi, na akabaini kwa haraka kuwa kicheko kile kilimhusu.

Anasema kutokana na kugundua kuwa alichotafsiri hakikuendana na yale aliyokuwa yaliyokuwa yazungumzwa, alilazimika kurekebisha makosa huku akiendelea na ukalimani lakini mwishowe aliomba radhi kwa tafsiri potofu jambo lililosababisha umati uwanjani kumshangilia.

Hata hivyo, amesema hayati John Magufuli ndiye amekipandisha Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha nne katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Pia kwa sababu hiyo alishiriki ukalimani mkutano wa SADC. Alisisitiza kuwa, amefanya ukalimani kwenye shughuli za uzinduzi wa miradi mbalimbali hapa nchini.

Pia amesema hata alipokuja Rais Ramaphosa kumtembelea Magufuli enzi za uhai wake ndiye aliyefanya ukalimani. Vilevile katika sherehe za kuapishwa Magufuli Dodoma pia alifanya kazi hiyo ya kukalimani.

Mwanataaluma huyo amesema ana uzoefu kwa zaidi ya miaka 20 kwenye ukalimani.

“Mkalimani anapaswa kuwa na misamiati ya kutosha  kuhusiana na lugha hiyo unayoifanyia ukalimani,” alisisitiza.

Aina za ukalimani

Ukalimani wa papo kwa papo

Wakalimani huwa kwenye vizimba na huvaa vifaa maalumu vya ukalimani na mara nyingi huwa hawaonekani, katika aina hii kama kama ni kupishana isizidi sekunde moja.

Ukalimani wa mfuatano

Ni ukalimani ambao unamfuata kwa nyuma mzungumzaji, yaani mnapeana nafasi. Anasema hata hivyo siku ya tukio la Dodoma ulifanyika ukalimani  wa aina ya kwanza na baadaye wakaagizwa ufanyike ukalimani wa mfuatano ambao hakukuwa na spika za kutosha kuwezesha usikivu.

Ukalimani wa alama

Huu ni ukalimani ambao unatumiwa na watu wenye ulemavu wa kusikia

Mkalimani anahitajika kuwa na stadi za lugha unazotaka kuzifanyia ukalimani. Jambo la muhimu uwe unatawala sarufi ya lugha.

Author: Gadi Solomon