MKWE WA RAIS-3

NA MTUNZI MUSTAPHA MTUPA ENDELEA SEHEMU YA TATU…

“Aya mimi nakuja kukuona na najua tangu asubuhi haujala, nikuletee nini?”

“Wewe leta unachojisikia, mimi nitakula tu kwa sababu yako”

“Mwanaume una mbwembwe yeye, haya ngoja nije”

Huyo alikuwa ni Ashura, mpenzi wa Fred ambaye alianza kuwa kwenye uhusiano naye tangu wakiwa wanasoma elimu ya sekondari.

“Mama jamani hata mimi?” Ilikuwa ni neno la kwanza la Ashura mara baada ya kufika nyumbani kwa kina Fred na kumkuta mama yake akiosha vyombo.

“Nini tena mwanangu?”aliuliza Mama Fred huku akinawa mikono yake.

“Huyu Jambazi anaumwa tangu jana usiku, yeye hajaniambia nawewe mama hujaniambia.”Aliongea Ashura huku akisogea karibu alipokuwa Mama Fred na mkononi akiwa ameshika mfuko mweusi.

“Mwanangu hiyo habari ya kuumwa ndio unaniambia wewe muda huu, mimi najua labda kama kawaida yake kulala kama samaki pono, sijuiii kabisaaa kama anaumwa,”

“Nilikwambia mama humu mtoto huna si bora ungeenda kumbadilisha na gunia la mpunga Morogoro ukapata faida ya kula ubwabwa.”

“Hilo gunia la mpunga nalo kubwa nigewe tu maji ndoo moja namtoa mimi” Mama Fred na Aisha wamezoeana kwa muda mrefu na mbali yakuwa mtu na mka mwanawe walikuwa ni marafiki pia hivyo mara kwa mara wamekuwa wakitaniana na kubwa zaidi Mama Fred alikuwa ni Mndengeleko na Ashura ni Mmakonde, hivyo walikuwa na utani wa asili.

Baada ya mazungumzo ya muda mfupi Ashura aliingia chumbani kwa Fred.

“Kama unakuwa unataka kufa unatuambia tukuletee sanda kabisa usiwe unajikausha kama hivi,”Mara baada tu ya kuingia ndani hiyo ndio ilikuwa kauli ya Ashura kumwambia mchumba wake Fred.

“Si nyie wamakonde mnanijaribu, jaribu subirieni zamu yangu ikifika nitampiga mtu kombola moja tu hatoamini.”alijibu Fred na wote wakacheka.

Baada ya stori na hadhithi za hapa na pale Fred aliamka na kuanza kukishambulia chakula alicholetewa na baada ya muda mama yake pia alimletea dawa za kumeza ili kupunguza maumivu.

“Hicho kichwa nimekwambia siku nyingi ni kipanda uso, nenda kwa mama yako mkubwa akakuchanje  hautaki. Utakula dawa kitapoa baada ya wiki kitauma tena, mtoto mbishi kweli wewe.”

”Basi mama nimekusikia nitaenda, acha kwanza hapa kipoe, maana hali ni mbaya”alijibu Fred na baada ya kula dawa na kupiga stori na Aisha kwa masaa kadhaa ikafikia wakati wa Aisha kuondoka, hivyo akamsindikiza hadi maeneo ya karibu na kwao kisha wakaagana.

“My nataka tuongee kitu, kesho kama utakuwa na nafasi,”alisema Fred.

“Tufanye nikirudi kazini, nitakupigia tukutane, kwanza ni kitu gani,”Alijibu na Ashura na kuongeza swali.

“Acha mapepe wewe, subiri utakijua hiyo hiyo kesho.”

Ndege hao wawili walikaa ndani kwa pamoja kwa muda usiopungua masaa mawili na baadae Ashura alishika njia na kuondoka eneo hilo.

Mitaa ambayo Fred alikuwa akiishi ilikuwa ni Tabata, Kimanga  ambapo pia Ashura alikuwa akiishi, ingawa utofauti ulikuwa ni kwamba Ashura aliishi Tabata, Mawezi na Fred aliishi Tabata Chama. Baada ya Ashura kuondoka Fred alirudi nyumbani na kuendelea kuuguza kichwa chake, mida ya jioni hivi baada ya kuona kimepoa akaamua kutoka nje kwenda kijiweni kupiga soga na vigano vya hapa na pale, pia kufungua biashara yake walau apate hata pesa ambayo itatumika kwa ajili ya vitafunio kesho yake asubuhi.

Kwa hakika Fred alikuwa kwenye kipindi cha mpito sana, ndoto yake kwa muda huo ilikuwa ni kutoboa kimaisha na hakuwa anaona uwezekano wa kufanikiwa kwa kuendelea kusalia nchini Tanzania kutokana na ugumu wa maisha ambao aliokuwa akikutana nao kwa wakati huo.

 Licha ya kupambana katika kipindi chote hicho bado hakupata hata nusu ya kiasi cha pesa ambacho alitakiwa kuwa nacho kwa ajili ya kuanza mchakato wa maombi ya hati ya kusafiria.

Baada ya kufika kijiweni na kufungua biashara yake, kwa sababu ilikuwa ni jioni baadhi ya marafiki zake walienda kukaa kwenye benchi lililokuwa pembeni ya genge na kuanza kumwaga maneno.

“Mwanangu hapa nitampata nani nimuuzie hili genge anipe hata laki mbili..?”Fred alimuuliza mmoja ya marafiki zake waliokuwa kwenye benchi kwa muda huo aliyeitwa Rama.

“Hahahahaha, ndugu yangu unachekesha sana ”Rama akajibu swali la Fred kwa kicheko na kumsifia kwamba alikuwa akichekesha.

“Sasa rafiki yangu mimi nakuuliza jambo la msingi wewe unaniambia nachekesha, nachekesha nini sasa hapo”Fred alijibu na kuonyesha kuwa hakuwa amependezwa na kicheko cha Rama.

“Nacheka kwa sababu unanichekesha, sasa unavyoona hilo genge lako ambalo halina chochote nani atakuwa amepungua akili kiasi cha kukubali kutoa laki mbili kulinunua” Rama alijibu.

“Aaah hiyo kianzio, kama hana laki mbili atashuka, atanipa hata laki.”

“Wewe sema unataka shingapi tujue moja, masuala ya kutumbia kama hana laki mbili sijui mtashuka, mtapanda ni kupotezeana muda tu” Rama aliongezea baada ya Fred kuonekana hana uhakika juu ya kiasi gani hasa cha pesa anakihitaji ili kuuza genge lake.

“Basi tusiongee sana mambo yakawa mengi, wewe chekecha unavyojua, mimi nataka laki nianzie mchakato hiyo wa kufuatilia kitabu(Pasipoti), wewe kama unamteja wa pesa hiyo mimi nachukua freshi,”alijibu Fred.

“Poa wewe nisikilizie, nitawashtua wadau kuanzia kesho… kama nitapata mtu..nitakupa taarifa”Rama alijibu na kufunga mjadala huo mzito uliokuwa unaendelea.

Uzuri wa Rama ni kwamba alikuwa ni mmoja kati madalali wanaoaminika katika  maeneo hayo, hivyo haikuwa ngumu sana yeye kutafuta wateja wanaoweza kutoa pesa kwa ajili ya genge hilo.

Baada ya kupita siku tatu mteja wa kununua genge alipatikana na akakubali kutoa shilingi laki moja.

Japokuwa haikuwa inatosha Fred hakuwa na jinsi Zaidi ya kukubali kwa sababu mwanzo wa mbili ni moja.

Bahati mbaya ni kwamba yeye ndio alikuwa akilisha pia familia hivyo kadri alivyokuwa anazidi kukaa nyumbani bila ya kazi ya kufanya ndivyo akawa anaichota ile aliyouzia genge kidogo kidogo.

Vilevile kiasi hicho cha pesa ilibidi pia kitumike kwenye kulipa kodi kwa sababu mwenye nyumba alikuwa akiwasumbua sana kwani walipitisha miezi minne bila ya kumlipa.

Hadi muda huo hakuwa amemwambia mama yake kwa sababu alikuwa akihofia kwamba huenda angetangaza halafu kwa ndugu zake wengine hivyo safari ingekuwa na gundu.

Siku ambayo aliweka ahadi ya kukutana na Aisha kwa ajili ya kumuambia suala hilo hawakufanikiwa kukutana..sababu ikiwa ni baada ya Aisha kupata msiba wa mmoja ya ndugu zake, hivyo walikutana baada ya wiki moja tangu wapeane ahadi.

“Unasemaaa? Haya unaenda kukaa kwa muda gani huko? Kwanza si ndio nasikia watu wanafanyiwa vitendo vibaya huko.. wanauliwa, wanatolewa mafigo wanateswa,”zilikuwa ni kauli za Ashura mara tu baada ya Fred kumfikishia taarifa za kwamba anafikiria kwenda zake Saud Arabia kwa ajili ya kutafuta kazi.

“Hizo stori tu.. ukiwasikiliza sana watu utakata tamaa, kwanza kuna muda huwa wanazusha zusha tu,” Fred alijibu.

“Fred Fred mama yako anakutegemeaa, acha ujinga,”Ashura akaongeza kwa msisitizo.

“Nisikilize Ashura mimi nilitegemea wewe ndio utakuwa mtu wa kwanza wa kunipa moyo kwa maneno ya matumaini lakini ndio unakuwa wakwanza kunipa maneno ya kunivunja moyo, kwanza hao ambao huwa wanateswa sijui na kutolewa mafigo ni wale wanaoenda kufanya kazi za ndani, mimi kwenye supamaketi hayo masuala ya kutolewa mafigo yatanikuta saa ngapi, halafu kule naenda kwa jamaa yangu mimi”Alisema Fred kwa uchungu huku akiwa anamuangalia Ashura.

Wawili hao muda huo walikuwa chumba kimoja na mmiliki wa chumba alikuwa ni Ashura, baada ya kusema maneno yale kwa uchungu Ashura alimsogelea Fred aliyekuwa kwenye kochi kisha akamkumbatia.

”Mimi sio kama sitaki uende huko Mpenzi wangu, lakini nahofia usalama wako ndio maana nakuwa na wasi wasi kama hivi, na yote hii kwa sababu nakupenda, sitaki uje kudhulika”Aliongea Ashura akiwa amekumbatia Fred huku nyuso zao zikiwa zinaangaliana..Mwisho wa tukio hilo lilikuwa ni siri ya kitanda.

Baada ya masaa kadhaa walipitiwa na usingizi hadi kufikia usiku kutokea asubuhi ambapo Fred aliingia kwenye chumba hicho.

“Mimi ngoja niondoke Ashura nafikiri tutaongea siku nyingine”alisema Fred huku akiwa anavaa suruali yake.

“Mmh! Kwahiyo tumefikia muafaka gasi sasa?” Ashura akaguna na kuachia swali lililomfanya Fred amtazame”

“Kuhusu nini?” Fred alijibu.

“Kuhusu hiyo safari yako”

“Wewe si umeniambia kwamba niende tu.”

“Ndio nimekwambia uende lakini hiyo pesa ya kwenda kuchukulia hiyo pasipoti sijui unaipata wapi na kile kigenge ndio ushakiuza,”Ashura alijibu na kumfanya Fred amtazame na asiwe na neno la kusema.

“Unaniangalia tu kama nimewekwa makumbusho ya taifa usoni..wakati nimekuuliza swali,”Ashura akaongeza.

“Daah! Ashura mimi hapa nilipo hata akili yangu imenisaliti, natamani kuondoka hii nchi lakini kila nikifanya jihitada naona naenda kukwama tu, yaani kama nimerogwa..”Fred akajibu na muda huo aliachana na zoezi lake la kuvaa suruali na akakaa tena kwenye kochi.

“Maskini wee! Sasa sikiliza mimi naweza kukukopesha kwa sababu naamini ukienda ukafanikiwa tutafanikiwa wote, lakini chonde chonde ukifika huko ukipata mshahara wako jambo la kwanza liwe ni kunirudishia pesa yangu, na sio sikupi hivi hivi tu, kuna sharti moja lazima ulitimize.”Aisha aliongea na kumfanya Fred atoe meno nje kama Ngiri na kusikiliza kwa makini sharti atakalopewa.

“Kuna wanawake wana sifa za kuolewa na kuna wanawake wamezaliwa kwa ajili ya kuolewa, wewe ni miongoni mwa wale waliozaliwa kwa ajili ya kuolewa, nashukuru sana Ashura.’’Fred aliongea na kumsogelea Ashura.

“Unanishukuru wakati unatumia pesa yako, yaani hii sikupi nakukopesha utairudisha tu na kama nilivyokwambia ni kwa masharti.”Ashura akamjibu Fred huku akitabasamu.

“Haya niambie ni sharti gani hilo?”Fred aliuliza.

“Lazima umwambie mama kwamba unataka kuondoka, tukubaliane mapema kama si hivyo pesa umekosa”
Aliongea Ashura na kumkazia macho Fred ambaye aliinama chini kwa dakika kadhaa.

“sawa, nitafanya hivyo.”

Mrembo huyo aliamua kutoa kiasi cha laki tatu ambacho alikiweka kwa muda mrefu kila alipokuwa anapokea mshahara wake lakini kwa sababu aliamini mwanaume huyo ni wa maisha yake alikitoa bila ya kusita.

Baada ya kupata pesa hiyo kesho yake ambayo ilikuwa ni jumatatu asubuhi na mapema aliamkia ofisi za uhamiaji na kuanza kufuatilia mchakato wa kupata hati ya kusafiria.

Kwa kiasi hicho cha 200,000  sambamba na kiasi kidogo cha pesa alichokuwa nacho mchakato ulienda vizuri na baada ya kuwasilisha nyaraka zote aliambiwa kuwa aende wizara ya mambo ya ndani kwa ajili ya kuchukua Pasipoti yake baada ya wiki moja.

Siku ya ahadi ilifika lakini akaambiwa kuwa haikuwa tayari, hivyo angehitajika kusubiri kwa wiki nyingine.

Hakuwa na budi ikabidi avute subira hadi wiki iliyofuatia ambapo alifanikiwa kuipata na hakutaka kupoteza muda alimjulisha Mudi kwamba tayari alikuwa ameshafanikiwa kupata Pasipoti ambayo ndio ilikuwa nyenzo muhimu kwa ajili ya kuunganishiwa mchongo.

“Mzee baba sasa wewe sikilizia kama wiki mbili hivi mimi naliseti jambo hapa, hadi muda huo kila kitu naamini kitakuwa tayari”Alisema Mudi mara tu baada ya Fred kumpa taarifa ya kwamba alishafanikiwa kuipata hadi ya kusafiria.

“Poa kaka mimi nipo nawewe na nakuaminia sana najua kila kitu kitaenda sawa kwa uwezo wa mungu”alijibu Fred ambaye alikuwa akiongea na Mudi kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp kupitia kisimu janja chake kidogo cha Tecno H5.

Baada ya kuona mchakato unakuwa sawa Fred alitenga muda na kuketi na mama yake kumwambia juu ya adhma yake ya kutaka kutoka nje ya Tanzania kwa ajili ya kutafuta maisha.

“Mwanangu mimi nakuombea na nakupa  Baraka zangu zote… maisha popote, wewe kama unaenda kufanya kazi..kafanye kazi kweli usije tena ukafanya ambayo hayajakupeleka huko,”zilikuwa ni kauli za mama Fred mara tu baada ya Mwanawe kumwambia mpango wake.

Fred alionekana kuwa mwenye mshangao kwa sababu hakutarajia mama yake angepokea suala lile kirahisi vile, lakini hakutana kuonyesha hali yoyote kwenye uso wake.

“Mama mimi naenda kupambana kuiondoa hii hali ya umaskini, mimi inaniumiza sana kila nikiangalia maisha ambayo tunaishi, naamini nitarudi na mafanikio makubwa.”

Siku zilikatika na baada ya kutuma baadhi ya nyaraka ambazo Mudi alikuwa akimwambia atume kila baada ya siku kadhaa..hatimaye  jioni ya Jumapili ya mwaka 2015, Mudi alimtumia ujumbe Fred kwamba kila kitu kilikuwa tayari na wiki ambayo ingefuatia angetumia makaratasi kwa ajili ya kuanza kufuatilia Visa kabla hajatumiwa tiketi ya ndege na kuanza safari.

Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa Fred baada ya kupokea barua hiyo na katika kipindi hicho kifupi kwa sababu hakuwa na kitega uchumi chochote ilimalizimu kufanya kazi za kiwandani kama kibarua ili kuhakikisha mkono unaenda kinywani.

Wiki iliyofuatia makaratasi yalitumwa na akaanza mchakato wa kufuatilia Visa na baada ya wiki kadhaa alijulishwa kuwa Visa yake ilikuwa tayari na baada ya hapo siku tatu mbele  alitumiwa tiketi ya ndege tayari kwa ajili ya kuianza safari.

“Fred usiwe na wasi wasi, najua hali ya mama ipoje mimi nitakakuwa natoa kila nitakachopata kuhakikisha yeye na ndugu zako wengine wanakula na mahitaji mengine hadi wewe utakapoanza kuwatumia pesa”
Yalikuwa ni maneno ya Ashura wakati wawili hao wapo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere sambamba na familia ya Fred wakiwa wanamsindikiza jamaa huyo kwenye safari yake ya matumaini.

“Nashukuru Ashura, mimi sina chakukulipa kwa upendo wako huu, nakuahidi sitokuja kukuona wanini mbele ya macho yangu, nakupenda sana.”alisema Fred kisha akamkumbia Ashura wakiwa bado wapo nje ya uwanja huo.

“Mwanangu mimi nimekupa Baraka zote wewe nenda kapambane na naamini mungu atakusimamia,”Mama Fred naye alitoa salamu zake za mwisho kwa mwanawe kabla hajaondoka.
Baada kuagana Fred alienda sehemu ya ukaguzi kisha akapewa Boarding Pass na akapita tena sehemu nyengine ya kukaguliwa kabla hajapanda juu kabisa kwa ajili ya kusubiria muda wa kuingia kwenye ndege na kuanza safari.

Alikuwa akitumia shirika la ndege la Fly Emirates na baada ya dakika kadhaa aliingia kwenye ndege na safari ya kuelekea mji wa Riyadh huko Saud Arabia ikaanza.

Kwenye mji huo ndiko alipokuwa anaenda kufanya kazi, lakini ndege hiyo ilitua kwanza Dubai na kukaa kwa lisaa limoja kisha ndio ikaanza tena safari ya kuelekea Saud Arabia.

Ndege aina ya boeing 787 ilikanyaga ardhi ya Saudia kiasi cha saa 4:00 usiku na baada ya kutua walichukuliwa na basi ambalo lilitembea kwa dakika 20 hadi kufikia sehemu ambayo walishushwa na kuingia rasmi sehemu za kukaguliwa kabla ya kuruhusiwa kuingia rasmi nchini humo.

Wakati anatoka Tanzania alikuwa akiwasiliana na Mudi ambaye alimwambia kuwa ilibidi afikie kwake, kisha baada ya siku kadhaa ndio angempeleka kwa waajiri wake ambao wangempa nyumba ya kuishi muda wote atakaokuwa anafanya kazi.

Kazi ambayo aliambiwa kuwa angeenda kufanya ilikuwa ni kuwa mpishi kwenye mgahawa mmoja wapo Mjini Riyadh.

Hivyo baada ya kutua ikabidi aunganishe WIFI kwenye simu yake na kuanza kuwasiliana na Mudi kumjulisha kuwa tayari alikuwa ameshafika.

Fred alipita kwenye sehemu kadhaa za ukaguzi ikiwa pamoja na dawati la uhamiaji kabla hajaruhusiwa kupita baada ya kuonekana kwamba alikuwa sawa.

ITAENDELEA…

Author: Gadi Solomon