MKWE WA RAIS-5

NA MTUNZI MUSTAPHA MTUPA

ENDELEA SEHEMU YA TANO..

Fred alivyoona mfarakano ule alisogea hadi eneo husika, na kujaribu kuuliza tatizo ni nini, mbona walikuwa wanamlazimisha mwanamke huyo kitu ambacho alikuwa hataki.

“Kaa mbali kijana, linaloendelea halikuhusu,’’mmoja kati ya wale majamaa alimwambia Fred mara tu aliposogea na kujaribu kuuliza.

“Hapa ni kazini kwetu, huyu dada ni mteja wetu haiwezekani mkamvuta vuta kama hivyo halafu mimi nikawaacha,’’aliongea Fred na kujaribu kumshika bega mmoja wao na katika hali asiyoitegemea akajikuta amesukumwa na kuanguka hadi chini.

Hasira zikampanda na akataka kunyanyuka na kurudisha ule msukumo lakini tayari baadhi ya wafanyakazi wenzake na Polisi walikuwa wameshafika eneo la tukio na wakamzuia kufanya alichokuwa anataka kukifanya.

Wakati huo huo wale majamaa wakashika njia na kuondoka na msichana yule wa kizungu kwenye eneo hilo.

Wale mabinti wengine pia walitolewa walipojificha nao wakachukuliwa na kuondoshwa kwenye duka hilo.

Fred alinyanyuka na kuendelea kufanya kazi yake ambapo haikumchukua muda sana akawa ameshamaliza, hivyo alijiandaa na kushika njia ya kurudi nyumbani.

”Siku ngumu sana hii” alijesema kimoyo moyo wakati yupo kwenye gari akirudi mahali anapoishi.

Alipofika alijimwagia maji na kujitupa kitandani asitake hata kula, hadi kesho yake asubuhi ambapo siku hiyo hakuwa anaenda kazini hivyo aliitumia kufanya fanya usafi wa chumba ambacho alipewa kukaa na Thoby.

Kwa kuwa hakuwa amewasiliana na mama yake na mchumba wake tangu awasili nchini Saudia, siku hiyo aliitumia kumpigia simu Ashura ambaye aliongea naye kwa kirefu na kumueleza hali aliyokutana nayo, kisha akamwambia kuwa ampelekee simu mama yake aongee naye pia.

Licha ya kumwambia ukweli Ashura…Fred alitaka mama yake asijue chochote kuhusu  mkasa wake wa kutelekezwa, hivyo alimuomba Ashura afanye siri.

“Usijali Fred, mimi ninamuangalia mama muda wote huu, wewe pambana, lakini ukipata huo mshahara tena usije ukahonga waarabu, nitakuroga urudi Tanzania…ukumbuke kututumiaga pesa ya matumizi..maana huku kwenyewe tunaishi kiugumu kama  balale”aliongea Aisha  maneno ya maana na kutia utani mwishoni mwisho uliosababisha wapenda nao hao wote wacheke, kabla ya kundelea na soga na mwisho kuagana.

Siku, wiki na miezi ilikatika na hatimaye Fred alitimiza miaka miezi minne tangu alipotua rasmi nchini humo.

Muda wote huo hakuwahi kuwa mtembeaji sana, hivyo wikiendi moja aliamua kutoka na kwenda kwenye moja ya fukwe ili kupata upepo wa bahari.

Saudia ni miongoni mwa nchi ambazo zimejaaliwa sana joto, hivyo kupunga upepo wa bahari kwenye fukwe ni miongoni mwa mambo ambayo yanafanywa kama starehe na watu waishio nchini humo, ingawa huwezi kukuta wanawake wengi sana kama ilivyo sehemu nyingine za fukwe kwa sababu sharia za nchi hiyo haziruhusu wanawake kuonyesha maumbile ya.

Wanawake wachache ambao hutembea ufukweni huwa wanavaa mabaibui na hata wakiwa wanaingia kwenye maji huwa wanaingia nayo.

Fred alifika ufukweni na baada ya kupunga upepo kwa muda, akajongea hadi sehemu palipokuwepo na pikipiki za kutembelea kwenye maji (Water motorcycle) ambapo alikodi moja ili kuinjoi neema za muumba wa mbingu na Ardhi kwa kutembea na kuyachezea maji ya bahari.

Kwa kuwa haikuwa mara yake ya kwanza hakuhitaji sana mafundisho.. zaidi aliitekenya na kuanza kuyakata maji.

Kwa sababu alikuwa akifahamu kuogelea alichochea moto na kwenda mbali zaidi na fukwe hadi akafika bahari ya kina kirefu, wakati anaendesha macho yake yalinasa kwenye boti moja ya kifahari(Yatch) ambayo kwa haraka haraka aliona kwamba ilikuwa kwenye shida kwani upande mmoja ulikuwa umeinama kuliko ule mwingine.

Akastaajabu na akasogea kwa karibu ili kuona nini kimetokea, eneo ambalo yeye alikuwa amesimama na piki piki yake na lile boti lilipokuwepo ilikuwa ni mbali kidogo kutoka ufukweli kwani hata wale watu wanaoogelea ufukweni hawaonekana zaidi ya majengo tu ambayo pia yalikuwa yakionekana kwa mbali.

Fred alisogea hadi eneo hilo na la haula, akakutana na sintofahamu ya watu wakitupiana makonde.. wakiwa juu kabisa ya boti hiyo ya kifahari.

Kwa haraka haraka watu hao hawakuwa ni raia wa Saudia kwani walikuwa ni wazungu, njemba hizo zipatazo sita zikiwa zimevalia suti nyeusi, zilikuwa zinapambana na njemba nyingine saba zilizokuwa zimevalia kombati za kijeshi huku nyuso zao zikiwa zimefunikwa kwa maski na vitambaa maalumu.

Mmoja kati ya wanaume wale waliovalia kombati za kijeshi na maski usoni alikuwa amemshika binti wa makamo wa kizungu ambaye alikuwa amevalia nguo za kuogelea.

Muda wote huo Fred alikuwa akitumbua macho asielewe kinachoendelea na katika kutupa tupa macho kwa mshangao wake wakati wanaume hao wanatupiana masumbwi, alimuona yule mwanamke ambaye alikutana naye kazini kwake, wakati huu alikuwa ameshikiliwa na yule njemba mmoja wa saba ambaye alikuwa amembana kisawa sawa.

Mgogoro wa nafsi ukamtafuna Fred, akawa anawaza je? “Niende nikajaribu kusaidia, au niendelee na mambo yangu?” baada ya kuwaza kwa muda akaona sio sawa, ngoja ajaribu kufanya kitu.

Alishuka kwenye pikipiki yake na haraka sana akaogea na kuingia kwenye boti hiyo ambayo wakati wote huo ilikuwa imesimama.

Alipoingia, alipanda haraka hadi kule juu palipokuwa panafanyika varangati, nayeye akajongea hadi kwa yule jamaa aliyemshika yule dada na kuanza kumsukuma ili amuchie mrembo huyo.

Walisukumizana kwa muda na yule njemba akadondoka chini na kumuachia yule dada.

 “Can you Swim? Go to my, Water motorcycle and start it(Unaweza kuogelea…?nenda kwenye pikipiki yangu ya maji na uiwashe..”ilikuwa ni kauli ya Fred mara tu baada ya yule jamaa kumuachia yule mwanamke na bila ya kupoteza muda mrembo huyo akaruka kutoka kwenye boti kisha akaogea hadi kwenye pikipiki aliyoelekezwana kisha akaiwasha.

Wakati yule njemba anajizoa zoa, Fred tayari naye alikuwa ameshachomoka eneo hilo la juu akaruka kwenye maji na kupanda pikipiki iliyokuwa inashikiliwa na yule mrembo na haraka wakatoka eneo hilo.

Wakati wanaondoka kuelekea nchi kavu wakiwa njiani walishuhudia ndege aina ya Helkopta ikiranda randa usawa wa ile boti..pia wakapishana na boti ya kwanza iliyojaa maaskari wa Kisaudia wakielekea eneo hilo.

Nyuma ya boti hiyo kulikuwa na boti nyingine yapili ambayo ilijaa maaskari pia lakini hii ilikata kona haraka na kusimama mbele yao, kisha wale maaskari wakawaonyeshea mitutu ya bunduki, ishara ya kuwataka wasifanye chochote.

“Mnafanya nini? Huyu amejaribu kunisaidia kutoka kwenye hatari, mnadhani ni Jambazi?”yule dada wa kizungu aliongea kwa hasira baada ya kuona maaskari hao wamenyoosha mtutu wa bunduki Fred na alifahamu kwamba hakuwa analengwa yeye bali mhusika zaidi alikuwa ni Fred.

“Kijana, fuata sheria, usijaribu kufanya chochote,”aliongea mmoja kati ya maaskari walionekana kuwa ni kiongozi.

Hadi muda huo Fred hakuwa anaelewa kile kilichokuwa kinaendelea, pengine alihisi ni kama muvi ya kihindi anayoiota usingizini lakini ukweli hayakuwa maigizo lilikuwa ni tukio la maisha halisi.

Ile boti iliyosheheni maaskari ilisogea hadi karibu yao na kuwachukua wote wawili kuwaingiza kwenye na askari mmoja alipanda kuendesha kile kipikipiki walichokuwa wanaendesha na safari ya kuelekea ufukweli ikaanza.

Baada ya kuwasili ufukweli wakakutana na gari nyingine nyingi za polisi, zikiwa zimesheni askari waliokuwa na mitutu, yule dada wa kizungu aliingizwa kwenye gari moja nyeusi na kuondoshwa eneo hilo haraka wakati Fred yeye akiingizwa kwenye moja kati ya magari ya polisi na safari ya kupelekwa kule ambako hakuwa anapajua ikaanza.

Gari hiyo ilitembea kwa lisaa limoja kisha ikaingia kwenye moja ya vituo vya polisi, Fred akashushwa huku mikono yake ikiwa imefungwa pingu na alikuwa amevaa kipensi tu na jezi, akapelekwa hadi lokapu.

Alikaa kwa masaa matatu kabla ya kutolewa na kupelekwa kwenye chumba cha mahojiano.

“Tuambie unashirikiana na nani katika ugaidi wako,” lilikuwa swali la kwanza Fred kuulizwa na askari aliyekuwa amepewa kazi ya kumhoji.

“Kaka sijakuelewa, nashirikiana na nani kwenye ugaidi gani?”Fred alijibu huku akimtazama yule askari.

“Unajifanya hujui eeh? Ni bora ukaongea mapema kabla ya mateso kuanza.”yule askari aliongea tena huku akiwa anamzunguka Fred.

Wakati anaendelea kufanya tukio hilo, ghafla aliingia askari mmoja na kumwambia kwamba kulikuwa na simu yake.

Akaacha kufanya kile alichokuwa anakifanya na akatoka kwenye chumba hicho ili kwenda kuisikiliza simu hiyo.

ITAENDELEA

Author: Gadi Solomon