MKWE WA RAIS-7

   NA MTUNZI MUSTAPHA MTUPA

ENDELEA….   

BAADA YA MIEZI MITATU

Fred alikuja kushtuka na kujikuta yupo kwenye mazingira ya Hospitali, huku mkono wake mmoja ukiwa umefungwa kwenye chuma cha kitanda alicholalia.

Wakati anajaribu kunyanyuka alihisi, maumivu kwa mbali kwenye shingo yake hali iliyosababisha atulie na kujilaza tena.

Tukio la mwisho alilokuwa analikumbuka  lilikuwa ni kupigwa risasi na bahati nzuri alikuwa akiwakumbuka hadi watu waliomfanyia unyama huo.

Baada ya dakika 15 tangu alipoamka, waliingia madaktari walioongozana na maaskari waliovalia gwanda zao.

“Habari, unajionaje, unakumbuka chochote?, jina lako nani?”

Mmoja ya madaktari alimpachika swali Fred ambaye alinyanyua mdomo kutaka kujibu lakini sauti haikuwa inasikika kwa urahisi, ilibidi hadi daktari yule asogeze sikio lake kwenye mdomo wake ili kusikia kile ambacho anasema.

“Na na na.. i..twa Fred “kwa tabu sana Fred aliongea.

“Ooh! Nimefanikiwa”yule daktari alisema hivyo kisha akatasamu.

“Kwa sasa hatoweza kutoa sauti kama ilivyo kawaida lakini anahitaji wiki kadhaa kurudi kwenye hali yake, hivyo mnaweza mkamchukua baada ya muda huo”alisema yule daktari kuwaambia wale Polisi alioongozana nao ambao walimuitikia na kutoka chumbani humo.

 “Pole sana kijana utakuwa sawa”yule daktari alimpa moyo Fred kabla ya kuondoka eneo hilo.

Nje ya wodi hiyo aliyolazwa kulikuwa na askari wawili waliowekwa kwa ajili ya kumlinda katika kipindi chote alichotakiwa kukaa hapo.

Muda wote huo hakujua ikiwa Thoby amefariki na wala hakuwa anaelewa wale Polisi walikuja kwa sababu gani na kwanini awekewe ulinzi.

Siku zilikatika na sauti yake ikaanza kurudi kidogo kidogo akiwa Hospitalini hapo, ingawa haikuwa na nguvu kama ilivyokuwa hapo wali.

Kwenye shingo yake alikuwa ameshonywa nyuzi kadhaa ambazo zilibabishwa na upasuaji aliofanyiwa kuondoa risasi ambayo ilikuwa imepita shingoni mwake.

“Daktari nafikiri kila kitu kipo sawa, tumekuja tumchukue kwa ajili ya mahojiano”ilisikika sauti kutoka kwenye ofisi ya dokta ambaye alikuwa na jukumu la kumtibia Fred hadi kufikia hatua ya kurudi kwenye hali yake ya kawaida kwa zaidi ya asilimia 90.

“Haina shida afande, niwaombe tu, mchunge sana, hali yake bado sio nzuri sana, hivyo msije mkatumia nguvu zaidi,”daktari aliwajibu maaskari waliokuwa kwenye ofisi yake kwa muda huo na baada ya hapo wakatoka kisha wakaelekea kwenye wodi ya Fred na wakamtaka ajiandae tayari kwa ajili ya safari.

“Tunaenda wapi wakuu?” Aliuliza Fred.

“Tuna mahojiano kidogo nawewe, ondoa shaka”Askari mmoja akajibu.

Baada ya  kuambiwa vile, hakutaka kupinga sana…alijiandaa na kuongozana nao hadi kituoni.

Baada ya kufika aliambiwa aache baadhi ya vitu alivyokuwa navyo kisha akapelewa kwenye chumba cha mahojiano.

Baada ya dakika 10, aliingia askari mwanaume, mrefu ambaye alikuwa na rangi nyeusi kabisa, pengine unaweza kudhania anatokea Afrika..lakini hiyo ni kawaida kwani kuna raia wengi wa Saudia ambao ni weusi kabisa.

“Ndugu Fred, hii biashara hii umeanza lini?”Huku akiwa anafununua makablasha yake yule askari alimtupia swali Fred ambaye alipatwa na mshangao juu ya swali hilo.

“Kamanda, biashara gani? Mimi mbona sina biashara yoyote”Fred alijibu kwa sauti ya upole.

“Tumekukuta kwenye nyumba moja na Thoby ambaye alikuwa akifanya kazi na wauzaji wa madawa tuliokuwa tunawatafuta kwa muda sana, yeye amefariki wewe umebaki, inaonekana mlishindwa kufanikisha moja ya kazi mlizopewa hadi bosi wenu akatoa amri muuliwe, ni kweli sio kweli?”

“Kamanda mimi sijui chochote kuhusu madawa, mimi nimekuwa nikifanya kazi za kawaida tu na..,”Fred alijibu.

“Nyamaza..! sijakwambia uniambie kazi unazofanya, nataka uniambie umeanza lini kujihusisha na biashara ya madawa, ni vizuri ukasema wakati nacheka, la sivyo nitakupa adhabu hadi shetani akuonee huruma,”yule kamanda akaongea na kusogeza uso wake mbele ya Fred ili kuonyesha msisitizo.

“Kamanda mimi sijui chochote, Nakaa na Thoby kwa sababu ndio kanipoke…”
Paa!, wakati Fred akiendelea kujieleza akashtukia kofi zito limetua usoni mwake na kumfanya ahisi kizungu zungu kwa muda.

“Sikilizaa! Tunaweza tukaangalia namna ya kukusaidia ikiwa utatumbia ukweli na kutupa ramani ya wapi anapopatikana bosi wako, la sivyo utajua nguvu yetu,”Alisema yule askari kisha akatoka nje ya chumba hicho.

Baada ya dakika tano wakaingia maaskari wawili ambao walimtoa Fred kwenye na kutembea naye hadi kwenye selo moja ya mlango wa chuma kisha wakaingia naye.

Ndani ya selo hiyo kulikuwa na mlango wa chini… mmoja ya wale askari aliufungua kisha wakamchukua Fred na kumsogeza hadi hapo kisha wakamuingiza lakini wakati wanamuachia kuingia kwenye selo hiyo  askari mmoja alimwambia kwamba ni bora akasema ukweli mapema maana mateso ya sehemu anayopelekwa ni makali sana.

“Ndugu ni bora ukasema ukweli mapema”

Hiyo ilikuwa ni selo ya kiza  ambayo jina lake la utani ni ‘Dark Tiger’..ilikuwa ni sehemu mahususi kwa ajili ya kutesea  wale majambazi sugu.

Ukiingia humo unakutana na maofisa wabobevu ambao kazi ni moja tu, kutesa na namna ya kuingia ni unaachiwa kama embe linatoka juu ya mti, na haijalishi utafikia shingo au mbavu vyovyote vile sawa.

Selo hiyo ilikuwa na kiza tupu lakini pale ambapo anasimama mtuhumiwa ndio huwa kuna mwanga unammulika na hata akisoge mwanga huwa unamfuata.

Mtuhumiwa huteswa hadi pale atakapokubali kusema ukweli ndio chumba hicho huwashwa taa chote na hapo atatolewa kwa ajili ya taratibu nyingine.

Rekodi inaonyesha asilimia 70 ya majambazi wote waliopelekwa kwenye chumba hicho walisema ukweli na asilimia 30 walifariki kutokana na mateso makali.

Mara baada ya kuingizwa mateso makali yalianza kwa Fred na ikapita wiki moja akiendelea kuishi kwenye selo hiyo kwa maumivu makali.

“Nitawaambia nitawaambia…mi..mi.. sio mhalifu…kama hamuamini nendeni  kwenye  vitu vyangu, mtakutana na mawasiliano ya….”akiwa anaongea kwa tabu Fred alijaribu kujitetea lakini kabla hajamaliza akazimia kutoka na kipigo alichopokea.

Akazinduka siku wiki moja mbele na alipoangalia pembeni ya kitanda alicholazwa alikutana na sura ya mtoto mzuri Linda ambaye baada ya kuona Fred ameamka aliachia tabasamu zito lililoakisi furaha yake.

“Umeamka..pole..”alisema Linda.

“Asant..ee nimefikaje hapa”akauliza Fred.

 “Hilo sio jambo la umuhimu kwa sasa, pumzika kwanza halafu hayo mambo tutaongea baadae”

Baada ya muda madaktari waliingia na kumfanyia baadhi ya vipimo, kisha wakamwambia kwamba anahitajika kupumzika kwa siku kadhaa ili mwili wake urudi kwenye hali ya kawaida.

“Nilikwambia ukipata shida yoyote unitafute, kwanini hukufanya hivyo Fred, hadi umefikia kwenye hali hii”Linda alimwambia Fred muda mchache baada ya madaktari kuondoka.

“Sikutaka kusumbua watu, matatizo mengine nilitakiwa niyamalize mwenyewe”

“Wewe unaona ya kawaida haya? Umeteswa hadi umefikia kulazwa unaona kawaida?”kwa sauti ya juu Linda alifoka.

“ough basi mama yameisha,nimekosea”Fred akajaribu kujishusha.

“Ungekumbuka mapema kuwaambia wanipigie usifengefikia huku, lakini nimekuja kupata taarifa dakika za mwishoni.”
“Enhee nakumbuka mara ya mwisho niliwaambia waangalie mawasiliano yako kwenye vitu vyangu”Fred alidakia.

“eee alinipigia simu askari akaniuliza kama nakufahamu, nikwamwambia ndio, nikamuuliza kuna shida gani? akanambia sijui umekamatwa, una kesi ya madawa, nikashangaa”alisema Linda na kuongeza

“nikawaambia walinzi wangu..tulipambana hadi tukakutoa lakini ulikuwa umeshakata moto, tumekuleta Hospitali ulizimia kwa wiki moja ndio umezinduka leo”

“Aaah, dunia naona inanikataa kila ninavyojaribu kuikumbatia, yaani kila nifanyalo, linakuwa mikosi”kwa masikitiko Fred aliongea.

“Hebu usiharibu hali ya hewa, achana na hayo mambo”Linda akajaribu kumtoa kwenye hali hiyo haraka.

“Ndio uhalisa Linda, maisha yangu yamekuwa kama mchezo wa maigizo”Fred aliendelea kulalamika.

“Stoop, we mwanaume nimekwambia acha hayo mambo, tuzungumze vitu vingine”Linda akamjibu.

Basi walikaa kwa muda kabla ya chakula kuingia na wakala kwa pamoja kisha iliopofika jioni, Linda alimuaga Fred na kuwambia kwamba angemuona kesho yake.

Wakati Linda anaondoka, wodini hapo njiani alipishana na mwanaume mmoja mweusi ambaye aliingia kwenye wodi aliyolazwa Fred.

“Siku nyingi sana kijana wangu..”alisema yule jamaa mweusi aliyeingia wodini na Fred alipogeuza sura yake kuangalia nani aliyekuwa  akisema maneno alitabasamu.

“Kaka upo?” aliuliza Fred kwa sauti ya furaha.

“Nipo, pole sana ndugu”

“Nishapoa..umejuaje kama niko hapa..”

“Niko nafanya kazi hapa..niliona wakati unaletwa..”akajibu yule jamaa.

“Daah kaka ndio hivyo..kila siku matatizo tu..”

“Shida nini hasa..maana naona mapicha picha tu”

Fred akasimulia kilichotokea hadi kufikia hapo jambo lililomtia huzuni sana mtu huyo aliyekuwepo wodini kwake kwa muda huo.

“Nishapoa ndio maisha, vipi msiba wa  Thobias umeshafanyika maana sina taarifa yoyoye”akauliza Fred baada ya kupokea salamu za pole.

 “Eeeh  tulishafanya mwili ulisafirishwa Kenya, tumezika kwenye makaburi ya Kijijini kwao”

“Aaah kama masihara, siku moja nitalipa kwa wema alionifanyia.”

“Usijali kaka ni kawaida kwenye maisha ya mwanadamu.”

Huyo jamaa aliyeingia wodini anaitwa John Matibwa, ni raia wa Kenya na alikuwa rafiki wa karibu sana na Thobias na alikutana na Fred kupitia Thobias ambaye aliwatambulisha kwa pamoja na kuanzia hapo wakawa na mawasiliano ingawa siyo ya kushibana sana…Huyu pia alikuwa ni daktari.

Basi baada ya kumpa pole walizungumza mawili matatu na hatimaye John alishika njia na kuondoka na kumuahidi kwamba kwa shida yoyote amtafute yeye, kwa sababu ndio mtu pekee anayeweza kumsaidia kwa muda huo baada ya Thobias kuwa amefariki.

“Wewe huo sio ugonjwa ni uvivu, una lala lala kila muda kama una mimba!”

Fred akiwa amejilaza, Linda alifungua mlango wa wodi na akaanza kumpachika maneno hayo bila hata ya salamu.

Fred alinyanyua macho yake na kumtazama Linda huku akijaribu kutabasamu.

“Sasa si hata unipe salamu kwanza, ujue nimeamkaje asubuhi hii”alisema Fred.

“Salamu yangu sio kwa watu wavivu”Linda akasema.

“Sasa uvivu wangu ni nini jamani?”

“Si huko kulala lala kwako, nahisi hata watoto wako watarithi huo uvivu”huku akiwa anakaa chini kwenye kiti kilichokuwa karibu na kitanda cha Fred, Linda alitupa dongo lingine na kumfanya Fred acheke kwa tabu.

“Usi si nichekeshe bhana”

“Cheka tu” akasema Linda.

Baada ya utani wa hapa na pale muda wa kunywa chai ulifika na wakanywa chai kwa pamoja.

“Hivi yule jamaa mweusi niliyemuona anaingia wodini humu jana ni nani?’’ muda mfupi baada ya kumaliza kunywa chai, Linda alimpachika swali Fred.

“Aa ah yule ni rafiki yangu, nilitambulishwa na Thobias ni daktari mwenzake anatoka Kenya, vipi kuna shida?”alijibu Fred kwa ufupi kisha akachia na swali.

“Hapana, nimeuliza tu” alijibu Linda kwa sauti ya upole ulio ashiria kuelewa alichoelezwa.

Baada ya lisaa limoja aliingia daktari na kumfanyia vipimo Fred kisha akamwambia kwamba alikuwa akiendelea vizuri na anahitaji siku kadhaa za kupumzika kabla ya kuruhusiwa.

Baada ya daktari kuondoka ilipofika mchana  Linda naye aliaga na kuondoka.

Siku zikakatika kama tikiti mbele ya kisu kikali na hatimaye wiki ikafikia..muda wote huo Linda alikuwa akimtembelea Fred kumjulia hali.

Asubuhi ya siku ambayo ameruhusiwa bahati mbaya Linda hakuwepo, kwa kuwa alikuwa na kiasi kidogo cha pesa alikodi taksi impelekea mahali alipokuwa anaishi.

Alipofika, alipanda lifti hadi kwenye ghorofa husika, cha ajabu kila alipokuwa akibonyesha namba ya siri kwa ajili ya kufungua mlango, ilikuwa ikimkatalia.

Alifanya zoezi hilo kwa zaidi ya mara nne lakini majibu yalikuwa  ni yale yale kwamba amekosea kuingiza namba ya siri.

Wakati akiwa kwenye mchakato huo ghafla akashtukia mlango umefunguliwa na macho yake yakagota kwa kijana wa makamo mwenye haiba ya urefu na unene.

“Nikusaidie nini?”yule kijana aliuliza.

“wewe ni nani?”Fred akajibu.

“Unasemaje? Yaani umekuja kwenye eneo langu halafu unauliza mimi ni nani?” alijibiwa kwa sauti ya juu.

“Aa h mimi nilikuwa naishi humu sasa nimeshangaa kukuona hapa”alisema Fred.

“Unaishi hapa? Mimi mbona nimehamia hapa mwezi wa tatu sasa huu, wewe pia ni muajiriwa wa Swadiq Hospital?”Akajibiwa.

“Sijakuelewa”Fred akasema.

“Hujaelewa nini, hili si jengo kwa ajili ya wafanya kazi wa Swadiq, sasa nakuuliza kwani wewe unafanya kazi hapo pia?”

Majibu yale yalitosha kumfanya Fred aishiwe nguvu na kijasho chembamba kimtokea, ikabidi amsimulie yule kijana madhila yaliyomkuta hadi kufikia hapo.

“Daah! Sasa hapo nimekuelewa lakini hili jengo ni kwa ajili ya wafanyakazi na familia zao, hivyo  hata huyo jamaa yako alikuwa anakaa kwa kivuli hicho,”Yule kijana akampa Fred maelezo mafupi yaliyojitosheleza.

“Ningekuwa naweza kukusaidia, ningefanya hivyo lakini humu ndani naishi na familia yangu na pia sikufahamu,’’aliongeza tena yule kijana ambaye alikuwa na asili ya Kihindi.

Fred aliaga na kusogea hadi kwenye lifti na kushuka chini.

Kwa kuwa alikuwa na kisimu kidogo ambacho alipewa na Linda aliamua kumpigia mrembo huyo na kumuelezea hali halisi.

Linda akaulizia anuwani ya eneo alilokuwepo na kiasi cha dakika 45 tayari alikuwa ameshafika akiwa na walinzi wake, akamtaka Fred aingie kwenye gari na safari ikaanza.

Muda huo hakuwa na chochote kwani hata baadhi ya vitu vyake viliyokuwemo mule ndani vilitupwa ili kupisha watu wakae.

Safari ya Linda na Fred ilikoma kwenye moja ya hoteli ambazo hazikuwa mbali na eneo ilipokuwepo ile ghorofa ambayo Fred alikuwa akikaa hapo awali.

Walishuka na Linda akashika njia hadi mapokezi ambapo alilipia kabisa na kuchukua funguo kisha akaongozana naye hadi kwenye chumba chake, kufikia hapo akawaambia wale walinzi wamsubirie kwa nje kisha yeye na Fred wakaingia ndani.

“Kwanini hukunipigia simu wakati unatoka Hospitali”akiwa amesimama Fred alishtukia ngumi ya mgongo aliyopigwa na Linda iliyosababisha ainame kuisikilizia.

“Jamani wee mwanamke mbona mbabe sana,”alisema Fred akiwa ameng’ata meno yake kuashiria uchungu wa kupigwa.

“Eee mimi mbabe kama unaweza nirudishie”Linda akajibu huku akiwa amekunja ngumi na kuachia tabasamu.

Fred alipopinduka hakutumia nguvu nyingi zaidi ya kugusisha vidole vyake viwili kwenye mbavu za Linda na kumfanya aruke kama mtu aliyenyanyuliwa na pembe za nyati mwenye hasira.

“Aaaaa wewe,”Hakuishia kuruka tu bali aliachia na ukulele.

“Nini? nimekupatia ee, si umesema wewe mbabe?”

“Umenipatia wapiii, umeniotea tu, kama unaweza njoo unishike tena uone” Linda akajibu raundi akiwa anasogea kitandani.

Fred hakufanya ajizi alimsogelea tena na akamshika tena mbavuni na Linda alishindwa kuhimili hadi akadondoka na kufikia kitandani na wakati huo alimvuta na Fred naye hivyo wote wakaanguka na nyuso zao zikawa zinaangaliana.

Uso wa Fred ulikuwa juu na ule wa Linda ukawa chini, ghafla hisia zao zikahama na wakabaki wanaangaliana.

Waswahili wanasema mwanamke ni matunzo, hivyo kwa Linda ukijumlisha matunzo na urembo wake, hakuna kasoro ambayo unaweza kuitoa kutoka kwa mrembo huyo, kuanzia kwenye sura, ngozi na muonekano wake kwa ujumla.

Moyo wa Fred chumba kimoja kati ya vinne kilikuwa kinamshawishi afanye jambo lisilompendeza Mungu na vyumba vingine vikawa vinamkataza.

Wakiwa kwenye butwaa hilo huku wakiangaliana, akili zao zikarudi kwa muda na Fred ndio alikuwa wakwanza kutoka kwenye hali hiyo na akakaa kitako.

Linda naye akanyanyuka na kukaa kitako na ukimya ukatawala kwenye chumba hicho kwa dakika kadhaa kabla  ya Linda kuuvunja.

“Mmmh umekula?”huku akiguna Linda akauliza.

“Sijala nina njaa kweli”alijibu Fred.

“Kufaa”akasema Linda huku akinyanyuka na akasogea hadi kwenye meza iliyopo mezani hapo kisha akanyanyua simu ya mezani na kuagiza chakula.

Baada ya dakika 10, tayari chakula kikawa kimefika.

“Njoo ule hapa usije kunifia humu ndani”Akasema Linda ambaye muda mwingi alionekana kuwa ni mtu wa matani.

Fred alisogea na kulitaka radhi tumbo lake na baada ya kumaliza kula waliongea kidogo kisha Linda akaaga na kuchomoka Hotelini.

Hadi giza linatamalaki siku hiyo, bado Fred alikuwa akimuwaza sana Linda na lile tukio lililotokea.

Aliona dalili zote za mrembo huyo kuwa amemzimia  naye pia alikuwa amemzia hivyo hivyo lakini hakuwa na ujasiri wa kumwambia ukweli juu ya hisia zake.

Siku hiyo ilikatika hivyo Fred akiwa hajui hatma ya maisha yake pia ikiwa atarudi nyumbani ama vipi kwani muda wote huo alichokuwa nacho ilikuwa ni hati yake ya kusafia tu zaidi ya hapo ni zile nguo alizovaa.

Asubuhi ya siku iliyofuatia Linda aliwasili hotelini mapema kabisa kisha akamwambia kwamba anahitaji aende naye mahali kwa ajili ya kumnunulia viwalo(nguo) na mahitaji mengine.

Fred akajiandaa haraka na kushuka hadi chini na kuanza safari ya kuelekea kwenye shopping hiyo.

Baada ya kufika kwenye duka moja kubwa(Mall), Fred alifanyiwa shopping ya kufa mtu ikiwa pamoja na kununuliwa nguo, saa na simu kali.

Pesa halikuwa tatizo kwa mrembo Linda kwani mbali ya urais ambao baba yake alikuwa nao, familia yao ilikuwa na kampuni kubwa za utengenezaji wa magari barani Ulaya sambamba na benki pia yeye ndio alikuwa mtoto pekee kwenye familia yao, hivyo alikuwa akiguna tu..anapata anachohitaji…

Baada ya kufanyia shopping, Linda na Fred walipanda kwenye gari moja na safari hii hawakurudi tena pale hotelini badala yake gari ilichochea mwendo hadi kwenye moja ya jengo.

“Tushuke tumefika” Linda akamwambia Fred ambaye alibaki ametumbua macho.

“Wewe panya tushuke, tumeshafika”Linda akasema tena na neno lile la kuitwa panya lilionekana kumkera kidogo Fred kwani alishuka bila ya kutia neno na hakuwa anatabasamu kama ilivyokuwa kawaida yake.

Author: Gadi Solomon