MKWE WA RAIS-8

NA MTUNZI MUSTAPHA MTUPA

ENDELEA…..

Shemeji leo nataka nije kukutembelea unapokaa”Ujumbe mfupi wa maandishi ulisomeka hivyo kwenye kioo cha simu ya Fred na jina la mtumaji lilisomeka kuwa ni Fayma.

Fred alishangaa kidogo na kupatwa na maswali mengi kichwani, juu ya mrembo huyo kutaka kumtembelea kwani licha ya kwamba walikuwa na mazoea kama mtu na shemeji yake lakini suala hilo lilikuwa ni geni.

“Leo nataka nitoke kidogo”
“Utoke..Weekend  yote hii unaenda wapi au kwakuwa shoga yangu haupo nawewe ndio unatafuta njiwa wengine?”

“Mmh, wanawake mna wivu nyie…Nataka tu niende kupunga upepo wa bahari”
“Hapana nina mashaka nawewe, au kuna mtu anaziba nafasi ya Linda hapo nyumbani ee? hutaki nije kwa sababu nitamuona eee?”

“Mtu atoke wapi, wakati mimi nishazama kwenye penzi la mtoto wa kizungu yule”
“Sasa kama kweli hakuna mtu niruhusu mimi nije leo..”
Fred alikuwa akijaribu kutafuta sababu ya kumkataa Fayma asiende nyumbani kwake lakini alijikuta akikosa.

“Au si usubiri Linda arudi uje naye”
“Hapana, mimi nataka nije leo”
“Mmh” Fred akaguna.

“Shemeji kweli hutaki nije hata kunywa maji nyumbani kwako?”
“Sio kama sitaki,”
“Kumbe?”

“Aya bhana, poa njoo..”Mwisho Fred akakubali.

“Haya nitumie Location haraka, niwachomoke hawa wazee(walinzi wake) nije hapo, sitokaa sana”
Fred alitoa anwani yake na ndani ya dakika 40, alisikia kengele ya mlangoni kwake inatoa sauti kuashiria kwamba kulikuwa na mtu anataka

kufunguliwa.

Alijinyanyua kiuvivu kwenye kochi alipokuwa amekaa na kwenda kufungua mlango.

“Mmh! Mbona ndani nasikia kama manukato yakike humu”
Yalikuwa ni maneno ya kwanza aliyosema Fayma mara baada ya Fred kufungua mlango.

“Sasa si ya kwako hayo..”Fred akajibu.
“Kwani yakwangu siyajui?”

“Eeeh bidada pita ndani bhana, nitakufungia mlango kwa nongwa zako”
Fayma akapita ndani na kuketi kwenye kochi, Fred akamuuliza kuwa angependa kutumia kinywaji gani.

“Nipe maji tu, maana najua hiyo juisi huna”
Fred akasogea hadi kwenye friji na kutoa chupa moja ya maji, kisha akaimimina kwenye glasi na kumpatia Fayma ambaye aliinyanyua glasi na kuyashusha vizuri kwenye koo lake na glasi ilipotua chini hapakuwa na maji tena.

Muda wote ambao Fayma alikuwemo ndani humo,Fred alikuwa akistaajabu tu, uumbaji wa Mungu kwa jinsi alivyomvika vazi la uzuri Fayma.

Ukumbwa wa macho yake sambamba na uzuri wa sura yake vilitosha kabisa kuteka mawazo ya mwanaume yoyote yule.

Waliendelea kupiga stori za hapa na pale kwa dakika 10, kisha Fayma akamwambia Fred kwamba alikuwa akijisikia njaa.

Fred akasogea jikoni haraka na kuchemsha tambi na baada ya dakika nane hivi tayari zilishaiva akapakua na kumpelekea mrembo huyo ambaye muda wote alikuwa ukumbini.

Wakati anampa ile sahani ya tambi mikono yao ikagusana na kusababisha waangaliane.

Fayma alishambulia zile tambi na baada ya kumaliza akataka kutoa vyombo lakini Fred akamkatalia.

“Achana bhana, wewe mgeni wangu hutakiwi kufanya kazi yoyote…”Alisema na Fred na Fayma hakujibu kitu zaidi ya kumuangalia tu.

“Haya nimeshiba sasa njoo unipepee”

“Hee! Tena”
“Tena nini, AC yako yenyewe haitoshi, nahisi joto, nitakuja nife humu ndani upate kesi…”
Fred alisogea kwenye kabati la karibu na akatoa sahani kisha akamsogelea Fayma na kuanza kumpepea.

“Yaani mumeo atapata tabu sana we mwanamke”alisema Fred huku akiendelea na zoezi hilo.

“Mume! wangu mimi hajazaliwa bhana, kwa sasa ni wewe tu”alijibu Fyma huku akicheka.

“Mmh nikiwaoa wewe na Linda humo ndani si patakuwa hapatoshi, maana wote vichwa vibovu nyie…..”

“Huoni ndio itakuwa raha, maana tutakufanya uchangamke muda wote”
“Raha wapi matatizo tu nyie”
“Kaa chini bhana, unasimama muda wote huo”wakati anampepea Fayma Fred alikuwa amesimama, hivyo binti huyo alimtaka Fayma akae chini kwenye kochi moja alilokaa yeye.

Kawaida Saudia na nchi nyingine za mashariki ya kati zimejaaliwa sana joto, huko joto ni kali sana kiasi ya kwamba hakuna nyumba ambayo inakosa kiyoyozi.

Hata wale maskini wa mwisho lazima nyumba yao itakuwa na kiyoyozi kutokana na hali hiyo ya joto.

Tangu amewasili ndani humo Fred hakuwa anaelewa kabisa  baadhi ya vitendo ambavyo Fayma alikuwa akivifanya.

Taa ya hatari kwenye kichwa chake tayari ilishawaka na kuona kuwa kuna uwezekano mkubwa binti huyo hakuwa hapo kwa ajili ya kumuona tu, bali alikuwa na mpango mwingine.

Lakini alitulia kuona mwisho wa drama hiyo utakuwaje, ingawa moyo wake ulikuwa na hofu kwa sababu alikuwa akifahamu kwamba binti huyo anatoka kwenye familia ya kifalme ingawa hakuwa anajua ni mtoto wa nani.

Baada ya kuendelea na lile zoezi la kumpepea kwa muda Fred alimwambia Fayma kuwa mkono wake ulichoka kufanya kazi hiyo.

“Bhana nipepee”alisema Fayma huku akiushika mkono wa Fred ambaye aliupeleka juu.

Kitendo cha Fred kuupeleka mkono juu wakati Fayma akijaribu kuushika, ikasababisha binti huyo ajikute anakosa balansi na hatimaye akaangukia kifua cha Fred na nyuso zao zikawa zinatazamana.

Tukio hilo lilizalisha hali nyingine ambayo Fred hakuitegemea kwani Fayma alipeleka uso wake karibu kabisa na midomo ya Fred ambaye alipigwa na butwaa tu asijue nini afanye.

Kilichoendelea hapo ikawa siri ya jambo ambalo wana ndoa hulifanya kwa siri na hawathubutu kusimulia.

Baada ya masaa matatu toka kufanyika kwa lile tukio pale kwenye kochi, safari ya Fayma na Fred iliishia kitandani na wakiwa wamejifunika shuka moja.

 “Nisamehe sana, nimeshindwa kujiuzuia Fred nakupenda”
Alisema Fayma huku akiwa amegeuza uso wake upande mwingine wa kitanda.

Fred hakujibu kitu kwani muda huo nafsi ilikuwa ikihisi majuto kwa kile ilichokifanya.

Baada ya kimya cha dakika moja tangu Fayma alipoomba msamaha na kufunguka kuwa alikuwa akimpenda mwanaume aliyekuwa naye kitandani muda huo, Fred alishuka na akasogea.. akaenda kusimama upande ambao Fayma alikuwa ameelekeza kichwa chake.

“Nakuomba sana, tulilofanya hapa liishie hapa hapa, mimi sina hisia nawewe na naomba sana Linda asije kujua hiki kilichotokea leo, tafadhali sana…Hii leo  ni shetani ametupitia lakini ukweli sihisi chochote kuhusu wewe, naomba ujiandae uondoke.”
Aliongea Fred na kutoka ndani ya chumba hicho kisha akaenda kuketi ukumbini.

Baada ya dakika kadhaa Fayma naye alitoka ndani akiwa ameshaoga na kwa sauti ya upole alimuaga Fred kisha akashika njia yake

Muda huo tayari jua lilikuwa likienda kuzama hivyo haikuchukua dakika nyingi kabla ya kiza kuingia.

Mawazo yaliandama sana kichwa cha Fred ambaye alikuwa akiwaza itakuwaje ikiwa Linda atajua uchafu huo alioufanya.

Siku ikapita salama na siku zikakatika hadi Linda akarudi kutoka nyumbani kwao Lithuania kwenye safari ambayo hakuwa anaihitaji hata kidogo.

 “Fred nakuja nyumbani kwako mpenzi wangu ila nakuja na rafiki zangu, kama unapika msosi pika wa kutosha”

“Poa malkia ndio naamka hivi”

“Wewe nawe mvivu basi haya sisi tutakuja hapo mchana.”
Yalikuwa ni mazungumzo ya Fred na Linda, hiyo ilikuwa ni wikiendi na ilikuwa ni siku tatu tu baada ya kurudi kutoka Lithuania.

Mrembo huyo alimuahidi Fred kuwa siku hiyo alitaka kuja na rafiki zake.

Hofu ilimpanda sana kidume hiyo, akifiria jinsi gani ambavyo ataangaliana na Fayma ambaye bila shaka atakuwepo kwenye msafara huo.

Tangu Fayma alivyoondoka kwenye nyumba ya Fred siku ile, wawili hao hawakupigiana tena simu wala kutumiana meseji.

Hivyo Fred alivyoamka alifanya kazi zake na akapika chakula cha kutosha kwa ajili ya wageni wake wa mchana kisha akatulia kwenye kochi kusubiri ugeni wake.

Saa nane mchana alisikia kengele ya mlangoni kwake inapiga kelele ishara ya kwamba kuna mtu anahitaji kuingia.

Fred akajua tu itakuwa ni Linda na shoga zake wamefika. Alisogea hadi mlangoni na kuufungua.

…….

Lakini ajabu hakukutana na kile alichodhania kwenye akili yake…Badala yake alikutana na askari sita wawili wakiwa ni wale walinzi wa Linda na wanne wakiwa ni wamevaliwa gwanda za kijeshi lakini walionekana kuwa ni askari wa jeshi la Saudia kwa sababu walikuwa ni waarabu.

“Kuna nini jamani?”bila ya salamu Fred alijikuta akiuliza swali.

Askari mmoja aliyevaa gwanda za kijeshi alitoa kitambulisho chake mfukoni na kukionyesha.

“Tafadhani tunaomba uongezane nasisi, tuna mazungumzo nawewe”Alisema yule askari baada ya kuonyesha kitambulisho chake.

“Kuna usalama?” aliuliza Fred.

“Utaenda kujua huku unapoenda tafadhali tunaomba ujiandae tuongezane”alijibiwa kwa mkato.

Hakukuwa na namna zaidi ya kukubaliana na hali halisi akajiandaa haraka na kutoka nje ambapo alikutana na gari mbili aina ya Jeep, akaelekezwa kuingia kwenye moja kati ya hizo kisha safari ikaanza.

Fred alikuwa anadhani kwamba alikuwa anapelekwa kwenye kituo cha polisi lakini alishangaa gari safari ilikuwa ndefu sana na ikakoma kwenye moja ya jumba kubwa nan je kulikuwa na bendera mbali mbali ikiwemo ya Saudia.

Hofu ilimpanda na wasi wasi ukaongezeka, ubongo wake ukawa unatafakari ni wapi hapo alipo.?
Baada ya kufika kwenye lango kubwa la kuingilia ambapo kulikuwa na wanajeshi wengi na baadhi yao walikuwa wameshika mapanga na wengine walishika bunduki, Fred aliamriwa ashuke.

Akazingiza kwenye chumba kidogo ambapo alikaguliwa na mtu, kisha akaingizwa kwenye chumba kingine alipokaguliwa kwa mashine maalumu,  Kisha akaambiwa akapande tena gari na safari ikaanza tena.

Kiukweli mjengo huo ulikuwa mkubwa sana hivyo gari ilitembea kwa mwendo wa dakika 20 hivi kabla ya kusimama kisha Fred akaambiwa ashuke.

Akaongozana na wale askari hadi kwenye mlango mmoja wapo ambapo alikaguliwa tena kisha akaruhusiwa kupita.

Alitembezwa kwa umbali kidogo kisha akaingia kwenye mlango mwingine.

Muda wote huo alikuwa akipishana na wafanyakazi mbali mbali ambao wote walikuwa ni waarabu na baadhi yao walikuwa wakimtumbulia macho kana kwamba wameona kitu cha ajabu.

Fred hakujali sana hali hiyo kwani hakuwa hata anaelewa nini kinaendelea, zaidi ya kuongoza tu gari bovu.

Baada ya kufunguliwa ule mlango wa mwisho na kuingia wale walinzi walimuacha hapo na kumwambia karibu.

Macho yake yalikutana na mwanaume mmoja mwarabu makadirio ya umri wake ni kati ya miaka 40 hadi 45 na mwanamke mmoja mzungu  ambaye alikuwa haiba sawa na hiyo ya mwarabu.

“Karibu ukae kijana”akiwa amesimama huku butwaa limemtawala yule mwarabu alimkaribisha.

Fred alishangaa kwa sababu alizitambua sura za watu wote hao wawili,  yule mwarabu alimfahamu kuwa ni mfalme wa Saudia kwa sababu alishamuona sana kwenye picha mbali mbali hospitalini na kwenye baadhi ya maofisi.
Vilevile yule mzungu naye alimfahamu kwa sababu alishamuona mara kadhaa kwenye simu ya Linda na alishamwambia kwamba huyo ni mama yake, swali lake kubwa alilokuwa anajiuliza kichwani ni kitu gani kimesababisha viongozi hao wenye nyadhfa kubwa kuwa hapo, wakimsubiria yeye?

….IKULU LITHUANIA SIKU MOJA KABLA….

“Huyu mtoto jamaniii! Baba yake akijua si atatunyonga sisi jamani”

“Haya hiyo mimba ni miezi mingapi?”

“Sio kubwa Mama, vipimo inaonyesha ina kama wiki mbili tu”

“Haya na huyo mwanaume..?”

“Ni Mtanzania, unaweza ukaangalia taarifa zake kwenye faili tulilokuletea”
“Baba yake alishaongea na familia ya Edward, hadi mipango ya ndoa ishaanza, leo linaibuka hili, huyu mtoto jamani si katuvua nguo huyu…jamani Linda!”

Yalikuwa ni mazungumzo ya Mama mmoja mzungu ambaye ndio alikuwa mama mzazi wa Linda, vipimo vya mtoto wake alivyopimwa na baadhi ya makachero baada ya kuchukua mkojo wake kwa siri vilionyesha kuwa binti huyo alikuwa na ujauzito.

Mama alimtilia mashaka Linda baada ya kuona kuna mabadiliko, ikiwa pamoja na kukataa baadhi ya vyakula alivyokuwa akivipenda sana… kutema sana mate na kutapika mara kwa mara na alipomuuliza Linda alisema alikuwa akisikia kichefu chefu na wala haumwi.

Hadi wakati huo tayari baadhi ya maaskari walikusanya taarifa juu ya nyendo za kila siku za Linda na kupata hadi taarifa zinazomhusu Fred kuwa ndio mchumba wake.

Mbaya zaidi Baba yake Linda alikuwa mkali sana linapokuja kwenye suala la mwanawe na alishamuandalia hadi mume wa kumuoa na ndoa ilipangwa kufanyika mara tu Linda atakapomaliza Chuo lakini sasa kila kitu kimebadilika kutokana na ujauzito huo alioupata.

“Naomba mumchukue Linda….mtoeni kabisa hapo Saudia na niandalieni safari nikakutane na huyo kijana niongee naye, yaani!”huku akiwa ameweka mikono yake kichwani yule mama alitoa maagizo hayo haraka na baadhi ya wasaidizi wake aliokuwa nao kwenye chumba cha mkutano kwa muda huo wakatoka kwa ajili ya kuanza kutekeleza maagizo hayo.

Jambo la ahueni kwa wakati huo ni kwamba Rais(Baba yake Linda) hakuwa nchini, alikuwa kwenye ziara zake za kikazi barani Asia.

Mchana wa siku hiyo ikatumwa taarifa nchini Saudia kwa walinzi wa Linda na tiketi ikaandaliwa ili Linda aondoke kesho yake mchana.

Kwa kuwa mrembo huyo hakuwa na taarifa, ndio maana alitoa hadi ahadi kwa Fred kwamba alikuwa akihitaji kwenda kumtembelea mchana, akajikuta anapewa taarifa kabla hata ya kukamilisha adhma yake ya kumuona kipenzi chake na kuondoka nchini Saudi halikuwa ombi bali ni lazima, hivyo masaa kadhaa kabla ya safari alipokonywa kila kitu hadi simu.

Akapandishwa kwenye gari hadi Uwanja wa ndege ambapo kulikuwa na ndege binafsi na safari ya kurudishwa Lithuania ikaanza.

Njiani kote Linda alikuwa akimwaga machozi… Kwani hadi anapandishwa ndege na kuchukuliwa mkuku mkuku hivyo hakuwa ameambiwa kuna shida gani.

Akili ya Linda ilihisi kunyanyaswa kwa kupelekeshwa pelekeshwa kisa tu baba yake ni Rais, alijihisi hana uhuru na anaonewa.

Wakati ndege binafsi ilimbeba Linda inaiacha ardhi ya uwanja wa ndege wa kimataifa uliopo Jijini Riyadh nchini Saudia, ndege iliyombeba mke wa raia wa Lithuania, bibie Maria ndio ilikuwa inatua kwenye uwanja huo.

Baada ya kutua mwana mama huyo  alipandishwa kwenye gari maalumu lilioongozwa kwa msafara hadi ikulu ya Saudia.

Kwa kuwa tayari alishaongea na mfalme hakukuwa na shida yoyote, aliwasili Ikulu na akapewa chumba cha kupumzika.

“Sina muda sana wa kupoteza ninachotaka ni kumuona huyo kijana.. Kabla hata sijala chakula cha mchana”dakika 20 baada ya kufika yule mama aliwaambia walinzi na wasaidizi wake aliokuwa nao chumbani.

“Sawa mama…” Walimuitikia na kutoka nje.

Msafara ukatoaka katika kasri la kifalme magharibi mwa Jiji la Riyadh na kufika hadi kwenye nyumba aliyokuwa anaishi Fred.

Walichukuliwa baadhi ya walinzi wa Linda ambao Fred alizoea kuwaona ili iwe rahisi kumchukua.

………Ikulu ya Saudia………..

“Usisimame, karibu ukae”Aliongea yule mfalme baada ya kuona Fred ametumbua tu macho huku akiwa amesimama.

Baada ya kukaribishwa akatembea taratibu na kuketi kwenye moja ya kochi, kisha macho yake yakawa yanatazamana na nyuso za watu wawili waliokuwa ndani humo.

“Unamfahamu Linda….”Bila hata salamu yule Mama alifungua mazungumzo kwa kunyoosha maelezo moja kwa moja.

“Ndi..ndio…”Fred alijibu kwa kusita sita.

“ok sawa, sasa mimi ndio Mama yake sijui kama unanifahamu au laa”aliongea yule Mama na kunyamaza kwa sekunde kadhaa.

“Kuna uhusiano gani kati yako na Linda?”akaendelea na kuachia swali kisha akamkazia macho Fred ambaye alipeleka uso wake chini.

“Nijibu bhana, sina muda wa kuangalia mapozi yako”yule mama akawaka tena.

“Ni ni mchumba wangu”kwa hofu Fred alijibu.

“Aaah! Mtoto huyuu, sijui alikuwa anatafuta nini…”Mama Linda aliongea kwa huzuni huku akitikisa kichwa kisha akakaa kimya kwa sekunde nane hivi, huku akiwa ameinamisha uso wake chini.

“Lengo la kukuita hapa ni moja tu…Kama ulivyosema kwamba wewe una uhusiano na mwanangu…sasa katika kukutana kukutana kwenu huko umempa ujauzito na hilo najua haulifahamu”

Ulikuwa ni ujumbe uliomshtua sana Fred hata akatoa macho kama mjusi alibanwa na jiwe, mapigo ya moyo yakamwenda kasi kama piki piki ya mashindano, alihisi jasho likimmiminika licha ya ukwasi wa viyoyozi uliokuwepo kwenye eneo hilo.

“Usishtuke, mlichokuwa mnakifanya matokeo yake ni hayo”

“Jambo pekee ambalo limenigusa ni kwamba wewe ni maskini..nafahamu kwamba huna nguvu ya kumshawishi mwanangu hadi akubali kukupenda, kwa namna yoyote Linda itakuwa ametaka mwenyewe, hivyo wewe sioni kosa lako”

“Shukuru sana kwamba nimekuwa wakwanza kufahamu suala hili, laiti kama baba yake atafahamu, atakufanya kitu kibaya, hatojali kwamba wewe ni maskini wala nini…”
Mama Linda aliendela kutema nyongo na Fred akawa anasikiliza kwa makini anachoambia licha ya kwamba akili yake ilishavurugika.

“Kwa sababu mwanangu alipenda mwenyewe.. Jambo pekee ninaloweza kukusaidia kwa sasa ni wewe kuondoka nchini humu, rudi kwenu, maana ukiendelea kukaa itakuwa hatari zaidi kwako na hata kwa wale ambao unawategemea ikiwa Baba Linda atafahamu ukweli”
“Nimekuandalia tiketi ya ndege na kiasi cha pesa, hivyo ndani ya saa 24 zijazo unatakiwa uwe tayari umeshaondoka nchini humu”
Mama Linda alimaliza kuongea kisha akaweka bahasha juu ya meza na kumuonyesha ishara Fred kwamba aichukue.

“Kijana jambo la kuzingatia kwamba kitendo cha uzinifu kwenye nchi yangu hakitakiwi, lakini Madam ameniomba sana nisichukue hatua yoyote juu yako.. Hivyo nafasi uliyoipata usije ukaitumia vibaya naomba uondoke na unapoenda nenda katubu ulichokifanya, ukivuka huo muda uliopewa, ukikamatwa ukaletwa hapa sitokuwa na msamaha tena”

“Nafahamu pia ulikuwa na binti yetu Fayma kwa masaa yasiyopungua matano nyumbani kwako.. sijathibitisha chochote lakini ikiwa umewachanganya wote wawili, sasa kabla ya jambo lolote kutokea naomba nisione sura yako ndani ya masaa hayo”

Wakati anachukua ile barua Mfalme naye aligongelea msumari kwenye kidonda na kufanya Fred hofu impande zaidi hadi akawa anatetemeka.

“Usiogope…Tumekwambia ukweli ambao utakusaidia, hivyo fuata tulichokwambia,”Akasema tena Mfalme.

Fred alichukua ile bahasha na kuifungua pale pale, ndani yake akakutana na tiketi ya ndege ya shirika la Fly Emirates ambayo ilikuwa inaonyesha kuwa atatakiwa kusafiri mchana wa siku iliyofuatia.

Pia kulikuwa na noti kadhaa za dola 100, ambazo hakuzihesabu zaidi aliifunga tena ile bahasha na baada ya muda wakaingia walinzi ambao walimchukua na kumtia kwenye gari ambayo ilifunga safari hadi mahali alipokuwa anaishi kisha akaachwa hapo.

Alishuka kwenye gari akitembea huku mawazo yakiwa yametawala vilivyo kwenye kichwa chake, aliwaza na kujiuliza Linda yupo wapi?, yupo kwenye hali gani…Mbona amekuwa na mikosi hivyo, kila likitoka hili linaingia lile, ina maana safari yake ya upambanaji ndo imeishia hapo?

Alitemba hadi ndani kwake ambapo alifikia ukumbini na akaanza kuangisha kilio cha haja.

Alilia kwa muda mrefu sana hadi kichwa kikanza kumuuma, akasahau hadi kula, alifika nyumbani kwake saa 12 jioni, lakini alilia hadi saa mbili na akasahau hata kupata chakula cha usiku.

Uchovu, mawazo na maumivu ya kichwa vilisababisha usingizi umchukue haswa hadi, alikuja kushtuka kesho yake saa 5:00 asubuhi.

Laa haulaa! Ndege ambayo ilibidi apande ilikuwa inaondoka saa sita kamili mchana, mapigo ya moyo yakamwenda kasi hakujua afanyaje maana aliona dalili zote za kuachwa na ndege.

Alinyanyuka pale kwenye kochi haraka na kuelekea kwenye kabati lake la nguo akachukua baadhi ya vitu vyake muhimu kwa ajili ya kusafiria ikiwemo na (Pasipoti) na safari ya kuondoka kwene jengo hilo ikaanza.

Hadi anafika uwanja wa ndege tayari ilishakuwa ni saa 05:49, mchana, alipojaribu kwenda kwenye mstari wa kufanya chek in(Sehemu ya ukaguzi maalumu kabla ya kwenda kwenye dirisha la kupewa Borading Pass), aliambiwa kwamba muda ulishaisha na abiria wote wameshapanda kwenye ndege,hivyo haiwezekani yeye kusidiwa.

Alijikuta akidondoka chini kama zigo la mahindi huku machozi yakimninika kwenye mashavu yake.

“Eee jamani jamani jamani”Alisema Fred huku akipiga piga chini mikono yake kwa uchungu.

“Kaka kama unaweza nenda kanunue tiketi nyingine, ubadilishe siku ya kuondoka”

Aliongea mmoja ya maofisa wa uwanja wa ndege.

Fred alikaa chini kwa muda kisha akanyanyuka na kusogea kwenye dirisha la Fly Emirates kuulizia uwezekano wa kupata tiketi, lakini akaambiwa tiketi atapata lakini itabidi asafiri siku tatu mbele.

Nguvu zikazidi kumuishia na akachukua jukumu la kumpigia simu Mr. John yule aliyemtembelea Hospitalini.

“Wakinikamata wataniua au wataninyonga tafadhali naomba unisaidie niondoke hapa kaka, nina familia inanitegemea, mimi ndio mototo tegemeo nyumbani tafadhali nisaidie niondoke”

“Naomba sana kaka, nisaidie, nisaidie”Yalikuwa ni maneno ya Fred mara tu baada ya John kupokea simu.

“Fred kuna shida gani tena?” kwa wasi wasi John aliuliza.

“Kaka majanga, majanga kaka”alijibu Fred na mwisho akamalizia na kilio.

“Niambie upo wapi nikufuate”

“Nipo Airport nipo Airport”

“Hii ya hapa Riyadh?”

“Ndio ndugu”

“Basi wewe usiondoke nisubirie hapo hapo, sawa?”

“Sawa”

Baada ya dakika 40, John aliwasili uwanja wa ndege na gari yake, akamchukua Fred hadi kwenye moja ya migahawa na kumtaka amsimulie tatizo haswa ni nini.

Fred hakuficha kitu alimpa mkasa wote hadi kufikia hapo na ndio hivyo yalishabakia masaa machache kabla ya ule muda aliopewa kumalizika.

“Kiukweli kesi yako ni ngumu sana na sijui hata nakusaidia vipi, ila ngoja tupambane tujue tunalimalizaje maana serikali ya nchi hii haina utani hata kidogo.”

“Kaka chonde chonde wewe ndio mtetezi wangu kwenye hili, ukiniacha nimeshikwa.”
“Nakuelewa usijali mimi nitajua chakufanya wewe sahizi twende wote kwanza Hospitalini maana nimechomoka tu pale, kisha baada ya muda tutajua nini chakufanya”
Waliongozana hadi Hosptiali ambayo John alikuwa akifanyia kazi, akamalizana na baadhi ya wagonjwa kisha wakatoka hapo hadi nyumbani kwa John, wakapata chakula cha usiku kilichoandaliwa na mke wa John ambaye pia alikuwa  ni Mkenya pia.

Baada ya kupata msosi ndio wakakaa mezani kujadili nini kifanyike, yumkini Fred hakuwa na lolote la kushauri zaidi alikuwa anataka kusikiliza maagizo juu ya nini afanye.

“Jambo la umuhimu kwa sasa ni wewe kuondoka nchi hii, na kwa ulinzi ambao upo uwanja wa ndege na jinsi utaratibu ulivyo nafikiri ni ngumu sana wewe kupita ukizingatia wameshaanza kukutafuta kwa kuwa masaa uliyopewa yameshapita”Alisema John kisha akaweka kituo.

“Nafikiri tujaribu kuangalia upande wa maji, kule inaweza kuwa rahisi wewe kupenywa kwa sababu tuna wenzetu kutoka Afrika mashariki wanafanya kazi kwenye mameli na pale bandarini, hivyo nafikiri niwasiliane nao wale ili tujue jinsi gani ya kukusaidia upenye pale.”

Aliongeza John kisha akachukua glasi ya maji iliyokuwepo mezani na kupiga funda moja.

“Kaka mimi nakusikiliza wewe, lolote lile linalowezekana tufanye mimi niondoke kwenye hii nchi”Kwa sauti ya upole Fred naye alichangia.

“Sasa chakufanya hapa itabidi niongee na majamaa kule waangalie meli itakayokuwa inaenda hata Afrika ya Kusini.. wakutie mule najua ukifika huko kufika nyumbani itakuwa rahisi kidogo..maana wabongo ni wengi wanaweza kukuachangia hata nauli au unaweza kufanya kazi ndogo ndogo na ukapata nauli ya kurudi bongo…”alisema John na baada ya dakika moja akanyanyuka pale mezani huku akibonyeza bonyeza simu yake kisha akaiweka sikioni na akawa anatembea kutoka eneo hilo huku akiongea.

Baada ya dakika tano hivi akarejea tena ndani na kumwambia Fred kwamba kila kitu kipo sawa.

Saa sita usiku gari ya wagongwa iliwasili kwenye nyumba hiyo na Fred sambamba na John wakapanda kwa nyuma.

Waliamua kutumia gari ya wagonjwa kwa sababu isingekuwa rahisi kugundulika kwani ilikuwa haikaguliwi, hivyo ilipita kwenye vikwazo vyote.

Gari ilishika njia kulitafuta Jiji la Dammam ilipo bandari ya King Abdul Aziz Port, kwa sababu ndani ya Riyadh hakukuwa na bandari inayoingiza meli kubwa.

Mpango wao ulikuwa ni Fred kupanda meli za mizigo ambazo zitaelekea nchi za kusini mwa Afrika ama mashariki.

Kutoka Riyadh hadi Dammam ni mwendo wa masaa matatu na dakika zisizopungua 50, lakini kwa sababu walitumia gari ya wagonjwa walitumia masaa mawili tu kufika.

Baada ya kufika nje ya bandari, John alimtazama Fred na kuwambia.

“Nafikiri kuna kitu hatujakiweka sawa.. Humo ndani kwa namna mchongo tulivyouseti  inabidi tukuingize kwenye sanduku kama maiti, hivyo jambo la kufanya hapa itabidi tukuchome sindano ya usingizi halafu tukutie kwenye sanduku”

“Sijaelewa kaka sindano yanini tena..?” Kwa wasi wasi Fred akahoji.

“Hujaelewa nini hapo ndugu, nimekwambia hao tumewaambia kwamba tunasafirisha mtu aliyefariki hivyo itabidi hapa uchomwe sindano ya usingizi halafu tukutie kwenye sanduku ndo tukuingize ndani maana kukupeleka hivi hivi itakuwa ngumu” Maelekezo ya John yalimchanganya sana Fred ambaye hakuwa ameelewa hata kwa asilimia 10 kile alichoelezewa.

“Yaani mimi sijaelewa si tumekubaliana kwamba nitasafiri na meli kama kawaida hadi Afrika, sasa hii ishu ya kuchomwa sindano mbona mpya?” Fred akahoji.

“Fred hatuna muda wa kupoteza muda unazidi kutusaliti… Fanya ninachokuelekeza.. Lasivyo tutabaki hapa hapa”alisema John na raundi hii alitumia sauti ya juu kuonyesha msisitizo.

Waswahili wanasema muhitaji huwa ni mtumwa, Fred hakuwa na budi zaidi ya kukubaliana na kile alichoambiwa ilimradi tu aondoke kwenye taifa hilo.

Dakika chache mbele akaingia jamaa mmoja aliyevalia mavazi ya kidaktari akiwa na  kiboksi kilichochorwa msalaba mwekundu.

Akamtaka Fred alalae katika kitanda cha wagonjwa kilichokuwemo ndani ya gari hilo, baada ya hapo akautafuta mshipa na kudumbukiza sindano.

“Unajisikiaje? Unaitwa nani?” Yule daktari akaendelea kumtandika maswali baada ya kumchoma ile sindano.

Fred akawa anaendelea kujibu maswali anayoulizwa na kila dakika zilivyozidi kwenda ndio akawa anahisi macho yake kuwa mazito zaidi na mwishowe akapatwa na usingizi mzito ndani ya dakika nne tu, asijue hata nini kiliendelea baada ya hapo.

Baada ya kuhakikisha kuwa Fred amelala kabisa John kwa kushirikiana na wenzake walimtoa Fred kwenye gari hiyo ya wagonjwa hadi nje ambapo kulikuwa na gari nyengine ya wagonjwa lakini ilikuwa ni kubwa zaidi ya ile iliyowasafirisha hadi katika eneo hilo.

Ndani ya gari hilo jengine kulikuwa na vifaa mbali mbali vya kufanyia upasuajili na mashine za kumsaidia mtu kupumua.

Akiwa kwenye usingizi mzito Fred alifanyiwa upasuaji wa masaa matatu kisha akashonwa na kutolewa kwenye gari hilo kupitia kitanda maalumu na kuingizwa bandarini ambapo walinzi waliokuwepo mlangoni waliwaongoza wale waliombeba hadi kwenye mlango mmoja wa meli kubwa akaingizwa na kwenda kufungiwa kwenye chumba maalumu.

“Ndio boss, kila kitu kipo sawa na mzigo tumeshaupata,”ilikuwa ni sauti ya John aliyekuwa akiongea  na mtu kupitia simu yake ya mkononi.

“Safi John… Nilitegemea tu, hutoniangusha, kazi nzuri, malipo yako utayapata kesho asubuhi”

“Nashukuru sana bosi, hapa kazi tu”

“Sawa, kuna mteja mwingine itabidi tuangalie namna ya kumsaidia apate mzigo nayeye, maana mgonjwa wake yuko kwenye hali mbaya, figo zote zimefeli na anaweza akapoteza maisha tukichelewa”

“Sawa bosi…Nimekuelewa acha tupambane”

“Poa, nakutakia safari njema ya kurudi”

Baada ya mazungumzo hayo mafupi yenye kueleweka John alikata simu na kutoka eneo hilo la bandari kwa kuwa kulishaanza kupambazuka.

John mbali yakuwa na kazi ya udaktari pia alijihusisha na biashara haramu ya uuzaji wa viungo vya binaadamu na sana ilikuwa ni uuzaji wa figo.

Yeye kazi yake ilikuwa ni kutafuta watu wa kuwafanyia kitendo hicho na kusaidia kwenye suala la upasuaji lakini kulikuwa na mkubwa wao ambaye ndio alikuwa akiratibu mtandao mzima.

Kawaida Upasuaji mkubwa kama wa figo ( kidney transplant surgery ) huchukua kati ya masaa matatu hadi manne na hii itategemea na uzoefu wa daktari anayefanya zoezi hilo, kuna wengine hufanya kwa muda  mrefu zaidi, lakini uzoefu wa madaktari waliokuwa wamemfanyia upasuaji Fred ulikuwa mkubwa zaidi hivyo zoezi hilo lilichukua masaa matatu hadi kukamilika.

Mchongo wa Fred kutolewa figo uulianza tangu John aliposaidia kumtoa uwanja wa ndege ambapo baada ya kujua sakata lake akaona hiyo itakuwa ni nafasi nzuri ya yeye kupiga pesa kwani hata akimtoa figo atakuwa hana uwezo wa kushtaki kwani wakati anazinduka tayari itakuwa ameshaondoka nchini humo na atakuwa kwenye meli.

….IKULU LITHUANIA…

“Dada, Madam anakuita ukumbini”Mhudumhu wakike aliingia kwenye chumba alicholala Linda na kumjulisha wito huo.

Lakini hakuna jibu alilopewa na Linda ambaye alikuwa amejikunyata pembezoni mwa kitanda chake kama mtu aliyekuwa akihisi baridi.

Macho ya Linda yalikuwa yamebadilika rangi kutokana na kilio alichokianzisha tangu hata hajapanda ndege ya kwenda Lithuania.

Moyoni mwake alikuwa akimuwaza Fred tu, aliona ni kama ndio mwisho wake kati yake na mwanaume huyo kwani hata simu aliyokuwa anaitumia alinyang’anywa.

Yule mhudumu baada ya kuona hapati majibu ya maagizo yake alitoka chumbani humo na kuelekea ukumbini.

“Amegoma mama, haongei chochote ameendelea kulua tu, siku yapili leo hajala chochote”

Alisema yule Mhudumu kumwambia mama Linda aliyekuwa ukumbini.

“Basi nenda, nitamalizana naye mwenyewe”akajibu mama Linda na punde tu akanyanyuka alipokuwa ameketi na akaenda hadi kwenye chumba cha Linda.

Baada ya kuingia alimkuta vilevile kama alivyokutwa na mhudumu.

“Mwanangu”aliita huku akimsogelea Linda.

“Sijaja hapa kama mama, nimekuja hapa kama rafiki yako, nina maswali yangu nitaomba unijibu kwa ufasaha kama rafiki yako sawa mama?” Kwa sauti ya upole alisema Mama Linda lakini binti huyo aliendelea kukaa kimya tu.

Mama Linda alimsogelea mwanawe na kuketi karibu yake, kisha akawa anamtazama usoni.

‘Naomba uniambie mara ya mwisho kuona siku zako ilikuwa lini..?”

Swali hilo lilimfanya Linda ashtuke na kuinamisha uso wake chini.

“Naomba tu, uniambie hapa nakuuliza kama rafiki yako na sio mama… Mimi ndio naweza kuficha siri zako”aliongeza tena mama Linda kauli ambayo ilimfanya Linda anyanyue jicho la wizi na kumtazama.

“Mu..da ki..d..ogo mama” akajibu Linda kwa kusita sita sita.

“Na hujafanya juhudi zozote baada ya kuona hali hiyo..?”

“Ha ha pana ma..ma, mzunguko wangu huwa unachanganya hivyo nilijua ni kawaida”

Baada ya kusema vile Mama Linda alinyoosha mkono wake na kumpa Linda kipimo cha mimba.

“Hiki ndicho ulichoenda kutafuta huko kwenye nchi za watu?…”Kipimo kilikuwa kinaonyesha mistari miwili ikiwa na maana kwamba aliyepimwa alikuwa ni ujauzito.

Macho yalimtoka Linda na mapigo ya moyo yakamwenda kasi kama Simba aliyeibiwa mtoto.

“Nakuuliza wewe mwanangu, hiki ndicho kilichokupeleka kule…?”Mama Linda alirudia tena swali lake baada ya kuona hajajibiwa.

Lakini Linda aliendelea kunyamaza kama mtu aliyekuwa amekatwa ulimi.. Akili yake ilikuwa imeshavuka hadi geti la ikulu, maswali mengi yakitawala ubongo wake.

“Hivi, unajua baba yako akijua, utaniweka kwenye mazingira gani mimi?”

“Mama  nisamehe, hiki sicho kilichonipeleka”

“Mimi hujanilkosea, umejikosea mwenyewe, baba yako akijua unafikiria ataamua nini juu yako…?”

“Si ulikuja wiki chache zilizopita hapa na akakuambia kwamba ukimaliza kusoma tayari mume ameshakutafutia…Haya hii skendo ya mimba ikisambaa unafikiria hiyo ndoa tena itakuwepo…?”Mama Linda aliuliza maswali mfululizo ambayo ubongo wa Linda ulikosa majibu sahihi ya kuyajibu.

“Mama nisaidie, mimi sikudhamiria…”Linda akaongea kwa sauti ya upole.

“Nakusaidiaje mtu usiyetaka kusaidika, ulikuwa hutaki hata kuniona haya endelea kujikunyata kama kuku na mayai yake..”

“Hapana mama, mimi sikujua umenitoa kule kwa sababu gani…”

“Hukujua ee!”

“Kwahiyo sasa umejua..Haya unataka kufanya nini?”

‘Mama nisaidie”akasema Linda na raundi hii machozi yalikuwa yakitiririka kwenye mashavu yake.

“Mimi chakukusaidia hapa sina… zaidi labda ukatoe huo ujauzito, tulifunike hili baba yako asijue”alisema mama Linda.

“Fred..Fred yupo wapi”Linda akauliza.

“Yaani, kwa hali uliyokuwa nayo muda huu  bado unamuwaza tu, yule ngedere”akajibu mama Linda kwa sauti kali iliyoashiria hasira.

 “Mama nataka kujua tu!”

“Nimemrudisha kwao, sasa sijui kafika au laa”
“Umemrudishaje mama?”
“Usiniulize sana kuhusu huyo mtu, utanichefua zaidi”Maneno makali ya mama Linda yalisababisha mrembo huyo macho yake yazidi kuangusha machozi.

“Sasa hapa jambo ni moja tu… ufanye mpango tu kutoa hiyo mimba au uache hadi baba yako ajue, aone namna atakavyokufanya yeye, mimi sina msaada mwingine zaidi ya huo…”Alimaliza kuongea mama Linda na kufunga mjadala kwa kunyanyuka na kuanza kutembea kutoka kwenye chumba hicho lakini kabla hajatoka mlangoni alipinduka na kumwambia Linda kwamba ana siku mbili za kuamua ikiwa atabakia na ujauzito hadi baba yake ajue ama atautoa na kila kitu kiishie hapo.

Author: Gadi Solomon