Morogoro Nitakuja

Niombacho majaliwa, siku nitajikongoja,
Bibi alipozaliwa, kupazuru nina haja,
Kitovu kilifukiwa, nyanya alipopataja,
Morogoro nitakuja, bibi alipozaliwa.

Wakami nawaiteni, wajomba zangu wa haja,
Wakutu wa mindukeni, watukuka ninyi waja,
Na Mgeta furahini, naja kuleta faraja,
Morogoro nitakuja, bibi alipozaliwa.

Siku hiyo tajilawa, tarehe sitoitaja,
Nisije nikachelewa, kwa kufanya ngojangoja,
Kwa mbeta tafurahiwa, Matombo mkiningoja,
Morogoro nitakuja, bibi alipozaliwa.

Mjomba wangu Mloka, naomba fanya halija,
Tambiko ninaitaka, siku nitakayokuja,
Tutambikie mizuka, na Kingalu kumtaja,
Morogoro nitakuja, bibi alipozaliwa.

Babu alipovutiwa, nije waonawambeja,
Mke akenda opowa, kwa muhunzi mwenye tija,
Binti Fundi akaowa, na babu kuvikwa koja,
Morogoro nitakuja, bibi alipozaliwa.

Matombo nitapumuwa, japo usiku mmoja,
Ngagili naye Mokiwa, niende nao pamoja,
Sadaka niende towa, Kolelo kwenye miuja,
Morogoro nitakuja, bibi alipozaliwa.

Kidodi sikosi tuwa, Muhuga si unde hoja,
Wala usiwe mkiwa, vibogwa tuje hamoja,
Kinole twenda kulowa, pale katika daraja,
Morogoro nitakujua, bibi alipozaliwa.

Tule vile vya kuliwa, na togwa liso mabuja,
Chigulubu na wazawa, niijege hamwe kuja,
Na Lupokela tukiwa, Mabutwa ninapataja,
Morogoro nitakuja, bibi alipozaliwa.

Najua nitahemewa, Msimbe lete kongoja,
Chamanyani naujuwa, mlima una viroja,
Hodi ya kwako mndewa, Juma Kibwana nakuja,
Morogoro nitakuja, bibi alipozaliwa.

Chang’asa kabene mihuwa, Tulo kose ngijangija
Bibi alipolelewa, mjukuu nimekuja,
Viatu vyangu navuwa, hapa namaliza haja,
Tulo mie nitakuja, bibi alipozaliwa.

                MKANYAJI
           Hamis .AS.Kisamvu.
                 0715311590
         Kissamvujr@gmail.com
         Baitu Shi ri- Mabibo
          Dar es salaam- Tanzania
                 20-Mei-2022

Author: Gadi Solomon