Makamu wa Rais aagiza mambo saba kukipa hadhi Kiswahili

Pelagia Daniel

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa maagizo na kusisitiza wataalamu na wapenzi na mabingwa wanaotumia lugha ya Kiswahili kutumia Kiswahili sanifu.

Pia amewapongeza wanaotumia mitandao ya kijamii na Tehama kuhamasisha matumizi ya Kiswahili kuwa waendelee na kazi hiyo. Pia amezipongeza balozi zilizopo nje kwa kuazimisha siku hii.

Dk Mpango ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Julai 7, 2022 wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimatifa wa Julius Nyerere (JNIC) jijini Dar es Salaam.

Akihutubia katika maadhimisho hayo, ameziagiza wizara na taasisi za Serikali kutekeleza maagizo yaliyotolewa juu ya matumizi ya Kiswahili. mikutano, warsha na mijadala ya umma iendeshwe kwa lugha ya Kiswahili.

 “Napenda kuelekeza kama ifuatavyo, jambo la kwanza Wizara na taasisi za Serikali ziendelee kutekeleza maagizo yaliyotolewa kwamba nyaraka za mawasiliano za wizara na idara zake ziwe kwa Kiswahili, mikutano, warsha na dhifa ziendeshwe kwa Kiswahili,” amesema Makamu wa Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi.  

 Amesema majina ya barabara, mitaa, mabango, fomu za usaili maelekezo ya matumizi ya dawa zote, bidhaa na huduma pia ziandikwe kwa Kiswahili.

 Dk Mpango ameagiza taarifa za miradi na mikataba inayowahusu wananchi ziwe kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa.

“Jambo la pili, taarifa za miradi na mikataba inayohusu wananchi ni lazima ziwe kwa lugha ya Kiswahili, zisiwe kwa lugha ya kigeni pekee lengo ni kuwawezesha wananchi kuelewa kila jambo muhimu katika ustawi wa maisha yao,” amesema Dk Mpango.

Jambo la tatu sheria na kanuni ambazo bado hazijatafsiriwa na ambazo zinapaswa kufanyiwa tafsiri kwa kushirikiana na mabaraza ya Kiswahili na ofisi ya mwanasheria wa mkuu wa serikali.

Jambo la nne, ameagiza vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili vihakikishe vinatumia Kiswahili fasaha na sanifu na vizingatie sarufi ya lugha sanifu na ikitokea anayezungumza hatumii lugha sanifu awepo mtu wa kutoa tafsiri ya lugha kwa Kiswahili. Lengo kuwafaanya wananchi waelewe kinachozungumzwa.

Jambo la tano kuanzisha vituo vya kujifunzia lugha ya Kiswahili, ameziomba balozi zote ziwatumie wataalamu waliosajiliwa katika kanzi data ya Bakita na Bakiza na kumuasa Waziri asimamie jambo hilo liweze kutekelezeka.

Ameagiza Bakita kwa kushirikiana na Bakiza waendelee kuwa wabunifu katika kuzalisha wa misamiati ya Kiswahili ili kuendana na kasi ya maendeleo ya kisayansi na teknolojia.

Jambo la saba, ameagiza wizara na taasisi husika kuhakikisha mfumo wa kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni kwa njia ya mtandao (Swahili prime) unatumika kikamilifu.

Amehitimisha hotuba yake kwa kuwaasa wananchi wajitokeze kikamilifu kushiriki sensa ya watu Agosti 23 mwaka huu.

Author: Gadi Solomon