Mpango ahamasisha matumizi ya Kiswahili kwa Diaspora Marekani

Nabil Mahamudu, SwahiliHub

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania waishio Newyork Marekani, mkutano huo uliaandaliwa na Dk Temba Anesedius ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya hiyo katika ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania, Marekani.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania waishio Newyork Marekani, mkutano huo uliaandaliwa na Dk Temba Anesedius ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya hiyo katika ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania, Marekani.

Dk Mpango amewapongeza wanadiaspora kwa jitihada wanazofanya za kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inatambua mchango wa wanadiaspora hao na itaendeleza kuunga mkono jitihada wanazozifanya.

“Niwaombe Watanzania mlioko nje muendelee kuchangia maendeleo ya taifa letu, lakini msisahau kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zinazopatikana nyumbani.”

Pia Makamu wa Rais amewaomba Wanadiaspora kuisadia serikali katika kutafuta wawekezaji katika miradi inayoendelea Tanzania, kusaidia kupatikana kwa masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nyumbani.

“Pia niwaombe kushiriki katika kazi ya kutusaidia kutafuta wawekezaji katika miradi mbalimbali inayoendelea nchini na mtusaidie kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali ambazo tunazalisha kule nyumbani.”

Kadhalika Dk Mpango amewaomba kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana Tanzania nzima na kushirikiana na serikali kuendeleza matumizi ya Kiswahili kupitia uanzishwaji wa vituo vya kufundisha Kiswahili katika ofisi za balozi.

“Mtusaidie kutangaza vivutio vya utalii Tanzania nzima bara na visiwani, lakini muendelee kushirikiana na serikali kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa kuanzisha vituo rasmi vya kufundisha Kiswahili, tamaduni, na sanaa mbalimbali za Kitanzania.” Amesema DK Mpango.

Naye Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Wizara yake ipo kwenye mchakato wa kutengeneza sera ya mambo ya nje ambayo inatambua mchango wa diaspora, aidha amesema Wizara itazindua Kanzidata ambayo itawezesha wanadiaspora kutambulika popota walipo duniani.

“Tumekuwa kwenye mchakato wa kutengeneza sera yetu ya mambo ya nje ambayo inatambua sana sana, kwa namna ya pekee mchango wa diaspora na tujiongeza jinsi gani ya kuendelea kuwasiliana na nyinyi lakini pia kuwa na Kanzidata kuweza kujua nani yuko wapi, nani anafanya nini, kwahiyo hivi karibuni tutazindua ‘diaspora digital’ hapa.” Amesema Balozi Mulamula.

Mwanzilishi wa Jumuiya ya watanzania waishio Newyork, Marekani Profesa Estomia Mtui ameishukuru serikali kupitia utaratibu uliowekwa ambao uliowawezesha kupata vitambulisho vya taifa na kuwashughulukia swala la hadhi maalumu kwa diaspora, kadhalika ameendelea kusema kuwa Jumuiya itaendeleza ushirikiano na kuchangia maendeleo Tanzania, kwani ni wajibu wa kila mtanzania kuchangia maendeleo kwa Taifa.

“Tunatoa shukrani nyingi kwa mchakato unaoendelea kwanza, kutupatia vitambulisho vya taifa tulikuwa na ‘secular’ Uingereza nafikiri hata hapa ipo ya mpangilio wa kuandikishwa ya kupata vitambulisho vya taifa, pia tuliomba kwa Rais wakati alipokuwa hapa, tupate vitambulisho vya kufanya uwekezaji na kutembelea nyumbani. Rais alitamka kwa kauli moja kuwa kutatokea hadhi maalumu kwa watu waliokuwepo nje na mchakato huu umeanza nilisikia hata bungeni ulianza kujadiliwa baada ya kuwasilishwa na Waziri husika.” Amesema Profesa Mtui

Makamu wa Rais yuko Marekani kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Tanzania katika mkutano wa Baraza la 77 la Umoja wa Mataifa, lakini wanadiaspora bado wana kilio cha muda mrefu ambacho ni uraia pacha.

Author: Gadi Solomon