Mtetezi

Hili natamka wazi, liwe andiko rejea,
Nimeichagua kazi, ya lugha kuitetea,
Sitakuwa na mbawazi, mtu akiikosea,
Nitasimama daima, kutetea kiswahili.

Tena pasipo henezi, wala kitu kuchelea,
Kukaa kando siwezi, watu wakikionea,
Waitwao wachochezi, hovyo wakikinenea,
Nitasimama daima, kutetea kiswahili.

Bila ya kipingamizi, naapa nitakemea,
Maovu na matatizi, lughani yakitokea,
Dhahiri lugha azizi, mbali iweze sogea,
Nitasimama daima, kutetea kiswahili.

Hakika wenye maozi, hili mtajionea,
Nitafanya ukombozi, watu nikiwaendea,
Pale pakusema jozi, wasije kusema pea,
Nitasimama daima, kutetea kiswahili.

Tama haya maamuzi, nanyi nawategemea,
Tuutumie ujuzi, lugha izidi kumea,
Tushikane kama nyuzi, koti tukajishonea,
Nitasimama daima, kutetea kiswahili.

Mshairi Machinga,
mfaumehamisi@gmail.com,
+255716541703/752795964,
Dar es salaam, Kkoo.

Author: Gadi Solomon