Muacha kweli


Naomba kwako Wahabu, iongoe yangu nia,
Nisingie majaribu, ikanicheka dunia,
Nazihofia harabu, za waja wasotimia,
Hakosi kuirudia, kwa kila muacha kweli.

Simi mzuri khatibu, kidogo tawagawia,
Kila jambo na sababu, mipango yake Jalia,
Kweli hazina ya babu, siache kukumbatia,
Hakosi kuirudia kwa kila muacha kweli.

Muacha kweli ja bubu, maneno humkimbia,
Hazimwishi tabutabu, hushika na kuachia,
Haaminiki janibu, hata na nyumbani pia,
Hakosi kuirudia kwa kila muacha kweli.

Ni mengi yata msibu, kuacha kilo sawia,
Hupoteza maswahibu, pa laki wabaki mia,
Ukweli ndiyo tabibu, vyema kuushikilia,
Hakosi kuirudia Kwa kila muacha kweli.

Kweli sawa na kibubu, akiba ilotulia,
Kwenye siku za adhabu, neemani yakutia,
Ukweli ja abuwabu, huwezi badili njia,
Hakosi kuirudia kwa kila muacha kweli.

Na hawezi ihujubu, na lengo likatimia,
Itakuja mdhurubu, hatiani akangia,
Ndanimwe ina thawabu, mlipa wake Jalia,
Hakosi kuirudia kwa kila muacha kweli,

Watama nilo khutubu, nia imeshatimia,
Wenye hila za kalubu, washakatika mikia,
Kurudi ndiyo wajibu, mja haujatimia,
Hakosi kuirudia kwa kila muacha kweli.
©MKANYAJI
HAMISI A.S.KISSAMVU
0715311590
kissamvujr@gmail.com

Author: Gadi Solomon