Muuaji asakwe

MUUAJI ASAKWE

Patrick J. Massawe

0715676249

Utangulizi

Mwanamke mrembo anauawa ndani ya bafu, nyumbani kwake, eneo la Tabata, Jijini Dar es Salaam. Kwanza kabisa, muuaji huyo katili alimtumia ujumbe wa vitisho muda mfupi tu kabla ya kutekeleza mauaji hayo. Pia, muuaji huyo alimbaka mrembo huyo kabla ya kumuua. Upelelezi wa Jeshi la Polisi, unafanyika mara moja. Msako mkali dhidi ya muuaji huyo unafanyika, na inagundulika siri nzito iliyojificha nyuma ya mapazia kuhusiana na kifo hicho chenye utata. Kama kawaida, mtunzi wako mahiri,  PATRICK J. MASSAWE anatiririka na hadithi hii ya kusisimua.     Fuatilia mpaka mwisho wake…

MCHANA  wa saa sita hivi, John Bosho  alikuwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Harrier  la rangi ya fedha, lililokuwa na kiyoyozi kilichompatia hewa nzuri ya ubaridi kiasi cha kulifukuza joto lililokuwa linafukuta huko nje.  Muda huo alikuwa anatafuta eneo la kupaki gari hilo, kwenye maegesho, nje ya Hoteli ya The Kibo II Anex, mtaa wa Kipata, eneo la Gerezani.

Hii ni hoteli iliyopo ndani ya jumba la ghorofa tano, linalopakana kabisa na jengo la ghorofa, linalomilikiwa na Shirikisho la Vyama vya Ushirika, katika Barabara ya Lumumba, umbali wa mita tano hivi, na pia siyo mbali sana na Viwanja vya Mnazi Mmoja. Baada ya kulipaki gari hilo, John Bosho alishuka na hatimaye kuingia ndani ya hoteli hiyo maarufu yenye hadhi, ambayo alizoea kwenda mara kwa mara kujipatia chakula cha mchana.

Kama kawaida, John Bosho alipoingia, alichagua meza moja ya pembeni na kukaa ili aweze kupatiwa huduma ya chakula. Kabla ya kuagiza chakula, aliangaza macho yake katika pembe zote za humo ndani, ambapo palikuwa na wateja kadhaa waliokuwa wanakula. Akiwa ni mwenyeji pale, aliweza kuhudumiwa chakula alichokipenda, aina ya wali kwa nyama ya ng’ombe.  Aliendelea kula taratibu huku akiangalia jinsi wateja wengine walivyokuwa wanaingia.

Wakati John Bosho akiendelea kula chakula chake taratibu, mara akaingia mwanadada mmoja, kimwana na mrembo wa haja, aliyekuwa anatembea kwa mwendo wa kunata. Moja kwa moja akaenda kukaa kwenye meza iliyokuwa pembeni, jirani yake tu. Mara baada ya kukaa, kimwana huyo aliangaza macho pande zote kuangalia alipo mhudumu, na mhudumu alipomwendea, alimwangiza chakula, wali kwa nyama ya kuku, pamoja na soda moja aina ya Mirinda.

Kimwana huyo alipohudumiwa chakula kile alichokuwa ameagiza, alinyanyuka na kunawa mikono yake katika sinki maalum lilokuwa umbali mfupi kutoka ilipokuwa meza yake. Alipomaliza kunawa, akarudi tena na kendelea kula taratibu, tena kwa mapozi ya hali ya juu, kwani hakuwa na haraka. Wakati wote huo alikuwa akiangalia chakula chake na wala hakuwa na muda wa kuangalia pembeni.

John Bosho aliendelea kumwangalia kimwana huyo kwa muda wote, ikiwa siyo mara yake ya kwanza kumwona akiingia hotelini pale. Ni mara nyingi walikuwa wanakutana, yaani ni kama bahati vile, kwani kila mmojawapo anapoingia, basi hujikuta wote wameingia, tena kwa wakati mmoja kana kwamba walikuwa wameahidiana.

Kwa kiasi fulani, mwanadada huyo mrembo wa nguvu, alikuwa amemwingia akilini John Bosho, kiasi cha kumfanya atamani kummiliki na awe wake. Hivyo akawa anageuza shingo yake mara kwa mara kumwangalia, na halikadhalika kimwana huyo alikuwa akimwangalia yeye, bila shaka akishangaa kwa kukutana kwao. Yeye John Bosho aliendelea kumkazia macho huku  akijaribu kumuundia tabasamu la nguvu, ambalo hata yeye aliliona na kulipokea kwa hisia kali.

Hata hivyo, mara baada ya kulipokea tabasamu hilo, kimwana huyo aliendelea kula chakula hicho, alichokuwa anakula kama vile hataki. Hakika Mwenyezi Mungu alikuwa amemjaalia kimwana huyo sura nzuri ya mviringo, iliyobandikwa macho mazuri, makubwa kiasi, malegevu, ambayo kama ukiyaangalia tu, hujikuta mtu akitoa salamu kwake, hususan mwanaume.

Kifua cha kimwana huyo mantashau, kilikuwa chembamba kilichobeba matiti madogo yaliyosimama wima, miguu yake ilikuwa minene kiasi iliyojaa nyama, na yenye matege ya kupendeza. Na miguu hiyo ikabeba makalio yaliyotuna kwa nyuma na kutikisika kila alipokuwa anatembea bila yeye mwenyewe kujua. Ni mtikisiko uliowaacha wanaume wengi wakiwa hoi kwa kudondosha udenda kwa kumtamani kimapenzi!

Akiwa ni kijana mtanashati, mwenye nguvu za kiuchumi, John Bosho aliamua jambo moja tu. Ni kwenda kumwingia kimwana huyo, ili aweze kumwaga sera zake. Yeye akiwa ni mwanaume wa shoka, asiyeogopa watoto wa kike wa aina ile, akaamua kunyanyuka kutoka katika meza yake. Baada ya kunyanyuka, akaelekea katika meza ile aliyokaa mwanadada huyo, kama vile walikuwa wanafahamiana kwa muda mrefu.

“Hali yako dada…” John Bosho alimsalimia huku akivuta kiti kimoja kilichokuwa upande wa mbele na kukaa huku wakitazamana.

“Nzuri tu,” kimwana huyo alisema huku akimwangalia John Bosho alivyokuwa amekaa kwenye kile kiti kilichokuwa kinatazamana na yeye.

“Samahani dada’ngu, nakaa kidogo bila idhini…” John Bosho akaendelea kumwambia huku akimtolea tabasamu jepesi.

“Kuwa huru, wala usijali…” kimwana huyo akamwambia kwa sauti nyororo ya kumtoa nyoka pangoni!

John Bosho akakaa na kubaki akimwangalia!

“Mimi nimekuja hapa kwa lengo moja tu,” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Ni kufahamiana na wewe. Tukiwa sote kama  Watanzania tunaoishi katika nchi ya amani, ni muhimu kufahamiana…”

“Unasema kufahamiana?” Kimwana huyo akamuuliza huku akiendelea kumwangalia kwa mshangao!

“Ndiyo. Ni kufahamiana tu, na si vinginevyo…” John Bosho akajibu kwa sauti ya upole huku akiirekebisha tai yake.

“Kwa hivyo umeona ufahamiane na mimi tu? Mbona humu hotelini wanaingia watu wengi tu?” Kimwana huyo akaendelea kumuuliza.

“Nina maana yangu…” John akamwambia.

“Maana ipi?”                           

“Ni historia ndefu…”

“Historia ndefu kivipi?”

“Unajua ni mara nyingi huwa naingia humu hotelini kula chakula mida kama hii,” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Lakini kila ninapoingia ni lazima nikuone na wewe unaingia. Nafikiri hata wewe umetambua hilo.”

“Eeh,” kimwana huyo akacheka kidogo na kusema. “Kwa hivyo ni hilo tu?”

“Ndiyo hilo tu. Naona kama nyota zetu zimelingana.”

“Sijui kama zimelingana. Lakini poa, kufahamiana siyo vibaya…” kimwana huyo akasema huku akiendelea kukata nyama ya kuku kwa kisu, kwa mtindo ule wa kujifanya kama alikuwa ameshiba. Na hiyo ilikuwa ni kwa akina dada wengi wanaojiona wazuri!

“Kwa jina naitwa John Bosho. Mimi ni Mtanzania, pia ni mfanyabiashara maarufu hapa Jijini Dar es Salaam, ninayeishi eneo la Ukonga. Bado sijaoa, niko ‘singo.’ Kadi yangu ya kibiashara hii hapa…” John Bosho akamwambia huku akifungua pochi yake iliyokuwa imetuna. Akatoa kadi moja ya kibiashara na kumpa. Ni kadi iliyokuwa na jina la kampuni, anuani, na namba za simu.

“Ahsante sana,” kimwana huyo akasema. Halafu akaipokea ile kadi ya kibiashara na kuitia ndani ya pochi yake iliyokuwa pale juu ya meza upande wa kushoto. Kisha akamwangalia John Bosho kwa nukta kadhaa katika kumsoma. Ni kweli alikuwa ni kijana mtanashati!

        ********

JOHN Bosho alikuwa ni kijana mwenye umri wa miaka ipatayo thelathini na sita mpaka arobaini hivi, akiwa ni kijana mwenye elimu ya kidato cha sita, aliyoipata katika Shule ya Sekondari ya Mirambo, Mkoani Tabora. Hata hivyo baada ya kuhitimu na kufaulu vizuri, alitakiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuendelea na masomo zaidi.

Lakini kwa sababu alizozijua mwenyewe, John Bosho hakuendelea na masomo, kwa kile alichokiona kama alikuwa anapoteza muda wa kuanza kuchakarika na maisha. Baadaye alijiunga na vijana wenzake na kujiingiza katika biashara za madini ya aina mbalimbali, dawa za kulevya, na nyinginezo haramu, zisizokubalika na jamii.

Akiwa ni mtu aliyejipanga kisawasawa katika kufanya shughuli zake za haramu bila kujulikana, aliamua kushirikiana na vijana wake maalum anaofanya nao kazi, ambao pia walikuwa wakifuata amri yake bila kupinga.

Vijana hao machachari na wasiokuwa na woga wa aina yoyote,  John Bosho aliwapata katika kona mbalimbali za jiji la Dar es Salaam baada ya kuhangaika sana, kwani kupata watu wa kukubaliana na amri utakayowapa  ni kazi sana. Na katika kujiimarisha katika shughuli zake za haramu, John Bosho aliamua kuwapa mafunzo maalum vijana wake, na kuweza kutumia silaha za moto, kama bunduki na bastola.

Baada ya kuhitimu vizuri katika matumizi ya silaha,  John Bosho aliamua kuwatuma sehemu mbalimbali nchini na kufanya vitendo vya uhalifu, ikiwa ni uporaji kwa wafanyabiashara wakubwa wenye fedha, hasa wanaojihusisha na biashara za madini, huko Mererani, mkaon Manyara, utekeji nyara na nyingine. Baada ya kufanikiwa katika ukamilishaji wa kazi hiyo haramu, vijana hao humkabidhi mali yote yeye, anayepanga utaratibu wa mgawo.

Kazi hiyo John Bosho alifanikiwa kuifanya kwa muda mrefu bila kushtukiwa, akionekana kama mfanyabiashara anayejihusisha na biashara maduka ya vifaa vya ujenzi. Alifanikiwa kufungua duka kubwa la vifaa vya ujenzi, katika mtaa wa Swahili, eneo la Kariakoo.

Ni duka ambalo lilikuwa linauza vifaa vya ujenzi kwa ujumla likiwa limejaa bidhaa za aina mbalimbali zinzohusika na shughuli za ujenzi kwa ujumla, kama vile, saruji, mabati ya aina mbalimbali, nondo na vinginevyo. Yote ile ilikuwa ni kivuli tu, ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi. Duka hilo lilijulikana kwa jina la  J. B. Enteprises Ltd.

Mbali na duka kumiliki duka lile, pia, John Bosho alikuwa anamiliki bohari kubwa la kuhifadhia bidhaa zake, lililoko eneo la Ubungo Machimbo ya Mawe. Ni bohari ambalo alikuwa amelikodi kutoka kwenye kampuni moja ya ujenzi, kwa ajili ya kuhifadhi mizigo yake anayoiagiza kutoka nchi za nje. Ndani ya bohari hilo, palikuwa na ofisi ya kuratibu mipango yake haramu, anapokutana na vijana wake.

Hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuwashtukia, John Bosho na wenzake, kwani walifahamika kama wafanyakazi wake waliokuwa katika mishughuliko ya kikazi. Alijitahidi sana kuratibu mipango yake bila kufahamika na kwa kiasi fulani alifanikiwa sana na kuendelea kujilimbikizia fedha na kufanya anachotaka, hata kujipatia wasichana warembo anaowataka!

      ********

JEURI yake ya fedha na kupenda wanawake, John Bosho alifanikiwa kumnasa mwanadada mmoja mrembo, aliyejulikana kwa jina la Helen Fataki, siku za nyuma. Huyo alikuwa ni mwanamke wa shoka na mfanyabisahara maarufu aliyekuwa katika umri  wa ujana, miaka ishirini na minane hivi.

Baada ya kumnasa na kuendelea naye kimapenzi kwa muda, walikuja kushindana baada ya Helen kugundua kuwa yeye alikuwa ni mtu anayejihusisha na kazi za uhalifu. Hivyo basi, John Bosho akaamua kujiweka kando na kuendelea na shughuli zake za kibiashara ndani ya jiji la Dar es Salaam na hata nje ya nchi.

Ingawa walikuwa wametengana, John na Helen walikuwa wanaishi kama ‘Paka’ na ‘Panya’, kwa kila mmoja akimwogopa mwenzake. John alimwogopa Helen asije akamchoma na kutoa siri zake kwa Jeshi la Polisi, juu ya kazi yake ya uhalifu aliyokuwa anaifanya, Helen Fataki naye alimwogopa John Bosho asije akamlipua na kumwondoa uhai ili asiweze kutoa siri zake nje, ambazo akiwa kama mpenzi wake, alikuwa anazifahamu!

Ni mara nyingi John Bosho alikuwa akimtishia maisha kwa kumwonya kutoitoa siri ile kamwe! Hivyo Helen Fataki akawa ameshikwa pabaya, akautia mdomo wake kufuli kwa kutoitoa siri ile kwa mtu yeyote. Basi ukawa mchezo wa kuwindana, hadi John Bosho alipokutana na mwanadada yule, Anita, ndani ya Hoteli ya The Kibo II Anex muda na wakawa wanafahamiana kwa undani zaidi!

Baada ya John Bosho kumkabidhi kadi yake ya kibiashara, mwanadada huyo akatabasamu kidogo, halafu akasema:

“Nashukuru sana kwa kunipatia kadi yako ya kibiashara….”

“Na mimi nashukuru pia, kwa kuipokea…” John Bosho akamwambia huku akiunda tabasamu pana.

“Kwa jina naitwa Anita Anthony. Ninafanya kazi katika shirika moja lisilo la kiserikali. Bado sijaolewa…”  akajitambulisha mwanadada huyo, aliyejulikana kwa jina la Anita.

Pia yeye akampatia kadi yake ya kibiashara kutoka katika pochi yake ndogo, aliyoitoa ndani ya mkoba wake uliokuwa pale juu ya meza.

“Nashukuru sana kwa kunipatia kadi yako. Utanisamehe sana, lakini huu ndiyo mwanzo wa kufahamiana…” John Bosho akamwambia Anita.

“Na mimi nashukuru pia…” Anita naye akamwambia huku akimwangalia kwa chati. Halafu akaendelea kumalizia chakula chake taratibu.

Mwadada huyo mrembo, Anita Anthony, alikuwa amezaliwa na kukulia kwenye familia iliyojimudu kimaisha. Alikuwa ni mtoto wa pekee wa kike kwa wazazi wake, jambo ambalo lilimfanya alelewe kwa kudekezwa kidogo. Alizaliwa na kukulia eneo la Kiwalani, Jijini Dar es Salaam, akiwa na wazazi wake, Mzee Anthony Mkonyi na mama yake mzazi, Bi. Matilda Msechu, wakiwa na asili ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Pia, Anita alikuwa na kaka zake wawili waliomtangulia, waliojulikana kwa majina ya Peter na Joseph. Alipata Elimu yake ya Msingi, katika  Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, jijini Dar, ambapo baada ya kumaliza, alifaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tambaza. Alisoma pale hadi alipohitimu kidato cha sita, ndoto ambayo alikuwa nayo muda mrefu hasa ukizingatia aliithamini elimu.

Baadaye alijiunga na Chuo cha Uhasibu Chang’ombe na kufanikiwa kupata Shahada yake ya Uhasibu. Hakika Anita alifurahi sana na hatimaye akaajiriwa na Shirika moja lisilo la Kiserikali, akiwa katika kitengo cha fedha, kama  mtunza fedha. Ofisi ya shirika hilo, iko ndani ya Jengo la Shirikisho la Vyama vya Ushirika, lililoko mtaa wa Lumumba, eneo la Mnazi Mmoja.

Anita aliipenda kazi hiyo na kuifanya kwa moyo mkunjufu, akiwa bado msichana mwenye umri wa miaka 26 hivi, mbichi kabisa. Tuseme alikuwa ni mtu mwenye kiu ya maendeleo, aliyependa kujiondoa katika tatizo la kuwa tegemezi. Hivyo basi, baada ya kukutana na John Bosho siku hiyo, naye alijikuta akimpenda kijana huyo mtanashati, ukizingatia naye alikuwa akimwona kila mara na kuridhishwa na ule utanashati wake.

Baada ya John Bosho na Anita kufahamiana, walikaa pale hotelini kwa muda huku wakishushia chakula kwa vinywaji baridi, wakiongea hili na lile kama vile watu waliokuwa wamefahamiana muda mrefu. Walipomaliza wakaagana na kuahidiana kukutana siku nyingine, na hata kuwasiliana kwa mawasiliano ya simu zao za kiganjani.

Anita alipotoka pale hotelini, alielekea ofisini, anakofanyia kazi, ndani ya Jengo la Shirikisho la Vyama vya Ushirika. Kwa vile hapakuwa mbali, alitembea kwa miguu tu huku wakiongozana na John Bosho. Walipofika nje, John Bosho akaliendea gari lake lililokuwa eneo la maegesho, akapanda na kuondoka kuelekea katika mishughuliko yake mingine ya siku ile.

 Anita alipoingia ofisini kwake, alikaa kitini na kufungua pochi yake aliyoitoa ndani ya mkoba. Akaitoa ile kadi ya kibiashara aliyopewa muda ule walipokutana na John Bosho, halafu akaiangalia kwa makini, na aliporidhika, akairudisha ndani ya pochi na kuendelea na kazi zilizokuwa zinamkabili.

Ukweli ni kwamba, ingawa Anita alikuwa ameshampenda John Bosho Lakini hakuwa akimjua undani wake sana, kwa vile ilikuwa ndiyo mara ya kwanza wamekutana.

*******      

WIKI moja ilipita tokea John Bosho walipokutana na mwanadada, Anita Anthony, katika Hoteli ya The Kibo II Anex, walipokwenda kula chakula cha mchana. Tuseme walikuwa hawajaonana tena baada ya John kupata safari ya kikazi, katika kuratibu mipango yake, ukizingatia alikuwa ni mtu wa kusafiri sana.

Lakini pamoja na kutoonana kwa muda wa wiki ile, kila mmoja alikuwa akimuwazia mwenzake. Ina maana John Bosho na Anita walikuwa wameshajenga kitu fulani ndani ya mioyo yao, yaani upendo wa dhati!

Hivyo basi, siku ya Ijumaa majira ya saa sita na nusu za mchana,  Anita Anthony alikuwa ndani ya ofisi yake, akijiandaa kutoka, kwenda kupata chakula cha mchana. Mara simu yake ya mkononi aliyokuwa ameiweka juu ya meza iliita, na alipoiangalia namba za mpigaji, akaona ni John Bosho!

Moyo ukamlipuka!

“Haloo…Anita naongea…” Anita Anthony akasema kwa sauti ndogo lakini. Yenye kusikika kwa mtu wa upande wa pili.

“Haloo…John Bosho hapa. Natumaini hujambo…” upande wa pili wa simu, John Bosho akasema.

“Mimi sijambo…”

“Nimeona nikupigie simu. Sijui leo una ratiba ya kwenda kula chakula cha mchana wapi?”

“Nitakula palepale The Kibo II Anex Hotel…”

“Leo usiende pale…”  John akamwambia.

“Kwa nini nisiende pale?”

 “Mimi nitakupitia hapo ofisini saa saba mchana. Tutakwenda kula sehemu nyingine.”

“Sawa, nitakusubiri.”

“Ok, niko njiani…”

Anita alisubiri akiwa palepale ofisini. Baada ya dakika kumi hivi, John Bosho akampigia simu na kumwambia kuwa alikuwa anamsubiri kwenye gari lililokuwa kule nje, kando ya Barabara ya Lumumba. Anita Anthony akauchukua mkoba wake na kushuka chini kwa kutumia lifti. Alipofika chini  akamkuta amelipaki gari kwenye maegesho akimsubiri, naye akaufungua mlango wa kushoto na kuingia ndani.

Ile kuingia ndani ya gari tu, harufu ya mafuta ya uzuri  ikaenea ndani ya gari na kuishia  katika pua ya John, kiasi cha kumpa burudani ya pekee na pia hisia za mapenzi zikimwingia!

“Habari za siku John…” Anita akamwambia punde tu baada ya kukaa.

“Nzuri tu. Nimerudi katika safari yangu…”

“Pole na safari…”

“Nimepoa,” John Bosho akasema na kuendelea. “Nimeona nikupitie tukale ‘lunch.’ Sijui unapendelea hoteli gani yenye hadhi?”

“Hoteli yoyote unayopenda wewe…” Anita akamwambia.

“Ok, twende New Africa Hotel…au unasemaje?”

“Hakuna shaka…tunaweza kwenda, ni katika kubadili uelekea…”

John Bosho akaliondoa gari na kuelekea katikati ya jiji la Dar es Salaam. Ingawa foleni ya magari iliwasumbua, lakini walifika katika Hoteli ya New Africa, iliyoko katika makutano ya mitaa ya Azikiwe na Sokoine Driver. Ni sehemu iliyokuwa na msongamano mkubwa wa watu, wengi wao wakiwa katika mihangaiko yao ya kutafuta riziki.

Baada ya kufika, John akalipaki gari katika sehemu ya maegesho iliyoko upande wa pili wa hoteli hiyo, halafu wakashuka na kuingia ndani.  Walifikia katika ukumbi wa chakula, uliokuwa katika hali ya utulivu kwa muda huo, ambapo walikaa na kuagiza  chakula walichopendea. Baada ya kuhudumiwa chakula, wakaendelea kula huku kila mmoja akiwa na mawazo yake kichwani.

“Anita,” John Bosho akamwita kwa sauti ndogo.

“Bee…” Anita Anthony akaitikia kwa sauti ndogo.

“Nimekuomba tuje kula hapa tuje kula chakula cha mchana, na pia ili tuweze kuongea mawili matatu. Nafikiri unajua tokea tufahamiane hatujaongea mambo mengi…” John Bosho akamwambia.

“Hiyo ni kweli kabisa, hatujaongea zaidi ya kusalimiana tu…”

“Vizuri sana,” John Bosho akasema na kuendelea. “Hivi mwenzangu, hapa Dar es Salaam, unaishi sehemu gani?”

“Mimi ninaishi eneo la Kiwalani…” Anita akasema.

“Umepanga au umejenga nyumba?”

“Hapana, bado sijafanikiwa kujenga,” Anita akasema huku akitabasamu. Kisha akaendelea. “Mimi naishi kwa wazazi wangu. Hivyo bado sijaanza maisha ya kupanga.”

“Aisee, unaishi kwa wazazi?”

“Ndiyo, kwani vipi?”

“Hupaswi kukaa na wazazi wako,” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Wewe ni mtu mzima unayepaswa kujitegemea na kujipangia mambo yako!”

“Hilo naelewa sana…” Anita akamjibu huku akitoa tabasamu dogo.

 “Ndiyo hivyo, utakosa vingi!” John Bosho akaendelea kumwambia Anita, huku akionyesha ujivumi wa fedha!

“Ni kweli unalosema. Lakini inabidi iwe hivyo, kwani niko peke yangu na sijaolewa, sasa haraka ya nini?” Anita akamwambia.

“Lakini ukiolewa utahama hapo nyumbani kwa wazazi wako?”

“Ndiyo, nitahama kumfuata mume.”

“Je, ukichumbiwa na kupangiwa chumba, utakubali?”

“Inategemea…” Anita akasema na kuongeza. “Mchumba akiwa mwaminifu nitakubali, maana siku hizi wanaume wengi siyo waaminifu kabisa…”

“Una maana gani kusema hivyo?”

“Nina maana kuwa, ninaweza kuchumbiwa na mchumba ambaye tutakuwa tumekubaliana. Halafu ananipangia chumba, kumbe mchumba mwenyewe anaweza kuja kuwa mwongo tu wa kunipotezea muda wangu, na baadaye kunitelekeza baada ya kunitumia vya kutosha!”Anita akamwambia John.

“Unalosema ni kweli,” John Bosho akasema na kuongeza. “Lakini siyo wanaume wote wanaofanya hivyo.”

“Na mimi sikusema wote, John…” Anita akamwambia baada ya kujua John alikuwa ana maana gani!

Alikuwa anajipigia debe yeye mwenyewe!

“Ok, tuyaache hayo. Je, unaweza kuwa na nafasi siku gani, ili tuweze kuongea mambo mengi na kufahamiana zaidi?” John Bosho akamuuliza Anita.

“Siku ambayo nina nafasi, ni Jumapili…” Anita akamwambia.

“Basi, nakuomba sana tukutane Jumapili inayokuja…”

“Tukutane wapi?”

“Naomba tukutane Zungwa Beach Hotel, Oysterbay. Hii ni sehemu iliyotulia sana, hakuna vurugu kama hoteli nyingine za uswahilini.”

“Sawa, kama umechagua twende huko, mimi sina kipingamizi.”

“Na kuhusu usafiri, nitakupitia sehemu, mbali kidogo na nyumbani kwenu, halafu tuongozane wote.”

“Hakuna shaka, na mengine tutawasiliana kwa simu…”

John Bosho na Anita walikaa hapo New Africa Hotel, huku wakiendelea kula na kunywa vinywaji baridi. Hapo waliongea mengi, hadi walipomaliza kula, ndipo walipotoka tayari kurudi katika sehemu zao za kazi, hivyo wakatoka nje tayari kwa kuondoka.

Hakika John Bosho alikuwa ameridhika sana baada ya kukutana na kimwana yule aliyekuwa amemwingia rohoni mwake. Na zaidi ni ile kumkubalia kukutana naye siku ya Jumapili kule Zungwa Beach Hotel, ili aweze kumjulisha azma yake. Baada ya kupanda gari, wakaondoka kumrudisha Anita kazini kwake, na yeye akaendelea na shughuli zake. Alishaamua kufanya urafiki na Anita, na hata ikiwezekana awe mke wake hapo baadaye.

        *******

SIKU ya Jumapili ilifika, na kama walivyokuwa wameahidiana, John Bosho na Anita walikwenda Zungwa Beach Hotel, iliyoko ufukweni mwa Bahari ya Hindi, kutembea na kupumzika katika kuifurahia mwisho wa wiki. Kama kawaida, John Bosho alimpitia nyumbani kwao, Kiwalani na kumchukua kwa gari lake.

Siku hiyo Anita alikuwa ameupara vizuri na kuonekana ule uzuri wake waziwazi kitu ambacho kilimvutia sana John.Baada ya kufika kwenye hoteli hiyo ya kifahari, iliyoko ufukweni mwa Bahari ya Hindi, siyo mbali sana na ufukwe wa Coco, John alilipaki gari katika sehemu ya maegesho ambapo palikuwa na magari mengine.

Baada ya kulipaki, wote wakashuka na kuelekea sehemu ya nyuma ya hoteli kwa mwendo wa taratibu kama vile wapenzi wawili wanaopendana, ambapo palikuwa na sehemu nzuri ya kupumzikia, iliyokuwa na mandhari nzuri hasa ukizingatia ilikuwa karibu kabisa na bahari.

Sehemu hiyo waliyokuwa wamekaa John Bosho na Anita, palikuwa na viti vilivyokuwa ndani ya kibanda cha makuti, waliagiza chakula na vinywaji, ambapo waliendelea kula na kunywa taratibu. Hapo ndipo John Bosho alipoanza kumwaga sera zake kwa Anita, katika kumwingiza katika mstari ulionyooka.

Vilevile walikuwa wakiongea mambo mengi na kujikuta wakiingia katika dimbwi la mapenzi, kwani kutokana na jinsi John Bosho alivyokuwa akipangilia maneno yake, na Anita alijikuta akikubali kila alichoambiwa. Walipomaliza kula na kunywa, walipanga chumba cha muda ndani ya hoteli hiyo ya kifahari, ambapo walipumzika humo na kujiliwaza kimapenzi kwa zaidi ya saa mbili.

Walipomaliza starehe yao ya kiutu uzima, walioga na kuvalia tena nguo zao, halafu wakaondoka kurudi katikati ya jiji. Walisumbuliwa sana na foleni ya magari barabarani, lakini John alimrudisha Anita nyumbani kwao, Kiwalani, akiwa salama. Hakika, kwa upande wa John, alikuwa amefurahi sana baada ya kumnasa mwanadada huyo mrembo, ambaye alifanana na mazingira yake anayoishi, akiwa ni mtu mwenye fedha za kutakata.

Kuanzaia hapo, John Bosho aliapa kuwa hatokubali ampoteze Anita, na atammiliki awe wake daima, na hakuna mwanaume mwingine atakayemwingilia katika penzi lake change!

        ********

BAADA ya miezi mitatu hivi, John Bosho na Anita walishakuwa marafiki na kushirikiana katika mapenzi. Wakajikuta kila mmoja akimhitaji mwenzake, kwa kila anapopata nafasi.

Hata hivyo ile kero ya kukutana katika mahoteli makubwa au katika n yumba za kupanga, kama vile Lojingi, hazikuwafurahisha wote wawili, hivyo John akaamua kumpangia Anita nyumba ya maana itakayomfaa, ambapo hakutaka apate shida.

Anita alifanikiwa kupata nyumba ya kupanga eneo la Tabata Mawenzi, ambapo akiwa mpenzi wake, John Bosho, akiwa ni mtu anayefahamika sana, alitumia madalali maarufu, ambao walimtafutia nyumba hiyo iliyokuwa katika kiwango alichokipenda.

Ni nyumba ndogo iliyojengwa kifamilia, ikiwa na vyumba viwili, sebule na stoo. Pia, huduma za choo zilikuwa mlemle ndani. Akalipa kodi ya mwaka mzima, na Anita akahamia mara moja, kutoka Kiwalani, nyumbani kwa wazazi wake alipokuwa anaishi kwa muda mrefu.

Mbali ya kumpangia nyumba hiyo, pia alimnunulia samani zote za ndani. Ni samani alizozinunua katika duka moja linalouza samani za gharama, lililopo  katika Barabara ya Nyerere. Baada ya kumfanyia yote yale, sasa John akapumua na kufurahia kummiliki mwanadada yule mrembo aliyekuwa anamezewa mate na wanaume wengi!

Kwa vile nyumba hiyo ilikuwa na usalama wa hali ya juu, John Bosho alikuwa anakwenda mara kwa mara na kupumzika, huku pia akijaribu kujikwepesha asijulikane na watu wengi sana ukiwa ndiyo utaratibu wake aliokuwa amejiwekea. Kufahamiana na watu ovyo, wataijua siri yake!

Ni mtu wa aina gani!

        ********

MARA baada ya John na Anita kuunganisha mahisiano na uchumba, Anita aliona ni vyema akutane na mama yake mzazi ili amfahamishe kuhusu jambo hilo ambalo kwa upande wake aliona kuwa ni la kheri kwani ni wanaume wachache sana siku hizi wanaopenda kuoa, na pia ni wanawake wengi ambao hawaolewi, hivyo ni bahati yake ya pekee ambayo kamwe hakupenda kuikosa.

Hivyo basi, Anita alimwomba mama yake wakutane faragha ili aweze kumdodosea. Siku hiyo ya Jumapili walikutana ndani ya sebule nadhifu, nyumbani kwao Kiwalani, ambapo Anita alimtembelea mama yake huyo, Bi. Matilda, ukiwa ni utaratibu wake wa kawaida aliokuwa amejiwekea.

Baada ya kufika pale nyumbani, aliwakuta wazazi wake, baba na mama yake ambao aliwasalimia, wakaongea mengi tu. Anita alihudumiwa kinywaji baridi huku akiendelea kunywa taratibu, na ndipo alipoanza kumweleza mama yake juu ya azma yake ile.

“Mama, nimekuomba kukutana na wewe, kwani nina maongezi muhimu sana,” Anita alimwambia mama yake ambaye walikuwa wamekaa naye kwenye sofa kubwa hapo sebuleni.

“Maongezi gani mwanangu,” mama yake, Bi. Matilda akamuuliza.

“Napenda kukujulisha kuwa nimepata mchumba,” Anita akamwambia huku akiunda tabasamu pana.

“Oh, umepata mchumba mwanagu?” Bi. Matilda, mama yake akamuuliza huku naye akiunda tabasamu pana.

“Ndiyo, mama, si unajua umri unazidi kwenda?”

“Ni kweli mwanangu, umri unazidi kwenda. Ni vizuri sana kama utaolewa mapema na kupata watoto mapema, kwani ukichelewa zaidi ya miaka mitatu kutokea sasa, basi ujue umezeeka! Itabidi uolewe na mtu wa makamo ambaye siyo kijana tena!”

“Na ndiyo hilo sitaki mama…”

“Basi, hilo ni jambo la heri,” mama yake akasema na kuongeza. “Lakini cha muhimu ni vyema kama unamuamini huyo mchumba, basi, afanye taratibu zote za kuja kujitambulisha kwetu na mambo mengine yafuata.”

“Yeye pia ana hamu kubwa sana ua kuja kujitambulisha,” Anita akasema na kuongeza. “Ukweli ni kwamba ni mtu ninayemuamini, na siamini kama atakuwa ni mwanaume mwongo.”

“Vizuri, nashukuru kwa kunieleza hayo. Mimi nitakaa na baba yako, halafu nimweleze jambo hili,” mama yake akamwambia kwa kumpa matumaini.

“Sawa, mama, nitashukuru sana.” Anita akasema.

Baada ya kumaliza mazungumzo yao ambayo hayakuichukua muda mrefu, Anita alibaki akimalizia kinywaji chake na pengine kuongelea mambo mengine yanayohusu maisha kwa ujumla.

********

WALIONEKANA ni wapenzi wawili waliopendana sana. Kila sehemu, John na Anita walikuwa wakifuatana wote, iwe kwenye starehe au hata kufanya manunuzi katika maduka mbalimbali ya bidhaa za chakula na hata nguo na vipodozi, jijini Dar es Salaam.

Baada ya mapenzi yao kukolea haswa, ndipo John Bosho alipofanya utaratibu mzima wa kujitambulisha kwa wazazi wa Anita. Alitafuta wazee wanaofahamika, akajitambulisha, utambulisho ambao ulifuatiwa na sherehe ndogo iliyofanyika katika ukumbi mmoja maarufu ulioko eneo la Kiwalani.

Hivyo basi, kuanzia hapo John Bosho akawa anafahamika kama mchumba, na mume mtarajiwa wa Anita, mwanadada mrembo, aliyekuwa ana husudiwa na wanaume wengi, ambao nao walipenda wammiliki.  Na ili kuondoa udhia kabisa, akaamua kumvisha pete ya uchumba ya gharama kubwa, iliyotenezwa kwa dhahabu, ili ijulikane kuwa ni mchumba wake halali, asije akaporwa na wanaume wengine wenye uchu mkali.

Mbali ya wazazi wake kumfahamu John, pia ndugu na jamaa nao walimjua kuwa alikuwa katika mpango wa kuja kumuoa Anita. Ikawa ni faraja kubwa kwa Anita kupata mchumba, heshima ikawa kwake, kwani aliheshimiwa na watu wote, wanaume kwa wanawake, kwa kujua sasa alikuwa amekata shauri la kuolewa na kuondokana na maisha yap eke yake.

Hali ilendelea kuwa hivyo, na hata ofisini kwake alipokuwa anafanya kazi, wafanyakazi wenzake walikuwa wameshajua kuhusu mwenzao kupata mchumba, kiasi kwamba hata wale mabosi waliokuwa na kijicho pembe cha matamanio, waliacha kabisa tabia hiyo ya kumtaka kimapenzi!

Mapenzi ya John Bosho na Anita yalikolea kadri siku zilivyokuwa zinakwenda. Muda wote huo, Anita alikuwa anajua kuwa mchumba wake huyo alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa mwenye biashara nyingi, lakini upande wake wa pili hakuujua undani wake kwa vile alikuwa ni mtu anayefanya shughuli zake hizo kwa siri sana.

********      

SIKU za nyuma, Anita na mwanadada, Getruda walikuwa ni marafiki wakubwa, waliokuwa wamesoma wote katika Shule ya Sekondari ya Tambaza, jijini Dar es Salaam. Lakini baada ya kumaliza masomo yao ya sekondari, kila mmoja aliendelea na shughuli zake, ambapo Anita alijiunga na Chuo cha Uhasibu, Chang’ombe, na Getruda akajiunga na kampuni moja ya simu za mkononi, akiwa Afisa Masoko.

Hata hivyo urafiki wao ulikuwa haujafa, kwani walikuwa wakitembeleana mara kwa mara wanapopata nafasi. Walionekana kama vile walikuwa ni ndugu waliozaliwa tumbo moja, mambo yalikuwa hayohayo mpaka wakati mwingine walipojikuta wakiwa bize sana na shughuli zao, kiasi cha kutoweza tena kuonana mara kwa mara zaidi ya kuwasiliana kwa simu zao za mkononi.

Siku moja ya Jumamosi, John Bosho, Anita na Getruda, walijikuta wamekutana katika viwanja vya starehe, wakijirusha na pengine kusuuza makoo yao kwa vinywaji. Walikutana kwenye Ukumbi wa Amana Club, Ilala, ambapo John Bosho alikuwa amekwenda na Anita kwa ajili ya kuburudika na Muziki wa Dansi wa Msondo Ngoma, unaoporomoshwa na Bendi ya Muziki wa Dansi ya Msondo.

John Bosho alikuwa ni mpenzi wa ‘Msondo,’ ambapo hakupenda kukosa hata mara moja katika siku za mwisho wa wiki. Wakiwa wamekaa katika meza yao, Anita aliweza kumwona Getruda akicheza muziki akiwa peke yake. Akanyanyuka baada ya kumuaga John na kumwendea Getruda pale alipokuwa na kumshika begani.

“Getu…” Anita akamwita kwa sauti ndogo huku akimgusa.

“Oh, Anita…waooo!” Getruda akasema huku akinyanyuka na kumkumbatia Anita, na pia akishangaa kumuona katika eneo lile.

“Za siku?”

“Nzuri, sijui wewe?”

“Mimi safi…”

“Uko na nani?” Getruda akamuuliza Anita.

“Niko na mchumba wangu, twende ukamfahamu…” Anita akamwambia huku akitabasamu!

Wote wawili wakaongozana huku wameshikana mikono yao, hadi pale kwenye kiti alipokaa John Bosho. Wakasalimiana na kutambulishana.

“Getu, huyu ni mchumba wangu, anaitwa John…” Anita akamtambulisha kwa mchumba wake.

“Nashukuru sana kumfahamu…” Getruda akasema huku akimwangaliam John ambaye naye alikuwa anamwangalia kwa jicho la kisanii!

“John, huyu ni rafiki yangu, anaitwa Getruda, ambaye tumesoma naye shule ya Sekondari…” Anita akamwambia John, ambaye bado alikuwa akimwangalia Getruda!

“Nashukuru kumfahamu…” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Anaishi wapi hapa jijini Dar es Salaam?”

“Anaishi Ilala, mtaa wa Moshi…siyo mbali sana kutoka hapa Amana…” Anita akasema.

“Oh, nashukuru sana,” John akasema huku akimpa mkono Getruda. Halafu akaendelea kusema. “Mimi ndiye John Bosho, kama ulivyotambulishwam, ninaishi huko Ukonga, lakini mwenzangu anaishi Tabata Mawenzi.”

“Nashukuru kwa kufahamiana…” Getruda akasema huku bado akiwa ameunda tabasamu pana.

Getruda alikuwa ni mwanamke aliyeumbika. Ni mwanamke mwenye lile umbile tata linalowasumbua wanaume wengi sana, akiwa amejaza makalio yaliyofuatiwa na nyonga iliyotanuka na umbile la namba nane! Kila akitembea makalio yalikuwa yanatikisika pasipo mwenyewe kupenda!

Hakika umbile hilo la Getruda, lilimsumbua sana John Bosho. Basi, tokea muda huo, akili yake ilikuwa haifanyi kazi tena baada ya kumwona Getruda akiwa na  lile gauni laini na la kubana alilovaa, ambalo liliruhusu mzigo wote wa makalio umwagike nyuma!

Huo ulikuwa mtego!

Siyo kwamba Anita alikuwa mwanamke mbaya ksura, kimaumbile au hata tabia, hasha. Isipokuwa ile ilikuwa ni tamaa ya wanaume wengi wasiokuwa na ustahimilivu baada ya kuona vitu kama vile! Lakini ukweli unabaki kwamba Getruda kwa usiku ule alikuwa tishio, na alimtamanisha kila mwanamke yeyote rijali!

Usiku huo waliburudika kwa muda mrefu huku wakiongea hili na lile. Kwa wakati wote John Bosho alikuwa akicheza muziki na wanawake wote wawili, Anita na Getruda; wala Anita hakuwa na wivu wala kumtilia mashaka mchumba wake, kwamba anaweza kumtaka kimapenzi rafiki yake huyo, kumbe huku nyuma, John alikuwa ameshamhusudu Getruda, hivyo akaamua kuwa ni lazima ampate!

Kazi hiyo!

Ndipo John Bosho alipopata wasaa wa kumuulizia sehemu anayoishi, nyumba na mtaa. Bila kutambua nia yake, Getruda alimjulisha kuwa yeye anaishi mtaa wa Moshi, Ilala, nyumba namba 003. Mbali ya kumfahamisha sehemu hiyo anayoishi, pia walipeana namba za simu zao za mkononi, ambapo wangeweza kuwasiliana kwa kusalimiana na kutakiana heri kwa ujumla.

Ukweli ni kwamba, Getruda hakujua kwamba John Bosho alikuwa ana nia mbaya dhidi yake, kwani alikuwa amechukua namba zake za simu ya mkononi, akiwa na lengo lake. Hivyo baada ya burudani ya muziki wa danisi kumalizika, ndipo wote walipoondoka kwa gari lao, ambapo John alimpitisha Getruda nyumbani kwake, mtaa wa Moshi, na kumwacha.

Akiwa ni mwenyeji tosha ndani ya jiji la Dar es Salaam, John Bosho aliweza kuitambua ile nyumba aliyokuwa amepenga Getruda, akaitia alama kichwani mwake. Baada ya kumshusha Getruda, wenyewe wakarudi  Tabata Mawenzi, alikompangia nyumba Anita, tayari kwa kupumzika. Siku hiyo John Bosho alilala hukohuko nyumbani kwa Anita.

********      

AKILI ya John Bosho hakutulia. Ilikuwa bado imezama kimapenzi kwa kimwana Getruda, rafiki yake mkubwa Anita, mchumba wake. Tamaa na uchu ulikuwa umemtawala pasipo kuweka tahadhari yoyote, hasa akilifikiria lile umbile tata alilokuwa nalo Getruda, ambalo likuwa limefichwa ndani ya magauni makubwa kama dera au nguo za kubana, kwa vyovyote alidhamiria kulionja.

Akiwa ni mtu mwenye kujiamini, na mwenye fedha vilevile, John Bosho hakukaa kimya, kwani aliamua kumtafuta Getruda, rafiki yake Anita, ili amweleze azma yake ile ya kumtaka kimapenzi, hata kwa kutumia fedha. Wakati huo hakuona ubaya wowote kumtaka, kwani yeye aliamini kuwa ana haki ya kumtaka kila mwanake anapopenda! Hakuna kinachoshindikana mbele ya fedha!

Kwa vile John Bosho alikuwa na namba za simu ya mkononi ya Getruda, basi akampigia na kumwomba wakutane sehemu watakayopanga, kwani alikuwa na mazungumzo naye, akiwa kama shemeji yake. Kwa vile Getruda hakumtilia mashaka, basi walikubaliana kukutana pale Msewa Bar & Lodging, iliyoko Buguruni, kunako majira ya saa moja za jioni. Hata hivyo, Getruda alikuwa akijiuliza kuwa John Bosho alikuwa anamwitia nini mpaka wakutane katika sehemu hiyo? Lakini akavuta subira mpaka watakapokutana.

Getruda alipotoka kazini jioni, aliamua kupitia nyumbani kwake, mtaa wa Moshi, Ilala, kwanza, halafu akaoga na kuvalia nguo nyingine nadhifu ukizingatia sehemu yenyewe aliyokuwa anakwenda, ilikuwa na mkusanyiko wa watu wengi. Baada ya kumaliza kuvalia, Getruda akatoka na kutembea kwa miguu hadi alipofika katika barabara kuu ya Uhuru, inayotokea katikati ya jiji kuelekea maeneo ya Buguruni na kwingineko.

Sehemu hiyo kulikuwa na teksi kadhaa zilizokuwa zimepaki zikisubiri wateja, hivyo Getruda akakodi teksi moja wapo na kumwambia dereva ampeleke Buguruni. Dereva akaiondoa teksi na kuifuata barabara ile ya Uhuru hadi alipofika Buguruni, eneo la Sokoni, halafu akamshusha Getruda. Sehemu hiyo palipokuwa na pilikapilika za watu wengi, hivyo nusu iliyobaki ambayo si mbali sana na ilipo Msewa Bar & Lodiging, alitembea kwa miguu kwa mwendo wa taratibu hadi alipoingia ndani ya baa ile maarufu.

Alipoingia tu, akaangaza macho yake pande zote, lakini hakumwona John Bosho kama walivyoahidiana kukutana katika eneo lile la baa. Hata hivyo akachukua simu yake na kumpigia, ili kujua alipo kwa wakati ule, na John akamjulisha sehemu ile alipokuwa na kumwambia amfuate ndani ya chumba maalum kilichokuwa na huduma zote zinazohitajika.

 Ni chumba kilichokuwa upande wa nyuma ya baa ile, ambapo palikuwa na vyumba vingine kwa ajili ya starehe za muda mfupi au kulala mpaka asubuhi, hivyo Getruda akaelekezwa na wahudumu, na kupelekwa hadi kule nyuma ya baa, ambapo aliingia ndani ya chumba kile na kumkuta John Bosho amekaa kwenye sofa dogo, mbele yake kukiwa na meza ndogo iliyokuwa na vinywaji.

Kilikuwa ni chumba kikubwa, kilichokuwa na seti moja ya makochi, friji ndogo, runinga, choo na bafu vilikuwa mlemle. Pia, palikuwa na sebule iliyokatwa kwa pazia kubwa lililotenga chumba kile, ambapo ndani kulikuwa na kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita.

“Karibu Getruda,” John Bosho akamwambia huku akitabasamu.

“Ahsante…” Getruda akasema huku bado amesimama!

 Alikuwa akishangaa kumkuta shemeji yake huyo, John Bosho akiwa katika sehemu kama ile yap eke yake!

Chumbani!

“Mbona unasita?” John Bosho akamuuliza huku akinyanyuka kutoka pale kwenye sofa alipokaa.

“Lazima nishangae…” Getruda akamwambia.

“Unashangaa nini sasa?”                                            

“Mbona hapa ni chumbani?”

“Ndiyo, ni chumbani….” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Ndivyo nilivyoamua, si unajua kuwa hapa kuna utulivu, tofauti na kule kwenye baa?”

“Yaani umeniita kwa mazungumzo ya kuongelea chumbani?” Getruda akamuuliza.

“Wala usihofu shem…” John akamwambia huku akimkalisha Getruda kwenye sofa lililokuwa pembeni.

“Haya…nakaa..” Getruda akamwambia huku akikaa.

“Hayo si ndiyo maneno?” John Bosho akamwambia huku naye akikaa kando yake. Chumbani hapo palikuwa kimya, isipokuwa ni sauti ndogo ya runinga ndiyo ilikuwa inasikika.

Baada ya kukaa kwa muda, John Bosho aliagiza vinywaji na mapochopocho kwa mhudumu maalum aliyekuwa anamhudumia kila mara anapokuwa anafika hapo. Wakaendelea kula na kunywa na huku wakiongea mambo mengi tu, kitu ambacho kilimshangaza Getruda, kwani John hakumwambia alichokuwa anamwitia!

“Shemeji John…” Getruda akamwita John kwa sauti ndogo.

“Naam shem…” John Bosho akaitikia huku akimwangalia Getruda.

“Naona muda unazidi kwenda…”

“Ni kweli unakwenda…”

 “Basi, naomba unieleze ulichoniitia…”

“Hakuna taabu. Nitakueleza tu…” John  Bosho akamwambia huku akiwaza la kufanya.

Ni kweli kwamba John alikuwa amemwita pale kwa ajili ya mazungumzo maalum na yeye, lakini tokea amefika, ameshindwa kumwambia alichomwitia zaidi ya kuonyesha matamanio tu kuuangalia mwili wake! Kwa vile alikuwa amedhamiria kumpata kimapenzi, shemeji yake huyo, Getruda, aliamua kufanya kitu kimoja kibaya sana.

Alipanga kuwa kabla ya kumwelezea kile alichomwitia, ni lazima afanye jambo fulani, ambalo litamlainisha mwanamke huyo aliyempania kupita kiasi. Yeye alikuwa ameshajiandaa kwa chochote tokea alipofika katika eneo lile husika. Hivyo aliamua kumtilia Getruda dawa ya usingizi, kwenye kinywaji chake, ambayo ni dawa yenye uwezo wa kumlegeza mwili wake haraka.

“Hebu naomba unieleze shemeji, maana unaniweka roho juu kwa kusubiri…” Getruda akaendelea kumwambia John Bosho

“hakuna taabu, shem, nitakueleza, kwani si jambo bay asana, mpaka likuweke roho juu sana…” John Bosho akamwambia.

“Sawa, ngoja nikajisaidie, nikirudi basi unieleze ili roho yangu itulie…” Getruda akamwambia huku akinyanyuka kuelekea msalani.

“Na kweli, utasuuzika na roho yako…”

Hivyo basi, mara baada ya Getruda kwenda kujisaidia ndani ya choo kilichokuwa mlemle chumbani, John Bosho alibaki akishangilia sana, huku akirusha ngumi yake hewani, akijua kuwa sasa mpango wake utafanikiwa, ni lazima atafune kitu roho inapenda!

Hakupoteza muda, kwani John alichukua ile dawa ya usingizi, iliyokuwa katika asili ya unga mweupe hivi. Akaunyunyuzia ndani ya glasi iliyokuwa na kinywaji alichokuwa anakunywa Getruda, halafu akamsubiri mpaka atakaporudi kutoka msalani!

      ********

HAIKUCHUKUA muda mrefu, Getruda alirudi kutoka msalani. Akafikia tena kwenye sofa na kuiangalia glasi yake iliyokuwa na pombe nusu, lakini hakuinywa kwanza, bali alimwangalia John Bosho aliyekuwa anamwangalia kwa uchu mkubwa.

Hata hivyo Getruda hakuweza kugundua mpango ule aliokuwa ameupanga John Bosho. Hivyo akainyanyua ile glasi na kunywa kinywaji kile cha bia kilichokuwa na mchanganyiko wa dawa ya usingizi aliyokuwa amemwekea, na alipomaliza kunywa, akaitua glasi chini.

“Shemeji…” Getruda akamwita.

“Naam…” John akaitikia.

“Nafikiri mimi nikimaliza kinywaji hiki, naondoka…”

“Unaondoka kabla sijakueleza nilichokuitia?”

“Usiondoke,” John Bosho akamwambia na kuongeza. “Basi, nitakueleza, tega sikio!”

Hata hivyo, kabla John hajaanza kumwelezea alichomuitia pale, dawa ile ikaanza kumlegeza na kumfanya kama amelewa kiasi cha kushindwa kustahimili, naye  John alipoona Getruda amelegea, ndipo alipoanza kumweleza alichomuitia.

“Shemeji Getruda…” John akamwita.

“Eeee…shem…” Getruda akaitikia kwa sauti ya kilevi.

“Unajua nilichokuitia?”

“Hapana…sijui…”

“Nisikilize…”

“Nakusikiliza…oh!”

“Unajua nakupenda?”

“Oh….unanipenda?”

“Ndiyo. Nakupenda shem…”

“Unanipenda kivipi?”

“Nakuhitaji. Nataka uwe mpenzi wangu…”

“Shemeji…ah! Haiwezekani…na Anita je?”

“Mambo ya Anita achana naye kwa wakati huu!”

“Nisijali vipi wakati ni mchumba wako?” Getruda akasema na kuongeza. “Isitoshe ni rafiki yangu!”

“Nimeshakwambia hayo usijali…”

“Ah, shem unaniweka katika wakati mgumu…”

John Bosho akiwa na ulimi wa kushawishi, kubembeleza na pia ukichangia na ile dawa aliyomwekea Getruda ndani ya kinywaji chake, akaendelea kumbembeleza. Akahamia katika sofa alilokalia Getruda, akifanikiwa kumshawishi na kukubaliana kukutana kimapenzi! Dakika tano zilizofuata, wote walikuwa wameshasaula nguo zao na kubaki kama walivyozaliwa!

Wakajikuta pia wakigaragara katika kile kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita ikifuatiwa na miguno hafifu ya kimahaba mazito! Baada ya kumaliza ile mechi nzito, kila mmoja alijitupa kivyake na hatimaye Getruda kupitiwa na usingizi mzito kutokana na ile dawa aliyokuwa ametiliwa kwenye kinywaji.

John Bosho aliufurahia ule ushindi wa kumpata kiumbe yule husika aliyekuwa na matamanio naye kwa muda mrefu, akajipongeza kwa hilo huku akiendelea kumwangalia zaidi na zaidi pale juu ya kitanda alipokuwa amejilaza Getruda katika umbile lile la utupu alilokuwa nalo! Ni hatari sana!

Getruda alijikuta akilala ndani ya chumba kile alichopanga John Bosho. Ni mpaka ilipotimu saa nne za usiku ndipo aliposhtuka kutoka kwenye usingizi mzito na kujikuta amelala kwenye kitanda kimoja na John, shemeji yake! Ni usaliti wa hali ya juu!

“Oh! Shem John!” Getruda akaita huku akinyanyuka kutoka pale kitandani nusu akipepesuka!

“Naam,” John Bosho akaitikia huku akimwangalia kwa kijicho pembe!

“Aisee? Umefanya nini?” Getruda akamuuliza huku akijiangalia katika hali ile ya utupu aliyokuwa nayo!

“Kwani vipi?”

“Huoni kama tumemsaliti Anita?”

“Kumsaliti?”

“Ndiyo manaake!”

“Hayo usijali sana…” John Bosho akasema huku akitabasamu na kuonyesha ujivumi kwa kumpata na kujifurahisha kingono!

“Nimefanya kosa kubwa sana…haya… nirudishe nyumbani!” Getruda akasema huku amechukia!

“Nenda kaoge mpenzi…” John Bosho akamwambia.

“Mpenzi tena…ala!” Getruda akamwambia huku akijifunga taulo kubwa.

“Kwani kosa kukuita mpenzi?”

“Ah, tuyaache hayo!”

Getruda akaingia bafuni ambapo alioga haraka haraka na kutoka. Halafu John naye akaingia na kuoga, huku akimwacha Getruda akijiandaa kuvaa nguo zake. Baada ya kumaliza kuvalia, wakatoka hadi nje ambapo walipanda gari la John, tayari kwa kumrudisha Getruda nyumbani kwake, mtaa wa Moshi, Ilala.

Walipofika nyumbani kwa Getruda, ilikuwa imetimu saa saa tano za usiku, na pilikapilika za watu zilikuwa bado zinaendelea katika mitaa ile ya Ilala, na nyumba aliyokuwa anaishi Getruda, ilikuwa bado haijafungwa.

Kabla ya kushuka garini, John Bosho akamkabidhi Getruda kitita cha fedha,  shilingi laki tatu, ambazo zilitosha kumlegeza. Akasahau mambo yote yaliyotokea nyuma, na wala hakugundua kama John alikuwa amemtilia dawa ya kulevya katika kinywaji chake ili aweze kutimiza azma yake ya kufanya naye mapenzi!

Basi, tokea siku ile ndiyo ukawa mchezo wao, ambao uliwafanya wanogewe na kuwa wanakutana mara kwa mara kwenye nyumba mbalimbali za wageni na kuivunja amri ya sita. Hata hivyo iliwabidi wafanye mambo yao kwa siri sana, ili Anita asiweze kuwashtukia, wakijitahidi kusafiri sehemu za mbali na kukamilisha kiu yao.

Kutokana na ubize aliokuwa nao Anita, hakuweza kuwashtukia kabisa, kama rafiki yake mkubwa, Getruda, alikuwa amemchukulia mchumba wake, John Bosho. Kila mmoja aliendelea na shughuli zake na siku zikawa zinasonga mbele. Lakini hakuna marefu yasiyokuwa na mwisho!

        ********

JUMATATU moja ambayo ni mwanzo wa wiki, Anita alikuwa amekaa ndani ya ofisi yao, pamoja na mfanyakazi mwenzake, Magret. Alionekana ni mtu mwenye mawazo mengi sana tangia alipoingia kazini asubuhi, kiasi cha kushindwa hata kufanya kazi. Pia, alikuwa ni mtu wa kujifyonza mwenyewe, ikionyesha kuwa kuna kitu alikuwa anawaza!

Ndipo Magret alipoamua kumsogelea karibu ili amuulize kulikoni mpaka awe katika hali kama ile ambayo siyo kawaida yake. Anita siku zote alikuwa ni mtu mcheshi na mchangamfu kwa kipindi chote cha kazi, na kila mmoja alimzoea hivyo.

“Vipi Anita, unaumwa?” Mage alimuuliza.

“Hapana, mimi siumwi…” Anita alimwambia Magret huku akimwangalia kwa sura ya huzuni.

“Sasa mbona uko katika hali kama hii?” Magret akaendelea kumuuliza.

“Ah, wewe acha tu Mage…” Anita akasema kwa sauti ndogo ya huzuni.

“Niache nini wakati nakuona hauko sawa?”

“Ni kweli Mage…siko sawa…”

“Ni kitu gani kinakusumbua?”

“Kuna kitu kinanisumbua,” Anita akamwambia na kuongeza. “Lakini hakifai kuongelea hapa ofisini Magret.”

“Kwa hivyo tukaongelee wapi?”

“Naona twende hapo The Kibo II Hotel, ambayo ni sehemu nzuri…” Anita alimwambia huku akinyanyuka kutoka kwenye kiti.

“Haya, twende…” Magret akamwambia Anita.

Anita na Magret walitoka pale ofisini na kuelekea The Kibo II Anex Hotel, ambayo haikuwa mbali na pale. Baada ya kuingia ndani, wakaagiza vinywaji baridi na kuendelea kunywa taratibu.

“Ndiyo ndugu yangu, naona kuwa huu ni muda muafaka wa kunielezea kilichokusibu…” Magret akamwambia Anita.

“Ni sawa, inabidi nikuelezee kila kitu, kwa vile wewe ni mtu wangu wa karibu…” Anita akamwambia Mage huku uso wake ukionyesha bado kuwa na huzuni.

“Nieleze mwaya, huwenda nikapata wazo la kukusaidia…”

“Hivi si unajua kuwa nina mchumba?”

“Ndiyo, najua kuwa unaye mchumba.”

“Lakini tatizo ni kwamba mchumba wangu huyo ananipa taabu sana.”

“Shida gani tena?”

“Ananitesa sana, sijui kwa vile anajua kuwa ninampenda? Maana nasikia anajihusuisha kimapenzi na shoga yangu, Getruda…”

“Unasema kweli?”

“Ninasema kweli, kwa sababu siku hizi ninaona wana ukaribu mkubwa sana.”

“Hali hiyo imeanza lini?”

“Imeanza mara baada ya mimi kumtambulisha kwake.”

“Je, una uhakika wana mahusiano?”

“Dalili zinaonyesha na pia nimeshauona ujumbe wa simu kwenye simu ya John Bosho. Hata hivyo alijitahidi kuukwepesha.”

“Ulishawahi kumuulizia Getruda juu ya tuhuma hizo?”

“Hapana, sijamuuliza…”

“Vizuri sana. Usimuulize kwanza, jaribu kufanya upelelezi kwanza na utakapogundua, ndipo utakapomweka kitako na kumuuliza.”

“Sawa Mage, nitajitahidi kufanya upelelezi juu ya hayo. lakini roho inaniuma sana… si unajua kuchukuliwa mwanaume kunavyouma?”

“Ni kweli kunauma sana, lakini ushauri ndiyo huo, fanya upelelezi kwanza! Mambo mengine yatafuata.”

“Sawa, nitafanya hivyo.”

Baada ya kumaliza mazungumzo yao, Anita na Magret walitoka pale hotelini na kurudi ofisini kwao. Kwa kiasi fulani Anita alikuwa ameridhika na tabasamu pana lilionekana usoni mwake.

********

HAKUNA siri ya watu wawili duniani. Anita alikuja kuujua ule uhusiano wa kimapenzi baina ya Getruda na mchumba wake, John Bosho. Aligundua hilo baada ya kudokezewa na kijana mmoja, mwendesha bodaboda, aliyeujua uhusiano ule usiokuwa rasmi. Yeye alikuwa akimbeba mara kwa mara  Anita, kumpeleka katika sehemu mbalimbali ambazo alihitaji kufika haraka.

Basi, akiwa katika kazi zake za kubeba abiria, ndipo kijana huyo alipoweza kuuona ule uhusiano wa Getruda na John Bosho, walivyokuwa wakijirusha na kutanua. Roho ikamuuma sana  kwa vile alikuwa anamheshimu Anita kama dada yake wa kuzaliwa tumbo moja. Hakuvumilia, hivyo akaamua kummwagia siri ile!

Kijana huyo mwendesha bodaboda maarufu, alijulikana kwa jina moja tu, Don, ambalo ni jina alilokuwa amekatiwa na vijana wenzake wa mtaani, na wala jina la pili halikujulina. Yeye alikuwa akifanya kazi ile kati ya maeneo ya Buguruni Shell na maeneo ya Tabata, na mara nyingine sehemu mbalimbali za jiji, kama atakuwa amepata mteja wa kumpeleka huko. 

Baada ya Don kumfikishia ujumbe huo Anita, alimshukuru sana kwa kumtoa tongotongo machoni mwake, kwani alikuwa hajui kitu kama hicho. Hivyo akaamua kuufanyia kazi, na pia kupanga kumpa kazi nyingine ya kuendelea kumpeleleza John Bosho bila yeye kufahamu. Vilevile hakuacha kumjulisha rafiki yake, Magret juu ya kuinyaka siri hiyo, ambaye naye alimpatia ushauri wake, kuwa ni vyema angeanza kufanya upelelezi wake binafisi, na hata kumtumia Don.

Na kweli, Anita aliamua kuanza kufanya upelelezi huo mara moja, baada ya kupewa ushauri na huyo Mage, mfanyakazi mwenzake. Pia, kwa bahati nzuri  Don, naye alikuwa anaujua uhusiano wa Anita na John, kama ni mtu na mchumba wake na mara nyingine aliwaona wakiambatana wote katika kilele cha mapenzi yao.

Hivyo basi, siku moja Anita alimkalisha kitako Don na kuanza kuongea naye kumwelezea masahibu yaliyompata, ambapo alitaka msaada wake wa hali na mali katika kukamilisha upelelezi wake.

“Kaka yangu, Don…” Anita alianza kumwambia.

“Naam, dada yangu,” Don aliitikia huku akimwangalia kwa makini.

“Samahani sana, leo nina mazungumzo muhimu sana na wewe,” Anita akaendelea kumwambia Don.

“Mazungumzo gani dadangu?”

“Ni mazungumzo yanayonihusu mimi na mchumba wangu, John Bosho. Natumaini unatambua kuwa uhusiano wangu naye.”

“Ndiyo, uhusiano wako na John mimi naufahamu…”

“Hivyo basi, nakuomba nikushirikishe huenda ukanipa ushauri cha kufanya…”

“Unaweza kunieleza dada, kama kuna ushauri bila shaka nitakueleza cha kufanya.”

“Natumaini unamfahamu vizuri mchumba wangu, John Bosho…”

“Ndiyo, namfahamu. Si yule anayeendesha gari aina ya Toyota Harrier?”

“Ndiye huyo huyo!” Anita akamwambia na kuendelea. “Ni mchumba wangu, ambaye tumevishana pete za uchumba. Lakini mwenzangu kwa kiasi fulani amekuwa siyo mwaminifu, nasikia anatembea na rafiki yangu, Getruda, anayeishi kule, Ilala!”

“Unasema kweli dada?” Don akamuuliza huku ameachama mdomo!

“Ni kweli kabisa. Hivyo basi, nakuomba uwe unafuatilia nyendo zao kwa vile wewe ni dereva wa pikipiki, hawataweza kukushtukia kamwe. Na hiyo ni ili tujue kama kinachozungumzwa ni kweli wana mahusiano, najua kwa vile unayo hiyo pikipiki, kazi haitakuwa ngumu sana. Hilo ndiyo ombi langu, siyo kama ninakulazimisha,” Anita akamaliza kusema huku akimwangalia kwa uchungu mwingi Don.

“Nimekuelewa dada Anita, kwa hicho ulichonieleza. Kumbuka kuwa mimi ni mwanaume, na sipaswi kuwa mmbea, lakini kwa shida uliyoipata, sina budi kukusaidia…” Don alimwambia Anita.

“Nitashukuru sana,” Anita akasema huku akitabasamu tabasamu la uchungu.

“Tena,” Don akaendelea kusema. “Mimi nimeshawahi kuwaona wakiwa katika sehemu mbalimbali za stareha, lakini sikujua kama walikuwa na mahusiano ya kimapenzi kabisa. Lakini maadam aumeniambia hivyo, sina budi kukusaidia…” Don akaendelea kumwambia Anita.

“Nitashukuru sana kakangu. Fuatilia na kila utakachokiona, nifahamishe, nitakutoa kwa chochote…” Anita akamwambia Don.

“Ah, hayo usijali dada, wewe wangu,” Don akamwambia.

Baada ya maongezi yao, Anita na Don waliagana kila mmoja akaendelea na shughuli zake.

Siku hiyo ikapita!

Mara baada ya Anita kuzipata taarifa za mchumba wake, John Bosho, alichanganyikiwa sana. Ili kuuokoa ule uhusiano wao wa uchumba, alimkabili na kumuulizia kuhusu tetesi zile, lakini John aliruka na kusema kwamba yale yalikuwa ni maneno ya watu tu yasiyowatakia maendeleo yao. Kamwe John  hakukubali kabisa kujihusisha kimapenzi kwa rafiki yake, Getruda.

Anita alinyamaza kimya huku akiendelea kufanya uchunguzi wake. Daima alijua kuwa njia ya mwongo ni fupi, na iko siku lazima atakuja kuwafumania wakiwa wawili, ndiyo, ni lazima!

Aliapa!

********

MIEZI mitatu ilipita tokea John Bosho na Anita walipoanza kuulizana juu ya ule usaliti wa mapenzi uliokuwa ukifanyika. Hata hivyo kila mmoja aliendelea na kazi, ambapo Anita alikuwa alijaribu kwa hali na mali kuyasahau yale yaliyopita nyuma, hasa ukizingatia kazi aliyokuwa anafanya, ilikuwa ikimweka bize sana.

Kila alipokuwa anatoka kazini huwa anachoka sana kiasi kwamba akifika nyumbani ni kupika, kuoga na kulala, basi. Lakini siku moja akiwa kazini, Anita aliupata ujumbe wa maandishi kwenye simu yake ya mkononi, kutoka kwa mwendesha bodaboda, Don, aliyekuwa anampa habari za mwenendo wa John Bosho na Getruda.

Ni ujumbe ambao uliozidi kumtia jereha moyoni mwake, hasa ukizingatia alikuwa ameshaanza kusahau! Ujumbe ule ulisomeka kwenye kioo cha simu, “Tafadhali dadangu, Anita…nenda Max Bar, Ilala, utawakuta John na Getruda, usifanye fujo. Ninachotaka ni uhakikishe kuwa mchumbako anakusaliti…”

Baada ya kuusoma ujumbe ule, Anita alichanganyikiwa sana, na hamu ya kufanya kazi ikamwisha. Akaamua kuaga kazini, akidai alikuwa amepigiwa simu ya dharura kutoka nyumbani. Akauchukua mkoba wake na kuupachika kwapani na kushuka kwa lifti hadi alipofika chini kabisa katika ghorofa ya mwisho. Akaelekea katika maegesho ya teksi yaliyoko upande wa pili wa Barabara ya Lumumba. Akakodi teksi hiyo impeleke Ilala, wakati huo ikiwa ni saa tisa za alasiri.

Anita alikuwa ameamua jambo moja tu, kuwafuata na kuwavamia ili wajue kwamba alikuwa ameshawashtukia, na pia auvunje uhusiano wa uchumba mara moja, ikiwa ni pamoja na kuivua ile pete ya uchumba na kumrudishia John Bosho. Kutokana na usumbufu wa foleni ya magari barabarani, hatimaye wakafika Ilala, kando ya Barabara ya Uhuru, na pale Anita akashuka na kumlipa dereva nauli yake, na yeye akachanganya miguu kuelekea usawa wa mlango wa kuingilia ndani ya Max Baa.

Mapigo ya moyo wake yaliongezeka na mwili kumtetemeka kwa hasira, lakini kila mtu aliyekutana naye, hakuna aliyemshtukia kama alikuwa katika hali kama ile. Alasiri hiyo wateja walikuwa ni wengi ndani ya baa ile maarufu, ambayo hutumiwa na wafanyabiashara wengi wanaoingia kuburudika baada ya shughuli za kikazi za kila siku.

Baada ya kuingia ndani, Anita aliyatupa macho pande zote za mle ndani ya baa, na kwa bahati nzuri alimwona Getruda na John wamekaa kwenye kona iliyokuwa upande wa kushoto, karibu kabisa na kaunta ya kuuzia vinywaji. Hasira zikaongezeka, hivyo akaanza kuvuta hatua moja baada ya nyingine kuwafuatilia pale walipokuwa wamekaa!

Ni kuanzisha tibwili!

      ********

JOHN Bosho na Getruda walikuwa wamezama katika mazungumzo yao, huku Getruda akiwa amempa mgongo, na John Bosho amekaa upande wa nyuma akiangalia watu wanapoingia. Meza yao ilikuwa na chupa kadhaa za bia, ambao walikuwa wanakunywa.

Kwa muda ule nishai ya pombe ilikuwa imeshaanza kuwaingia wote hasa ukizingatia walikuwa wameanza kunywa muda mrefu, tokea saa nane za mchana,  ikiwa ni yeye John aliyemwita Getruda baada ya kumpigia simu na kumsisitiza wakutane hapo! Ama kweli alikuwa ameshanogewa naye!

John Bosho alikuwa wa kwanza kumwona Getruda alivyokuwa anaingia. Akashtuka na kujiuliza imekuwaje awe pale kwa muda ule? Hata hivyo  akabaki akimwangalia jinsi Anita alivyokuwa anawajongelea. Getruda naye alishangaa baada ya kumwona John amepigwa na bumbuwazi huku akiangalia nyuma yake! Ndipo naye akageuka kuangalia nyuma!

Akamwona Anita!                                                                   

Akashtuka sana!

 Abaki ameachama mdomo wake!

Anita akavuta kiti  na kukaa huku akipumua kwa nguvu!

“Habari zenu…” Anita akawaambia huku akiwa bado amesimama karibu yao.

“Nzuri…karibu…” John Bosho akajitutumua na kumwambia. Lakini Getruda alinyamaza kimya huku akiiona ile hatari iliyokuwa inamkabili, kwa kusimamiwa na rafiki yake mkubwa, ambaye alionyesha dhahiri alikuwa ana hasira kali!

“Naona wenzangu mnaburudika…”  Anita akaendelea kuwaambia.

“Ah, ndiyo hivyo. Tunapooza makoo baada ya shughuli za kazi…” John Bosho  akasema huku akijiumauma!

“Getruda,” Anita akasema huku akimgeukia.

“Bee…” Getruda akaitikia huku aiangalia chini.

“Naona umeamua kustarehe na shemeji yako…”

“Ndiyo shoga’ngu…tumekutana tu…”

“Si kweli…” Anita akasema na kuonyesha kutomwamini Getruda.

“Huo ndiyo ukweli…nimekutana naye tu, ndiyo maana nikamkaribisha, na mimi sioni ubaya wowote!” John Bosho akadakia!

“Ukweli sasa umejulikana!” Anita akasema na kuongeza. “Nilikuwa nakueleza John, kuwa una uhusiano na shoga’ngu, lakini ukanibishia. Sasa nimewakuta!”

“Yaani kutukuta tumekaa wote ndiyo useme kuwa tuna uhusiano?” John Bosho akamuuliza Anita!

“Ndiyo maana yake…” Anita akamjibu!

“Kwa hivyo?” John akauliza.

“Hakuna cha zaidi, mimi naona kuwa, wewe uendelee na rafiki yangu, Getruda, na mimi niendelee na ustaarabu wangu!” Anita akamwambia kwa hasira John!

“Usifanye hivyo Anita. Mbona unataka kujaza inzi hapa?”

“Ndicho ulichokitaka wewe…”

Wakati wote huo, Getruda alikuwa amenyamaza kimya huku bado akiwa na wasiwasi. Ukweli ni kwamba alikuwa amechanganyikiwa sana, akitamani ardhi ipasuke ajichimbie! Lakini uzuri mmoja ni kwamba Anita akiwa mtu msomi, hakupenda kuzozana mpaka kila mteja aliyekuwa mle ndani ya baa ile ajue kuwa walikuwa wanagombana.

Hivyo basi, Anita aliongea kwa upole huku pia roho ikimuuma sana, na baada ya kumaliza kuwapasha, akauchukua mkoba wake na kuondoka huku akiwaacha John na Getruda wakiwa wanashangaa!

Ukweli ni kwamba lilikuwa fumanizi la nguvu!

“Unaona sasa?” Getruda akamuuliza John!

“Nimeona nini?” John Bosho akamuuliza!

“Si mchumba’ko Anita katukuta? Sijui nani kamwambia tuko hapa?” Getruda akaendelea kusema huku akiwa na wasiwasi mwingi sana!

“Si bure,” John Bosho akasema na kuongeza. “Inawezekana kuna mtu anafuatilia nyendo zetu!”

“Basi, nimetosheka. Sina hamu na kinywaji, mimi naondoka kwenda nyumbani…” Getruda akamwambia John.

“Sawa, tuondoke,” John akasema huku wote wakijiandaa kutoka.

John Bosho na Getruda wakanyanyuka huku wakiacha baadhi ya vinywaji vyao juu ya meza, ambavyo vilikuwa havijamalizika. Kwa mwendo wa taratibu wakatoka hadi nje ya Max Bar, mita chache tu kutoka katika Barabara ya Uhuru iliyokuwa inakatiza mbele ya baa hiyo maarufu.Wakati huo ikiwa imetimu saa moja za usiku, hivyo wakaelekea sehemu ya maegesho alipokuwa amepaki gari lake, ambapo walipanda na kulitoka eneo lile.

John Bosho alimpitisha Getruda nyumbani kwake, Ilala, mtaa wa Moshi, na kumwacha akiingia ndani, halafu yeye akaondoka huku nafsi yake ikimsuta kwa kitendo kile cha kukutwa akiwa na Getruda. Kwani ule ulikuwa siyo uaminifu angali akijua alikuwa na mchumba wake, Anita, waliokuwa wakitarajia kufanya utarataibu wa maandalizi ya kufunga ndoa.

Ni usaliti!

Hata hivyo, baada ya John Bosho kumfikisha Getruda nyumbani kwake, alipanga kwenda Tabata Mawenzi, nyumbani kwa Anita, usiku ule ule ili akamwombe radhi kwa kitendo kile alichokuwa amemfanyia. Ndiyo, alijiamini kuwa angemwagia maneno matamu ya kimapenzi ambayo yangemlainisha na kumfanya asahau masahibu yaliyomkuta!

********          

ANITA alikodi teksi punde tu baada ya alipotoka ndani ya Max Bar. Hakupenda kukaa muda mrefu katika eneo hilo kwa jinsi alivyokuwa amechukia, na alijua kuwa inawezekana John akamfuata nyuma na kuanza kumbembeleza kama ilivyo kawaida yake, ndiyo maana akapenda aondoke eneo hilo haraka sana.

Teksi iliondoka hapo Ilala, na kuifuata Barabara ya Uhuru, ambayo kwa muda huo ilikuwa na foleni kubwa ya magari. Anita alikuwa amekaa kwenye kiti cha nyuma huku amejiegemeza kama mtu anayelala. Hakika hakuamini kile alichokiona kwa macho yake, na hata teksi ilivyokuwa inaendelea na safari kuelekea Tabata, hakuwa na habari kabisa zaidi ya kuzama katika mawazo mazito.

Teksi ilimfikisha nyumbani kwake, Tabata Mawenzi, bila yeye kufahamu kutokana na kuwa na mawazo mengi sana. Ni dereva aliyekuwa anaendesha ndiye aliyemshtua na kumuuliza kuwa anashukia wapi. Ndipo aliposhuka na kulipa fedha, kisha nusu iliyobaki akatembea kwa miguuu kwa kuufuata uchochoro unaolekea nyumbani kwake, ambao unapitia nyuma ya Mawenzi Bar.

Baada ya kufika katika eneo la nyuma yao, akaingia ndani kwa kupitia katika mlango mdogo ulioko katika geti dogo lililotokeza uani. Kisha akaiendea nyumba yake iliyokuwa kule uani, ambayo ni kati ya nyumba zilizojengwa kwa kila mpangaji kujitegemea, inayofahamika kama ‘appatment,’ na kuzungushiwa uzio uliokuwa na urembo wa matundu yanayowezesha kuona upande wa nje.

Nyumba yake aliyopanga, ilikuwa imejengwa kifamilia, ikiwa na vyumba vitatu, sebule, stoo, jiko na huduma ya choo ikiwa mlemle ndani. Mlango mkubwa wa kuingilia ulikuwa upande wa nje kutazamana na uwanja mdogo uliokuwa na bustani nzuri ya maua na miti iliyofungamana na kufanya kuwe na kivuli kizuri wakati wa mchana. Pia, eneo zima lilikuwa limezungukwa na huo ukuta madhubuti.

Anita akatoa ufunguo ndani ya mkoba na kuufungua mlango ule mkubwa. Akaingia ndani na kupokewa na ukimya wa aina yake ukizingatia alikuwa anaishi peke yake. Baada ya kuingia ndani, akawasha taa, halafu akafikia kukaa kwenye sofa lililokuwa pale sebuleni na mkoba wake akauweka juu ya meza. Akabaki akitafakari juu ya kumkuta Getruda na mchumba wake John Bosho wakiwa wamekaa pamoja.

Hata hivyo baada ya kukaa kwa muda, Anita alinyanyuka na kuingia chumbani kwake ili kubadili nguo na kuendelea na ratiba nyingine ya usiku ule.  Alipomaliza kubadili na kuvalia upande wa kitenge, akaingia bafuni na kuoga. Alipomaliza kuoga akarudi tena sebuleni ambako alifungua friji na kuchukua soda moja aina ya Mirinda na kukaa tena kwenye sofa.

Anita aliendelea kunywa soda taratibu, kwani hakuwa na hamu ya kula chakula kabisa, au tusema aliamua kutokula chochote kwa siku ile. Alichokuwa anawaza ni kuachana na mchumba wake, John Bosho mara moja, na pia kuvunja urafiki wake na rafiki yake, Getruda, ambaye kwa muda ule alimfananisha na msaliti aliyeingilia penzi lake.

Ili aweze kuyapunguza mawazo yale, Anita aliwasha runinga na kuendelea kuangalia vipindi vilivyokuwa vinaendelea ingawa ni kwamba alikuwa haelewi chochote zaidi ya kuona kama ni kivuli tu kilichokuwa mbele yake. Mawazo yalikuwa yamemzidi kupita kiasi, hata hivyo, hakupenda mawazo hayo yamwandame zaidi, isipokuwa alichukua simu yake na kuamua kumpigia simu rafiki yake, Getruda, ili amweleze ukweli juu ya kile kitendo alichokuwa amemfanyia!

        ********

UPANDE wa pili. Getruda alibaki hana raha kabisa baada ya kukutwa na rafiki yake, Anita, akiwa na mchumba wake, John Bosho. Ukweli ni kwamba aliweza kuiona hatari iliyokuwa inamkabili, akiwaza kuwa ni lazima Anita angemfanyia kitu kibaya ingawa alikuwa ni rafiki yake wa damu, kutokana na kitendo kile alichofanya.

Getruda alishindwa kabisa hata kumpigia simu rafiki yake, Anita, angalau hata amwombe radhi kwa kile kilichotokea baada ya kumkuta amekaa na mchumba wake, John Bosho. Je, hata angempigia simu, angemwambia nini wakati alikuwa ameshakasirika?”

Wakati Getruda akiwa katika mawazo yale, simu yake ya mkononi iliita. Akaichukua na kuangalia namba za mpigaji, ambayo ilionyesha ni za shoga yake, Anita! Kwanza kabisa kabla hajaipokea simu ile, mapigo ya moyo wake yakaongezeka huku bado akiiangalia ile simu ilivyokuwa inaita.

“Haloo…Anita…” Getruda akaipokea.

“Natumaini hujambo Getruda…” upande wa pili wa simu ukasema.

“Mimi sijambo…”

“Umefurahi sana kunichukulia mchumba wangu sivyo?”

“Hapana Anita…usiseme hivyo!”

“Unabisha?”

“Sibishi…isipokuwa…”

“Sikiliza…” Anita akamwambia na kuendelea. “Sina muda wa kulumbana na wewe! Ukweli ni kwamba umenikwaza sana, na kuanzia leo hii, mimi na wewe urafiki basi, kila mtu aendelee kivyake. Na pia huyo John nakuachia uendelee naye! Nawapa Uhuru!”

“Usifanye hivyo Anita, hayo ni mambo ambayo yanaweza kuzungumzwa. Tambua kuwa tumetoka mbali sana!”

“Kama ulikuwa unatambua kuwa tumetoka mbali, usingenifanyia hayo. Hivyo mimi sina mjadala na kwa heri!” Anita akamaliza kusema!

Akakata simu!

“Mungu wangu!” upande wa pili Getruda akasema na kubaki ameshika simu yake mkononi!

Getruda alikuwa ameshaupata ujumbe ule kutoka kwa rafik yake, Anita. Hivyo hakuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na uamuzi ule, ingawa kwa masikitiko makubwa!

        ********

ALIPOMALIZA kuongea kwa simu na rafiki yake, Getruda, Anita alijibwaga tena kwenye sofa. Wakati akiwa bado amekaa hapo, mara mlango wa nje uligongwa mara mbili. Akashtuka na kubaki akiuangalia huo mlango mkubwa kana kwamba ndiyo kwanza alikuwa ameuona! Mapigo ya moyo wake yakapiga kwa kasi, Je, ni nani anayegonga usiku huo? Hakujua!

Kabla hajanyanyuka kwenda kuufungua huo mlango, mara ukafunguliwa na John Bosho, ambaye aliingia hadi ndani hapo sebuleni, ambapo Anita akiwa bado amekaa, alibaki akimwangalia tu bila kumsemesha, hadi alipoenda kujikalia kwenye sofa dogo la pembeni. Hakutaka kumsemesha Anita ambaye alionekana kuchukia sana, ukizingatia siyo muda mrefu alikuwa akinywa soda yake taratibu tu, kana kwamba hakumwona alivyokuwa akiingia.

“Anita mpenzi wangu…” John Bosho akaamua kumwita baada ya kuvumilia kunyamaza kwa muda.

“Bee,” Anita akaitikia huku akimwangalia kwa huzuni.

“Naona umechukia sana…” John akamwambia kwa sauti ndogo.

“Ni kweli…nimechukia sana!” Anita akamwambia na kuendelea. “Na hata ninapokuona hapa, ni kwamba naona kichefuchefu!”

“Unaona kichefuchefu?” John Bosho akamuuliza!

“Ndiyo, naona kichefichefu! Huwezi kunichanganya mimi na rafiki yangu, Getruda!”

“Ndiyo maana nimekuja tuyamalize mpenzi wangu…”

“Uyamalize na nani?”

“Si wewe mchumba wangu?”

“Haitawezekana kamwe!” Anita akamwambia na kuendelea. “Yaani kuanzia leo hii mimi na wewe basi! Uchumba wetu uishie hapa hapa! Nakuchukia sana!”

“Kwa nini iwe hivyo?”

“Nimejaribu kukuchunguza kwa muda mrefu sasa, na kugundua kuwa wewe siyo mwaminifu kabisa. Hivyo nilichopanga mimi ni kuuvunja uchumba wetu rasmi, hakuna mjadala!”

“Usifanye hivyo Anita…” John Bosho akawa anambembeleza.

“Ndivyo nilivyoamua, mwanaume wewe, unaweza kuniua kwa ukimwi!”

“Usiseme hivyo, ukimwi tena?”

“Ndiyo, huoni unavyoutembeza? Huridhiki na mimi mchumba wako?” Anita akaendelea kusema na kuendelea. “Na kwa taarifa yako, na hii pete ya uchumba uliyonivisha naivua hii hapa!”

“Usiivue tafadhali!” John Bosho akaendelea kumsihi.

“Sikuelewi kabisa!” Anita akasema huku akiivua hiyo pete iliyotengenezwa kwa dhahabu!

John Bosho akabaki akitumbua macho! Baada ya kumaliza kuivua, akampa  pete hiyo ya uchumba kwa kumpatia mkononi mwake, na Jophn akabaki amechanganyikiwa na kuiangalia, kwani hakuamini hicho alichokuwa anakiona! Yaani kurudishiwa pete yake, ambayo alikuwa ameshamvalisha?

“Halafu hatua itakayofuata…” Anita akaendelea kumhabarisha. “Ni kuirudisha nyumba hii uliyopangishia kwa mwenyewe, na mimi narudi nyumbani kwa wazazi wangu, kule Kiwalani, ili niweze kukuachia uhuru wa kutanua vizuri na Getruda! Nimeamua hivyo na hakuna wa kuyabadili mawazo yangu!”

“Unasema unarudi nyumbani kwa wazazi wako?” John Bosho akamuuliza kana kwamba alikuwa hajamsikia vizuri!

“Sina jinsi John. Ukweli ni kwamba nilikupenda sana,” Anita akamwambia na kuendelea. “Lakini sina budi kufanya hivyo!”

“Sijakupata vizuri Anita, ina maana na hii nyumba niliyokupangishia?”

“Hakuna jinsi John, itabidi tuirudishe kwa mwenyewe!”

“Oh,”  John Bosho akaishia kuguna huku akiendelea kumwangalia mchumba wake huyo alivyokuwa amechukua kupita maelezo.

“Halafu kitu kingine ambacho nitakifanya John,” Anita akaendelea kumwambia. “Itabidi nitoe siri zako zote, ambazo nilikuwa nimezificha muda mrefu sasa, kuwa wewe ni mtu mwovu, ni jambazi!”

“Mh! Umefika mbali sasa Anita!” John Bosho akamwambia huku akimwangalia kwa hamaki!

“hapana, sijafika mbali!”

“Ina maana unataka kunichoma?” John Bosho akasema huku akiyatoa macho yake pima!

“Ndiyo, nitafanya hivyo! Na kuanzia sasa hivi ondoka hapa nyumbani!” Anita akamwambia huku akiwa  amechachamaa na povu likimtoka mdomoni!

“Yaani unanifukuza Anita? Hakika siamini!”

“Ndiyo, kuanzia sasa amini! Sitaki mawasiliano na wewe!”

“Hutaki mawasiliano na mimi sivyo?”

“Ndiyo, sitaki!”

“Basi, na mimi nakushauri kuwa fikiria mara mbili mbili juu ya kauli yako ya kutaka kunichoma kwa Jeshi la Polisi! Achana na wazo hilo kabisa!” John Bosho akamwambia Getruda huku akinyanyuka!

“Kwani utafanya nini?”

“Nitajua cha kufanya, naona unajiamini sana wakati unatambua fika kuwa mimi ni mtu wa aina gani!”

“Kabla hujanidhuru, utakuwa umeshatiwa mbaroni!”

“Haya, tuone nani mtoto wa mjini! Mimi naondoka zangu!” John Bosho akamwambia Anita!

Baada ya mabishano yale, John Bosho akaamua kuondoka, kwani hakutaka kubishana na Anita, kitu ambacho kingejaza watu usiku ule. Lakini baada ya kuondoka, alibaki akiwa amechanganyikiwa baada ya Anita kumwambia kuwa angemchoma kwa Jeshi la Polisi, kuwa anajihusisha na ujambazi!

Jambo hilo ndilo lililomuuma zaidi John Bosho! Aliona kama Anita angetoa siri zake, basi huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuangamia kwake! Hivyo akaamua jambo moja tu, ni kumwondoa uhai wake haraka iwezekanavyo!

*********          

WIKI moja ilipita tokea John Bosho na Anita kutibuana, mara baada ya kugundulika kuwa yeye ana uhusiano wa kimapenzi na Getruda, rafiki yake Anita. Ukweli ni kwamba wiki hiyo ilikuwa ngumu sana kwa wapenzi wale waliokuwa wameshazoeana. Kila mmoja hakuamini kile kilichokuwa kimetokea zaidi ya kuuamia rohoni.

John Bosho aliendela kumwomba msamaha na kumbembeleza sana, mchumba wake, Anita, lakini hakuambulia kitu zaidi ya kupewa maneno ya kashfa. Kwa vile alikuwa bado anampenda, roho ilikuwa inamuuma sana, hivyo akaamua kukutana na vijana wake wa kazi ili kupanga mkakati maalum.

Walikuwa ni vijana waliokuwa wanajulikana kwa majina ya, Chogolo, Muba, Kessy na Chikwala, ili awaelezee juu ya azma yake ya kutaka kumwondoa uhai Anita, aliyetishia kuitoa siri zake. Kwa kumsikiliza bosi wao, vijana hao wakakubaliana naye na kuzidi kumpa moyo! Ni kumtoa uhai wake mara moja!

Sasa kilichobaki kwa John Bosho, ilikuwa ni juu ya kupanga kifo cha Anita kitakavyotekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu. Kwa upande wake hakupenda kutumia silaha yake katika kutimiza lengo lake, isipokuwa aliamua kutumia sumu kali aina ya nyongo ya Mamba, ambayo huua mara moja mara baada ya mlengwa kuitumia.

Sumu hiyo kali, John Bosho alikuwa anaihifadhi nyumbani kwake kwa malengo maalum, ikiwa katika hali ya unga, lakini akitaka kuitumia, huichanganya na maji tayari kwa kudunga sindano, au unga huo  kwa kuunyunyizia sehemu husika anayokusudia, kama vile kwenye vyakula, maji ya kunywa, vinywaji nk. Hivyo, John Bosho aliamua kummaliza Anita kwa kumdunga sindano ya sumu ile itakayotiwa ndani ya bomba la sindano.

Basi siku hiyo ya kutekeleza kazi yake, John aliiandaa sumu hiyo na kuichanganya na maji, halafu akaiweka kwenye kichupa kidogo, ambacho alikihifadhi ndani ya droo ya gari lake. Baada ya kukamilisha kila kitu, akatoka nje ya nyumba yake, eneo hilo la Ukonga, halafu akapanda gari lake aina ya Toyota Harrier, kuelekea kwenye mizunguko yake mingine ya kibiashara katikati ya jiji la Dare s Salaam.

Alipomaliza mizunguko yake hiyo, ndipo aliposhika uelekea wa kwenda eneo hilo la Tabata Mawenzi, alipokuwa anaishi Anita, mchumba wake waliohitilafiana. Wakati huo ilikuwa imetimu saa saba na nusu za mchana, na yeye alijua kwamba  Anita alikuwepo nyumbani. Hivyo aliifiata Barabara ya Mandela moja kwa moja kutokea Biguruni. Na alipfika eneo la Tabata, alipinda kulia na kuifuata barabara inayoelekea maeneo ya Tabata Bima na kwingineko.

Aliifuata barabara hiyo kwa mwendo wa taratibu tu na baada ya kufika eneo la Tabata Aroma, John Bosho alilisimamisha gari kando ya barabara karibu na kituo cha daladala, halafu akashuka garini na kuelekea kwenye duka moja la kuuza dawa za binadamu, lililokuwa katika jengo lile Aroma, lenye ghorofa tatu.

John Bosho akaingia ndani ya duka hilo kwa kuusukuma mlango wa kioo uliokuwa na fremu ya aluminiam, na baada ya kuingia ndani, alipokewa na hewa ya ubaridi wa kiyoyozi. Humo ndani  alimkuta mwanadada mmoja mwenye umri wakati, aliyekuwa anauza dawa, ambaye alimkaribisha kwa sauti ya kibiashara:

“Karibu…”

“Ahsante…” John Bosho akasema huku akimkagua!

“Nikusaidie…” mwanadada yule akamwambia.

“Ninahitaji bomba la sindano?”  John akamwambia.

“Unahitaji mangapi?…” mwanadada yule akamuuliza.

“Nahitaji bomba moja la sindano…”

“Bomba moja tu?” Muuzaji akauliza baada ya kumshangaa kwa kuchukua bomba moja tu, kwani alitakiwa achukue zaidi ya moja.

“Ndiyo, moja linatosha, kwani vipi?”tu…” John akamwambia huku akimwangalia mara mbili mbili!

 “Naona ungechukua na akiba…moja halitoshi…”

“Kwani unajua nataka kufanyia kazi gani?”

“Si kwa kuchomea dawa?”

“Basi moja linatosha…”

“Haya…” muuzaji huyo akamwambia.

Muuzaji wa dawa akafungua kabati lililokuwa linatunzia dawa, halafu akachukua lile bomba la sidano na kumwekea kwenye bahasha ya rangi nyeupe kwa ajili ya kuwapa wateja. John Bosho akalipokea na kumlipa fedha baada ya kuchomoa noti ya shilingi efu kumi kwenye pochi yake, na kabla hajarudishiwa chenji yake, akaanza kuondoka kuonyesha alikuwa na haraka sana!

John Bosho alifanya hivyo, kwani hakutaka kuulizwa maswali mengi na yule muuzaji, na pia aliogopa sije akamkariri sura itakapogundulika kama ni yeye atakayekuwa ametekeleza mauaji ya Anita, ambapo ndipo alipokuwa anaelekea huko!

“Kaka chenji yako!” Muuzaji yule akamwambia baada ya kuona amesahau!

“Ah, hiyo chenji chukua tu,” John akamwambia, halafu akatoka nje kwa hatua za haraka.

“Ahsante,” muuzaji akasema huku akishangaa kuachiwa fedha na mteja yule!

John Bosho alipofika nje sehemu ile alikopaki gari lake, akaufungua mlango na kuingia ndani. Kabla ya kuondoa gari, akakaa kwa muda, ambapo alifungua droo moja iliyokuwa hapo mbele kwenye ndashibodi ya gari, halafu akatoa kichupa kidogo, ambacho  kilichokuwa na ule mchanganyiko wa maji na sumu kali ya nyongo ya Mamba. Akakakiangalia kichupa hicho huku akitabasamu, hasa akifikiria kuwa ndiyo alikuwa anakwenda kuitumia kwa mlengwa aliyemkusudia!

Mara baada ya kukiangalia kile kichupa kwa muda, akalitoa lile bomba la sindano ndani ya bahasha, na kuinyonya ile sumu kiasi cha kulijaza lile bomba lote, kisha akalirudisha ndani ya bahasha tena na kichupa kukirudisha ndani ya droo. Hapo ndipo alipovuta pumzi ya nguvu na kuishusha, halafu akayatupa macho yake pande zote, kulia na kushoto. Hakuna mtu yeyote kati ya wapiti njia aliyemuoa zaidi ya kila mmoja akiwa katika shughuli zake.

Baada ya kumaliza kuhakikisha hakuna mtu aliyemwona, ndipo John Bosho alipolitia moto gari lake na kuliondoa kwa mwendo wa taratibu, kuliingiza katika barabara kuu, kuelekea Tabata Mawenzi, nyumbani kwa Anita kutimiza azma yake ya kuuondoa uhai wake! Akiwa ndani ya gari huku akiendesha kwa mwendo wa wastani, alichomoa simu yake ya mkononi na kumpigia Anita kumtaarifu kuwa anakwenda hapo nyumbani kwake.

Simu ikaanza kuita!

********         

MAJIRA ya saa nane za mchana, Anita alikuwepo nyumbani kwake, Tabata Mawenzi. Wakati huo ndiyo alikuwa amepumzika kwenye sofa sebuleni, huku akiwa na mawazo mengi sana. Tokea akorofishane na mchumba wake, John Bosho, alikuwa hana raha kabisa, na alikuwa anapanga kurudisha nyumba na kuondoka haraka sana!

Simu ya mkononi iliyokuwa juu ya meza ndogo ya kahawa hapo sebuleni, umbali mfupi tu na aliokuwa amekaa kwenye sofa, ilianza kuita. Akanyanyuka kivivu na kuichukua, akiwa na hamu ya kutaka kujua mpigaji wa simu hiyo, hasa ukizingatia siku ile hakuwa katika hali nzuri kabisa, alihitaji kupumzika.

Lakini Anita alipoangalia namba za mpigaji wa simu hiyo, aliona ni ya siri isiyoonyesha namba ya mpigaji kwa tarakimu, akaduwaa kwanza, halafu akaipokea kwa sauti ndogo, “Anita anaongea…”

“Oh. hujambo mpenzi wangu?” Upande wa pili wa simu ukasema kwa sauti nzito, ambayo siyo ya mtu mwingine zaidi ya John Bosho, mchumba wake waliokorofishana. Na wakati huo ndiyo alikuwa ndani ya gari lake, akielekea nyumbani kwa Ania katika kutekeleza adhabu yake aliyokuwa amempangia!

“Si…sijambo…” Anita akaitikia kwa kusita kidogo mara baada ya kuitambua sauti ya huyo mpigaji wa simu hiyo!

“Ni mimi mchumba wako, John Bosho…” John Bosho akajitambulisha kwani alijua kuwa namba haikusomeka kwenye kioo cha simu.

“Nimeshajua ni wewe John…unasemaje?” Anita akauliza kwa hasira!

 “Vipi tena?” John Bosho akauliza. “Mbona unakuwa mkali mpenzi Anita?”

“Mimi siyo mpenzi wako, John …naomba unisahau na usinijue!”

“Usifanye hivyo…naomba tukutane ili tuweze kulitatua tatizo hili…”  John Bosho akaendelea kumsihi Anita.

“Haiwezekani, sitaki kuonana na wewe kabisa!” Anita akamwambia na kukata ile simu, huku akifyonza kwa nguvu!

Baada ya kuikata ile simu, Anita akaiweka mezani na kuendelea kuwaza. Hata hivyo ile simu ikaita tena, mpigaji akiwa ni mtu yule yule mchumba wake, John Bosho! Hivyo akaamua kumsikiliza ingawa ilikuwa kero kwa upande wake!

“Unasemaje? Mimi naona kama unanisumbua!”

“Naomba uwe mtulivu Anita. Daima mvumilivu hula mbivu…” John akaendelea kumwambia Anita.

“Sikiliza John. Natumaini wewe ni mtu mwelewa sana! Siwezi kuwa mtulivu…si unajua kwamba umeamua kunisaliti kwa penzi la rafiki yangu Getruda? Basi endelea naye na mimi uniache nilivyo!” Anita akamwambia kwa sauti iliyojaa uchungu mwingi!

“Ok, hayo tuyaache…mimi nitakutembelea hapo nyumbani jioni ya leo ili tuyamalize. Mbona ni mambo madogo sana?”

“Wewe unaona haya ni mambo madogo? Hapana, naomba usije John…” Anita akaendelea kumwambia!

“Sasa nisikilize kwa makini sana Anita,” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Mimi nitakuja hapo nyumbani upende usipende. Hakuna mtu asiyejua kuwa mimi ni mmoja wa wahusika wa hapo. Nafikiri unanijua kwamba mimi ni mtu wa aina gani! Ukicheza nakuondoa uhai wako mara moja!”

“Oh, Mungu wangu!”

“Mwombe sana huyo Mungu wako!” John akamaliza kusema!

Simu ikakatwa!

Anita akavuta pumzi ndefu na kuzishusha, halafu akajiegemeza kwenye sofa huku mawazo yake yakiwa mbali. Hakujua John Bosho alikuwa anahitaji kitu gani kutoka kwake, wakati alishamwambia kuwa hataki uchumba tena, na pete yake alikuwa ameshamvulia na kumrudishia!

Anita aliiangalia saa yake, ambayo ilionyesha imetimu saa nane mchana, hivyo hakuwa na jingine zaidi ya kuingia chumbani ili kupumzika chakula kiteremke. Baada ya kujilaza tu, alipitiwa na usingizi mzito uliochanganyika na mawazo aliyokuwa anawaza, na pia jinsi John alivyomchanganya!

Anita alianza kuota ndoto za kutisha, huku akikumbwa na majinamizi, ikiwa ni ndoto ambayo alikuwa hajawahi kuota hata siku moja, ikiashiria ni ndoto ya kifo! Ndani ya usingizi huo, aliota akijiona anaruka angani kwa kasi, akiyapita mabonde na milima mikubwa, ambayo aliweza kuiona kwa chini. Hatimaye akaenda kutua juu ya mlima mmoja mrefu uliotengenishwa na bonde lenye kina kirefu ajabu.

Kwa mbele nako aliuona mlima mwingine mrefu kama ule aliokuwa amesimama yeye, ambao uliwatengenisha kwa lile bonde. Mara muungurumo kama wa radi ulitokea na kulipuka katika mlima ule wa pili, ambapo alitokea mtu mmoja aliyekuwa amevalia mavazi meupe yanayong’aa. Mtu yule akanyoosha mkono wake wa kulia na kusema kwa sauti iliyokuwa inatoka kwa mwangwi uliotetemesha!

“Anitaaa….aaaa!”

“Beeee!” Anita akaitikia kwa hofu!

“Wewe mwanadamu…nakukaribisha huku kwetu!” Mtu yule akaendelea kumwambia!

“Hivi huku ni wapi?” Anita akauliza huku akiwa na wasiwasi mkubwa.

“Nilisikilize kwa makini wewe mwanadamu. Huku ni peponi!”

“Lakini mimi siwezi kufika huko mpaka nivuke bonde hili!”

“Ni kweli huwezi kuvuka katika bonde hili!” Mtu huyo akamwambia na kuongeza. “Unahitaji kutubu dhambi zako…na ukitubu tutakukaribisha!”

“Oh, basi nitatubu ili  niweze kuvuka…”

“Nasikitika sana mwanadamu! Umechelewa…huu siyo muda wake!”

“Oh, Mungu wangu! Kwa nini?”

“Napenda kukutaarifu ujiandae…Muda siyo mrefu utakuja huku. Lakini hutanifikia katika himaya hii ya peponi.!”

“Sitafanikiwa?” Anita akauliza. “Isipokuwa?”

“Ni lazima utazama ndani ya bonde hili!”

“Kwa nini nizame?”

“Utazama kwa ajili ya dhambi zako zilizotukuka!”

“Mamaaa..aaa!” Anita akalia kwa kupiga ukulele mkubwa! Ni ukulele ambao ulitoa mwangwi ulioenea kote!

“Haya, jiandae kuja huku! Karibu sana katika himaya ya peponi” Mtu huyo akamwambia huku akimnyooshea kidole!

Muungurumo mkubwa ukatokea! Mtu huyo akazama katika mawingu meupe yaliyokuwa yametanda angani!

“Ooohps!” Anita akapiga yowe kubwa na kushtuka katika usingizi ule wa mchana!

Anita akayafikicha macho yake na kuona kuwa alikuwa ndani ya chumba chake, ambapo alikuwa amelala siyo muda mrefu. Hatimaye baada ya kugundua kuwa alikuwa chumbani mwake, akashuka kitandani na kukaa huku akitafakari ndoto ile. Ukweli ni mkwamba ilikuwa inatisha ilikuwa inatisha!

Je, iliashiria kitu gani?

Hivyo basi, Anita akanyanyuka kutoka pale  kitandani. Halafu akachukua taulo lililokuwa limetundikwa, pamoja na upande wa kitenge, ambao alijifunga na kuamua kwenda kujimwagia maji ndani ya bafu lililokuwa mle ndani, ili kuondoa uchovu uliotokana na usingizi wa mchana.

        ********   

John Bosho alisimamisha gari lake katika uwanja mdogo uliokuwa mbele ya maegesho ya kuegesha magari, jirani na Mawenzi Bar, eneo la Tabata Mawenzi. Sehemu hiyo iliyokuwa na miti ya muarobaini iliyokuwa na kivuli, pia, palikuwa na magari mengine kama matatu hivi yaliyokuwa yamepaki hapo, hivyo yeye akalipaki la kwake katikati ya hayo magari.

Majira hayo ya saa tisa za alasiri, jua lilikuwa bado ni kali, kiasi cha kuleta kero kwa watembea kwa miguu na wasafiri wanaotumia mabasi ya daladala, ambao wengine walijificha katika vivuli vya miti. Baada ya kupaki lile gari, John akashuka na kuufunga mlango wa gari huku akihakikisha kama ameufunga vizuri, halafu akaondoka kwa mwendo wa taratibu kuufuata uchochoro mmoja uliotenganisha nyumba na nyumba.

John Bosho alitembea kwa mwendo wa kawaida tu, huku katika mkononiwake wa kushoto ameshika bahasha ndogo iliyokuwa na kitu muhimu, bomba moja la sindano lililokuwa na sumu kali ndani yake, ambayo ni ya kumshughulikia mchumba wake, Anita. Hivyo akaendelea kuufuata ule uchochoro na kutokea kwenye eneo hilo lililokuwa liimezungukwa na uzio wa ukuta uliojengwa kwa matofali. Ndani yake ndipo palipokuwa na nyumba kama tano hivi, ambapo nyumba aliyopanga Anita ilikuwa moja wapo.

Pale John akasimama kwa muda huku akichungulia ndani kwa kutumia matundu madogo yaliyokuwa katika ukuta, ambayo yalitengenezwa kama urembo, na pia kuwezesha upepo kuingia ndani, lakini hakuona mtu yeyote, aliyekuwa pale uani. Palikuwa kimya kabisa, na kitu alichoweza kuona, ni bustani ya maua na miti iliyokuwa pale.

Basi, ndani ya nyumba moja wapo, ambayo haikuwa mbali na uzio wa ukuta, ambapo pia siyo mbali na hapo alipokuwa amesimama nje ya ukuta,  ndipo alipokuwa anaishi Anita, mchumba wake. Vilevile, wakati huo alikuwepo ndani kwake, ikiwa ni muda mfupi tu tokea amempigia simu na kumjulisha kuwa yeye atakuwa mgeni wake, ingawa alikataa.

Hapo alipokuwa amesimama John Bosho, palikuwa na miti ya muarobaini iliyofungamana. Hivyo hakupoteza muda, akauruka ule uzio kiufundi bila kuonekana na mtu yeyote hadi alipoibukia ndani ya ua wa nyumba hiyo, umbali mfupi kutoka katika nyumba anayoishi Anita. Baada ya kuingia, akajibanza kwenye kona moja iliyokuwa na maua yaliyofungamana, tayari kulivizia windo lake, mchumba wake, Anita!

Ni kwamba John Bosho alikuwa amepanga aingie mle ndani ya nyumba ya Anita bila kuonekana na mtu yeyote, ili amfungie kazi, ukizingatia alifika pale kwa kazi moja tu ya kuua, na si vinginevyo! Hivyo akaendelea kubanisha pale kwenye kivuli cha maua ili kuvuta subira mpaka atakapomwingilia mle ndani kwake kwa kupitia katika mlango mkubwa aliokuwa anauangalia kwa makini! 

Baada ya kuhakikisha kila kitu kilikuwa shwari pale uani, John Bosho alijitoa pale mafichoni na kuuendea mlango ule wa kuingia ndani ya nyumba ya Anita. Baada ya kuufika, akaufungua taratibu na kuingia ndani huku akinyata. Akaanza kumtafuta Anita kila kona, hadi alipogundua kuwa alikuwa ameingia bafuni kuoga na kuufunga mlango bila komeo, kwa vile ilikuwa ni ndani kwake, na alikuwa peke yake.

John Bosho aliuendea mlango ule wa bafuni, ambao pia aliufungua taratibu, ambapo pia aliweza kumwona Anita akiuvua ule upande wa kitenge aliokuwa amejifunga pamoja na taulo, na vyote kuvitundika kwenye kamba iliyokuwa mle ndani. Akabaki uchi na kujiandaa kujimwagia maji bila kujua kuwa kuna mtu aliyekuwa anamwinda pale mlangoni!

        ********

MARA baada ya Anita kuvua kienge na kubakia uchi kama alivyozaliwa, na kabla hajajimwagia maji, alijiangalia takriban dakika moja hivi, na kujiona alivyokuwa na umbile zuri na la kuoendeza. Hapohapo akajiuliza, imekuwaje John Bosho, mchumba wake, amkinai na kumkimbilia Getruda rafiki yake? Ni kitu gani alichokosa mwilini mwake?

Hata hivyo, Anita akayatupilia mbali mawazo hayo, halafu akaliangalia bomba la mvua lililokuwa juu, ambalo alikuwa tayari kulifungua ili aanze kujimwagia maji. Lakini kabla hajafanya lolote, akashtukia akirukiwa na kiumbe chenye nguvu mithili ya mnyama,  Simba, na kiumbe hicho kikamng’ang’ania maungoni mwake!

Anita alichanganyikiwa kwa kitendo hicho kilichotokea ghafla kana kwamba alikuwa ndotoni, na kutaka kupiga kelele za kuomba msaada. Hata hivyo sauti yake haikuweza kutoka, kwani alizibwa mdomo na mkono wenye nguvu nyingi!

“Oooohpsi!” Anita akapiga kelele ambayo haikuweza kusikika mbali kwa vile alikuwa amezibwa mdomo!

“Tulia!” John Bosho akamwambia kwa sauti ndogo lakini nzito!

“Ooh! Unataka nini?” Anita akamuuliza!

“Ni mimi John Bosho!” Akamwambia kwa sauti kavu na kuendelea “Nimekuja kama nilivyokwambia muda siyo mrefu kwenye simu! Hivyo nakusihi utulie kimya kabla sijakumaliza!”

“Oohps….Ooohps!” Anita akatoa sauti baada ya mdomo wake kuachiwa na John aliyekuwa amemziba kwa mkono wenye misuli!

“Nakuonya tena! Tulia!” John Bosho akaendelea kumwambia huku akimwonyesha bastola aliyokuwa ameikamata mkononi!

“Oh, umepitia wapi mwanaume wewe?” Anita akamuuliza huku bado wasiwasi mwingi umemjaa!

“Unashangaa? Nimepitia mlangoni!” John Bosho akaendelea kusema huku amekunja uso wake! Ni uso uliokuwa unatisha mithili ya jitu la porini!

“Mbona unanifuata sana?” Anita akamuuliza huku akiwa na wasiwasi!

“Ni kama nilivyokwambia mwanzo Anita!..” John Bosho akamwambia huku akimwangalia kwa uchu wa ngono, ukizingatia alikuwa na umbile zuri la kike lenye kutamanisha! Halafu akamvutia kwake na kutaka kumkumbatia!

“Tafadhali toka, usiniguse!” Anita akamwambia huku akikunja uso wake!

“Lazima nikuguse mpenzi!”

“Nitakupigia kelele!” Anita akasema huku akimsukuma John Bosho.

“Huwezi kupiga kelele, naomba uwe mtulivu, na kutulia kwako ndiyo usalama wa maisha yako!” John akamwambia Anita huku akimfuata!

“Unataka kufanya nini?”

“Nataka nikufanye kwanza, halafu adhabu nyingine ifuate baadaye!”

“Ooohpsi!” Anita akapiga ukelele mdogo!

“Usiniwangie mchana!” John Bosho akamwambia Anita. Halafu akamkamata kwa nguvu na kumwangusha chini sakafuni!

Kwa vile Anita alikuwa uchi wa mnyama, uchu wa ngono ukaendelea kumwandama John Bosho, na baada ya kumwangusha chini, akafungua zipu ya suruali yake na kutoa ‘dhakari’ yake. Akaanza kumbaka  Anita mbaye kwa muda ule hakuwa na nguvu yoyote baada ya John kumbana kwa nguvu pale sakafuni hadi alipomaliza haja yake huku akichekelea!

Ni unyama wa kutisha!

Alipomaliza kumbaka Anita, John Bosho akampiga kofi moja la nguvu lililomfanya achanganyikiwe na kuona nyota nyota! Halafu bila kupoteza, akachukua ile bahasha ndogo aliyokuwa nayo, na ndani yake kulikuwa na bomba la sindano, lililokuwa na sumu kali aliyokuwa ameitayarisha kwa ajili ya kazi ile. Akamchoma Anita na sumu yote ikamwingia mwilini mwake!

Baada ya John kumaliza kumchoma ile sindano, akalichomoa lile bomba na kulitia ndani ya ile bahasha, ambayo aliiacha kando ya mwili wa Anita uliokuwa umelala pale kwenye sakafu ya bafuni. John akasimama kwa muda huku akiuangalia ule mwili mwororo wa Anita, ambao muda siyo mrefu alikuwa akijiburudisha juu yake. Akatikisa kichwa kwa uamuzi ule alioamua kumfanyia mwanadada huyo, ambaye kamwe hakupaswa kupewa adhabu kama ile ya kinyama!

Kwa upande wa John, aliamua kumuua Anita kwa kutumia njia ya sumu, kwani hakupenda kutumia bastola ingawa alikuwa nayo muda wote. Sumu ile ikaendelea kuingia na kusambaa katika mwili wa Anita na kumfanya apate maumivu makali sana huku nguvu zikimwishia na kuona giza!

“Ooohpss!” Anita akendelea kupiga kelele!

“Utakoma kuringa!” John Bosho akaendelea kumsimanga!

“Oh, unaniua John…oh!”                         

“Sikuwa na jinsi…siri zangu nyingi unazijua! Hivyo huna budi kufa!”

“Oh, Mungu wangu!” Anita akaendelea kusema huku akifumba macho!

“Kwa heri Anita…kawasalimie kuzimu!” John Bosho akamwambia huku akijiandaa kuondoka.

“Mungu atalipa…” Anita akamaliza kusema huku roho ikianza kuachana na mwili!

Baada ya kuhakikisha Anita amekufa, John Bosho akatoka  mle ndani ya bafu lile kwa njia ileile aliyoingia nayo, hadi alipofika nje. Halafu akatoka nje kabisa wa nyumba ile, kwa kuuruka ukuta ule wa upande wa nyuma na kutokomea kuufuata ule uchochoro hadi sehemu ile aliyokuwa amepaki gari lake. Hakuna mtu yeyote aliyemshtukia kuhusiana na mauaji yale aliyofanya, na alipolifikia gari lake akapanda na kuondoka eneo lile haraka sana akiwa na matumaini!

Baada ya kufika mbali na eneo lile la tukio, akiwa ndani ya gari lake, ndipo John Bosho alimpigia simu Getruda, na kumjulisha kuwa alishamaliza kazi ya kumuua mchumba wake, Anita!

“Haloo…John…” Getruda akasema.

“Ndiyo Getu…” John Bosho naye akasema.

“Unasemaje?”

“Nakujulisha kwa mimi ndiyo nimetoka kummaliza Anita!”

“Umemuua?”

“Ndiyo!”

“Oh, Mungu wangu!”

“Ni kama nilivyokuwa nimepanga! Sasa nakuonya kwamba usije ukatoa siri hiyo! Hakuna aliyeona!”

“Oh, siwezi kusema…”

“Haya kwaheri!” John Bosho akasema na kukata simu!

Upande wa pili alipokuwa Getruda, alibaki ameing’ang’ania simu yake mkononi! Alikuwa amechanganyikiwa sana, yaani amemuua mchumba wake Anita?

Hakuamini!

*******

KELELE za kuomba msaada ndizo zilizowashtua majirani waliokuwa wanaishi katika nyumba nne zilizokuwa mle ndani ya uzio alipokuwa anaishi Anita, ambao walikuwa vyumbani mwao, pamoja na majirani wengine wanaozizunguka nyumba hizo zilizojengwa kwa mtindo wa kupendeza ndani ya uzio madhubuti.

Ni kelele ambazo Anita alipiga pale mwanzoni wakati John Bosho alipokuwa akimdhibiti kule ndani kwake, bafuni, katika kutaka kumtoa roho yake. Hakika ni kelele zilisikika kama mtu aliyekuwa anakoroma kwa kubanwa pumzi. Majirani walitoka vyumbani mwao haraka haraka, ndani ya zile nyumba nyingine ziliyokuwa jirani na anayoishi.

Majirani hao walikuwa pamoja na mama mwenye nyumba aliyopanga Anita, Bi. Debora Mjema, ambaye naye alikuwa anaishi humohumo katika moja ya nyumba hizo tano. Halafu wakaelekea ndani ya nyumba hiyo aliyopanga, iliyokuwa hatua chache, ambapo kelele zile zilitokea. Baada ya kufika pale nje, walikuta ule mlango mkubwa umefungwa kwa ndani bila komeo.

Haraka wakaufungua mlango ili kujua kilichokuwa kimemsibu mwanadada Anita, na kumfanya apige makelele ya kuomba msaada. Hatimaye majirani wawili walifanikiwa kuingia mle ndani ya bafu alilokuwa anaoga. Wote walikuwa ni wa wanaume, ambao baada ya kuingia walishangaa kuukuta mwili wa Anita ukiwa umelala sakafuni umetulia kimya, tena ukiwa uchi wa mnyama!

Mwili huo wa Anita uliokuwa bado umelala pale sakafuni, ulionyesha dalili zote kwamba alikuwa ameshakata roho muda mrefu! Michirizi ya damu ilionekana ikichuruzika kutoka mdomoni na puani, kiasi cha kuwafanya wale wanaume wawili watoke nje mbio, hadi walipofika sebuleni!

“Kuna nini jamani?” Mtu mmoja akauliza kati ya wale majirani.

“Mh, hatari!” Akajibu mmoja wa watu wawili waliotoka mle bafuni kuangalia!

“Hatari ya nini?”

“Tumemkuta Anita amelala sakafuni,” mtu mwingine akasema na kuongeza. “Tena yuko uchi!”

“Amefanya nini sasa?” Akaendelea kuuliza kijana mwingine aliyetaka kujua kilichojiri.

“Bila shaka amepata matatizo mazito!” Mwanaume huyo aliyetoka mle bafuni akasema.

“Jamani, akina mama ingieni mumvishe hata upande wa khanga!”

“Ooohpsi!” Akina mama wakapiga kelele baada ya kujua kuwa mambo yalikuwa yameshaharibika!

Mara baada ya kusema vile, akina mama wawili waliokuwa pale waliingia mle ndani ya bafu. Baada ya kuingia humo bafuni, waliukua mwili wa Anita ukiwa umelala uchi pale sakafuni. Haraka wakatoa upande a kitenge na kuufunika vizuri mwili huo, na hatimaye wakatoka mle bafuni na kujiunga na watu wengine, akiwemo mama mwenye nyumba, ambao walikaa na kutafakari cha kufanya.

Kwa vile mwili huo wa Anita haukuonyesha uhai wowote,  ndipo ilipojulikana kwamba alikuwa ameshakufa! Watu wengi walianza kukusanyika wakiwemo majirani na wapita njia waliofika kushuhudia tukio lile la kutisha jioni hiyo, kila mmoja akitokwa na machozi ya uchungu kwa kushindwa kuvumilia!

Vilionekana vikundi kadhaa vya watu waliokuwa wakiongea hili na lile. Hata hivyo hawakujua ni mtu gani aliyesababisha kifo hicho cha kutatanisha! Simu ya dharura ikapigwa na mmoja wa mashuhuda, ili kuwajulisha Jeshi la Polisi juu ya tukio hilo la kifo cha mwanadada, Anita Anthony.

*********   

NDANI ya Kituo cha Polisi Buguruni, Jijini Dar es Salaam, shughuli za kazi zilikuwa zinaendelea kama kawaida jioni hiyo. Hata hivyo, baada ya muda, simu ya matukio ya dharura ilipigwa na kupokelewa na askari polisi aliyekuwa zamu katika chumba maalum cha simu, ndani ya Ofisi  ya Idara ya Upelelezi.

Baada ya kupokelewa kwa simu hiyo iliyoelezea juu ya mauaji yaliyotokea eneo la Tabata Mawenzi jioni hiyo, kwa kuuawa kwa mwanamke ndani ya bafu, ilifanyiwa kazi haraka iwezekanavyo, kwa kujulisha katika sehemu zote zinahusika kwa kutumia redio za mawasiliano.

Mkuu wa zamu katika Kitengo cha Matukio siku hiyo, alikuwa ni Kachero Inspekta Malik Mkoba, ambaye alikuwepo ofisini muda huo wa saa kumi za jioni. Alikuwa na kazi ya kuyapitia mafaili kadhaa yaliyokuwa mezani mwake, hivyo akajulishwa taarifa hizo za kifo cha mwanadada, Anita, hivyo akaamua kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo, kama ilivyo kawaida katika kazi yake ya upelelezi.

Kachero Inspekta Malik Mkoba naye aliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Buguruni, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, ambapo alimpatia taarifa hiyo, na mkuu huyo akampangia kuianza kazi hiyo mara moja, ili kujua chanzo cha mauaji hayo. Ndipo alipotoka ofisini kwake, halafu akateua askari polisi wa Kikosi Maalum waliokuwa zamu.

Vilevile walikuwepo na wale wa Forensic Bureau Investigation, wakiwemo wataalam, wapiga picha kutoka Kitengo cha Matukio (Scene of  Crime), wakiwemo pia wataalamu wa alama za vidole na wengineo. Baada ya kuwa tayari, askari wote wakatoka na kupanda gari lao aina ya Toyota Land Cruiser, na kuelekea eneo la Tabata, Mawezi, yalipotokea mauaji yale ya aina yake.

Walikuwa ni askari polisi kumi na mbili, waliokuwa wanaongozwa na Kachero Inspekta Malik Mkoba, ambapo baada ya kufika eneo hilo la tukio,  gari lilisimamishwa nje ya nyumba hiyo, askari wakashuka na kuingia hadi sehemu ya uani, ndani ya nyumba aliyokuwa anaishi Anita. Baada ya kuingia ndani, wakaliendea bafu lile lililokuwa mle ndani, ambapo mwili huo ulikuwepo, umefunikwa shuka ili kuusitiri.

Kachero Inspekta Malik Mkoba na askari wawili waliingia mle bafuni na kuanza kuuchunguza kwa makini ule mwili. Wakaona kuwa haukuwa na jeraha lolote, ingawa ulianza kuvimba na kuwa na rangi nyeusi. Upande wa kushoto mwa mwili ule, palikuwa na bomba la sindano ya kudungia binadamu, likiwa nusu limezama ndani ya bahasha ndogo ya rangi nyeupe, iliyokuwa  imepigwa muhuri uliokuwa na maandishi yaliyosomeka ‘Kishada Medics.’

Kachero Inspekta Malik alipomaliza kuisoma ile bahasha, akaitumbukiza ile sindano pamoja na bomba lake, ambavyo vyote alivichunguza kwa muda. Kazi nyingine iliyobakia ilikuwa ni kuwaacha wataalamu wengine, kama mpiga picha, mchukua alama za vidole na mchora ramani kufanya kazi yao. Hakika kila mmoja alifanya kazi yake kwa utaalamu wa hali ya juu ili wasiweze kuharibu ushahidi.

Kachero Inspekta Malik Mkoba alipomaliza kufanya uchunguzi wake, akaandika baadhi ya mambo muhimu kwenye kitabu chake cha kumbukumbu. Alipomaliza kuandika, akawaamuru wale askari polisi alioongozana nao, waupakie ule mwili wa Anita ndani ya gari, na bila kupoteza muda wakaupakiza kwa kutumia machela, tayari kwa kuupeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

********

UMATI wa watu ulikuwa umejazana katika mtaa mdogo uliokuwa unaelekea katika eneo uzio wa nyumba aliyokuwa anaishi Anita. Jioni hiyo kunako majira ya saa kumi na moja kasorobo, watu hao walikuwa wameshuhudia mwili huo uliofunikwa  vitenge ukiondolewa ndani ya nyumba na Maafisa wa Jeshi la Polisi. Mwili huo ulikuwa umewekwa katika machela na kupakizwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser.

Kati ya watu waliokuwepo katika mkusanyiko ule uliofika kushuhudia mauaji ya mwanadada, Anita, alikuwepo kijana Don, ambaye alikuwa ni dereva wa bodaboda, aliyekuwa anamwendesha Anita wakati alipokuwa katika shughuli  ya mizunguko yake. Hakika alikuwa na huzuni kubwa kwa vile alikuwa ni mtu wake wa karibu, waliyekuwa wamezoeana.

“Duh, huwezi kuamini, yaani mwanadada yule ndiyo amekufa?” Mwananchi mmoja akasema kwa masikitiko makubwa kwa jinsi alivyokuwa anamfahamu Anita!

“Ndiyo, amekufa bwana…” mtu mwingine akadakia.

“Sijui ni nani aliyemuua?” Kijana mwingine akasema huku akivuta hisia zake juu ya mwanadada huyo mrembo, aliyekuwa anavutia mbele ya macho ya watu.

“Ni kitu cha kushangaza kwa vile muda siyo mrefu nilimwona akipita hapa…”

“Aisee, sijui amewakosea nini dada wa watu?”

“Hivi huyu si anamshikaji wake, yule anayeendesha Harrier?”

“Ndiyo, huwa anakuja nayo mara kwa mara. Ndiye aliyempangishia nyumba…”

“Hapana…mauaji haya yana sababu…” Don alisema.

“Sababu gani?”

“Unajua Anita alikuwa na bifu na mchumba wake, John Bosho?”

“Ugomvi gani tena?”

“John alikuwa anamchukua rafiki yake Anita, na kumfanya mpenzi wake!”

“Una uhakika?”

“Ndiyo, nina uhakika na yeye ndiye aliyeniambia…”

“Basi, inawezekana John andiye aliyemuua?”

“Inawezekana ndiye.”

“Utakubali kuwa ushahidi mshikaji?”

“Sasa ushahidi kwa kitu nisichokuwa na ushahidi nacho?”

“Hapo ndiyo tatizo…”

Hatimaye vijana hao walimaliza maongezi yao na kuanza kuendelea kubaki katika eneo hilo, lakini kwa Don, alijua kuwa lazima John Bosho ndiye aliyehusika na mauaji ya mchumba wake, Anita. Hata hivyo, mara baada ya gari lile lililouchukua mwili wa marehemu kuondoka, umati wa watu wote ukatawanyika!

********

NYUMBA moja iliyojengwa mjengo wa kisasa, ilionekana  katika hali ya utulivu wa hali ya juu katika eneo hilo la Kiwalani, jijini Dar es Salaam. Nyumba hiyo iliyokuwa imezungukwa na uzio wa marofali na mbele kukiwa na geti kubwa jeusi, ilikuwani inamilikiwa na mzee Anthony Mkonyi, baba yake mzazi na Anita.

Kunako majira ya saa kumi na moja za jioni, mzee Anthony Mkonyi, ndiyo kwanza alikuwa ametokea kwenye mihangaiko yake ya kibiashara katika maeneo mbalimbali. Baada ya kuliingiza gari lake aina ya Toyota Prado, ndani ya uzio, akalipaki sehemu ya maegesho. Halafu akashuka na kuingia ndani ya nyumba yake kwa mwendo wa taratibu.

Wakati huo mke wake, Bi. Matilda alikuwepo akishughulika na kazi ndogondogo za kufanya usafi katika mabanda ya kuku yaliyokuwa nyuma ya nyumba yao. Lakini mzee Anthony hakuwa na shida naye, bali alielekea katika chumba maalum cha mapumziko, ili kuipumzisha akili yake kutokana na mihangaiko ya mchana kutwa. Lakini wakati akielekea chumbani kule, mara simu ya mkononi iliita, akaichukua na kuisikiliza.

“Haloo…” mzee Anthony akasema.

“Haloo…Kituo cha Polisi Buguruni hapa…” upande wa pili wa simu ukasema, ikiwa ni simu inayotokea katika Kituo cha Polisi!

“Unasema kituo cha polisi?” Mzee Anthony akauliza huku akikunja sura yake!

“Ndiyo, hapa ni kwenye kituo cha polisi…” sauti hiyo ikasisitiza!

“Ndiyo, niwasaidie tafadhali…” mzee Anthony akasema huku mawazo yake yakiwa yameshatibuka! Mambo ya polisi tena?

“Natumaini wewe ni mzazi wa Anita Anthony Mkonyi…”

“Ndiyo, mimi ndiye mzazi wake…”

“Basi, nakuomba ukaze moyo…”

“Nikaze moyo? Sjakuelewa…”

“Ndiyo, mzee…” sauti ile ikasema na kuendelea. “Kuna taarifa siyo nzuri. Mwanao Anita amepata matatizo…

“Matatizo gani tena?”

“Ameshambuliwa na mtu asiyefahamika huko nyumbani kwake, Tabata Mawenzi. Hivi sasa amepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili…”

“Hali yake ikoje?”

“Ukweli ni kwamba hali ni mbaya…unatakiwa ukamwone!”

“Oh, ahsante kwa taarifa, nitaenda huko Muhimbili…”

“Sawa, pole sana…”

Baada ya kupewa taarifa ile. Mzee Anthony alichanganyikiwa sana baada ya kuambiwa kwamba binti yake ameshambuliwa na mtu asiyejulikana? Je, meshambuliwa kwa sababu gani? Na mpaka muda ule hali yake ilikuwa inaendeleaje huko hospitali alikopelekwa? Hapana, lazima aende haraka sana ili ajue kinachoendelea. Hivyo basi, hakupoteza muda, alitoka mle chumbani na kuelekea kule uani alipokuwa mke wake, Bi. Matilda, akisafisha banda la kuku.

“Mama Anita,” mzee Anthony akamwita.

“Bee,” Bi. Matilda akaitikia huku akiacha kusafisha banda la kuku.

“Hebu njoo kidogo…” mzee Anthony akasema kwa sauti ya unyonge.

“Sawa, baba…” Bi. Matilda akamwendea taratibu. Akamwona jinsi mume wake alivyohamanika na kuchanganyikiwa, kitu ambacho kilimfanya naye atake kujua kulikoni!

“Mbona hivyo baba Anita?” Bi. Matilda akamuuliza huku ameshika kiuono chake!

“Nimepigiwa simu kutoka polisi, kuwa mtoto wetu, Anita ameshambuliwa na mtu asiyejulikana!” Mzee Anthony akamwambia mkewe.

“Unasema Anita meshambuliwa?” Bi. Matilda akamuuliza!

“Ndiyo, polisi wanasema kuwa hali yake mbaya, yuko Hospitali ya Muhimbili!”

“Unasema kweli?”

“Ndiyo, ni kweli…” mzee Anthony akasema na kuongeza. “Hatuna muda wa kupoteza, twende huko Muhimbili tukamwangalie!”

“Ni sawa, oh, mwanangu…” Bi. Matilada akasema huku akiweweseka!

Mzee Anthony na mkewe, Bi. Matilda waliingia ndani na kuvalia harakahara nguo, halafu wakatoka nje na kuliendea gari lao, Toyota Pradao na kupanda. Geti likafunguliwa na mtumishi wa hapo, na mzee Anthony akaliondoa kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Waliamua kwenda kushuhudia kuumia kwa mtoto wao, na wala hawakujua kama alikuwa ameshakufa muda mrefu.

        ********

FOLENI ilikuwa kubwa, hata hivyo ya magari hatimaye wakafika katika Hospitalini ya Taifa ya Muhimbili, na mzee Anthony akalipaki gari katika sehemu ya maegesho, palipokuwa na magari mengine yamepaki hapo. Wakashuka na kuelekea moja kwa moja sehemu ya mapokezi, wanapopokelewa majeruhi wa wanaopata ajali katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es salaam. Hapo palikuwa na wahudumu kadhaa, wakaulizia juu ya Anita.

Kwa bahati nzuri baada mzee Anthony kufika hapo mapokezi, pia alikuwepo, Kachero Inspekta Malik Mkoba,  ambaye alikuwa akiushughulikia na mwili wa marehemu Anita mara baada ya kuufikisha hapo, kutokea kule Tabata. Na muda huo mwili huo ulikuwa umeshapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, baada ya kuthibitishwa na daktari kuwa ameshakufa!

“Habari za kazi kijana,” mzee Anthony akamsalimia Kachero Inspekta Malik Mkoba.

“Nzuri, mzee,” Kachero Inspekta Malik akaitikia huku akimwangalia.

“Mimi ni mzazi wa Anita…” mzee Anthony akasema na kuendelea. “Nimeambiwa kuwa mtoto wangu ameletwa hapa hospitali baada ya kushambuliwa na mtu asiyefehamika…”

“Oh, pole sana mzee wangu…” Kachero Inspekta Malik akamwambia kwa huzuni huku akimvuta pambeni ili mke wake asiweze kusikia atakachomweleza.

Baada ya kufika kando kidogo, ndipo alipomalizia kwa kusema, “Wewe ni mzee wetu, na mtu mzima, hivyo haina budi kujikaza kiume!”

“Ndiyo, kijana, hebu nieleze kitu nikuelewe…” mzee Anthony akamwambia baada ya kuona kama alikuwa anazungushwa!

“Ni kweli, tumemletwa hapa hospitali muda siyo mrefu, akitokea nyumbani kwake, Tabata Mawenzi, lakini tunasikitika kwamba amefariki dunia!”

“Unasema binti yangu amefariki?” Mzee Anthony akamuuliza kwa hamaki!

“Ndiyo, mzee, jikaze kiume. Ameshambuliwa na mtu asiyefahamika majira ya saa tisa za alasiri na hapa ndiyo nataka kuwasiliana na daktari juu ya kuufanyia uchunguzi huo mwili wake…”

“Oh, Mungu wangu!” Mzee Anthony akasema huku ameshika kichwa chake.

“Jikaze mzee…” Kachero Inspekita Malik Mkoba akamwambia huku akimshika.

“Aisee…oh! Naweza kuuona mwili wake?””Mzee Anthony akauliza.

“Ndiyo, mzee…unaweza kuuona…”

Wakati huo, mke wake, Bi. Matilda alikuwa amekaa upande wa nje, mbali kidogo na walipokuwa wao. Hivyo basi, asimshtue,  mzee Anthony na Kachero Inspekta Malik walikwenda kuuangalia mwili ule uliokuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, na kumwacha amekaa hapo kwenye benchi upande huo wa mapokezi. Hivyo hakujua kuwa walikuwa wameelekea kwenye chumba cha kuhifadhia maiti, ambacho kiko mbali bna pale.

Baada ya kufika kwenye chumba hicho, walionana na Daktari Kenedy Mushumbuzi, ambaye ndiye aliyetakiwa kuufanyia uchunguzi mwili huo. Mwili wa marehemu Anita, ulitegemewa kufanywa  uchunguzi jioni ile ile na majibu yake kutolewa kesho yake asubuhi.  Kachero Inspekta Malik na Mzee Anthony waliingia ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti, ambapo walifunguliwa droo moja na mhudumu wa hapo, na kuuona huo mwili wa marehemu Anita, na kuhakikisha kuwa ni kweli alikuwa ni mtoto wake wa kumzaa, Anita. Ndipo mzee huyo alipovumilia kama mwanaume, na kupanga cha kumweleza mke wake baada ya kutoka hapo hospitali.

Kachero Inspekta Malik alielekea ndani ya chumba cha Daktari Kenedy Mushumbuzi, mara baada ya kuachana na mzee Anthony, ambaye kwa muda huo alikuwa ameshachanganyikiwa baada ya kujua kuwa ni kweli binti  yake alikuwa amekufa. Alipoingia ofisini kwake,wakaongea mawili matatu juu ya uchunguzi wa maiti huyo, na baada ya kukubaliana, walipanga kwamba aende kuyachukua majibu hayo kesho yake asubuhi.

Mzee Anthony alipotoka hapo, alikwenda kuonana na mke wake, Bi. Matilda, ambaye alikuwa amemwacha kule mapokezi. Alimwendea kwa unyonge mkubwa kiasi kwamba alishtuka na kumuuliza:

“Vipi baba Anita, umepata taarifa gani?”

“Acha tu…” mzee Anthon akamjibu hivyo.

“Niache nini sasa? Hali ya Anita ikoje?”

“Hebu njoo huku tuongee…” mzee Anthony akamwita kando.

Mzee Anthony na mke wake, Bi. Matilda, walikwenda kusimama kando. Wakati wote huo, Bi. Matilda bado alikuwa na wasiwasi mkubwa sana, kwani alikuwa hajajua hali ya mtoto wake, Anita, inaendeleaje.

“Vipi baba Anita, mbona tumekuja huku sehemu ya mapokezi, kwa nini tusiulize kama yuko wodini?” Bi. Matilda akaendelea kumuuliza.

“Turudi nyumbani…” mzee Anthony akamwambia.

“Kwa nini turudi nyumbani bila kujua hali ya Anita?”

“Ndiyo maana nakwambia turudi,” mzee Anthony akamwambia na kuongeza. “Hali ya Anita ni mbaya sana!”

“Kama ni mbaya, nataka kumwona, kwani yuko chumba cha wagonjwa mahututi!”

“Ndiyo manaake, huwezi kumwona, turudi nyumbani kwanza!” Mzee Anthony akamdanganya, kwani aliona akimwambia ukweli kuwa alikuwa amekufa, angeanza kupiga makelele hasa ukizingatia alikuwa anampenda sana mtoto wake huyo wa kike.

Bi. Matilda hakufanya ubishi, alikubaliana naye bila kumwona mwanawe, hivyo wakaondoka pale katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kurudi nyumbani, Kiwalani, huku wakiwa na huzuni kubwa sana!

********      

GETRUDA alizipata rasmi habari za kifo cha Anita baada ya John Bosho kumpigia mara alipotoka kumuua, nyumbani kwake, Tabata Mawenzi. Hata hivyo, kunako majira ya saa mbili za usiku,  alipigiwa tena simu na ndugu za Anita, kumjulisha juu ya kifo hicho, hasa ukizingatia wale walikuwa ni marafiki waliokuwa wamezoeana.

Hata hivyo, familia hiyo hawakujua kama watu hao wawili walikuwa na mgogoro mkubwa baada baada ya kuchangia mwanaume mmoja, ukizingatia ilikuwa ni siri yao kubwa. Baada ya kupata taarifa hiyo ya pili, ambayo ilimpa nguvu kidogo, Getruda akajiandaa kuelekea huko msibani, ambapo alichukua mkoba wake, ambao aliweka nguo chache kama khanga na vitenge, kisha akaaga majirani zake na kuondoka hapo nyumbani kwake, Ilala, mtaa wa Moshi.

Getruda akapanda teksi, ambayo ilimpeleka mpaka Kiwalani, nyumbani kwa wazazi wa marehemu Anita. Mara baada ya kufika eneo hilo la Kiwalani, Getruda akamwambia dereva amshushie mbali kidogo na ilipo nyumba ya wazazi wa Marehemu Anita. Na ile ilisababishwa na msongamano wa nyumba zilizojengwa bila mpangilio au kufuata ramani za jiji.

Eneo lile halikuwa na mitaa iliyowezesha kufika hadi katika nyumba husika. Getruda akashuka katika barabara ya lami iliyokuwa inaelekea maeneo mengine, halafu akamlipa dereva wa teksi. Kisha akaanza kuangalia pande zote na kuona kila mpita njia alikuwa na shughuli zake na wengine wakiwahi kurudi majumbani baada ya kutoka kwenye mihangaiko ya kazi.

Getruda akaupachika mkoba wake begeni na kuanza kuelekea nyumbani , katika sehemu ile yenye msiba kwa mwendo wa taratibu, wakati huo giza lilishaanza kuingia. Mwili wake ulikuwa mzito, akili imechoka kutokana na kile kifo cha rafiki yake, Anita. Akaendelea kuufuata mtaa ule mdogo na kutokeza pale nyumbani ambapo kwa wakati ule palikuwa pamejaa watu wengi waliofika kwa ajili ya kuwapa pole wafiwa.

Vilio vya watu waliokuwa wanalia viliweza kusikika, hadi Getruda alipofika na kukaribishwa na watu maalum waliokuwa wamepangwa kwa ajili ya kazi hiyo. Alikaribishwa na kuelekea upande wa wanawake, ambao walikaa sehemu ya ndani. Baada ya kuingia ndani, akakaa kwenye jamvi kubwa lililokuwa limetandikwa ndani ya sebule kubwa, ambayo kwa wakati ule samani zote zilikuwa zimeondolewa.

Muda wote ule Getruda alikuwa analia kilio cha uchungu, hasa ukizingatia msiba huo ulikuwa unamhusu sana, kwa vile aliyekufa alikuwa rafiki yake, aliyemfananisha na ndugu waliozaliwa tumbo moja. Mbali na hayo, pia mara nyingi walikuwa wakiwatembelea pale nyumbani kuwasalimia wazazi wake, wakiwa wameongozana wote. Sasa mwenzake, Anita ameshakufa!

Ukweli ni kwamba tukio hilo lilimfanya uchungu uzidi kumwandama moyoni mwake, akalia kwa majuto mpaka machozi yakamkauka. Baada ya kulia vya kutosha, ndipo Getruda aliponyanyuka na kuelekea upande wa pili aliokuwa amekaa mama yake mzazi na marehemu Anita, Bi. Matilda, ambaye alionekana kuwa na huzuni kubwa.

Kwa muda ule Bi. Matilda alikuwa amejitanda khanga, na alipomwona Getruda, ndipo uchungu ulivyomzidi! Akaanza kulia tena wakiungana na Getruda, wakiwa wamekumbatiana. Walipotosheka kulia, ndipo Getruda alipomwambia kwa sauti ndogo:

“Oh, mama, pole sana…”

“Oh, ahsante mwanangu, pole na wewe…Anita ametutoka na sasa hivi amelala ‘Mochwari.’Ametutoka kama mchezo…oh!” Bi. Matilda akasema kwa uchungu mwingi!

“Pole sana mama…tuwe wavumilivu katika wakati huu mgumu…” Getruda akaendelea kusema.

“Ni kweli mwanangu…lakini kinachoniuma ni kwamba Anita hakuugua…ameuawa…ni kwa nini?” Bi. Matilda akaendelea kusema.

“Hilo ndiyo la kujiuliza. Ni kwa nini ameuawa? Na muuaji alikuwa na lengo gani?…Lakini kazi yote tutawaachia Jeshi loa Polisi, ambao wataujua ukweli na muuji atapatikana…” Getruida akaendelea kumfariji Bi. Matida, huku nafsi yake ikimsuta ukizingatia yeye alikuwa anajua chanzo cha kifo cha Anita, muuaji alikuwa ni John Bosho, na pia akiwa ndiye mchangiaji mkuu!

“Sawa, mwanangu…tutawaachia polisi…” Bi. Matilda akamaliza kusema, halafu akabaki akiendelea kuwaza na pengine akilia. Kamwe hakuna mtu asiyejua uchungu wa mwana, hasa kwa upande wake, ambapo alikuwa ni mtoto wake wa pekee wa kike, ukiacha kaka zake wawili wa kiume!

Baada ya kumaliza maongezi na kupeana pole, Getruda akaondoka na kwenda kujumuika na waombolezaji wengine, ambao walikuwa wakiongea hili na lile, kila mmoja akisema lake juu ya kifo cha Anita, ili saa zilikuwa zinakwenda.Hata hivyo baada ya muda, simu ya Getruda iliyokuwa kibindoni, ambayo hata hivyo alikuwa ameiondoa mlio, iliita kwa kumtetemesha. Akaichukua na kuangalia namba za mpigaji.

Ni John Bosho!

Getruda hakupenda kuisikilizia simu ile pale mbele ya watu wengi, hivyo akanyanyuka taratibu na kutoka nje. Akaenda kuisikilizia mbali kwa kuhofia mtu kuwasikiliza mazungumzo yao ambayo kwa vyovyote yangekuwa nyeti!

      ********

USIKU huo, John Bosho alikuwa amekaa upande wan je palipokuwa na bustani. Alikuwa anakunywa pombe kali aina ya Jack Daniels, iliyokuwa juu ya meza ndogo mbele yake. Pia, juu ua meza hiyo, palikuwa na glasi ndefu iliyokuwa na pombe nusu. Taa ya nje ilikuwa inawaka mwanga mkali uliomfanya aone kila kitu kilichopo hapo mbele ya nyumba yake ya kifahari.

Ukweli ni kwamba pamoja na kumuua Anita, lakini nafsi yake ilikuwa inamsuta John, na hofu ikimjia, akiwazia juu ya askari polisi wa upelelezi, ambao mara nyingi hufanya kazi zao kitaalam zaidi  za kumkamata muuaji! Hata hivyo, wakati akiwa katika mawazo hayo, ndipo alioamua kumpigia simu Getruda ili amuulizie yuko wapi!

“Haloo…John…” upande wa pili Getruda akaipokea kwa sauti ndogo.

“Uko wapi?”  John Bosho akamuuliza.

“Niko msibani…nyumbani kwa wazazi wa Anita, Kiwalani…”

“Oh, umeshafika huko?”

“Ndiyo, kwani wewe huji huku msibani?”

“Hapana…siji huko…”

“Kwa nini?”

“Nimuue mimi mwenyewe halafu nije?”

“Ndiyo, lazima uje. Hujui watakutilia mashaka?”

“Watahisi ni mimi niliyemuua?”

“Ndiyo manaake…”

“Kwani ugomvi wetu walikuwa wanaujua? Anita alikuwa msiri sana. Ugomvi wetu ni yeye, mimi na wewe tu, basi! Hivyo ni siri!”

“Kwa hiyo huji?”

“Mimi siji, na nimeaga kuwa nimesafiri…”

“Mama yangu!”

“Cha muhimu nakusisitiza!” Akaendelea kusema John Bosho. “Usimwambie mtu yeyote, tafadhali tunza siri! La sivyo sikwambii kitakachofuata!”

“Simwambii mtu!” Getruda akasema huku akiwa na wasiwasi mwingi!

“Ok, fanya hivyo…kwaheri!” John Bosho akamaliza kusema na kukata simu!

Baada ya kukata simu, upande wa pili Getruda alibaki amechanganyikiwa. Aliona jinsi John Bosho alivyokuwa anaendelea kumwandama na yeye hata baada ya kumuua rafiki yake Anita. Ukweli ni kwamba aliona hatari iliyokuwa inamkabili, kwani alijua John angemdhuru kweli kama angeitoa ile siri kwa mtu yeyote!

Sasa afanyeje?

Ukweli ni kwamba Getruda hakuwa na la kufanya zaidi ya kuutia mdomo wake kufuli! Na mara baada ya kumaliza kuongea na John, akajiondoa  na kurudi kuungana na waombolezaji wengine. Akajumuika nao katika maombolezo huku nafsi yake ikimsuta ukizingatia mkasa mzima alikuwa anauelewa.Na yeye alikuwa mhusika mkuu!

Baada ya kumaliza kuongea na Getruda, John Bosho alibaki akiiangalia ile simu yake. Halafu akaiweka juu ya meza na kujiegemeza kwenye kiti cha mbao kilichokuwa nje ya nyumba yake sehemu hiyo ya kibarazani, karibu na bustani. Alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu huku akitafakari juu ya mauaji yale ya mchumba wake, Anita aliyoyafanya.

John Bosho alikumbuka kuwa wakati akitekeleza mauaji yale kule ndani ya bafu la kuogea, hakuweza kuacha alama zozote za vidole, ambazo hutumika kama ushahidi, zaidi ya lile bomba la sindano na bahasha aliyonunua. Hata hivyo, hakuridhika na lile bomba la sindano aliloliacha mle bafuni, kwani lingemletea matatizo hasa wakifuatilia katika duka alilonunua  katika duka la dawa, pale Aroma, Tabata. Sasa afanyeje? Hakuwa na la kufanya zaidi ya kujifariji!

Hata hivyo, John Bosho aliendelea kunywa pombe kwa wingi huku akiangaza macho yake pande zote za himaya ya nyumba yake ile ya kifahari, ambayo kwa muda ule ilikuwa imepooza. Mle ndani ya nyumba hiyo, walikuwa wao wawili tu, yeye pamoja na mlinzi wake mmoja wa jamii ya Kimasai, ambaye kwa muda ule alikuwa akizunguka eneo zima ili kujionyesha kwa bosi wake, kuwa alikuwa anawajibika kikazi.

Pia, mlinzi huyo alikuwa akimvizia John Bosho ampe angalau pombe kidogo anywe, kitu ambacho alikuwa anafanya mara kwa mara anapokuwa amefurahi. Lakini kwa siku ile, hakuwa na furaha yoyote, alikuwa na huzuni kubwa, hivyo hakuwa na muda wa kuchangamkiana na huyo mlinzi, ambaye muda huo alikuwa amejitanda lubega lake la rangi nyekundu. Kwanza kabisa, alikuwa anawaza sana juu yake, kama anaweza kupambana na maswali ya kipolisi endapo wangefika kumhoji baada ya kumshtukia.

Wasiwasi ulimpata John kiasi kwamba alipanga kuwa ni lazima ambadilishe haraka sana mlinzi huyo wa kimasai na kumweka mlinzi wa kampuni ya binafsi aliyepitia mafunzo ya ulinzi. Alipanga kuwa kesho yake tu, atawasiliana na kampuni moja ya ulinzi, iliyoko katika eneo la Ukonga Banana, ambayo itampatia mlinzi wa kulinda hapo kwa mkataba maalum

Baada ya kuona hapewi chochote na tajiri yake, yule mlinzi aliondoka eneo hilo na kuhamia sehemu nyingine ya lindo lake. Akamwacha John Bosho akiendelea kunywa pombe ile taratibu hadi alipokuwa chakari, akajilaza palepale nje, kwenye kibaraza sehemu iliyokuwa na upepo mwanana. Hatimaye alikuja kushtuka kwenye majira ya saa nane za usiku, ndipo alipojikokota na kuingia ndani kulala!

********

MAJIRA ya saa nne na nusu za asubuhi, ilimkuta  Kachero Inspekta Malik Mkoba akiwa barabarani, kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ili kupata taarifa ya Daktari Kenedy Mushumbuzi, aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, Anita, jana yake mara baada ya kufikishwa hapo.

Mwili huo ulitakiwa ufanyiwe uchunguzu haraka ili ibainike ni kitu gani kilichomdhuru, au kama ni sumu, je, ni sumu ya aina gani iliyosababisha kifo chake. Huo ni utaratibu wa kawaida kabisa wa kipolisi, kabla ya mwili huo kukabidhiwa kwa familia yake tayari kwa maziko.

Kachero Inspekta Malik Mkoba aliamua kutumia gari lake la binafsi, aina ya Nissan Laurel, kutokana na uhaba wa magari ya polisi hasa wakati wa dharura kama zile, ambazo huwa zinatokea katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam. Asubuhi hiyo alikuwa amevalia nadhifu, suti yake ya rangi nyeusi, shati jeupe na tai ya rangi nyekundu liyochanganyika na bluu. Hakika alipendeza sana na kuonekana ni kijana anayejipenda.

Ingawa magari yalikuwa ni mengi barabarani na yaliyosababisha foleni kubwa, Kachero Inspekta Malik Mkoba alifanikiwa kufika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, halafu akalipaki katika sehemu ya maegesho. Kisha akashuka na kuelekea ndani ofisi, iliyoko jirani chumba cha uchunguzi wa maiti, ambapo alimkuta daktari yule aliyeufanyia uchunguzi mwili wa mwanadada, Anita. Alikuwa ni Dokta Kenedy Mushumbuzi, ambaye ni mtaalam na maalum kwa kazi  zile za uchunguzi wa maiti zilizokuwa na utata, zinazohusiana na Jeshi la Polisi.

Muda ule Daktari Kenedy Mushumbuzi alikuwa ndani ya ofisi yake nadhifu na safi, amekaa kwenye kiti cha mzunguko, nyuma ya meza yake akiandika taarifa fulani hivi. Wakiwa ni watu wanaofahamiana sana katika shughuli zao za kikazi, daktari huyo alimkaribisha Kachero Inspekta Malik Mkoba kwa ukarimu.

“Karibu Inspekta Malik…”

“Ahsante sana Dokta Mushumbuzi…” Kachero Inspekta Malik akasema huku akikaa kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake.

“Natumaini umekuja kupata taarifa za uchunguzi wa mwili wa marehemu, Anita ulioletwa hapa jana jioni…” Daktari Kenedy Mushumbuzi akamwambia huku akiirekebisha miwani yake mieupe.

“Ndiyo, Dokta, nimeifuata ripoti hiyo. Si unajua tena kazi zetu, nataka kuanza upelelezi mara moja!” Kachero Inspekta Malik akasema.

“Hakuna tatizo,” Daktari Kenedy Mushumbuzi akasema. Halafu akalifungua kabati moja na kutoa faili ambalo aliliweka pale mezani na kulifungua. Akaendelea kusema, “Nimeufanyia uchunguzi mwili ule na kugundua marehemu amekufa baada ya kudungwa sindano iliyokuwa na sumu kali sana, ambayo ina uwezo wa kuua haraka sana kwa kusimamisha mapigo ya moyo…” Daktari Mushumbuzi akanyamaza kidogo huku akimwonyesha Inspekta Malik ile taarifa.

“…Sumu hiyo ilifanya damu igande na kusababisha mapigo ya moyo yasimame. Hivyo basi, kutokana na hali hiyo, ndiyo maana mwili wa marehemu umevimba sana kiasi cha kubadilika rangi na kuwa mweusi. Pia, nimegundua kuwa marehemu alibakwa kabla ya kuchomwa ile sindano ya sumu; kwa sababu katika sehemu zake za siri kumekutwa mbegu za kiume. Nafikiri umenipata vizuri Inspekta Malik, kwa taarifa hii!”

“Nimekuelewa vizuri Dokta. Tunashukuru sana kwa ushirikiano, ambao utatusaidia katika upelelezi wetu,” Kachero Inspekta Malik akasema.

“Basi, huo ndiyo uchunguzi nilioufanya. Hivyo mwili wa marehemu unaweza kuchukuliwa na ndugu zake kwa ajili ya maziko. Pia, taarifa zote za uchunguzi wa kifo chake watazipata…” Daktari Fabian Mushumbuzi akaendelea kusema huku akichambua makaratasi yenye taarifa ile.

Baada ya Kachero Inspekta Malik kupata taarifa zile za kifo cha Anita, akamuaga Daktari Mushumbuzi na kuondoka, huku akisindikizwa naye hadi nje ya ofisi yake ambapo walipeana mikono na kuagana. Malik akaliendea gari lake na kupanda, halafu akaliotoka eneo lile la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kuelekea ofisini. Muda wote alikuwa na mawazo juu ya yule mtu aliyefanya mauaji yale ambapo kwa muda ule alikuwa hajamgundua kama ni mtu hatari, John Bosho!

Vilevile Kachero Inspekta Malik alijiuliza kwamba muuaji yule alipitia wapi na kufanya mauaji yale ya kinyama na hatimaye kumbaka marehemu Anita mle mle! Na pia alitoka vipi wakati wapangaji wa nyumba ile waliwahi kutoka nje baada ya kusikia makelele yale ya kuomba msaada na kwenda kusimama karibu na mlango wa bafu, ambao nao ulikuwa haujafungwa kwa ndani! Kwa vyovyote alijua ni mtu hatari sana!

Hatimaye Kachero Inspekta Malik alifika kituoni na kuingia ofisini kwake. Baada ya kukaa, kitu cha kwanza kukumbuka, ni ile bahasha ndogo aliyoikuta ndani ya bafu, ambapo ndani yake palikuwa na lile bomba la sindano. Jana yake aliiweka ndani ya droo yake mara baada ya kurudi kutoka Tabata lilipotokea tukio lile la mauaji, hivyo akaifungua droo na kuitoa ile bahasha ambayo alianza kuikagua kwa makini na kuiona ilikuwa ya kawaida tu, iliyokuwa na maandishi ya muhuri yaliyosomeka ‘Kishada Medics.’

Baada ya kumaliza kuisoma, akairudisha ndani ya droo, ikiwa na lile bomba la sindano ndani yake. Kachero Inspekta Malik akaona kuwa lilikuwa ni jambo la busara kuuanza upelelezi wake katika lile duka la dawa, lililokuwa eneo la Tabata Aroma. Ni duka lililokuwa linauza madawa baridi ya binadamu, ambalo linajulikana sana, ukizingatia liko sehemu ya wazi tu. Kwa vyovyote ilionekana kwamba muuaji yule alikuwa amenunua lile bomba la sindano kwenye duka lile wakati alipokuwa anakwenda kutenda unyama dhidi ya mwanadada Anita!

Hata hivyo, Kachero Inspekta Malik aliendelea na kazi nyingine zilizokuwa zinamkabili, kiwa ni pamoja na kuyashughulikia mafaili kadhaa ya makosa mbalimbali. Wakati akiendelea na kazi, pia, alipanga kuwa ni lazima ahudhurie mazishi ya marehemu Anita, yaliyotegemea kufanyika kesho yake jioni, nyumbani kwao, Kiwalani. Kwa vyovyote alijua kwamba asingekosa kupata mambo mawili matatu yatakayoweza kumsaidia katika upelelezi wake, kwani kifo kile kilikuwa na utata mkubwa uliokuwa umemweka njiani panda!.

********          

SHUGHULI za mazishi zilikamilika, ambapo marehemu Anita alizikwa siku ya tatu yake jioni, katika makaburi ya Kiwalani, na maziko hayo yaliyohudhuriwa na watu wengi, wakiwa ni wakazi wa Kiwalani, ndugu jamaa na marafiki, pia akiwemo rafiki yake, Getruda. Huzuni ilitawala kote kutokana na kifo kile cha kutatanisha kilichowaacha watu njia panda bila kujua muuaji ni nani.

Vilevile walikuwepo ndugu, jamaa na marafiki, bila kukosa Kachero Inspekta Malik Mkoba. Yeye alihudhuria pale bila mtu yeyote kumshtukia katika eneo la msiba, kwani alijaribu kuvalia mavazi yaliyombadili kidogo, na kuonekana ni mmoja wa watu wanaohusika na msiba huo kwa namna moja ama nyingine.

Lakini cha kushangaza ni kwamba mtu aliyekuwa mchumba wake, John Bosho, hakuhudhuria katika msiba ule ingawa ulimhusu sana, ukizingatia marehemu Anita alikuwa mchumba wake walioahidiana kuoana. Baada ya kumaliza kuzika, watu wakatawanyika na kubaki baadhi ya ndugu, na muda wote kachero Inspekta Malik alikuwa akijiuliza juu ya kutomwona, ingawa alikuwa ametajwa kwenye risala iliyosomwa pale makaburini.

Baada ya kumalizika kwa mazishi hayo ya mwanadada, Anita Anthony, wazazi wake waliamua kukaa kikao cha faragha hapo nyumbani kwao, Kiwalani, ambapo walikuwa wanajadili juu ya John Bosho, mchumba wa Anita kutokufika kwenye msiba mara baada ya yeye kuuawa na mtu asiyejulikana. Kamwe haikuwaingia akilini kuwa, kuwa, mtu aliyekuwa ameshajitambulisha na anatambulika na familia nzima, halafu asifike kwenye msiba kwa kusema eti amesafiri? Hiyo inaingia akilini kweli?

“Hivi mke wangu, unafikiria nini juu ya John Bosho, aliyekuwa mchumba wa marehemu mwanetu, Anita?” Mzee Anthony alimuuliza mkewe, Bi. Matilda.

“Hata mimi nashangaa, sijui inakuwaje mchumba wake amekufa halafu yeye haonekani katika msiba, mpaka anazikwa?” Bi. Matilda akasema huku akitikisa kichwa chake!

“Tokea msiba umetokea, nimejaribu kumpigia simu, lakini hapatikani. Na mara ya mwisho nilimpata lakini akasema kuwa yuko safarini nje ya jiji la Dar es Salaam…” Mzee Anthony akasema huku amechukia.

“Hivi inawezekana mtu afiwe na mchumba wake lakini ashindwe kufika kwa ajili ya safari? Si anahairisha na kurudi haraka? Safari ina umuhimu kuliko maisha ya binadamu kweli?”Bi. Matilda akaongeza kusema.

“Hata mimi sipati jibu,” mzee Anthony akasema kinyonge.

“Jambo la muhimu ni kuwasiliana na Jeshi la Polisi, kwani inawezekana akawa ni mtuhumiwa namba moja,” Bi. Matilda akasema na kuongeza. “Ni kweli kabisa, mimi ninawasiwasi na mwanaume huyo, kamtoa kafara mwanetu ili aimarishe utajiri wake!”

“Itabidi tufanye hivyo, mpigie simu aje hapa nyumbani.”

Mzee Anthony alimpigia simu Kachero Inspekta Malik Mkoba, na kumwomba wakutane katika kujadili suala lile. Malik ambaye ndiye mpelelezi wa suala lile, hakukawia kufika mara moja pale nyumbani, Kiwalani. Baada ya kufika alikaribishwa vizuri, ambapo walitafuta sehemu nzuri na kuanza kuongea kwa kina.

“Ndiyo mzee wangu, nimeitikia wito wako…” Kachero Inspekta Malik akasema.

“Nimekuita Inspekta, juu ya kifo hiki cha mwanangu, Anita, unajua kina utata kidogo….” mzee Anthony akasema.

“Ndiyo, ni kifo chenye utata, ndio maana tunataka tumjue muuaji!” Kachero Inspekta Malik alimwambia.

“Lakini kuna kitu kimoja kinanishangaza. Kuna huyu mtu anayejiita mchumba wake, ambapo tokea mwanangu amefariki na kuzikwa, hajafika hapa nyumbani…”

“Ni kwa nini hajafika msibani?”

“Hata sisi tunashangaa wakati Anita alikuwa mchumba wake! Hivyo kwa namna moja ama nyingine namtilia shaka kuhusika na kifo hicho!”

“Kwani walikuwa na ugomvi?”

“Kama walikuwa na ugomvi sielewi, lakini mara nyingi walikuwa wakitofautiana kutokana na uchelewaji wa masuala ya kufunga ndoa…”

“Sasa hicho unahisi hicho ndicho kilichosabaisha mauaji?”

“Ndiyo maana nikakuomba uje. Unaweza kutusaidia kwa hilo, ukimpata John Bosho, unaweza kuupata ukweli wa haya yote tunayojiuliza,” mzee Anthony akaendelea kumwambia Kachero Inspekta Malik Mkoba.

“Hakuna wasiwasi mzee, nitafanya hivyo. Nitamtafuta John Bosho na kumhoji kuhusu hilo, na kama akibisha nitamkamata na kumhoji akiwa chini ya ulinzi!” Kachero Inspekta Malik Mkoba akamwambia mzee Anthony.

Baada ya maongezi yale kumalizika,  Kachero Inspekta Malik aliaga na kuondoka pale nyumbani kwa mzee Anthony, Kiwalani. Kichwani mwake alipanga kumtafuta John Bosho kwa hali na mali, ili aweze kufanya mahojiano naye ya kina, huenda akaambulia chochote juu ya mauaji ya mwanadada, Anita. Hata hivyo, aliamua kumweka kiporo, ili amfuatilie nyendo zake kujua alikuwa na agenda gani za siri!

        ********

WAKATI watu wanaendelea na shughuli za mazishi ya mwanadada, Anita Anthony, John Bosho likuwa ana mipango yake mingine kabisa, akitapatapa katika kutaka kujinasua katika tuhuma za mauaji ya mchumba wake huyo ambaye alikuwa hana hatia yoyote. Kivuli cha Anita kilikuwa kinamsumbua sana, na kuanza kujutia mara dufu!

Siku hiyo John Bosho hakushinda nyumbani kwake, Ukonga. Alikuwa amekwenda Chamazi, nyumbani kwa mganga mmoja wa jadi, aliyejulikana kwa jina la mzee Chiloto Bandua, ambaye ni mtu aliyekuwa anawasaidia sana katika shughuli zao haramu. Mganga huyo aliaminika kuwa alikuwa na uwezo wa kutengeneza dawa za mazindiko, ambazo pia zinaweza kukufanya usiweze kutambulika kama umefanya uhalifu .

Sababu kubwa iliyokuwa imempeleka kwa mzee Chiloto Bandua, ni juu ya kupata ushauri baada ya kutekeleza mauaji yale ya mchumba wake, Anita, ili ampatie dawa zitakazomfanya asikamatwe na Jeshi la Polisi, ambao kwa vyoyote watakuwa wameshaanza upelelezi wao. Ukweli ni kwamba ni mara nyingi mganga huyo aliweza kuwapatia dawa nyingi, ikiwa ni pamoja na ya kujizindika mwilini, katika azma ya kutimiza kazi zao za ujambazi.

Tuseme ni kwamba, kabla ya wao kwenda kufanya kitendo cha uhalifu eneo fulani, ilikuwa ni lazima wapatiwe dawa maalum na mganga huyo, kwa ajili ya kujizindika mwilini na hata katika silaha zao watakazotumia, kwa kile walichoamini kuwa kingewasaidia kutimiza malengo yao bila kukamatwa, kwa vile polisi wasingeweza kuwaona kamwe! Ni giza tupu!

Hivyo basi, siku hiyo John Bosho akitumia gari lake, Toyota Harrier, aliondoka nyumbani kwake kuelekea huko Chamazi, wala hakujali chochote kuwa siku ile ndiyo kulikuwa na mazishi ya marehemu Anita, aliyekuwa mchumba wake. Tokea mwanzo alikuwa ameshapanga kutohudhuria, ukizingatia yeye ndiye muhusika mkuu wa mauaji. Hata hivyo, alijua kuwa habari za mazishi hayo atazipata kwa Getruda, ambaye alikuwa amekwenda kuhudhuria msiba ule tokea jana yake.

Hatimaye baada ya kusumbuana na foleni ya magari barabarani, katikati ya jiji, John Bosho alifika katika Barabara ya Kilwa, ambayo aliifuata hivyo ambayo haikuwa na usumbufu wa foleni. Hatimaye alifanikiwa kufika Chamazi, nyumbani kwa mganga, mzee Chiloto Bandua. Akalipaki gari lake mbali kidogo na nyumba ile, halafu nusu iliyobaki akatembea kwa miguu hadi alipofika eneo husika, ambapo alipokewa vizuri na kukaribishwa kama mteja wa kawaida aliyekuwa amezoeleka pale.

Wote wawili waliingia ndani ya chumba maalum kinachohusika na shughuli za uganga, kilichokuwa kando ya nyumba yake kubwa. Baada ya kuingia katika chumba kile cha uganga, ambapo yeye alipokewa na harufu nzito ya dawa za mitishamba, mavumba, pamoja na udi. Kwa kiasi fulani haikumpendeza, lakini hakuwa na la kufanya hasa ukizingatia alikuwa amekwenmda kuganguliwa.

Hivyo basi, wakakaa kwenye jamvi lililokuwa limetandikwa karibu nusu ya chumba kizima kilichokuwa tupu bila viti. John Bosho hakupoteza muda, akamweleza mzee Chiloto Bandua juu ya jambo lililompeleka hapo nyumbani kwake.

“Mzee wangu, nimekuja kwako tena…” John Bosho akamwambia mganga huyo.

“Karibu sana, bwana mdogo…” mzee Chiloto Bandua akamwambia huku akimwangalia kwa makini.

“Huko nilikotokea nimeharibu mzee wangu!”

“Umeharibu nini?”

“Nimeua!” John Bosho akasema na kuendelea. “Mbaya zaidi nimemuua mchumba wangu mwenyewe, si unaona kazi hiyo?”

“Umemuua mchumba wako? Siyo kusaka fedha tena kutoka kwa matajiri?”

“Ndiyo, nimemuua kwa sababu alikuwa anataka kunichoma kwa polisi. Sasa huoni kama lilikuwa ni jambo la hatari sana kwa upande wangu na kwako pia?”

“Ni kweli kabisa, huyo mchumba wako alikuwa hakutakii mema. Kwa hiyo unatakaje?”

“Ninataka unitengenezee dawa nisoweze kukamatwa na polisi…maana najua saa hizi wako mbioni kumsaka muuaji!”

“Aisee, kweli kuna kazi…” mzee Chiloto Bandua akasema huku ameshika kidevu chake. Alimwelewa na kuona kuna haja ya kumpatia ufumbuzi wa suala lile, ingawa pia kwa upande wa pili aliona ni suala zito sana. Lakini akiwa ni mganga asiyependa kushindwa, na shida yake ikiwa ni fedha, akaamua kumpa ushauri wa uongo!

Mzee Chiloto Bandua akavuta pumzi ndefu na kusema kwa sauti ndogo lakini yenye msisitizo, “Ndiyo bwana mdogo…nimekuelewa vizuri. Si unasema unataka dawa ya kufanya usikamatwe na Jeshi la Polisi?”

“Ndiyo hivyo mzee…hakuna jingine!”

“Dawa nitakupa. Lakini…” mzee Chiloto Bandua akasema na kusita.

“Lakini nini mzee?” John Bosho akamuuliza huku amemkazia macho!

“Kuna masharti kidogo…”

“Masharti gani? Naomba unieleze…”

“Nitakueleza kijana wangu…usiwe na wasiwasi. Natumaini unaelewa kuwa dawa zangu ni kiboko!”

“Lazima niwe na wasiwasi, si unajua nimeua mtu mzee? Na pia ndiyo maana sisi tunakuja kwako, na kazi nyingi tumefanikiwa bila matatizo yoyote!”

“Sawa, ili usiweze kukamatwa na Jeshi la Polisi, ninakupa kazi moja ngumu kidogo. Lakini ndiyo suluhisho ya tatizo linalokukabili…”

“Kazi ngumu?”

“Ndiyo…”

“Hebu niambie kazi hiyo.

“Ni kwamba, ili ufanikiwe kukwepa kitanzi hicho, inakubidi ufanye kazi ya ziada. Ukafukue kaburi alilozikwa mwanamke uliyemuua!”

“Mh, unasemaje” John Bosho akaguna baada ya kusikia kuwa alifukue lile kaburi la Anita.

“Unaguna hata sijakueleza?” Mzee Chiloto Bandua akamwambia na kuendelea. “Basi naona kuwa wewe huna shida ya kupata dawa!”

“Nataka mzee…” John Bosho akasema huku akijifanya kuufukuza ule woga wa kulifukua lile kaburi la Anita!

 Na kweli ilitisha!

“Basi,” mzee Chiloto Bandua akaendelea. “Baada ya kulifukua hilo kaburi, mtaitoa ile maiti ndani ya sanduku. Baada ya kuiondoa maiti hiyo, mtazikata baadhi ya sehemu za siri kwa kuzinyofoa, kisha ziletwe hapa kwangu haraka sana, tayari kuzifanyia dawa ambayo itakayofanya usikamatwe wala kuhisiwa na Jeshi la Polisi kama wewe ni mhusika mkuu wa mauaji ya mchumba wako!”

“Nimekuelewa mzee, lakini…” John Bosho akasema huku wasiwasi ukiongezeka.

“Lakini nini kijana? Naona kama wewe huna haja ya kufanikiwa!” Mzee Chiloto bandua akamwambia kwa ukali kidogo!

“Masharti magumu kidogo mzee…”

“Ugumu wake nini bwana mdogo?”

“Kulifukua kaburi…ninaweza kushtukiwa na wakazi wa eneo lile!”

“Hilo siyo sharti gumu! Je ningekwanbia ukamchinje mwanao, mkeo au mama yako mzazi?”

“Mh, na hiyo ni kali zaidi!”

“Basi hilo ni sharti dogo!”

“Sawa mzee, Nitafanya hivyo!”

“Baada ya kuniletea viungo nilivyokutuma, mambo yatakuwa mazuri. Nakuomba uzingatie hilo!” Mzee Chiloto Bandua akaendelea kumsisitiza John Bosho, ambaye alimwelewa vizuri. Lakini ukweli unabaki kuwa alikuwa na wasiwasi mkubwa!

Baada ya makubaliano yale, John Bosho na mzee Chiloto Bandua wakaagana, yeye akapanda gari lake na  kuondoka pale Chamazi, kurudi jijini. Njia nzima alikuwa akiendesha gari, na mawazo mengi sana yakimkaba kichwani mwake, akiwazia kama kazi ile ya kuufukua mwili wa Anita kama itafanikiwa, na katika masharti yote aliyokuwa anapewaga na mganga yule, yale yalikuwa kiboko!

Alipofika nyumbani kwake, Ukonga, John Bosho alijimwagia maji ya baridi, kiasi kwamba mwili wake ulipata nguvu. Halafu akakaa na kuwapigia simu vijana wake wawili wa kazi, Chikwala na Robi, ambao ni kati ya vijana wengine, Muba, Kessy na Chogolo, ambao aliwaambia na kuwa kesho yake wakutane katika kikao cha dharura.

Ahadi hiyo ilikuwa ni ya kukutana  ndani ya bohari la siri lililoko eneo la  Ubungo Machimbo ya Mawe, ili wapange mikakati ya kazi iliyokuwa inawakabili mbele yao. Vijana hao, ambao wako makini sana, walimwelewa bosi wao, na kuahidi kukutana kwa muda muafaka kama walivyokubaliana!

      ********

SIKU hiyo ya Jumapili, majira ya saa nne za asubuhi, vijana wa John Bosho, Chogolo, Chikwala, Robi, Muba na Kessy, walikuwa wamejichimbia ndani ofisi yao iliyoko ndani ya bohari, eneo la Ubungo Machimbo ya Mawe. Walikuwa katika harakati za kupanga mikakati ya kazi yao iliyokuwa inawakabili, ambayo siyo nyingine zaidi ya kwenda kulifukua kaburi alilozikwa marehemu Anita.

Wote walikutana pale baada ya kupewa maelekezo na John Bosho, kiongozi wao, kama yeye alivyokuwa ameelekezwa na mganga wa jadi, mzee Chiloto Bandua, anayeishi huko Chamazi.  Akiwa amekaa kwenye kiti kilichokuwa mbele yao, akiwaangalia wote, alivuta pumzi ndefu na kuzishusha, halafu akaanza kuwaambia:

“Jamani, nimewaiteni hapa, kuna kazi nyingine tena…”

“Sawa, bosi…” wote wakaitikia huku wakimwangalia kwa makini katika kusikiliza maelekezo yanayotolewa.

“Ni kama mnavyojua, baada ya mimi kutekeleza mauaji ya mchumba wangu, Anita, niliamua kurudi kwa yule mganga, mzee Chiloto Bandua ili aweze kunigangua,” John Bosho akasema na kuendelea. “Baada ya kuongea naye jinsi ya kuweza kujinusuru nisijulikane kama ni mimi niliyefanya unyama huo, amenipa ushauri mmoja ambao kwa kiasi fulani hivi, umenichanganya sana!”

“Ni ushauri gani unaokusumbua bosi?” Robi akamuuliza.

“Ameniambia kuwa ili nifanikiwe katika azma yangu, ni lazima tufukue kaburi la marehemu Anita, kule Kiwalani!” John Bosho akawaambia huku akiwaangalia kwa zamu.

“Ndiyo, bosi…” wakasema kwa pamoja.

“Baada ya kulifukua hilo kaburi, tutoe baadhi ya viungo muhimu vilivyoko katika mwili wa marehemu. Na kazi hiyo inahitajika kufanyika usiku wa leo hii!”

“Tunakupata, bosi,” wote wakaendelea kusema.

“Vizuri kama mmenipata. Je, mko tayari kuifanya kazi hiyo?”

“Tupo tayari bosi!”

“Vizuri sana, kama mko tayari katika kazi hiyo, itabidi tutumie gari lile aina ya Toyota Land Cruiser, ambayo ni nzuri. Majira ya saa moja za usiku tukutane pale njia panda ya uwanja wa ndege, mkiwa mmeshachukua vifaa vyote, sururu, sepetu, nyundo na chochote kinachohitajika,” John Bosho aliendelea kuwapa maelekezo.

“Sawa, tutafanya hivyo,” wakakubali wote!

“Mara mtakapokuwa tayari, tutawasiliana kwa simu.”

“Sawa,” Vijana hao waliendelea kuitikia tu, kwani hakukuwa na mtu wa kuweza kumpinga John Bosho kwa jinsi alivyokuwa ni mtu katili na mwenye fedha nyingi!

Baada ya kumaliza kupeana maelekezo yale, wote waliondoka mle ndani ya bohari. Kila mmoja akelekea na njia yake, ambapo John Bosho alielekea nyumbani kwake, Ukonga kupumzika.Ukweli ni kwamba bado alikuwa amechanganyikiwa na kile kifo cha mchumba wake, Anita, ambapo sasa aliona kama kinataka kumtokea puani kwa jinsi mambo yalivyokuwa yanaonekana.

John Bosho alipofika nyumbani kwake, Ukonga, alipiga honi mara mbili, halafu geti likafunguliwa na mlinzi. Gari likaingia ndani na kupaki kwenye uwanja mkubwa uliokuwa mbele ya nyumba yake, sehemu ya maegesho, na yeye akashuka na kuingia ndani. Alifikia kukaa kwenye sofa hapo sebuleni, na kabla hajaamua cha kufanya, alichukua simu yake na kumpigia simu Getruda. Mara baada ya kupiga, simu hiyo ikaanza kuita.

“Haloo…” upande wa pili wa simu ukasema. Alikuwa ni Getruda.

“Haloo Getruda, habari za saa hizi…”

“Nzuri…” Getruda akaitikia kwa kusita.

“Nisikilize Getruda kwa makini,” akamwambia kwa misistizo. “Nakuomba uje hapa nyumbani kwangu, Ukonga, nina maongezi muhimu na wewe…”

“Maongezi gani tena?” Getruda akamuuliza baada ya kuona kuwa inakuwa kero.

“Ni maongezi muhimu sana, juu ya mustakabali wetu, mimi na wewe…”

“Mustakabali gani tena? Kuhusu marehemu Anita?”

“Hapana, ni mengineyo!”

“Sawa, nitakuja. Utakuwepo nyumbani?”

“Ndiyo, niko hapa nyumbani nakusubiri.”

“Haya, nitakuja…”

Baada ya John Bosho kumaliza kuongea na Getruda, akakata simu yake na kujiegemeza kwenye sofa pale sebuleni. Mawazo yake yalikuwa mbali sana!

Siku hiyo John Bosho aliamua kushinda hapo nyumbani kwake, mpaka ilipofika majira ya alasiri hivi. Muda huo alikuwa akimsubiri  Getruda ambaye alikuwa amempigia simu muda mrefu na kumwambia afike pale kwake jioni hiyo, kwa ajili ya mazungumzo maalum. Ni mazungumzo ambayo mpaka muda huo alikuwa akiyapanga kichwani mwake jinsi ya kumweleza ili wakubaliane!

      ********

HAKUCHELEWA sana. Getruda alifika hapo nyumbani kwa John Bosho, Ukonga, kama alivyokuwa ameamriwa. Alifika kwa kutumia usafiri wa teksi, ikiwa ni kuitikia wito wake, akijua kuwa alikuwa ni mtu mkorofi aliyekuwa anamtafutia sababu za kumfanyia kitu kibaya kama alivyomfanyia Anita, rafiki yake

Baada ya kumlipa dereva, Getruda akaijongelea nyuma ile kubwa ya kifahari iliyokuwa imezungukwa na uzio wa ukuta madhubuti na geti kubwa la chuma. Eneo la nje ya nyumba ile, palikuwa na mlinzi mmoja wa jamii ya kimasai, aliyekuwa amesimama akiwa amevalia mavazi yake ya jadi, lubega nyekundu. Ni mlinzi wa muda mrefu aliyekuwa ameajiriwa na John,  ambaye pia alimfahamu fika kama Getruda alikuwa ni mpenzi wa bosi wake.

“Habari yako yero…” Getruda akamsalimia.

“Nzuri, karibu…” mlinzi yule alimwitikia na kumkaribisha.

“Ahsante, bosi yupo?”

“Eee…mzee yuko ndani…”

“Haya, nakwenda kumwona…” Getruda akamwambia mlinzi yule, kisha akapenya katika mlango mdogo uliokuwa pale getini, na kuingia ndani ya himaya ya kasri ya John Bosho.

Baada ya kuingia tu, Gertuda alimkuta John Bosho amekaa pale nje katika bustani nzuri ya maua iliyozungukwa na miti yenye kivuli cha kutosha. Pia, ni sehemu iliyokuwa na viti na meza za plastiki maalum za kupumzika. Pale juu ya meza palikuwa na mzinga wa pombe aina ya ‘Jack Daniels,’ chupa kubwa ya maji ya kunywa na glasi ndefu, ambayo John alikuwa anatumia kunywea pombe.

Vilevile pale chini ya meza palikuwa na ndoo ndogo iliyokuwa imejaa vipande barafu, na ndani yake palikuwa na vinywaji vya aina mbalimbali, kama, bia, soda na vinginevyo. Mbali ya hayo, palikuwepo na pakiti kubwa lililokuwa na korosho mbichi, ambazo pia alikuwa akizitafuna John ili kusindikizia kile kinywaji alichokuwa anakunwa.

“Oh, karibu Getruda…” John Bosho akamwambia huku akitoa tabasamu pana.

“Ahsante,” Getruda akasema, halafu akavuta kiti kimoja kati ya vinne vilivyokuwa pale, akakaa huku wakitazamana.

“Habari yako Getu…” John Bosho akamwambia.

“Habari ni nzuri tu…” Getruda akasema kwa sauti ya kinyonge akionekana mtu mwenye mawazo.

“Mbona unaonekana mnyonge?”

“Ah, basi tu…”

“Basi nini mpenzi?”

“Majonzi tu…” Getruda akasema na kuendelea. “Ni kuhusu kifo cha Anita. Ukweli ni kwamba hakupaswa kufa! Hakuwa na hatia yoyote!”

“Usiseme hivyo…” John Bosho akasema huku akimwanglia Getruda na kuendelea. “Tambua kwamba Anita alikuwa ni mchumba wangu, na siri nyingi alikuwa ameshazijua kuhusu mimi. Sasa baada yakumtibua si ingekuwa rahisi kwake kunichoma kwa Jeshi la Polisi kiasi cha kuniharibia mipango yangu hi ambayo watu wengi hawaijui, au unasemaje?”

“Hilo naelewa, John… ”

“Basi, ndiyo maana nikammaliza!”

“Maadam yametokea ni basi, hakuna cha kufanya zaidi ya kujihami usije ukajulikane kama wewe uliyehusika na mauaji ya mchumba wako, Anita!”

“Hilo ndiyo la kusema!” John Bosho akadakia na kuendelea. Na pia polisi hawawezi kujua chochote, kwani mauaji yale nimeyafanya kisayansi, hakuna anayeweza kutegua kitendawili hicho! Labda awe mchawi!”

“Hebu tuyaache hayo. Nieleze jambo uliloniitia hapa nyumbani kwako!” Getruda akamwambia John kwa kumsisitiza!

“Usiwe na shaka, nitakwambia. Lakini ni vyema ukapata kinywaji cha kulainisha koo…” John Bosho akamwambia huku akiangalia kile kindoo kilichokuwa na vinywaji na mabonge ya barafu. Getruda akainama na kuchomoa soda moja aina ya Fanta na kuendelea kujihudumia kwa kuifungua na kuinywa taratibu.

“Vizuri sana,” John Bosho akamwambia Getruda. “Nimekuita hapa kwa ajili ya maongezi muhimu na wewe, ukiwa kama mpenzi wangu. Natumaini unajua kuwa nakupenda sana, na pia ni tegemeo langu kwa sasa!”

“Hilo naelewa kuwa unanipenda…”

“Ndiyo, basi wewe ndiye tegemeo langu. Nimeshamuua Anita, ambaye alikuwa kikwazo kwetu…hivyo narudia kusema kuwa nakutegemea wewe!”

“Kunitegemea kivipi?”

“Kukuoa na kuwa mke wangu!”

“Kunioa mimi?”

“Ndiyo…kukuoa, kwani vipi?”

“Mh, lakini…”

“Lakini nini?”

“Unafikiri watu watatufukikiriaje?”

“Kutufikiria kivipi?” John Bosho akauliza huku akimkazia macho na kuendelea. “Ina maana wewe unaishi kwa kuangalia watu watakufikiriaje?”

“Siyo hivyo John…basi tutapanga!”

“Mambo si hayo?” John Bosho akasema huku akikenua meno yake!

“Mungu wangu!” Getruda akasema kwa sauti ya chini ambayo John hakuweza kuisikia.

Ukweli ni kwamba Getruda alimwitikia kwa shingo upande. Alishaanza kumwogogopa kiasi cha kumfananisha na mnyama aina ya Simba! Ikiwa aliweza kumuua fafiki yake Anita, pia ingekuwa rahisi kumuua hata yeye endapo wangekorofishana! Hata hivyo Getruda hakuwa na lakufanya, kwani thamana ya uhai wake ilikuwa mikononi mwa John Bosho.

Ilimbidi Getruda afuate amri yake kwa kila atakalosema, na baada ya kumaliza mazungumzo yao, wakaendelea na mengine huku wakinywa vinywaji katika ile bustani nzuri na ya kupendeza, kama wapenzi wawili waliokuwa wakipanga mipango yao ya kimaisha. Hawakuonyesha huzuni juu ya kifo cha Anita, ambacho kwa namna moja ama nyingine kilikuwa kimesababishwa na wao wawili!

 Ni hatari!

********

WAKIWA bado pale nje kwenye bustani, wakiendelea na mazungumzo yao, mara simu John Bosho iliyokuwa pale juu ya meza iliita. Haraka akaichukua na kuangalia namba za mpigaji, ambayo kwenye kioo ilionyesha ni mmoja wa vijana wake wa kazi aitwaye Chikwala. Hivyo akajua kuwa alikuwa amempigia akitaka apewe maelekezo.

Kwa vile John Bosho hakupenda Getruda ayasikie mazungumzo yao, akanyanyuka na kwenda kusikilizia mbali kidogo na sehemu waliyokuwa wamekaa. Baada ya kufika kwenye kona ya nyumba, ndipo alipoanza kuwasiliana na Chikwala:

“Haloo Chikwala…lete habari…”

“Mambo safi bosi. Tumeshajiandaa kwa ile kazi uliyotupangia…”

“Ok, kama mko tayari, nisubirini pale Asenga Pub, uwanja wa ndege. Nitawakuta hapo punde tu, kwani kwa sasa nina mgeni.”

“Sawa bosi, utatukuta hapo.”

“Lakini jihadharini sana ili mtu yeyote asiweze kugundua nyendo zenu!”

“Hakuna shaka bosi..”

Simu ikakatwa.

John Bosho akarudi pale alipokuwa amemwacha Getruda, ambaye kwa wote alikuwa akimwangalia  jinsi alivyokuwa akiongea na simu ile, huku wakati wote akionyesha kwa vitendo. Baada ya kukaa tu, Getruda akamwuliza:

“Ulikuwa unaongea na nani?”

“Ah, nilikuwa naongea na jamaa yangu. Ni katika shughuli zetu za kikazi…” John akamwambia Getruda akijua kwamba ni uongo mtupu!”

“Sawa, sasa kinachoendelea?”

“Mimi sina la zaidi. Nilichokuitia ndiyo hicho nilichokueleza mpenzi!”

“Haya, nashukuru, sasa mimi naondoka kurudi nyumbani, Ilala, kwani kumeshakuchwa!”

“Ni sawa mpenzi, lakini itabidi uchukue teksi, kwani kwa muda huu sipendi kutumia gari langu kwa sababu ya kiusalama zaidi!”

“Hakuna tatizo, nitachukua teksi,” Getruda akakubaliana na uamuzi ule.

John Bosho akaingia ndani na kumwacha Getruda amekaa pale nje. Alipoingia ndani, alivalia kivingine, ukizingatia alikuwa harudi tena baada ya kumsindikiza Getruda. Kama kawaida alivalia mavazi ya kazi, halafu akachukua bastola yake iliyosheheni risasi na kuichomeka kibindoni kwa ajili ya kujihami endapo angevamiwa ghafla. Akiwa kama jambazi sugu, alijua kuwa muda wowote, saa yoyote, angeweza kukurupushwa na polisi! Ni lazima awe macho, piga nikupige!

Baada ya kumaliza kujiandaa, John na Getruda walitoka wakiongozana hadi nje ya geti. Kule nje mlinzi wa kimasai alikuwepo, ambapo John alimuaga na kumwambia anamsindikiza mgeni na hatokawia kurudi. Basi, wakatoka huku wakitembea kwa miguu hadi eneo la Ukonga Mombasa, sehemu iliyokuwa na pilikapilika nyingi za watu, kukiwa na kituo kikuu cha mabasi ya daladala na teksi.

John Bosho akachomoa pochi yake kubwa iliyotuna, halafu akachomoa fedha, noti tano nyekundu, shilingi elfu hamsini, akampatia Getruda, ikiwa ni nauli ya teksi. Getruda akazipokea na kushukuru, halafu wakaagana. Akapanda ndani ya teksi moja wapo kati ya zilizokuwa katika eneo lile, ambayo iliondolewa kuelekea mjini, ambapo John alibaki akiianglia ile teksi iliyombeba Getruda hadi ilipoishia machoni mwake kuelekea katikati ya jiji.

Getruda alipoondoka, ndipo John Bosho alipokumbuka kuwa alikuwa na ahadi ya kukutana na vijana wake wa kazi, katika kuifanya kazi ile muhimu aliyoelekezwa na mzee Chiloto. Hivyo naye akachukua teksi na kumwambia dereva ampeleke njia panda ya uwanja wa ndege wa Julius  Nyerere, alipokuwa ameahidiana kukutana  na vijana wake, katika kazi iliyotakiwa kufanyika usiku ule wa aina yake! Ni kazi ngumu ambayo walikuwa hawajawahi kuifanya tokea wazaliwe!

********        

Asenga Pub haikuwa mbali sana na barabara kuu inayoelekea maeneo ya Ukonga, Gongo la Mboto, Pugu, Kisarawe na kwingineko, njia panda ya kuelekea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, eneo la ‘Terminal 1.’ Ni sehemu iliyochangamka sana, kwa sababu pana pilikapilika nyingi za kibiashara zilizoshamiri.

Teksi ile ilipomfikisha John Bosho, akashuka na kumlipa dereva, halafu akachanganya miguu kuelekea ndani ya Pub ile iliyokuwa umbali wa mita mia moja hivi kutoka katika barabara kuu. Giza lilikuwa limeshaingia na kumpa faraja ya kutoweza kuonekana na baadhi ya watu waliokuwa wanamfahamu, ambao wengi wao wangeweza hata  kumpotezea muda wake kwa kuongea maongezi mengi yasiyokuwa na mwisho, na hata wengine kumbomu fedha. 

Baada ya kuingia ndani, sehemu maalum iliyokuwa imejificha kiasi, na palipokuwa na taa yenye mwanga hafifu wa rangi ya bluu, akawakuta vijana wale wawili, Chikwala na Robi wamekaa katika sehemu ile iliyotulia sana, na haikuwa na watu. John akavuta kiti kimoja na kukaa huku akivuta pumzi ndefu, na pia akiwaangalia kwa zamu.

“Karibu, bosi…” Chikwala akamwambia John Bosho.

“Oh, ahsante sana,” John Bosho akasema huku akiangaza macho yake pande zote. “Naona mmenisubiri sana!” Akaendelea kuwaambia.

“Ah, kiasi tu…” Chikwala akasema.

“Siyo sana, bosi,” akaongeza Robi.

“Basi ni vizuri, sasa ni vyema tunywe huku tukipanga mipango yetu, au siyo jamani?” John Bosho akawaambia huku akitaka kuagiza vinywaji.

“Ni jambo la busara bosi,” Chikwala akasema.

Vinywaji iliagizwa. Wakaendelea kunywa taratibu huku kila mmoja akiwa na mawazo yake kichwani, hasa Robi na Chikwala, ambao walishajua kile walichokuwa wameitiwa na bosi wao, kwa mujibu wa zile taarifa alizowapa asubuhi ya siku ile kule katika bohari lao, Ubungo Machimbo ya Mawe.

Hata hivyo walijua kuwa ilikuwa ni mipango yao ya kazi na siyo zaidi, ambapo John akiwa ni mtu makini, na asiyependa mambo yake yajulikane kwa urahisi, akaendelea kuyazungusha macho yake pande zote za ukumbi. Akaridhika kuwa hali ni shwari, hivyo akakohoa kidogo kusafisha koo lake, na pia akiwaangalia vijana wake Robi na Chikwala kwa zamu kana kwamba alikuwa anawakagua.

“Ni matumaini yangu kuwa nyote mko tayari kwa kazi niliyowaambia mchana, ikiwa ndiyo utaratibu wetu,” John Bosho akawaambia kwa sauti ndogo.

“Tuko tayari kwa kazi bosi…” Wote wakasema.

“Basi, nisikilizeni kwa makini,” John Bosho akaanza kuwaambia.

“Tunakusikiliza bosi…” wote wakasema.

“Ni kama nilivyowaeleza tokea mwanzo,” John Bosho akasema na kuendelea. “ Nimeamua kumuua mchumba wangu Anita, baada ya yeye kunikataa, huku akiwa ameshaijua siri yangu kuwa mimi ni mtu wa aina gani.

Hivyo basi, ili nisiweze kukamatwa kuhusiana na tuhuma za mauaji, ndiyo niliamua kwenda kwa mganga wetu, mzee Chiloto, kule Chamazi…” John Bosho akanyamaza kidogo huku akiwaangalia Robi na Chikwala walivyokuwa wanamsikiliza kwa makini.

“Ndipo mzee Chiloto aliponipa yale masharti,” John Bosho akaendelea kusema. “Ili nisiweze kukamatwa na polisi, ni lazima nimpelekee baadhi baadhi ya viungo vya mwili, katika maiti ya Anita, ambavyo ni kama, maziwa na sehemu za siri, ili azifanye dawa ya kunikinga polisi wasinigundu. Mmenipata?”

“Mh!” Robi akaguna.

“Aisee?” Akadakia Chikwala!                         

“Mnaguna?” John Bosho akauliza. “ Itabidi mnielewe ninachosema!”

“Tumekuelewa bosi!” Wote wakaitikia kwa pamoja baada ya bosi wao kuwashtukia!

“Ok, sasa ndiyo kazi tunayotaka kwenda kufanya usiku wa leo. Ni kulifukua lile kaburi alilozikwa Anita, kule Kiwalani. Halafu tunalitoa sanduku lenye maiti na kuvinyofoa viungo vile muhimu ninavyohitaji kwa dawa. Natumaini mpaka hapo mnanielewa vizuri sana.”

“Tumekuelewa bosi!” Chikwala akasema kwa niaba yao wawili. Lakini ukweli ni kwamba walikuwa na wasiwasi mkubwa!

 Ni kazi ngumu na ya hatari!

“Nitawalipa vizuri sana!” John Bosho akaongeza kusema baada ya kuwaona Robi na Chikwala wakiwa na wasiwasi.

“Hakuna shaka bosi,” Chikwala akasema kwa msisitizo.

“Natumaini pia, zile zana za kufanyia hiyo kazi mmeziweka tayari…”

“Ndiyo, zana zote, sepetu, nyundo, na sururu tumeshaviweka ndani ya gari,” Robi akasema na kuendelea. “Na gari lenyewe tumelihifadhi kule upande wa nyuma ili watu wasiweze kulishtukia na kulisoma namba, hasa ukizingatia tumeweka namba za bandia kwa usalama wetu zaidi.”

“Vizuri, basi tuendelee na vinywaji mpaka muda ufike. Agizeni vinywaji mvipendavyo, msihofu!”

“Hakuna taabu bosi…” wote wawiliwakasema.

Robi na chikwala wakaagiza vinywaji na kuendelea kunywa, na pengine wakiendelea na maongezi mengine nje ya kazi ile iliyokuwa inawakabili kwa usiku ule. Wakati wote huo mawazo ya John Bosho yalikuwa mbali sana, akiwazia juu ya utekelezaji wa kazi ile, ambayo hakujua kama wataikamilisha bila kushtukiwa, hasa ukizingatia kwa kipindi kile kulikuwa na doria kali ya Jeshi la Polisi dhidi ya wahalifu.

Ama kweli kitendo cha kulifukua kaburi na kuutoa mwili wa mtu aliyekuwa ameshazikwa zaidi ya siku mbili, ilikuwa ni hatari sana! Lakini hawakuwa na la kufanya!

********                            

SAA tano za usiku, John Bosho na vijana wake, Robi na Chikwala, walinyanyuka kutoka katika viti vyao baada ya kuona muda muafaka ulikuwa umefika. Wakatoka katika eneo lile la  Asenga Pub, na kuliendea gari lao, aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa limepaki mbali na hapo, upande wa nyuma wa Pub ile, likiwa ni gari maalum walilokuwa wanalitumia mara kwa mara kwa ajili ya kufanyia kazi kama zile, ambalo waliliwekea namba za bandia ili kuwavunga watu.

Na mara nyingi hulitumia katika kazi za kijambazi, na nyingine za haramu ambazo huwaingizia kipato  njia ya mkato. Baada ya kulifika gari, wote wakapanda, na dereva akiwa ni Chikwala, ambaye alilitia moto na kuliondoa kwa mwendo wa taratibu na kuliingiza katika barabara kuu kuelekea mjini.Walikuwa wameshajiandaa na kuwa na vifaa vitakavyotumika katika kazi ile, na vyote walikuwa wameviweka nyuma ya buti ya gari.

Waliifuata Barabara ya Nyerere moja kwa moja hadi walipofika eneo la Kipawa, kwenye taa za kuongozea magari. Pale Chikwala akapinda kulia na kuifuata barabara inayoelekea Jet Club, ambayo aliifuata moja kwa moja, halafu akapinda kulia kuifuata barabara nyingine inayoelekea Kiwalani. Ni hadi walipofika eneo la Kiwalani, sehemu yalipo makaburi yale yaliyokuwa yaliyozungukwa na miti mingi, pamoja na vichaka vilivyosababisha kuwe na kiza kizito.

Wakaliacha gari lile mbali na yalipo makaburi, na siyo jirani sana na nyumba za wakazi, ili wasiweze kushtukiwa na wakazi wa eneo lile. Wakiwa kama watu waliokuwa katika shughuli zao, wakashuka na kuanza kuangaza macho pande zote ambapo palikuwa na giza zito lilitokana na ile miti iliyofungamana na kuwafanya wasiweze kuonekana.

Bila kupoteza muda, Robi akazunguka nyuma ya gari na kufungua buti, halafu akatoa zile zana zote za kazi, mifuko mieusi,laini ya nailoni, sururu, sepetu na nyundo, halafu wakaongozana kuelekea ndani ya makaburi yale, wakiwa na tahadhari! Makaburi yalikuwa ni mengi sana, hivyo wakaanza kulitafuta lile kaburi alilozikwa marehemu Anita, ambalo lilikuwa katikati ya makaburi mengine.

Hawakupata shida ya kuliona kaburi hilo, ambalo juu yake palikuwa na mashada mengi ya maua yaliyokuwa yamewekwa na waombolezaji. Pia, lilikuwa na msalaba uliosimikwa, ambao ulikuwa umeandikwa maandishi ya jina la Anita, tarehe ya kuzaliwa, tarehe ya kufa pamoja na mwaka aliokufa.  Kabla ya kuanza kulifukua, wakaliangalia kwanza na kuvuta pumzi ndefu! Ama kweli ilikuwa kazi nzito na ya kukata na shoka!

Kama vile walikuwa wamekurupushwa, walilizunguka lile kaburi na kuanza kulifukua mara moja kwa kasi ya ajabu, hasa ukizingatia walikuwa wameshavuta misokoto kadhaa ya bhangi, ili waweze kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi. Kwa  vile kaburi lenyewe lilikuwa siyo la muda mrefu, wakalifukua na kumaliza, kisha wakalitoa lile sanduku na kuliweka juu kando ya kaburi.

Walilifungua sanduku hilo kwa kutumia ile nyundo nadi walipofanikiwa. Waliukuta mwili ule wa Anita, uliokuwa umevikwa nguo alizozikwa nazo, kwa haraka wakautoa na kuuvua nguo na kuziweka kando, kisha Robi akatoa kisu chake, aina ya ‘Okapi’ na kuanza kazi ya kuziondoa kwa kuzikata zile sehemu zilizokuwa zinahitajika na mganga.

Akiwa na roho iliyojaa ukatili, Robi akafanikiwa kuyakata maziwa na sehemu za siri, vitu ambavyo alikuwa ameagiziwa na mganga. Baada ya kuzikata, akaziweka ndani ya mfuko ule maalum wa nailoni wa rangi nyeusi. Baada ya kumaliza kazi yao, wakajiandaa kuurudisha ule mwili ndani ya sanduku kama ulivyokuwa mwanzo kabla ya kufukuliwa.

Muda wote huo, John Bosho alikuwa amesimama huku akiangaza macho yake pande zote ndani ya kiza kile, ili kuangalia kama kuna mtu yeyote anayeweza kuwatibulia mpango wao ule. Hata hivyo, ziliweza kusikika sauti ya watu waliokuwa wanapita sehemu ya nje usawa ule wa makaburi, na pia mwanga wa tochi uliokuwa unamulika chini na kuonyesha kuwa walikuwa wanapita.

Lakini ghafla wakauona ule mwanga wa tochi iliyokuwa ikimulika, ukielekezwa usawa wa kule makaburini walipokuwa wao.Wote watatu wakachuchumaa chini na kuangalia kule mwanga wa tochi ulipotokea! Walikuwa ni walinzi wa sungusungu waliokuwa zamu usiku ule, na sauti zao katikati ya usiku ule ziliweza kusikika wazi kumaanisha kwamba walishangaa kuwaona watu wale wakiwa ndani ya makaburi!

“Nani hao wanamulika na tochi?” John Bosho akauliza huku macho yake kayatoa pima!

“Inawezekana ikawa ni walinzi wa sungusungu hao!” Chikwala aliyekuwa ameshika sepetu akadakia na kuongeza. “Watatuletea mkosi sasa!”

“Na kweli ni sungusungu!” Robi akasema huku naye akiyakaza macho yake katika kiza kile kizito!

 Akaweza kuona kundi la watu!

“Basi, acheni, chukueni mzigo wetu tuondoke zetu!” John Bosho akawaambia Robi na Chikwala kwa sauti ya msisitizo!

Wote wakaondoka kwa mwendo wa kasi na wa kuinama, huku wakitimua mbio kuelekea kule walikoliacha gari lao. Lile sanduku la maiti wakaliacha pale pale juu bila kulifukia, na huku mwili wa Anita ukiwa kando ya sanduku, siyo mbali na lilipokuwa shimo!

Ni ushenzi mtupu!

“Simameni!” Sauti kali ikatokea katikati ya miti iliyofungamana  ndani ya eneo la makaburi!

 Sauti ile ilikuwa ni ya kiongozi wa kundi lile la sungusungu, ambaye alioendelea kuwamulika kwa tochi iliyokuwa na mwanga mkali! Hata hivyo, John Bosho, Robin na Chikwala walifanikiwa kutimua mbio hadi walipofika kwenye uchochoro mmoja, sehemu ile sehemu walipoliacha gari lao.  Kwa haraka wakafungua milango na kupanda, na kabla milango haijafungwa vizuri, Chikwala akalitia gari moto na kuliondoa kwa mwendo wa kasi!

“Tumenusurika!” John Bosho akasema.

“Duh, yule sungusungu mnoko sana! Unajua karibu atuharibie kazi!” Akadakia Robi!

“Sijui wametokea wapi wale washenzi! Tena kidogo wangetuwahi kabla hatujakamilisha lengo letu!” Akaongeza Chikwala huku akipangua gea na kuongeza mwendo wa gari mara tu baada ya gari lile kufika katika barabara ya lami inayoyoelekea eneo la Vingunguti, hadi walipotokeza katika Barabara ya Nyerere. Usiku ule magari yalikuwa machache sana, hivyo Chikwala akaliingiza moja kwa moja barabarani!

“Tunaelekea wapi bosi?” Chikwala akamuuliza John Bosho!

“Tunakwenda Chamazi kwa mzee Chiloto Bandua!” John Bosho akawaambia Chikwa.

“Sawa bosi!” Chikwala akasema huku akiifuata Barabara ya Nyerere kuelekea maeneo ya Tazara.

Baada ya kufanikiwa kulitoka eneo lile la Kiwalani bila kukamatwa na wale walinzi wa Sungusungu waliokuwa kazini, John Bosho na wenzake hawakujua kilichoendelea tena kule nyuma. Kwa vyovyote walijua ni lazima kutakuwa na msako mkali unafanyika dhidi yao, punde tu baada ya kuukuta ule mwili wa Anita ukiwa umeondolewa ndani ya sanduku!

Mbio za gari ziliendelea hadi walipofika Tazara, kwenye taa za trafiki, Chikwala alipinda kulia na kuifuata Barabara ya Mandela moja kwa moja hadi Kwa Sokota. Hapo wakaifuata  inayoelekea Chang’ombe, ambayo waliendelea nayo huku wakikatiza katika vichochoro, ili kukwepa kama walikuwa wanafuatiliwa nyuma!

Hatimaye mbio hizo zikaishia kule Chamazi, nyumbani kwa mzee Chiloto Bandua, mganga wa jadi. Chikwala akalisimamisha gari mbali kidogo na kwenye makazi ya mganga huyo, halafu wakashuka na kuanza kutembea kwa miguu kuiendea nyumba. Sehemu yote ya Chamazi ilitisha kwa usiku huo, kukiwa kimya kabisa, lakini wanaume wale wa shoka hawakuwa na wasiwasi wowote. Tuseme ni kwamba walikuwa wanajiamini sana ukizingatia ni watu waliozoea kazi zile za hatari siku zote!

********

NYUMBA ya mzee Chiloto Bandua ilikuwa ya kawaida tu, ambayo imejengwa kwa matofali na kuezekwa kwa mabati, ujenzi ambao haukukamilika vizuri. Kama walivyozoeleka kama wateja wake, baada ya kufika, John Bosho na wenzake walikaribishwa na kuingia ndani ya chumba kimoja ambacho ni maalum kwa kazi za kiganga.

Kwa vile ilikuwa ni usiku, paliwashwa taa ya kandili iliyotoa mwanga hafifu, lakini uliowezesha kumwona mzee Chiloto Bandua aliyekuwa amekaa mbele yao katika jamvi lililotandikwa chini. Akiwa ni mzee mwenye umri wa miaka sitini hivi, alikuwa amekaa huku amezungukwa na vibuyu vidogovidogo, pamoja na madawa mengine ya aina mbalimbali. Aliwakodolea macho yake makali na kuwaangalia kwa zamu.

“Ni matumaini yangu kuwa mmekuja na ule mzigo niliouagiza!” mzee Chiloto bandua akawaambia.

“Ndiyo  mzee…tumekuja nao…” John Bosho akasema huku akiwa na matumaini.

“Vizuri sana,” mzee Chiloto Bandua akasema na kuendelea. “Sasa nyie wawili tokeni nje. Mimi nitabaki na huyu mmoja tayari kwa kumganga!”

“Sawa mzee…” Chikwala akasema.

Robi na Chikwala wakanyanyuka na kutoka nje ya chumba kile na kwenda kukaa sehemu iliyokuwa na viti maalum kwa ajili ya wateja. Pale chumbani wakabaki mzee Chiloto na John Bosho aliyesubiri kufanyiwa uganga.

“Hebu nipe huo mzigo,” mzee Chiloto Bandua akamwambia John ambaye alikuwa na mawazo mengi yaliyokuwa yamemjaa kichwani.

“Mzigo huu hapa!” John Bosho akasema huku akimkabidhi mzee Chiloto ule mfuko mweusi uliokuwa na mzigo.

“Oh, vizuri sana,” mzee Chiloto Bandua akasema huku akiupokea ule mfuko na kuanza kuufungua kwa makini akitegemea kukiona kilichoko ndani yake!

Baada ya kuufungua ule mfuko, mzee Chiloto Bandua akavitoa viungo ile vilivyokuwa katika hali ya nyamanyama hivi. Kisha akaviweka ndani ya chungu kimoja kilichokuwa pale kando. Halafu akachanganya na maji na kuanza kukoroga kwa nguvu huku akitamka maneno fulani, ambayo hata upande wa John hakuyaelewa kamwe. Muda wote alikuwa akimwangalia alivyikuwa anafanya kazi ile ya uganga, kumganga yeye!

Alipomaliza kuongea maneno yale, mzee Chiloto  Bandua akachukua wembe mpya na kuanza kumchanja chale mwili mzima katika sehemu muhimu. Halafu akampaka ile dawa iliyokuwa ndani ya chungu kile alichoweka viungo vya binadamu. Ni dawa iliyokuwa inauma sana ilipokuwa inaingia mwilini mwake katika zile chale.

 John Bosho akawa anajitingisha kadri alivyokuwa anapakwa hadi mzee Chiloto Bandua alipomaliza. Baada ya hapo, akampa dawa nyingine ambayo ingemfanya asiweze kujulikana na polisi, au mtu yeyote kwamba ndiye mhusika mkuu wa mauaji yale ya mwanadada Anita!

“Naona mambo yote tayari… tumeshamaliza kazi yetu!” mzee Chiloto Bandua akamwambia John Bosho.

“Oh, nashukuru sana,” John Bosho akasema huku akinyanyuka kutoka pale kwenye jamvi alipokuwa amekaa. Ukweli ni kwamba alikuwa ana matumaini!

“Mambo shwari sasa!” mzee Chiloto Bandua akaendelea kumwambia John.

“Ina maana hapa ndiyo kiboko! Hakuna mtu yeyote atakayekugundua!” Mzee Chiloto bandua akaendelea kumwambia John.

“Unasema kuwa polisi hawataona ndani?”

“Waone ndani? Wataona giza tupu!”

“Basi poa,” John Bosho akasema huku akichomoa pochi yake na kuanza kuifungua. “Ni shilingi ngapi mzee?” Akamuuliza.

“Ah, wewe ni mteja wangu wa kila siku… nifikirie kiasi cha mboga tu,” mzee Chiloto bandua akamwambia huku akikenua meno yake.

“Haya, chukua pesa hii, natumaini inatosha…” John Bosho akamwambia na kumpatia shilingi laki moja.

“Oh, nashukuru sana…” mzee Chiloto bandua akasema huku akitabasamu kwa kuona kiasi kile cha fedha!

“Mimi natoka mzee,” John Bosho akaaga.

“Haya kijana, karibu tena…” mzee Chiloto Bandua akamwambia huku akimwangalia John Bosho alivyokuwa anatoka nje ya kibanda chake.

Ukweli ni kwamba mzee Chiloto Bandua alikuwa anasikitika sana, kwa vile alikuwa anamdanganya tu, hakuwa na uwezo wa kumtengenezea kinga ya kummfaya asikamatwe na Jeshi la Polisi. Ni njaa tu iliyokuwa inamfanya mzee huyo afanye kazi kama ile ya utapeli, kwa kuwadanganya watu kuwa alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwakinga na dawa zake za asili. Na kwa vile watu wengi wanahusudu mambo ya ushirikina, basi aliweza kuwapata kwa wingi sana, maisha yakawa yanasonga mbele.

Baada ya kumpatia zile fedha, mzee Chiloto Bandua, John akatoka ndani ya chumba kile na kuungana na wenzake, Chikwala na Robi, waliokuwa wanamsubiri kando ya chumba kile. Wote wakaondoka nyumbani kwa mganga huyo, na kuelekea sehemu ile walipoliacha gari lao, wakiwa na matumaini kuwa siri ile isingeweza kujulikana kabisa baada ya bosi wao kupata kinga! Walipofikia gari, wakapanda na dereva akiwa Chikwala, ambaya alilitia moto na kuliondoa kwa mwendo wa wastani kuelekea katikati ya jiji.

********* 

MZEE Chiloto Bandua alipokabidhiwa zile fedha na John Bosho, alitoka ndani ya kibanda chake uganga, halafu akarudi ndani ya nyumba kubwa na kuungana na mke wake, Bi. Neema binti Shamte, aliyekuwa amekaa akiangalia runinga sebuleni.

Hakika mzee huyo alikuwa na furaha baada ya kulipwa fedha zile, kiasi cha shilingi laki mbili kwa mara moja, tena fedha iliyomjia usiku akiwa hana uhakika wa kuingiza kiasi hicho. Baada ya kukaa kwenye kochi, kando ya mke wake, akapumua kwa nguvu na kumwambia:

“Oh, mke wangu, nimeshamaliza kazi…”

“Umeashamaliza sivyo?” Bi. Neema akamuuliza kana kwamba hakumsikia.

“Ndiyo, nimemaliza. Unafikiri ilikuwa kazi kubwa sana mke wangu? Ni ya mara moja tu hata isiyotoa jasho!”

“Mh,” Bi. Neema bint Shamte akaguna huku akimwangalia kwa uso uliojaa woga! Halafu akamwambia. “Mume wangiu wewe… mzee Chiloto…”

“Labeki mke wangu…” mzee Chiloto Bandua akaitikia huku akimwangalia mkewe.

“Mbona unajitafutia balaa?” Bi. Neema akaendelea kumwambia.

“Balaa gani tena mke wangu?”

“Si kuhusu hao wateja wako?”

“Kwani vipi?”

“Hivi ni kweli unawatibu?”

“Ni kweli nawatibu, kwa nini unawauliza hivyo?”

“Nauliza kwa sababu mwanzo kabisa ulikuwa unatibu wateja wa kawaida wenye matatizo kama ya kulogwa, kusafisha nyota, kupata bahati, na mengineyo,” Bi. Neema akasema na kuongeza. “Hivi naona umeanza kutibu hata majambazi! Hakika iko siku watakuja kukugeuka endapo hawatafanikiwa katika malengo yao!”

“Usiwe na wasiwasi mke wangu. Mimi huwa natibu watu wa aina zote, haichagui majambazi, kwa vile hawana alama usoni. Dawa zangu ni kiboko!”

“Haya, mimi kazi yangu ni kukwambia kwa jinsi ninavyoona, lakini nakupa tahadhari!” Bi. Neema akaendelea kumwambia.

“Yaani tahadhari unanipa mimi mganga wa waganga?”

“Ni lazima nikwambie, siku yakiharibika mimi nakimbia, siwezi kupigwa risasi nikijiona!” Bi. Neema akasisitiza!

“Huo ni uchuro sasa, tuendelee na mengine!” Mzee Chiloto Bandua akamwambia mkewe baada ya kuona alikuwa anamletea mikosi sasa!

Mjadala ukaisha!

Mzee Chiloto Bandua na mke wake, Bi. Neema bint Shamte walimaliza yale majadiliana yao, huku mzee huyo akiona kuwa ule ulikuwa ni ukweli aliokuwa anaambiwa na mke wake, hasa ukizingatia baadhi ya wateja zake alikuwa akiwadanganya ili aweze kupata fedha za kujikimu. Siku zote alikuwa akisema wajinga ndiyo wali wao!

Hata hivyo siku zake zinahesabika!

********     

KACHERO Inspekta Malik  Mkoba aliamka kunako majira ya saa kumi na mbili za asubuhi. Baada ya kujiswafi alivalia nguo zake nadhifu, ambazo zilimpendeza baada ya kujitazama kwenye kioo kikubwa kilichokuwa ukutani. Yeye alikuwa bado kijana  mbichi tu, mwenye umri wa miaka 35 hivi,  na mmoja wa makachero shupavu na mchapakazi katika Jeshi la Polisi, hususan kitengo cha Idara ya Upelelezi.

Kwa muda wote, kimakazi, alikuwa anaishi nyumbani kwake, eneo la Ilala, Shariff Shamba,  alipokuwa anaishi pamoja na wadogo zake wawili, Toni na James aliokuwa anawasomesha.Ni kwamba, alikuwa bado kijana mwenye malengo na bado hajaoa, lakini alikuwa na mchumba aitwaye Dora Damas, ambaye walikuwa katika harakati za mipango ya harusi, ambayo ingefanyika wakati wowote mambo yatakapotengamaa.

Kachero Inspekta Malik alipohakikisha kila kitu tayari, alitoka nje ya nyumba yake na kuliendea gari lake aina ya Nissan Laurel, ambalo lilikuwa limepaki upande wa mbele ya nyumba yake katika uwanja mdogo wa maegesho. Baada ya kulifikia, akafungua mlango na kupanda, halafu kalitia moto na kuliondoka hadi nje ya geti la kutokea ambalo lilikuwa limeshafunguliwa. Baada ya kulitoa nje, akaifuata barabara ndogo ya udongo iliyotokeza katika barabara kuu ya Uhuru.

Alipoifikia barabara hiyo, akapinda kulia kuifuata hiyo barabara ya Uhuru kwa mwendo wa wastani hadi alipofika kwenye kituo cha Polisi Buguruni. Ni kituo ambacho hakikuwa mbali sana, ni umbali kama wa kilometa mbili na nusu kutoka pale nyumbani kwake, Shariff Shamba, Ilala. Baada ya kufika kituoni, akalipaki gari sehemu ya maegesho iliyokuwa kando ya kituo.

Kachero Inspekta Malik akashuka na kuiedea ofisi yake kwa mwendo wa kikakamavu hadi alipoingia na kuketi, tayari kuanza kazi zilizokuwa zinamkabili. Hata hivyo hakupoteza muda, alianza kuyapekuwa mafaili kadhaa aliyotakiwa kuyashughulikia likiwa lile la marehemu Anita. Lakini kabla hajafika mbali na upitiaji wa mafaili, akaingia Kachero Sajini Joel Kidampa, huku akitoa heshima kwa nidhamu.

“Karibu Joel…” Kachero Inspekta Malik akamwambia.

“Ahsante afande…” Kachero Sajini Joel Kidampa akasema huku akiwa bado amesimama.

“Nipe taarifa…”

“Kuna taarifa muhimu imetufikia muda huu afande…”

“Taarifa gani?”

“Afande, kuna wakazi watatu wa eneo la Kiwalani, akiwemo mjumbe wa nyumba kumi, na mzazi wa marehemu Anita, wamefika hapa kituoni asubuhi hii. Wamesema kuwa lile kaburi alilozikwa Anita juzi, limefukuliwa usiku wa kuamkia leo. Na haijulikani ni watu gani waliyelifukua; na walikuwa na maana gani!” Kachero Joel Kidampa akamaliza kusema, kisha akabaki akimwangalia Malik.

“Mh,” Kachero Inspekta Malik akaguna na kusema. “Unasema kaburi limefukuliwa?”

“Ndiyo afande…limefukuliwa…”

“Hao watu wako hapo nje?”

“Ndiyo, wako hapo nje…”

 “Hebu waambie waje hapa ofisini.”

“Sawa afande…” Sajini Joel Kidampa akasema, kisha akatoka na kwenda kuwaita watu wale.

Baada ya dakika mbili tu, Joel akaingia pale ofisini akiwa na wale watu watatu, Mjumbe wa Nyumba Kumi, mzee Shogholo Uledi, baba wa marehemu, mzee Anthony Mkonyi, pamoja na mkazi mwingine mwenye umri wa kati, Mwaipaja Mwanjelwa.

“Karibuni wazee…” Kachero Inspekta Malik akawakaribisha.

“Ahsante…” mzee Shogholo Uledi akasema.

“Ahsanter kijana…” mzee Anthony naye akasema huku wakiingia pale ofisini.

Wazee wote watatu wakakaa kwenye viti.

“Ndiyo wazee wangu, karibuni na mnieleze kilichojiri…” Kachero Inspekta Malik akawaambia.

“Tumefika hapa kituoni ili kueleza kilichotokea usiku wa jana huko katika eneo la Kiwalani tunapoishi,” mzee Shogholo Uledi, Mjumbe wa Nyumba Kumi akaanza kueleza. “Ni kwamba sisi huwa tuna mpango wetu wa kufanya doria za mara kwa mara nyakati za usiku ili kudhibiti wimbi la uhalifu kwa ujumla, ambapo huwa tunawashirikisha wakazi wa mtaa katika kujilinda…”

“Hilo ni lengo zuri sana, katika Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii, katika kutusaidia sisi askari polisi kudumisha ulinzi na amani,” Kachero Inspekta Malik akadakia.

“Ni kweli kabisa, dhana hiyo tunaifahamu sana. Basi, wakati tukiwa doria katika eneo la makaburi ya Kiwalani, ndipo tuliposikia sauti za watu waliokuwa wakiongea ndani ya makaburi hayo. Hivyo tukanyatia taratibu na kukuta kuwa ni kweli kulikuwa na watu ambao idadi yao haikufahamika, wakiwa wanafukua kaburi moja wapo. Baada ya kutuona, wakakimbia na kuondoka na gari lao walilokuwa wamefika nalo hapo…” mzee Shogholo Uledi akanyamaza kidogo huku akimwangalia Malik.

“Watu wale walipokimbia, sisi tulikwenda mle ndani ya makaburi, na baada ya kufanya uchunguzi, ndipo tulipokua kaburi la marehemu, Anita, mtoto wa mzee mwenzangu hapa, likiwa limefukuliwa na mwili kutolewa ndani ya sanduku….” mzee Shigholo Uledi alieleza yote yaliyotokea kule kitu ambacho kilimshangaza sana Kachero Inspekta Malik.

“Oh, poleni sana, je, baada ya watu hao kukimbia, mliweza hata kumtambua mmoja wao?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza mzee Shogholo Uledi.

“Hapana, kwa kweli hatukuweza kumtambua hata mtu mmoja, hasa ukizingatia kulikuwa na giza,” mzee Uledi akasema.

“Pia umesema kuwa walifika pale kwa gari, je, ni gari ya aina gani?”

“Kama sikosei ilikuwa ni Toyota Land Cruiser…”

“Ulifanikiwa kuisoma namba?”

“Hapana, sikufanikiwa kuisoma namba…”

Mahojiano yakaendelea juu ya tukio lile la kukuta kaburi limefukuliwa usiku wa kuamkia siku hiyo, na baada ya mahojiano yale, Kachero Inspekta Malik akampa majukumu Kachero Sajini Joel Kidampa na askari wengine wawili wa magwanda, waondoke pale kituoni kuelekea eneo la tukio, Kiwalani. Hakika Malik alikuwa ametandwa na giza mbele yake na kujiuliza kuwa watu waliokuwa wamefukua kaburi lile walikuwa na maana gani?

Hakujua!

        ********

WOTE waliondoka hapo kwenye Kituo cha Polisi Buguruni kwa kutumia gari la matukio aina ya Toyota Land Cruiser , iliyokuwa na namba za kiraia. Walitumia kama saa moja na nusu tu kufika katika eneo la makaburi ya Kiwalani. Baada ya kufika, waliukuta umati mkubwa wa watu ukiwa umejazana, wengi wao wakishangaa juu ya kufukuliwa kwa kaburi lile lenye mwili wa Anita ambao ulishazikwa!

Kwa vile watu walikuwa wengi, wakafanya kazi ya ziada kuwatawanya ili waweze kupita na kuingia kule makaburini bila bughudha. Makachero wale wakaingia katika eneo la makaburi, ambapo waliukuta mwili wa Anita ukiwa kando ya kaburi, ukiwa umeondolewa ndani ya sanduku, na baadhi ya viungo vimeondolewa kwa kukatwa!

Baada ya uchunguzi mdogo, Kachero Inspekta Malik akalifananisha tukio lile na imani za kishirikina, kwa vile ulikuwa umeondolewa baadhi ya viungo. Hata hivyo akauruhusu uzikwe tena, na wakazi wa pale wakauzika  ule mwili, na makachero wale wakajiandaa kuondoka kurudi kituoni. Habari zile za mauaji ya kutisha na kufukuliwa kwa maiti ya Anita zikaendelea kutapakaa kote jijini  Dar es Salaam!

Baada ya mwili wa Anita kuzikwa tena, Kachero Inspekta Malik akaona kulikuwa na usiri uliokuwa umejificha nyuma ya kifo cha Anita. Hata hivyo kabla ya kuondoka eneo hilo la Kiwalani, aliona lilikuwa ni jambo la busara kuwahoji wazazi wa Anita, ili aweze kupata mambo muhimu kutoka kwao, ambayo yangemsaidia katika upelelezi wake.

Kachero Inspekta Malik alifika nyumbani kwa mzee Anthony, baba yake Anita, ikiwa ni mara ya pili tokea siku ile alipokwenda baada ya wao kumwita. Wakampokea vizuri, akaingia ndani na kufikia sebuleni. Mzee Anthony alikaa kwenye kochi dogo lilikuwa upande wa kushoto, na Bi. Matilda alikaa kwenye kochi kubwa. Yeye Malik alikaa kwenye kochi kubwa, ambapo aliweza kuwaangalia vizuri wazee wake.

“Habari za hapa wazee wangu…” Kachero Inspekta akawaambia.

“Nzuri, karibu sana…” mzee Anthony akasema,

“Kwanza natanguliza tena, poleni kwa msiba…” Kachero Inspekta Malik amamwambia.

“Ahsante sana,” wote wakajibu kwa pamoja.

“Najua bado mna uchungu wa kufiwa na mtoto wenu mpendwa, lakini kwa sisi kama Jeshi la Polisi, inabidi tufanye kazi yetu ili kuupata ukweli!”

“Hakuna shida baba, fanya kazi yako…” mzee Anthony akamwambia.

“Narudia tena kuuliza swali lilelile nililowahi kuuliza mwanzoni nilipokuja hapa. Hivi Anita alikuwa na maadui?” Kachero Inspekta Malik akauliza.

“Hapana, ni kama tulivyokueleza. Anita hakuwa na adui yeyote. Yeye alikuwa ni mtu mpole sana mwenye kufanya mambo yake kwa akili sana…” mzee Anthony akajibu.

“Huyo mchumba wake alikuwa ni John Bosho sivyo?”

“Ndiyo, alikuwa ni John Bosho…”

“Mchumba mwenyewe si mlikuwa mnamfahamu vizuri?”

“Tulikuwa tunamfahamu, lakini si sana.”

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Ni mtu wa kusafiri sana. Na hata kwenye msiba ndiyo vile hakuwepo. Alipopigiwa simu, akasema amesafiri…”

“Na nyie mliridhika na mchumba huyo?”

“Ilibidi turidhike, kwani watoto wa siku hizi wana uhuru wao wa kujitafutia wachimba, na siyo kama enzi zetu.”

“Sasa nyie mnafikiri ni nani aliyehusika na mauaji ya Anita?”

“Kwa sasa hatuwezi kumhisi mtu, kwa vile hatujui mwenendo mwingine wa marehemu…”

“Labda alikuwa na wanaume wawili?”

“Kwa hilo sidhani…”

“Au ni imani za kishirikina?”

“Kwa hilo ninaweza kufikiria hivyo. Inawezekana huyo mtu aliyemuua alikuwa na maana hiyo, lakini mengine tunawaachia nyie polisi kuifanya kazi hiyo.”

“Sawa, nashukuru sana. Sisi polisi tutajitahidi kufanya upelelezi na apatikane!”

“Ahsante baba…”

Baada ya mahojiano yale, Kachero Inspekta Malik aliaga na kuondoka kurudi kituoni akiwa na makachero wenzake. Habari za mauaji ya kutisha na kufukuliwa kwa maiti ya Anita zikaendelea kutapakaa jijini Dar es Salaam. Vyombo vya Habari, redio, magazeti na televisheni vilitangaza tukio lile la kusikitisha, na kusisitiza kwa Jeshi la Polisi lijitahidi kufanya uchunguzi wa kina na kuweza kuwapata wale watu waliofanya tukio hilo la kishenzi! Ni kitendo ambacho kisingeweza kuvumilika kwa udhalilishaji wa ile maiti ya Anita iliyokuwa imeshazikwa!

Kachero Inspekta Malik alipofika ofisini hakukaa sana, aliyapitia mafaili yaliyokuwa yanamkabili kwa harakaharaka na kuyamaliza. Halafu akajiandaa kwa safari ya kwenda eneo la Tabata Aroma, lilipo lile duka la kuuza dawa baridi za binadamu, ambalo lilijulikana kwa jina la Kishada Medics.

******** 

DUKA la dawa la Kishada Medics, liko eneo la Tabata Aroma, na limepakana na Jengo la ghorofa la Aroma, lililoko umbali wa mita ishirini kutoka barabara kuu inayoelekea Segerea na kwingineko. Baada ya kufika eneo hilo, Kachero Inspekta Malik akalisimamisha gari sehemu ya maegesho yalipokuwa magari mengine yamepaki ya wateja wanaofika kupata huduma.

Kabla ya kushuka ndani ya gari, Kachero Inspekta Malik akayatupa macho yake katika sehemu ile na kuweza kuliona duka hilo lililokuwa upande wa kushoto. Ndipo aliposhuka akiwa na ile bahasha iliyokuwa na bomba la sindano ndani yake, akaliendea kama mteja wa kawaida aliyekuwa anakwenda kujipatia mahitaji yake ya ununuzi wa dawa.

Ni duka kubwa kiasi, ambalo limejengwa na kuwekwa mlango wa kioo, uliowezesha kuonyesha mpaka ndani. Yeye aliamua kwenda kufanya upelelezi kwa kuhojiana na muuza duka lile, ukizingatia tukio zima lilianzia pale kwa muuaji kununua bomba la sindano. Ukweli ni kwamba bahasha ile iliyokuwa imehifadhi lile bomba la sindano, ilikuwa na muhuri wa duka lile kudhihirisha kwamba aliyefanya mauaji ya Anita, alinunua mahitaji yake dukani pale, na kutimiza azma yake ya kuua.

Kachero Inspekta Malik alipofika aliusukuma mlango na kuingia ndani ambapo alipokewa na hewa ya ubaridi iliyotoka kwenye kiyoyozi, na kwa kiasi fulani harufu ya madawa iliweza kusikika mle ndani. Pia, alikuwepo mwanadada mrembo, ambaye ndiye muuzaji wa duka lile. Akawa namwangalia Malik alivyokuwa anaingia ndani kwa hatua fupi, na kwa sauti nyororo ya kibiashara akamwambia:

“Karibu kaka…”

“Ahsante sana…” Kachero Inspekta Malik akasema huku akilikagua kwa macho duka lile. Halafu akamsalimia na kuanza mazungumzo yaliyompeleka pale.

“Nikusaidie kaka…” mwanadada yule akamwambia.

“Naomba msaada wako…mimi ni Kachero Inspekta Malik,” akajitambulisha. “Natokea kwenye Kituo cha Polisi Buguruni, na nimekuja hapa kwa kwa jambo muhimu…”

“Karibu sana…” mwanadada yule akasema huku akimwangalia Malik kwa wasiwasi kidogo!

 Kachero!

“Sijui unaitwa nani?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza huku amemkazia macho.

“Naitwa Paulina Mbagga.”

“Oh, vizuri sana,” Kachero Inspekta Malik akasema huku akichukua kijitabu kidogo na kuanza  kuandika kile alichoona kinafaa.

“Hili ni duka linalomilikiwa na nani?”

“Ni duka la shemeji yangu….” mwanadada yule akajibu.

“Basi, naomba unijibu maswali kadhaa nitakayokuuliza…wala usiwe na wasiwasi wowote!”

“Unaweza kuniuliza tuu…”

“Ni kuhusu yale mauaji ya mwanamke mmoja yaliyotokea kule Tabata Mawenzi siku tatu zilizopita…”

“Mauaji?” Paulina akauliza kana kwamba hakumsikia.

“Ndiyo, mauaji, natumaini umeyasikia…”

“Ndiyo, nimeyasikia…” Paulina akasema na kuongeza.

“Oh, Mungu wangu! Mauaji hayo yananihusu nini mimi?”

“Hapana…usihofu wala hayakuhusu kabisa. Ila nakuuliza kwamba umewahi kuiona bahasha hii?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza huku akimwonyesha ile bahasha iliyokuwa na muhuri wa duka lile.

“Ndiyo…nimewahi kuiona. Bahasha hii iliyopigwa muhuri pamoja na nyingine zilizokuwa hapa, huwa nazitoa kwa wateja wanapokuja kununua dawa, kwani vipi?” Paulina akasema huku wasiwasi ukiendelea kumwandama!

Mbona yamekuwa hayo tena?

“Ina maana bahasha hii ni wewe uliyeitoa kwa mteja siku hiyo?” Malik akaendelea kuuliza.

“Ndiyo ni mimi, kwa sababu hakuna mtu mwingine anayeuza hapa dukani zaidi yangu.”

“Unaweza kukumbuka ulimuuzia nani, na lini huyo mteja wako? Pia, unaweza kukumbuka jina lake? Tafadhali naomba unisaidie…”

“Nakumbuka siku tatu zilizopita, kunako majira ya saa nane za mchana hivi, alifika mteja mmoja hapa dukani…”

“Baada ya kufika?”

“Alipofika alinunua bomba moja la sindano. Yeye alikuja akiwa na gari lake, ambalo alilisimamisha kando ya barabara, karibu na sehemu ya maegesho. Baada ya kununua bomba hilo, akaondoka zake…” Paulina akasema lakini hakuweza kuelezea lile tukio la John Bosho kumuachia chenji baada ya kununua lile bomba la sindano na kutoa fedha kubwa!

“Alikuja na gari gani?”

“Kama sikosei ilikuwa ni Toyota Harrier ya rangi ya fedha…”

“Aisee, vizuri sana, je, namba zake ulizisoma?”

“Hapana, sikuzisoma, na wala sikuwa na sababu ya kuzisoma…”

“Uliwahi kulijua jina lake?”

“Silifahamu… na pia sikuona sababu za kumuuliza jina lake.”

“Je, ukiiona sura yake utaikumbuka?”

“Pia, siikumbuki sura yake kwa sababu wateja ni wengi sana huwa wanakuja hapa kununua dawa kila siku.”

“Na kweli…” Kachero Inspekta Malik akasema huku akifikiria.Ukweli ni kwamba aliona kile alichosema Paulina, ni ya kweli, hivyo hakuona sababu ya kuendelea kumhoji.

Kachero Inspekta Malik akamuaga Paulina, halafu akaondoka huku akiwa amegundua kuwa muuaji huyo alikuwa amenunua bomba la sindano katika duka hilo. Lakini hakuwa na la kufanya, kwani muuzaji hakuwa kumbukumbu zozote juu ya mnunuaji yule. Alipotoka hapo dukani, akaamua kuelekea Tabata Mawenzi, kwenye nyumba ile aliyokuwa anaishi marehemu Anita ili kuendelea na upelelezi.

        *********

ALITUMIA kama dakika ishirini hivi kufika Tabata Mawenzi. Baada ya kufika, Kachero Inspekta Malik akalipaki gari lake upande wa pili wa uzio wa nyumba ile aliyokuwa anaishi Anita, halafu akashuka garini na kuiendea kwa mwendo wa taratibu. Alipokewa  na mama mwenye nyumba, Bi. Debora, ambaye alimkaribisha vizuri. Wote wakafuatana hadi walipoingia katika sebule nadhifu na kukaa kwenye sofa.

“Karibu sana baba..” Bi. Debora akaendelea kumwambia Malik.

“Ahsante sana…poleni kwa msiba…”

“Ahsante, ndiyo hayo yametokea. Labda ni mipango ya Mungu aliyepanga Anita afe kwa kifo kile!”

“Basi, ndiyo kama nilivyokueleza tokea mwanzo, mimi ni Kachero Inspekta Malik, ninayepeleleza juu ya mauaji ya mpangaji wako, Anita, ili tuweze kumkamata muuaji!”

“Ni sawa baba, sasa nikusadie nini? Bi. Debora akamuuliza huku akimwangalia kwa huzuni!

“Naulizia kwamba, je, vyombo vya marehemu bado viko chumbani?”

“Ndiyo…vyombo vyake bado viko chumbani. Hakuna aliyevigusa, kwani tunasubiri ndugu zake waje kuvichukua punde msiba utakapomalizika!”

“Funguo za chumba hicho unazo?”

“Ndiyo, funguo ninazo mimi…”

“Basi, naomba ufunguo wa chumba alichokuwa anaishi marehemu Anita. Nataka kuingia na kufanya uchunguzi huenda nikapata mambo mawili matatu.”

“Hakuna tatizo baba…”

Kacheri Inspekta Malik alipewa ufunguo wa nyumba ya marehemu Anita. Akaufungua mlango na wote wawili wakaingia ndani ya hadi katika sebule nadhifu, kwa haraka Malik akatupa macho yake na kuanza kuchunguza, ambapo ndani ya sebule ile, palikuwa na seti moja ya sofa, kabati kubwa la vyombo, runinga, redio kubwa na vitu vingi tu. Hakika palikuwa pameenea ipasavyo na kuonyesha alikuwa ni mtu mwenye kujipenda sana na kuwa msichana wa kileo!

 “Tuingie chumbani sasa,” Malik akamwambia Bi. Debora, ambaye alionyesha kuwa na wasiwasi.

“Sawa,  baba…” Bi. Debora akasema.

“Usiogope mama…”

“Hapana…siogopi…”

Kachero Inspekta Malik akaufungua mlango wa chumbani, halafu wakaingia na kukiona kilikuwa ni chumba chenye ukubwa wa wastani. Upande wa kushoto palikuwa kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita, pamoja na kabati la nguo lililokuwa kwenye kona ya chumba. Malik akaliendea na kulifungua huku Bi. Debora akiwa amesimama akimwangalia kila alichokuwa anafanya.

Baada ya kulifungua, Malik akaanza kulipekua na kutoa nguo moja baada ya nyingine kwa umakini, na kuziweka kando. Alipomaliza kupekua, akakuta bahasha mbili za khaki na albamu moja kubwa ya picha, ambavyo vyote vilikuwa chini kabisa. Akavichukua na kumwendea Bi. Debora aliyekuwa bado amesimama. Akamwambia kwa sauti ndogo lakini iliyosikika:

“Natumaini umeniona nilivyokua napekua ndani ya kabati la nguo…”

“Ndiyo baba, nimekuona…” Bi. Debora akasema.

“Hivyo basi, nachukua hii albamu ya picha pamoja na hizi bahasha mbili nilizozikuta ndani ya kabati. Nakwenda navyo kituoni kuzifanyia kazi, halafu nitarudi kesho.”

“Unaweza kuchukua tu baba…” Bi. Debora akamwambia.

Kachero Inspekta Malik akachukua ile albamu pamoja na zile bahasha mbili za khaki, halafu wote wakatoka hadi nje ya chumba kile cha marehemu Anita. Baada ya kutoka, Malik akaagana na Bi. Debora, kisha akapanda gari lake na kuondoka katika eneo lile la Tabata Mawenzi.

*******

Vijana wapatao sita walikuwa wameizunguka meza moja kubwa mfano wa meza ya kulia chakula, iliyokuwa na viti vitatu kila upande. Wote walikuwa wamemwangalia mtu mmoja, aliyekuwa amekaa katika kiti cha peke yake akiwa tayari kuwapa maelekezo.

Ilikuwa ni ndani ya chumba maalum, kilichoko ndani ya bohari, katika maficho ya siri, eneo la Ubungo Machimbo ya Mawe. Ni kikundi hicho kilichokuwa kinaongozwa na John Bosho,  ambaye alikuwa amekaa kikao na vijana wake, Robi, Chikwala, kessy, Chogolo, Shabani na Muba. Alikuwa amewaita pale kwa dharura ili awahabarishe habari muhimu sana.

“Jamani nimewaiteni tena hapa ili tupange mikakati yetu…”  John Bosho akawaambia vijana wake huku akiwaangalia kwa zamu.

“Ni sawa, mkuu!” Chikwala akasema.

“Tupo mkuu!” Robin naye akasema.

“Tunakusikiliza!” Wakaongeza Kessy, Chogolo na Shabani kwa pamoja.

“Mambo yanazidi kuwa mazito kwa upande wangu…” John Bosho akaendelea kuwaambia.  “Kwa nini mkuu?” Chikwala akamuuliza.

“Natumaini nyote mnamfahamu Kachero Inspekta Malik Mkoba, wa Kituo cha Polisi Buguruni!”

“Ndiyo, tunamfahamu…” akadakia Chikwala na kuendelea. “Hakuna asiyemfahamu yule kachero machachari anayejulikana katika jiji lote la Dar es Salaam. Kwani imekuwaje bosi?”

“Basi, yeye ndiye mpelelezi wa kesi ya mauaji ya Anita, ambapo nimehakikisha mwenyewe baada ya kupata taarifa kwa mtu wangu aliyemwona alipokwenda kuchunguza katika eneo la tukio kule makaburini, wakati akilishughulikia lile tukio, baada ya sisi kulifukua usiku. Hivyo ndugu zangu, kama Malik akigundua kama ni sisi tunahusika, basi mjue tumekwisha, kwani polisi watagundua shughuli zetu zote tunazofanya!”

“Aisee?” Chikwala akasema.

“Mh!” Robi akaguna, lakini wale vijana wengine, Kessy, Chogolo, Shabani na Muba wakabaki wameyatumbua macho yao!

“Basi, kuanzia sasa!” John Bosho akaanza kutoa maagizo kwa vijana wake. “Nakuteua wewe Chikwala, kumfuatilia Inspekta Malik popote pale alipo, na anapotembelea. Utakapopata mwanya mlipue mara moja! Sijui umenipata?”

“Bosi, nimekupata vizuri sana, hakuna tatizo. Kazi hiyo nitaifanya na matokeo yake utayaona!”

“Vizuri sana! Huo ndiyo moyo wa kijasiri! Unafaa kwa kazi hiyo!”  John Bosho akamwambia.“Tena nitaanza kumfuatilia leo hii, kwani sehemu zote anazostarehe nazifahamu sana!” Chikwala akaendelea kusisitiza na pia kujiamini.

“Ok, nakuamini sana, basi fanya hivyo. Na nyie wengine mtabaki mkiwa macho na kujiandaa kwa jambo lolote ambalo linaweza kutokea. Pia, msizime simu zenu kwani wakati wowote mnaweza kupokea maagizo kutoka kwangu kadri mambo yanavyokwenda!”

“Sawa bosi, tumekuelewa!” Wote wakasema kwa pamoja kudhihirisha wamemwelewa.

“Ok, tunaweza kuendelea na shughuli nyingine!” John Bosho akawaambia vijana wake na wote wakamwelewa.

Kikao kikafungwa.

Wakati huo ilikuwa imetimu saa saba za mchana siku ya Jumamosi ya mtafutano!

********  

CHIKWALA Bwanga alikuwa ni kijana hatari anayeijua kazi yake, tokea alipojiunga na kundi lile linaloongozwa na mtu hatari sana, John Bosho. Alikula kiapo cha utii kwa kufanya kazi yoyote atakayopangiwa na bosi wake, hata kama ni kuifuata roho ya mtu kuzimu kama kulikuwa na uwezekano.

Kamwe Chikwala hakuona hurunma yoyote kwa kuutoa uhai wa binadamu mwenzake, ili mradi afanikiwe katika maisha yake! Baada ya kutoka ndani ya chumba kile cha mkutano walipokuwa wanapewa maagizo na bosi wao, Chikwala  aliamua kuianza kazi ile mara moja. Walipofika nje ya bohari, walipanda gari lao, Toyota Corolla, na kuondoka eneo lile la Machimbo ya Mawe, na kurudi katikati ya jiji.

Chikwala aliamua kushukia pale Buguruni Sheli, Barabara ya Nelson Mandela, na wenyewe wakaendelea na safari, kuendelea na mipango mingine. Akiwa amejiandaa vya kutosha, Chikwala alikuwa ameichimbia kibindoni, silaha yake aina ya bastola, iliyosheheni risasi. Ni silaha ambayo huwa anatembea nayo anapokuwa katika kazi muhimu sana inayopaswa kutumika kwa silaha inapobidi!

Baada ya kushuka, akatembea kwa miguu kuifuata Barabara ya Uhuru hadi alipofika eneo la Soko la Buguruni, mkabala na kituo cha daladala kinachotumika kushusha abiria wanaotoka mjini na kwingineko. Lile ni eneo lenye pilikapilika nyingi za watu, wakiwemo wafanyabiashara na wasafiri wanaoshuka na kupanda daladala.

Basi, yeye akaelekea katika baa moja ambayo kwa muda ule wa saa sita za mchana, ilikuwa na uhaba wa wateja, ukizingatia ulikuwa ni muda wa kazi. Baada ya kuingia ndani, Chikwala akatafuta sehemu nzuri iliyokuwa karibu na mlango wa kuingilia na kutokea, halafu akavuta kiti na kukaa huku akiangalia upande wa nje inapopita Barabara ya Uhuru. Ni sehemu ambayo pia aliweza kuwaona watu au askari waliokuwa wanaingia au kutoka ndani ya kituo kile cha polisi.

Hivyo basi, Chikwala aliona pale ndiyo sehemu nzuri ya kuweza kuliwinda windo lake, Kachero Inspekta Malik, na akipata mwanya amlipue kwa risasi.  Ni kweli kwamba Chikwala aliweza kumwona Kachero Inspekta Malik alipokuwa anarudi kwa gari lake, akitokea Tabata, ambapo alikuwa amekwenda kumhoji Bi. Debora, mama mwenye nyumba aliyokuwa amepanga marehemu, Anita. Lakini hakuweza kufanya lolote kwa vile palikuwa na mkusanyiko wa watu wengi na atakachofanya ni lazima akamatwe.

Baada ya kushuka garini, Kachero Inspekta Malik, ambaye hakujua chochote kilichokuwa kinaendelea,  aliingia ndani ya kituo cha polisi, na hakutoka tena, bali aliendelea na kazi nyingine zilizokuwa zinamkabili.  Hata hivyo Chikwala aliyekuwa anamwinda hakukata tamaa, kwani aliendelea kunywa kinywaji kama wateja wengine, na pengine akitaniana na wale wahudumu warembo wa baa ile, waliokuwa wamevalia nguo fupi zilizoyaacha maungo yao wazi.

Ni hadi ilipotimu saa moja za usiku, ndipo Chikwala alipomwona Kachero Inspekta Malik akitoka na kuingia ndani ya gari lake, ambalo alilitia moto na kuliondoa kwa mwendo wa taratibu kwa kuifuata Barabara ya Uhuru hadi alipofika kwenye taa za trafiki, kwenye makutano ya barabara ile ya Uhuru na ya Nelson Mandela, gari la Malik likaifuata Barabara ya Mandela na kwenda kusimamishwa mbali kidogo na maegesho ya Kimicho Bar, iliyoko kando ya barabara hiyo ya Mandela, eneo la Buguruni.

Chikwala ambaye alitoka ndani ya baa ile kumfuatilia, aliongeza mwendo kwa kutembea kwa miguu, ili amuwahi Malik asije akampotea na itakapobidi, ndipo angekodi teksi kumfuatilia. Chikwala alifanikiwa kuliona gari la Malik,  lakini alichelewa na kumwona akishuka na kuingia ndani ya baa ile ya Kimicho. Akamfuatilia ndani ya hiyo baa aliyoingia, halafu akaenda kukaa sehemu iliyokuwa na uficho, na kuendelea kumchunguza kwa makini kwa kila anachofanya.

Hakika ilikuwa ni kazi ngumu sana kwa kumwinda mtu zaidi ya saa sita, lakini kwa mtu kama yeye alishazoea. Muda wote ule alikuwa ana silaha yake kibindoni, pamoja na simu, ambayo muda wote alikuwa akiwasiliana na John Bosho kwa kila hatua inavyokwenda. Hata hivyo baada ya kukaa kwa muda, Chikwala akaona afanye jambo moja. Akajifanya kama anakwenda msalani na kupita karibu na alipokuwa amekaa Kachero Inspekta Malik, ambapo palikuwa na giza kiasi lililosababishwa na mwanga hafifu wa taa ya rangi ya kijani iliyokuwa inamulika eneo hilo.

Chikwala aliyatupa macho yake katika pande zote za ukumbi wa baa ile ya Kimicho. Wateja wengi walikuwa wakiburudika na vinywaji na wengine wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika vipindi vya runinga, akiwemo Kachero Inspekta Malik. Utulivu ule ukampa mwanya Chikwala apange cha kufanya, ambapo ni kitendo bila kuchelewa!

Akachomoa bastola yake!

********       

AWALI Kachero Inspekta Malik alipolipaki gari lake mbali kidogo na Kimicho Bar, kando ya Barabara ya Nelson Mandela, ilikuwa imetimu majira ya saa moja na nusu za usiku. Alishuka na kulifunga gari lake vizuri, kisha akaondoka kwa mwendo wa taratibu na kuingia ndani ya baa hiyo iliyokuwa na ukumbi mkubwa wa kuchezea dansi.

Mbali ya kuwa na ukumbi wa dansi, pia kulikuwa na kumbi nyingine na sehemu za kukaa wateja wanaofika kwa ajili ya kujipatia vinywaji. Baada ya kuingia, alitafuta sehemu nzuri ya kukaa, ndani ya ukumbi wa vinywaji, iliyokuwa kwenye kona, ambapo aliweza kuwaona watu waliokuwa wanaingia ama kutoka ndani ya baa ile.

Huo ni utaratibu aliokuwa amejiwekea ili aweze kuona watu waliokuwa wanaingia na kutoka. Mhudumu, mwanadada mrembo wa haja alipomwendea, alimwagiza kinywaji, bia mbili aina ya Safari, ambayo alipendelea kunywa. Na baada ya kuhudumiwa, Kachero Inspekta Malik akaendelea kunywa taratibu huku akiangalia runinga iliyokuwa ikiendele na vipindi vyake, na pia akiangalia watu waliokuwa wakiingia na kutoka ikiwa ni moja ya sehemu yake ya kazi.

Lakini wakati Kachero Inspekta Malik akiwa amezamisha mawazo yake katika kazi ile iliyokuwa inamkabili, ghafla akasogeza mkono wake wa kulia ambao uliigusa glasi iliyokuwa na pombe pale juu ya meza. Baada ya kuigusa glasi ile,  ikadondoka chini na kupasuka vipande vipande ambavyo vilitawanjika sakafuni! Malik akajiuliza imekuwaje? Akainama haraka kwa ajili ya kuangalia pale sakafuni jinsi glasi ile ilivyosambaratika. Ni kitendo kilichochukua kama sekunde moja hivi.

Lakini ghafla tena, milio miwili kama ya nyuki ilimpitia karibu na kichwa chake, halafu ikafuatiwa na mlipuko wa risasi! Ni risasi ambazo ziligota ukutani nyuma yake na kuchimba katika ukuta na kumrushia vipande vya mchanga mwilini! Tuseme kama angechelewa tu, basi risasi zile zingefumua kichwa chake mara moja! Kutokana na milio ile ya risasi, watu waliokaa ndani ya baa, wakaanza kutawanyika kila mmoja kivyake.

Kwa haraka Kachero Inspekta Malik akalala chini na kuanza kutambaa kama nyoka kuelekea mlangoni, huku akikwepa viti vilivyokuwa vimezagaa ovyo baada ya watu kukimbia. Alipofanikiwa kutoka nje ya baa ile, akamwona mtu mmoja akikimbia kwa kasi huku akirusha risasi ovyo angani, akikimbilia usawa wa kituo cha mafuta kilichoko karibu na taa za trafiki, kwenye makutano ya Barabara za Uhuru na Mandela.

Watu wakaendelea kukimbia ovyo kila mmoja akitaka kunusuru maisha yake. Hakuna asiyejua madhara ya risasi. Mtu yule aliyekuwa anakimbia, ni Chikwala, ambaye alitaka kuvuka barabara kuelekea upande wa pili ili kuyawahi magari yaliyokuwa yanasubiri kuruhusiwa na taa ya kijani. Alipoanza kuvuka tu, ndiyo magari yalikuwa yameruhusiwa na taa, hivyo gari moja aina ya Mitsubishi Pajero lililokuwa upande wake, lilimgonga punde tu alipoutua mguu wake barabarani, akarushwa juu na kutua kando ya barabara!

Gari lililomgonga Chikwala halikusimama zaidi ya kuongeza mwendo kuelekea eneo la Ubungo. Damu ikatapakaa pale barabarani alipoangukia Chikwala, huku umati wa watu ukikisanyika kumwangalia, wengine wakiwa ni vibaka waliokuwa na madhumuni ya kumsachi. Kachero Inspekta Malik hakuchelewa kufika sehemu ile alipoangukia huyo mtu na kuwasukuma watu waliokuwa pale na kumfikia  tayari kwa kuanza kumpekua na pia kumtambua ni nani?

Baada ya upekuzi wa awali, Kachero Inspekta Malik alimkuta Chikwala akiwa na bastola moja aina ya ‘Star’ iliyokuwa imedondoka kando yake huku ikifuka moshi wa baruti. Lakini simu yake ya mkononi, ambayo nayo iliangukia mbali kidogo, iliokotwa na mmoja wa watu waliofika kwa ajili ya kutoa msaada, ambaye alitoweka nayo.

Malik akaiokota ile bastola na kuihifadhi, halafu akaendelea kumchunguza na kumkuta bado akihema kwa mbali. Ili kupata machache kutoka kwake, akamwinua kichwa chake na kukiegemeza kwenye goti lake, na pia akimpatia huduma ya kwanza kwa kumpepea!

“Haloo…vipi hali yako?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza.

“Oh…Oh…” Chikwala alikuwa anaguna kwa maumivu!

“Hebu niambie…jina lako nani?” Kachero Inspekta Malik akaendelea kumuhoji.

“Oh, naitwa Chikwalaaa…Oh!”

“Chikwala?”

“Ndi…yooo…oh!”

“Nani kakutuma kufyetua risasi?”

“Oh…nimetumwa…nikuue…oh!”

“Umetumwa na nani?”

“Hik… hik!…” Chikwalaa akatoa kwikwi na kuendelea.

“Ni nani kakutuma?” Kachero Inspekta Malik akaendelea kumuuliza.

 “Nimetumwa na yule aliyemuua Anita…hik…hik…!” Chikwala akaendelea kusema kwa shida kuonyesha kutokuwa na matumaini ya kuishi tena, ukizingatia damu zilikuwa zinamtoka kwa wingi katika sehemu mbalimbali za mwili!

 “Chikwala…” Kachero Inspekta Malik akaendelea kumwambia na kuongeza. “Hebu niambie jina la mtu huyo aliyekutuma kuniua mimi tafadhali…”

“Hik! Oh!” Chikwala aliendelea kutoa kwikwi mfululizo na hakuweza kusema kabisa. Akaendelea kutoa macho yake hadi alipokata roho na kukilaza kichwa chake!

“Shenzi sana!” Kachero Inspekta Malik akasema kwa hasira! Ukweli ni kwamba alikuwa amechukia baada ya kushindwa kulipata jina la muuaji wa Anita!

Hata hivyo muda siyo mrefu, gari moja la polisi aina ya Toyota Land Cruiser Hard Top, lilifika pale likiwa na askari polisi kumi. Kachero Inspekta Malik akajitambulisha, halafu akamwita kiongozi wa askari wale, aliyekuwa na cheo cha Sajini na kumpa maagizo.

“Sajini!”  Kachero Inspekta Malik akamwita.

“Afande,” akaitikia Sajini.

“Pelekeni maiti hii katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na muikabidhi, kwani huyu ni mtuhumiwa aliyefyetua risasi muda siyo mrefu, mimi nitakuja baadaye!”

“Sawa afande…” akaitikia Sajini yule wa polisi.

 Askari wale hawakupoteza muda, wakauchukua mwili wa Chikwala na kuupakiza ndani ya gari lao, kuupeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Ule umati wa watu ukatawanyika baada ya askari wale kuondoka.

Baada ya gari lile la polisi kuondoka, Kachero Inspekta Malik aliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, ambaye naye hakukawia kufika katika eneo lile la tukio.

Wakati huo askari wengine wa doria walikuwa wamejaa na na kulizunguka eneo lote la Kimicho Bar, kutokana na ile Mirindimo ya risasi iliyolipuliwa na Chikwala. Malik na Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo, wakishirikiana na askari wengine wakafanya uchunguzi wa awali, ambapo walifanikiwa kuyapata yale maganda mawili ya risasi. Wakayachukua na kuyaweka katika mfuko laini wa nailoni kisha wakarudi tena kituoni na kuyahifadhi katika ghala la silaha.

Alfred Gonzo, ambaye alishtushwa na shambulio dhidi ya kijana wake, Kachero Inspekta Malik, hakuishia pale, bali alimwambia Malik waelekee katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakaikague ile maiti ya Chikwala, kama atakuwa ni mmoja wa majambazi wanaotafutwa na polisi kutokana na kufanya matukio mengi ya kihalifu.

Walitumia gari la Malik na kuelekea Muhimbili, huku Malik akiwa na mawazo mengi sana juu ya mtu yule aliyemkosakosa kwa risasi! Malik alijiuliza kuwa, Je, ni nani aliyemtuma? Ama kweli kifo cha Anita kilikuwa na usiri mkubwa! Hata hivyo ilimbidi awe macho kwa kujilinda na watu wale, ambao ilionyesha walikuwa wamejizatiti!  Walipofika Muhimbili, Alfred Gonzo na Inspekta Kachero Inspekta Malik, walifikia sehemu ya mapokezi na kujitambulisha, ambapo waliruhusiwa kuuangalia mwili ule wa Chikwala.

Mwili huo ulikuwa umehifadhiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti, ukiwa umelezwa katika machela. Wakauangalia kwa makini lakini hawakuweza kumtambua, hivyo wakaondoka na kusubiri mpaka kesho yake watakapojitokeza ndugu zake baada ya kutolewa taarifa juu ya mtu aliyegongwa na gari alipokuwa katika harakati za kukimbia baada ya kufyetua risasi katika tukio ambalo huwezi kuliita la kijambazi!

Walipotoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ilikuwa yapata majira ya saa tano za usiku. Foleni ya magari haikuwepo usiku ule kiasi cha kuwasaidia kupunguza urefu wa safari yao. Baada ya kumshusha Mkuu wa Upelelezi, Gonzo kituoni, Malik akaelekea  nyumbani kwake, Shariff Shamba, kupumzika kutokana na uchovu wa siku ile.

Kachero Inspekta Malik alipofika nyumbani kwake, Ilala, Shariff Shamba, ilikuwa imetimu saa sita za usiku. Akalipaki gari ndani, sehemu ya uani, halafu akashuka na kuingia ndani, ambako aliwakuta wadogo zake, Toni na James wakimaliza kujisomea, na pengine kumsubiri yeye, akawasalimia na kupitiliza moja kwa moja hadi chumbani ili kufanya utaratibu wa kuoga na kuondoa uchovu wa mchana kutwa.  Baada ya kumaliza kuoga, hakuwa na hamu ya kula chakula kabisa, hivyo akajitupa kitandani huku akiwazia upelelezi wake!

********    

SAA moja kabla Chikwala Bwanga hajafayetua risasi ndani ya Kimicho Bar, Buguruni, John Bosho alikuwa amebanisha mafichoni, sehemu maalum, akifuatilia nyendo za Chikwala. Kutwa nzima tokea alivyompa ile kazi ya kumfuatilia Kachero Inspekta Malik, alijaribu kuwa naye sambamba, na muda wote simu haikumtoka mkononi, akitaka kupata taarifa kwamba kachero huyo mahiri ameshauawa.

Ni mpaka ilipotimu majira ya saa mbili za usiku, ndipo Chikwala alipomjulisha kuwa alikuwa anamfuatilia Kachero Inspekta Malik, ambaye alikuwa ameingia ndani ya Kimicho Bar, Buguruni muda siyo mrefu.

“Bosi…nimemwona Malik…” Chikwala alimjulisha baada ya kumpigia simu.

“Unasema umemwona?” John Bosho akamuuliza!

“Ndiyo…ameingia Kimicho Bar…” Chikwala akamwambia.

“Usifanye makosa, mfuatilie na kumlipua hukohuko”!

“Nitafanya hivyo mkuu!”

“Ok, baada ya kufanikisha unijulishe!”

“Nitakujulisha bosi…”

Baada ya mawasiliano yale, John Bosho akawa anaendelea kusubiri matokeo. Lakini baada ya nusu saa nzima kupita, tokea awasiliane na Chikwala, akajaribu tena kumpigia simu, ambayo iliita kwa muda halafu ikapokewa na mtu mwingine!

“Chikwalaaa…”  John Bosho akasema kwa hamaki!

“Hapana…mimi siyo Chikwala…” upande wa pili ukasema na kumshtukiza John Bosho!

“Ni nani sasa?”

“Ni msamaria mwema tu…”

“Mh, mbona sikuelewi?”

“Utanielewa tu…sikiliza!”

“Unasema?”

“Hii simu ni ya mtu aliyegongwa na gari muda siyo mrefu…”

“Amekufa?”

“Ndiyo, nafikiri amekufa…na maiti yake imechukuliwa na askari polisi kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili…”

“Amechukuliwa na polisi?”

“Ndiyo, kwani ni ndugu yako?”

“Ni ndugu yangu…”

“Basi, mfuatilie Muhimbili…”

“Wewe ni nani…halooo…”

“Nenda Muhimbili…kwaheri…”  mtu yule akasema.

Halafu akaizima ile simu!

John Bosho akawa kama mwendawazimu baada ya kuzisikia habari zile. Na ile ilikuwa ni kwa sababu walikuwa wameshaongea na Chikwala muda siyo mrefu na kusema kwamba alikuwa anamfuatilia Kachero Inspekta Malik amlipue! Sasa imekuwaje tena?

Hakupata jibu!

John Bosho alikurupuka na kuwasiliana na vijana wake wawili, Robi na Chogolo, ambao baada ya kuwapata akawaelekeza tukio lilivyotokea na walipolifuatilia katika vyanzo vingine vilivyokuwa Buguruni, ndipo walipozipata habari kamili! Chikwala alikuwa amekufa baada ya kugongwa na gari wakati alipokuwa anakimbia baada ya kufyetua risasi ndani ya Kimicho Bar.

John Bosho akawapa majukumu vijana hao, Robi na Chogolo, kwa kutumia simu yake ya mkononi, kuwa wamfuatilie hatua kwa hatua, Kachero Inspekta usiku uleule, mpaka nyumbani kwake, Shariff Shamba, Ilala na kuhakikisha wanamwingilia kigaidi ndani kwake na kumlipua mara moja! Kamwe hakupenda wampe nafasi hata kidogo, kwani angewaharibia mambo yao!

Vijana wale hatari walijiandaa, halafu wakaenda katika maficho yao na kuchukua silaha zao, bunduki moja fupi, aina ya Uzi Gun, pamoja na bastola moja. Wakapanda gari lao, Toyota Corolla na kuelekea nyumbani kwa Kachero Inspekta Malik, ambapo walikuwa wanapafahamu. Kwa vile walikuwa na ufunguo wa bandia, hawakuwa na wasiwasi wowote wa kuingia ndani ya nyumba hiyo iliyokuwa katika makazi ya watu na kumpata mhusika wao pasipo kushtukiwa na mtu yeyote!

Usiku ule kulikuwa kimya kabisa, na baada ya kutoka huko kwenye maficho yao walipokwenda kuchukua silaha zao, Robi alikuwa anaendesha gari lile kwa mwendo wa kawaida akiifuata Barabara ya Uhuru, kama anaelekea katikati ya jiji. Muda huo wa saa saba za usiku, magari yalikuwa ni machache sana nay a kuhesabika tu barabarani, na walipofika eneo la Bungoni, Ilala, Robi alikata kushoto na kuifuata barabara nyingine ya udongo iliyokuwa inakatiza katika makazi hayo ya watu, kuelekea eneo la Shariff Shamba.

Waliifuata barabara hiyo, ambayo ilikuwa na nyumba  za wakazi pande zote. Kwa mbali kama mita ishirini hivi, waliiona nyumba ya Kachero Inspekta Malik Mkoba, ambayo  ilikuwa imezungukwa na uzio wa ukuta na mbele yake kukiwa na geti kubwa la chuma. Wakaiendea nyumba hiyo kama vile walikuwa ni wapiti njia tu wanaopita kwa gari lao! Mtaa huo ulikuwa kimya kabisa, labda na mambwa koko na mapaka shume yaliyokuwa yakizunguka kwenye mapipa ya takataka kutafuta makombo ya vyakula.

“Nafikiri unaiona nyumba ya Malik?” Chogola akamwambia Robi aliyekuwa anaendesha gari.

“Nimeiona, si hiyo hapo mbele?” Robi akasema huku akiiangalia kwa makini

“Sasa usisimaishe gari hapo karibu, twende mbele kidogo…” Chogolo akamwambia.

“Ni kweli, ngoja nikasimame pale mbele, karibu na mti wa mkungu, ili tuweze kupoteza lengo…”

“Ni jambo la maana…tusipende adui atutambue haraka!”

Robi akaendelea kuendesha gari kuelekea mbele kidogo, halafu akalipaki gari karibu na mti mmoja mkubwa wa mkungu. Wakabaki ndani ya gari kwa muda huku wakijipanga cha kufanya, kabla ya kumwingilia kachero huyo waliokuwa wanamfuatilia!

“Unajua kabla ya kumwingilia Malik, lazima tusome mazingira?” Robi akamwambia Chogolo.

“Ni kweli, lazima tujue pa kuingilia na kutokea, si unajua mtu huyo ni askari mahiri? Lazima tujipange…” Chogolo akasema.

“Nimeona hapo nje kwake, karibu na uzio kuna mti mmoja wa mwembe, ambao umezungukwa na miti mingine ya muarobaini…”

“Ni kweli, hata mimi nimeuona…”

“Tena una matawi makubwa yanayoshukia ndani . Hivyo hapo ndipo tutakapopitia na kuingia ndani kama nyani vile!” Robi akamwambia mwenzake.

“Poa, kama ni hivyo, basi tujiandae kwenda, akitokea mtu wa kututibulia mpango wetu tu, ni kumlipua mara moja!” Chogolo akasema huku akiikamata bunduki yake vizuri!

Wakajiandaa kushuka!

********

MTAA mzima wa Shariff Shamba, Ilala, ulikuwa kimya kabisa usiku ule wa aina yake. Akiwa ni askari shupavu anayelala kiaskari, ilipotimu majira ya saa saba za usiku, Kachero Inspekta Malik Mkoba alishtuka kutoka usingizini, ikiwa ni baada ya kuusikia muungurumo wa gari lililokuwa linapita katika ule mtaa mdogo usiokuwa na jina, jirani kabisa na ukuta wa uzio wa nyumba yake.

Ukweli ni kwamba haikuwa kawaida kwa gari kupita katika mtaa huo usiku mwingi namna hiyo, hivyo machale yakamcheza Malik na kuanza kuhisi hali ya hatari. Akanyanyuka kutoka hapo kitandani, halafu akaliendea dirisha kubwa lililokuwa upande unaotazama barabarani karibu na uzio wa ukuta ulioizunguka nyumba yake. Akalifungua pazia na kuchungulia nje, ambapo aliweza kupaona viziri kwa kupitia kwenye matundi yaliyokuwa kwenye uzio.

Baada ya kuchungulia, akaliona gari moja dogo aina ya Toyota Corolla lenye rangi nyeupe, limesimamishwa mbali kidogo na ilipo nyumba yake, chini ya mti wa mkungu. Pia,  sehemu iliyokuwa na miti ya muarobaini iliyofungamana na kufanya kuwe na giza kiasi. Hakuyabandua macho yake katika gari hilo, na baada ya muda akawaona watu wawili wakishuka, wote  wakiwa wamevalia mavazi yaliyoshabahiana na giza, pamoja na kofia kubwa zilizoweza kuficha sura zao.

 Kwa usiku ule watu hao walikuwa wanatisha sana, na waliposhuka, wakaanza kutembea kwa mwendo wa taratibu kuifuata nyumba yake. Wotewalionekana kuwa na silaha, Robi alikuwa na bastola mkononi na Chogolo alikuwa amekamata bunduki fupi aina ya ‘Uzi Gun,’ iliyotengenezwa nchini Israel. Kwa tahadhari kubwa, Malik akajitoa pale dirishani na kuiendea bastola yake iliyokuwa imesheheni risasi, halafu akarudi hapo dirishani na kujiweka tayari kwa lolote litakalotokea!  

Watu hao waliokuwa wanaijongelea nyumba yake walikuwa ni Robi na Chogolo, vijana wa John Bosho, ambapo alikuwa amewatuma kumsaka yeye tena, na kuhakikisha wanammaliza baada ya kumkosakosa mara ya kwanza! Walitembea hadi walipofika karibu na ukuta wa uzio, ambapo palikuwa na mti mmoja mwingine wa mwembe. Ni mti ambao matawi yake yalikuwa yameingia hadi sehemu ya ndani ya ua ule. Hivyo wakaupanda mti huo kwa ufundi mkubwa na kutua ndani bila kishindo, na baada ya kutua ndipo walipouendea mlango wa kingilia mle ndani.

Ukweli ni kwamba mambo yao walikuwa wakiyafanya kwa utulivu wa hali ya juu kiasi kwamba hata majirani wa nje hawakuweza kujua zaidi ya yeye Malik. Mara Malik akasikia mlango huo wa mbele kabisa, unaotokeza sebuleni ukifunguliwa kwa kutumia ufunguo bandia, tena kwa utaratibu bila kufanya kelele za aina yoyote. Baada ya mlango kufunguliwa, akaona watu wale wakiingia hadi pale sebuleni na kusimama huku wakiongea kwa sauti ya chini, kuashiria kwamba walikuwa wanakitafuta chumba cha anacholala.

Pale alipokuwa amesimama kachero Inspekta Malik, alikuwa akiwaangalia tu, na jirani yake palikuwa na swichi maalum, ambayo ikiwashwa hutoa mlio wa king’ora, kwa ajili ya kudhibiti wezi, au jambo lolote la hatari linapotokea! King’ora hicho alikuwa amekifunga muda mrefu sana kwa ajili ya kujihami, akiwa kama askari aliyeamua kuishi uraiani. Na kweli siku hiyo ndipo alipoona alifanya la maana baada ya kuingiliwa na wale wakora wawili, Robin na Chogolo. Hivyo, kabla Robin a Chogolo hawajanyanyua hatua, Malik akabonyeza kile king’ora ambacho kilianza kutoa mlio mkali sana, kitu ambacho kiliwafanya washtuke katika giza lile!

Chogolo na Robi wakaangaliana mara baada ya kuusikia mlio huo wa king’ora, ingawa hawakuonana hapo sebuleni kutokana na giza! Wakaona usalama wao ukiwa mdogo mara baada ya kuingia ndani ya himaya hiyo ya mpiganaji mahiri!

“Robi!” Chogolo akaita kwa sauti ndogo!

“Sema mtu wangu!” Chogolo akasema huku akiyatumbua macho yake katika giza!

“Unaona hatari inayotukabili lakini?”

“Ni kweli naiona mshikaji, ni sawa na kuingia katika choo cha kike!”

“Jamaa kajiandaa, na siyo muda mrefu atatunyeshea mvua ya risasi!”

“Ni kweli! Tuanze!”

Baada ya Robin a Chogolo baada kushauriana, waliamua kutoka mle ndani kwa kasi, huku kile king’ora kikiendelea kulia. Wakaufikia uzio wa ukuta ambao waliuruka na kutua nje kisarakasi, na kulikimbilia gari lao ambalo lilikuwa umbali mfupi tu kutoka kwenye nyumba hiyo. Walipolifikia wakapanda haraka haraka na Robi akaliondoa kwa mwendo wa kasi kwa kuufuata mtaa ule mdogo na kupotea gizani!

Hapo ndipo Kachero Malik alipojitoa mafichoni na kwenda kuufunga ule mlango mkubwa kama ulivyokuwa mwanzo ikiwa ni baada ya kukizima kile king’ora alichofunga. Hali ikarudi shwari kama mwanzo kama vile hakikutokea chochote, hivyo akaamua kufanya uchunguzi wa awali, na akaona kuwa hakuna kitu chochote kilichoguswa pale sebuleni, zaidi ya mlango ule mkubwa, uliofunguliwa kwa ufunguo bandia.

Pia, Kachero Inspekta Malik aligundua kuwa watu wale walipitia kwa kuuruka uzio wa nyumba yake kitu ambacho kiliwafanya wafanikiwe kuufungua mlango ule. Kutokana na hali hiyo, akajua kuwa vita vilikuwa vimeanza, ambapo aliunganisha tukio hilo la hapo nyumbani kwake, na lile la kuvamiwa ndani ya baa ya Kimicho, usiku usiku wa siku ile. Pia, aliunganisha na tukio la mauaji ya mwanadada Anita. Hivyo akaona mauaji hayo yana uhusiano wa karibu kwa kuwa na mkono wa mtu aliyekuwa akipanga mipango ile michafu!

Hata hivyo kwa kujihami, Kachero Inspekta Malik alipiga simu katika Kituo cha Polisi Buguruni, na kuwajulisha juu ya tukio hilo. Haikuchukua muda mrefu, askari polisi wa doria waliokuwa kwa magari na miguu wakaanza kufanya msako wa nguvu kuwasaka watuhumiwa hao, Robi na Chogolo, ambao walikuwa wameshaondoka na kukimbilia kwenye ngome yao iliyoko Machimbo ya Mawe!

Hivyo hawakupatikana!

********        

MZEE Bwanga Feruzi alizipata habari za mtoto wake, Chikwala, kugongwa na gari eneo la Buguruni Sheli, katika Barabara ya Mandela, na maiti yake imepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Yeye alikuwa ni baba yake mzazi  Chikwala, akiwa mtoto wa tatu, kati ya watoto wake sita aliowazaa.

Baada ya kuzipata habari hizo, wanandugu walijikusanya na kupanga shughuli za msiba, zilizopangwa kufanyika nyumbani kwao, Yombo Dovya, Wilayani Temeke. Mzee Bwanga na wenzake wakaelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kufanya taratibu za kuichukua maiti hiyo, lakini wakanyimwa na kuambiwa wawasiliane na Jeshi la Polisi kwanza kama maagizo yalivyokuwa yametolewa.

Kachero Inspekta Malik Mkoba alipigiwa simu kesho yake asubuhi, wakati alipokuwa ameshafika ofisini kwake. Baada ya kuhakikisha ameshughulikia mafaili kadhaa, haraka sana alipanda gari lake na kuondoka kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa ajili ya kufanya mahojiano na mzee Bwanga, ili aweze kuupata ukweli wa kifo cha mtoto wake, Chikwala.

Hatimaye Kachero Inspekta Malik alifika hapo hospitali na kulipaki gari lake katika sehemu ya maegesho. Akashuka na kuelekea katika ofisi ya Daktari Kenedy Mushumbuzi, ambaye ndiye anayeshughulika na maiti zenye utata. Baada ya kumwona daktari huyo, ndipo alipokutanishwa na mzee Bwanga Feruzi., aliyekuwa amefuatilia maiti ya motto wake, Chikwala.

Mzee Bwanga alikuwa amevalia shati la rangi nyeupe iliyofifia karibu ifanane na rangi ya kahawia, na suruali ya rangi ya ugoro. Kichwani mwake alikuwa amevalia kofia ya baraghashia iliyofubaa, na pia iliyoweza kuonyesha nywele zake chache zilizokuwa na mvi chini yake. Chini miguuni alikuwa amevalia makubazi. Baada ya kukaa katika sehemu ya faragha, akamwita mzee huyo na kuanza kumhoji, ukiwa ndiyo utaratibu wa polisi.

“Kwanza kabisa pole na msiba…” Kachero Inspekta Malik akamwambia mzee Bwanga.

“Ahsante sana baba…ni kazi ya Mungu, kama alipanga mwanagu afe kwa kifo hicho, basi ndiyo yametimia…” mzee Bwanga akasema huku akionyesha mwenye huzuni sana.

“Basi, mzee, kwa utaratibu wetu wa kipolisi, naomba kukuhoji maswali machache kwa vile marehemu kabla ya kupatwa na umauti nilimwona.” Kachero Inspekta Malik akamwambia mzee Bwanga.

“Unasema ulimwona?” Mzee Bwanga akamuuliza huku akiwa bado amepigwa na butwaa!

“Ndiyo, nilimwona,” Kachero Inspekta Malik akasema na kuongeza. “Yeye alikuwa amedhamiria kuniua mimi kwa risasi, lakini akanikosa, ndipo alipokimbia na hatimaye kugongwa na gari!”

“Alitaka kukuua?” Mzee Bwanga akauliza huku amekunja sura yake!

“Ndiyo…alitaka kuniua…”

“Kukuua kwa sababu gani?”

“Sijui, ndiyo maana nataka kukuhoji ili niweze kuujua ukweli, kwa kuijua historia ya marehemu kwa vile wewe ndiye mzazi wake.”

“Sawa, baba, unaweza kunihoji tu…”

“Naomba unieleze historia fupi ya marehemu mwanao…”

“Kwa jina anaitwa Feruzi Chikwala Bwanga, ambaye nilimzaa miaka thelathini iliyopita huko Kisarawe. Amesoma mpaka kidato cha nne na baada ya hapo akajiajiri mwenyewe…”

“Je, unajua kazi aliyokuwa anaifanya mwanao?”

“Ndiyo…”

“Ni kazi gani?”

“Biashara…alikuwa anauza katika duka la vifaa vya ujenzi…”

“Ni duka lake?”

“Hapana, si lake…”

“Ni la nani?”

“Ni la tajiri mmoja ambaye hata mimi simfahamu…Chikwala alikuwa msiri sana!”

“Je, ameoa?”

“Hapana hajaoa…”

“Anaishi wapi?”

“Hata sijui…”

“Yaani hujui mwanao anaishi wapi?”

“Alikuwa msiri sana mtoto yule…oh!”

“Basi, mwanao alikuwa jambazi!”

“Unasema kweli?”

“Ni kweli. Kwa sababu alitaka kuniua mimi kwa vile nafuatilia kesi fulani…”

“Basi, mimi ndiyo kwanza nasikia hayo!”

“Kama ndiyo kwanza unasikia, basi ujue hilo. Ni jambazi anayeshirikiana na huyo tajiri yake katika kuendesha vitendo viovu!”

“Mh, mtoto ana laana huyo!” Mzee Bwanga akasema huku akitikisa kichwa chake!

“Inawezekana ana laana, ndiyo maana yamemkuta hayo…” Kachero Inspekta Malik akamuunga mkono!

“Sasa naomba utaratibu wa kuuchukua mwili wa marehemu…” mzee Bwanga akamwambia.

“Sawa mzee, nakuruhusu kuuchukuwa mwili wa mwanao kwa ajili ya maziko….” Kachero Inspekta Malik akamwambia mzee Bwanga.

“Sawa kijana wangu…” mzee Bwanga akashukuru na kwenda kuungana na wenzake kuendelea na taratibu za kuuchukua mwili wa marehemu.

Kachero Inspekta Malik aliamua kuwaruhusu baada ya kuwasiliana na Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo. Hawakuona haja ya kuizuia maiti ile, kwani haikuwa na uwezo wa kusema!

********           

JUMAPILI asubuhi majira ya saa tatu, kama kawaida ilimkuta Kachero Inspekta Malik akiwa eneo la Tabata Mawenzi katika nyumba aliyokuwa anaishi marehemu Anita. Ni katika juhudi za kuendelea na upelelezi wake, kwani alikuwa amemwahidi mama mwenye nyumba, Bi. Debora, kwamba angerudi tena kesho yake baada ya kuichukua ile albamu ya picha na picha mbili zilizokuwa kwenye bahasha ya khaki.

Baada ya kusalimiana, Kachero Inspekta Malik alimwomba Bi. Debora waongee tena kuhusu marehemu Anita. Wakaongozana wote mpaka pembezoni mwa nyumba ile palipokuwa na bustani ya maua iliyokuwa na kivuli, pamoja na viti vya mianzi. Wakakaa pale huku wakitazamana tayari kwa mahojiano.

“Kama nilivyokuelezea tokea jana, nimerudi tena katika upelelezi wangu…” Kachero Inspekta Malik akamwambia Bi. Debora.

“Karibu sana baba…usijali sana…hapa ni nyumbani kwako…” Bi. Debora naye akamwambia.

“Sasa kuna zile picha nilizochukua jana, ambazo nimezichunguza sana na kuona zina watu tofauti tofauti, akiwemo kijana mmoja. Ni kijana ambaye amepiga picha mara nyingi akiwa na marehemu Anita. Hebu chukua hii moja uniambie huyo kijana ni nani, au alikuwa na uhusiano gani na marehemu…” Kachero Inspekta Malik akasema huku akimkabidhi zile picha.

Bi. Debora akazipokea picha hizo na kuanza kuziangalia kwa makini huku akitikisa kichwa na kusema kwa sauti ndogo, “Huyu kijana mimi namfahamu kwa sura tu, na ni mara nyingi alikuwa akimtembelea marehemu, jambo ambalo linaonyesha walikuwa na uhusiano wa karibu.”

“Ina maana hukuwahi kumuuliza marehemu juu ya kijana huyo, akiwa ni mpangaji wako mliozoeana?” Kachero Inspekta Malik akaendelea kumuuliza Bi. Debora.

“Hapana…sikuwahi kumuuliza, na wala sikupendelea kuingilia uhuru wa mtu. Maadam alikuwa ananilipa kodi yangu basi!”

“Aisee, basi ulifanya kosa sana kumuuliza, ukiwa ni utaratibu wa mtu unayeishi naye. Kijana huyo ndiye angetusaidia katika upelelezi wetu, Jeshi la Polisi…” Kachero Inspekta Malik akamwam,bia huku akionyesha kusikitika kidogo.

“Oh, masikini…” Bi. Debora akasema na kuendelea. “Kweli simfahamu kijana huyo, wala sehemu anayoishi hapa Dar au hata anakofanya kazi.”

“Oohps! Basi iko kazi!” Kachero Inspekta Malik akasema huku akivuta pumzi na pia akimwangalia Bi. Debora.

“Labda, ninachoweza kukusaidia mimi, labda uende kwa aliyekuwa rafiki yake wa karibu wa marehemu anayeitwa Getruda…”

“Unasema rafiki yake wa karibu?”

“Ndiyo.”

“Na picha yake iko katika albamu hii?”

“Ndiyo, ni huyu hapa…” Bi. Debora akaonyesha kwenye picha ambayo walipiga na Anita. “Ni wazi kwamba huyo kijana anatambulika na huyo rafiki yake, kwani mara nyingi walikuwa wanaongozana wote…”

Kachero Inspekta Malik akamwelewa vizuri sana Bi. Debora, hivyo akamuuliza swali jingine. “Je, huyo rafiki yake, Getruda, anaishi sehemu gani hapa jijini Dar?”

“Anaishi mtaa wa Moshi, Ilala, nyumba namba 003. Ni nyumba inayotazamana na Kanisa la Anglikana la Ilala, sehemu ambayo huwezi kupotea…”

“Nashukuru sana mama. Mimi natoka na kama kuna mengine nitarudi tena unisaidie,” Kachero Inspekta Malik akamwambia.

“Sawa baba…karibu tena…” Bi. Debora akasema.

Kachero Inspekta Malik alipotoka pale Tabata Mawenzi, aliamua jambo moja tu! Ni kuelekea mtaa wa Moshi, Ilala, anapoishi mwanadada huyo anayejulikana kwa jina la Getruda. Alijua kuwa ni lazima atampata, kwani picha yake alikuwa nayo na hata sura yake aliweza kuikariri na kuiweka kichwani. Alijua fika kuwa, akikutana naye, anaweza kuambulia chochote cha maana, ambacho kitamsaidia kutatua kitendewili kinachomsumbua!

********       

ALIFIKA katika eneo la  Bungoni, Ilala, kwa kuifuata Barabara ya Uhuru, ambayo kwa kiasi fulani ilikuwa na foleni ya magari iliyokuwa inakwenda mithili ya mwendo wa Kinyonga. Kachero Inspekta Malik Mkoba akapinda kulia kulia kuufuata mtaa wa Kasulu, kiasi cha mita ishirini hivi, halafu akapinda tena kushoto kuufuata mtaa wa Moshi huku akitupia macho namba za nyumba zilizokuwa mlangoni.

Mbele kabisa Malik aliliona lile Kanisa la Anglikana, lililozungukwa na uzio wa ukuta. Ni kanisa lililojengwa zamani sana, ambalo lilikuwa katikati ya makazi ya watu. Alipotupa macho kushoto kwake, ndipo alipoiona ile nyumba namba 003 mlangoni, ambayo aliambiwa kuwa anaishi Getruda. Hivyo akasimamisha gari kando ya barabara, halafu akabakia humo ndani ya gari kwa muda wa dakika tano hivi, huku akichunguza eneo lile kwa ujumla kabla ya kushuka.

Kachero Inspekta Malik akaiangalia nyumba ile ya kota iliyokuwa katikati ya nyumba nyingine zilizokuwa katika mtaa ule. Pale barazani alikuwepo msichana mmoja aliyekuwa anashona nguo kwa cherahani, akionekana kama ni mwenyeji katika nyumba hiyo. Pia, akauangalia mtaa ule wa Moshi kwa pande zote, unakoanzia na unakoishia, akaona kuna watu waliokuwa wanapita wakielekea katika shughuli zao, na magari vilevile yalikuwa yanapita ingawa hayakuwa mengi zaidi ya watu waliokuwa na ratiba zao eneo lile.

Ndipo aliposhuka garini na kuiendea ile nyumba kwa mwendo wa taratibu hadi alipomfikia yule msichana aliyekuwa anashona nguo.

“Hujambo binti?” Malik akamsabahi.

“Sijambo…shikamoo…” msichana yule akaitikia huku akimwangalia na kuacha kushona nguo. Mkono mmoja akauacha juu ya Cherahani.

“Marahaba binti…” Kachero Inspekta Malik akaitikia huku akimsogelea karibu.

“Karibu kaka…”

“Ahsante sana…wewe ni mwenyeji katika nyumba hii?” Malik akamuuliza.

“Ndiyo, mimi ni mwenyeji, ninaishi humu ndani…” msichana yule akamjibu.

“Vizuri, kama ni mwenmyeji, naona utanisaidia sana. Naomba kumuulizia dada mmoja anayeitwa Getruda, ambaye nimeelekezwa anaishi hapa…sijui nimemkuta?”

“Hapana, dada Getruda hujamkuta,” msichana yule akamwambia huku akimwangalia kwa makini.

“Aisee?”Malik akasema na kuendelea. “Amekwenda wapi?”

“Amekwenda kusali kanisani.”

“Kanisa hilo hapo?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza akimaanisha lile Kanisa la Anglikana lililopo mtaa wa Moshi.

“Hapana…amekwenda Kanisa Katoliki la Msimbazi, ambalo huwa anasali. Siyo hilo la Anglikana.”

“Basi, nilikuwa na shida naye, kwani ni watu  tunaofahamiana. Lakini hakuna tatizo, namfuata hukohuko. Nitamsubiri mpaka atakapotoke…”

“Haya kaka, karibu…”

Kachero Inspekta Malik akajiondoa pale barazani na kuliendea gari lake, ambalo alipanda na kuodoka katika mtaa huo wa Moshi, kuelekea kwenye Kanisa Katoliki la Msimbazi, ambalo ni kanisa lililoko umbali wa mita mia moja kutoka barabara kuu ya Rashid Kawawa, eneo la Mchikichini. Pia, Kanisa hilo ambalo limejengwa miaka mingi na Wamishenari wa kikoloni, limezungukwa na uzio wa ukuta,  pamoja na femu za maduka ya biashara, na kwa mbele sehemu ya kuingilia pana na geti kubwa la chuma.

Baada ya kufika katika eneo hilo, Kachero Inspekta Malik akalipaki gari lake katika sehemu ya maegesho mbele ya maduka yale, halafu yeye akajisogeza na kusimama karibu na lango kuu la kutokea pale kanisani. Aliamua kusimama eneo hilo ili ammsubiri Getruda atakapotoka, aweze kumtambua na kumfuatilia, na kwa sababu Malik alikuwa na picha yake, akajua asingepata shida ya kumtambua kwa kutumia ujuzi wa kipolisi kwa kuangalia.

Baada ya kusimama hapo kwa muda wa nusu saa nzima, kengele ikagongwa kuashiria kumalizika kwa ibada, hivyo waumini walikuwa mbioni kutoka. Malik akakaa tayari kwa kukodoa macho yake kuelekea katika lango kuu la kutokea!

********  

GETRUDA alikuwa ni mmoja wa waumini wa mwanzo kutoka kanisani. Aliondoka huku akifuatana na waumini wenzake, akiwa na wazo moja tu, kwamba afike kwenye kituo cha daladala, apande daladala kuelekea nyumbani kwake, Ilala, akapumzike ukizingatia alikuwa amechoka kimwili na roho kutokana na matukio yale ya kutisha yaliyokuwa yametokea siku chache zilizopita.

Muda wote nafsi yake ilikuwa ikimsuta Getruda kwa vile alikuwa ametoka kusali, lakini roho yake ikiwa chafu, imekaliwa na shetani, kwa yeye kuhusika kwa asilimia zote na kifo cha rafiki yake, Anita. Hakika mwenyezi Mungu kama angetaka kutoa adhabu kwake, angempatia muda wowote ule kwa vile alikuwa anamkejeli!

Ndivyo alivyowaza!

Hatimaye Getruda alitoka nje ya lango, na kuelekea usawa wa Barabara ya Kawawa kwa mwendo wa taratibu. Muda wote, Kachero Inspekta Malik aliyekuwa amekaa pale karibu na lango, aliendelea kukodoa macho yake, na kwa bahati nzuri aliweza kumwona Getruda akiwa katikati ya watu, ameshika biblia na kitabu cha nyimbo, akitembea mwendo wa taratibu na kuonyesha alikuwa na mawazo mengi sana.

Kachero Inspekta Malik aliendelea kumkazia macho huku akimfuata nyuma. Getruda akavuka Barabara ya Kawawa hadi upande wa pili, kwani alitegemea kupanda daladala kurudi nyumbani kwake. Malik naye akavuka barabara hadi alipofika karibu yake, na kuendelea kumfuata nyuma huku akiusanifu mwili wake uliokuwa umesanifiwa vizuri na pia kutamanisha.

Ni mwili ambao ulikuwa umefichwa ndani ya gauni la kitenge cha Wax, lilishonwa kulandana na mwili wake uliokuwa na umbile tata lililosumbua wanaume wengi, mmoja wapo akiwa John Bosho aliyeamua kumsaliti Anita!

Si mchezo!

Ni hadi walipofika kwenye kituo cha daladala zinazoelekea Kariakoo, Buguruni, Chang’ombe na kwingineko, ndipo Malik alipoamua kujaribu kumwita kwa vile alikuwa na uhakika kuwa ni yeye Getruda.

“Dada Getruda…” Kachero Inspekta Malik akamwita kwa sauti ndogo kana kwamba walifahamiana.

“Bee…” Getruda aliitikia kwa sauti ndogo yenye wasiwasi. Akageuka nyuma na kuangalia aliyemwita.

Malik akamwonyeha ishara ya kumwita kwa mkono!

“Unaniita mimi?” Getruda akamuuliza Malik.

“Ndiyo, ninakuita wewe dada…” kachero Inspekta Malik akamwambia huku akimsogelea na kumtolea tabasamu laini. Baada ya kumfikia wakasalimiana na kupeana mikono. Wakati wote ule Getruda alikuwa bado na wasiwasi na kutomfahamu Malik.

“Nafikiri hunifahamu dada…” kachero Inspekta Malik akamwambia Getruda.

“Ni kweli…sikufahamu… ”

“Vizuri,  kwa jina naitwa Maliki Mkoba …”

“Malik …sawa kaka, unasemaje?”

“Nina shida na wewe, na kwa ufahamisho zaidi, najulikana kama, Kachero Inspekta Malik Mkoba, nimetokea katika Kituo cha Polisi Buguruni, na safari yote hii nimekufuata wewe!”

“Umenifuta mimi?” Getruda akamuuliza Malik huku wasiwasi ukiwa bado umeongezeka!

“Ndiyo, nimekufuata wewe, ili nikuulize maswali machache….”

“Maswali gani tena?”

“Ni kuhusu kifo cha rafiki yako Anita, kwani nimeambiwa alikuwa mtu wako wa karibu. Tafadhali naomba unisaidie dada’ngu!”

“Ah, polisi bwana…” Getruda akasema na kuendelea. “Ni nani aliyekwambia?”

“Ni mama mwenye nyumba aliyokuwa anaishi kule Tabata, anayeitwa Bi. Debora. Natumaini na wewe unamfahamu sivyo?”

“Ndiyo, Bi. Debora namfahamu. Na ni kweli marehemu Anita alikuwa rafiki yangu mkubwa,” Getruda akasema huku akilengwalengwa na machozi, ambayo yalikuwa yanadondoka!

“Oh, pole sana, lakini naona hapa hapafai kuongelea mambo haya. Ni bora twende ofisini kwangu ili tuweze kuongea kirefu,”  Kachero Inspekta Malik akatoa pendekezo.

“Ni sawa tu,” Getruda akakubali.

“Basi, twende kwenye gari langu,” Kachero Inspekta Malik akamwambia.

Wote wawili wakaongozana na kuelekea katika gari lake lililokuwa upande wa pili wa barabara, halafu wakapanda na kuondoka kuelekea katika kituo cha Polisi Buguruni. Kwa muda wote Getruda alijiona kama mtu aliyekuwa ndotoni, baada ya kutokewa na afisa yule wa polisi, anayepeleleza mauaji ya rafiki yake, Anita.

Hakika Getruda alikuwa na wasiwasi hasa ukizingatia kwamba ni yeye aliyeingilia penzi la rafiki yake, baada ya kushawishiwa na John Bosho. Na pia, muuaji wa Anita alikuwa anamfahamu. Hata hivyo akajiapia moyoni kuwa asingemtaja muuaji wa Anita, Samson Kashaga, hasa ukizingatia alikuwa na mtandao mkubwa wa ujambazi!

        ********

KITUO cha Polisi Buguruni kiliwalaki, ambapo Kachero Inspekta Malik Mkoba aliliingiza gari na kulipaki katika sehemu ya maegesho iliyokuwa upande wa pili wa kituo. Wakashuka na kuingia ofisini na kukaa, ilhali Getruda akiisikia harufu ya u-polisipolisi na hata bado akijisikia kama alikuwa katika ndoto fulani isiyoeleweka kabisa!

Bila kupoteza muda Kachero Malik alifungua droo ya kabati na kutoa ile albamu ya picha pamoja na zile picha nyingine zilizokuwa ndani ya bahasha. Akampa Getruda ambaye alianza kuziangalia kwa makini, huku akifungua ukurasa mmoja baada ya mwingine.

Akakubali kuwa alikuwa ameshaziona.

“Vizuri kama umeangalia…sasa naomba unitajie jina la huyu kijana, sehemu anapoishi na  anapofanyia kazi…”  Kachero Inspekta Malik akmwambia Getruda kwa sauti ndogo ya kirafiki, ukizingatia aliuona ule wasiwasi aliokuwa nao!

“Mh!” Getruda akavuta pumzi ndefu na kubaki akimwangalia Malik aliyekuwa anamsubiri amjibu swali lake alilomuuliza.

“Mbona unaguna?”

“Hapana…”

“Hebu nieleze basi…”

“Kijana huyu anaitwa John Bosho, na alikuwa mchumba wa Anita. Pia, walikuwa wamepanga kwamba wangeoana baadaye.”

“Anafanya kazi gani?”

“Ni mfanyabiashara maarufu sana hapa jijini Dar  es Salaam, na mikoani vilevile.”

“Na anaishi sehemu gani?”

“Anaishi Ukonga.”

“Ukonga kubwa…sehemu ipi?”

“Anaishi Ukonga Mombasa, nyuma ya Kambi Kuu ya Askari wa Kutuliza Ghasia Ukonga. Pale amejenga nyumba yake kubwa iliyoko kando ya reli ya kati, ni nyumba nzuri iliyozungukwa na uzio na inaonekana kwa uwazi zaidi….”

“Unaweza kuniambia kuwa kabla ya kifo chake, marehemu alikuwa na mpenzi yupi zaidi ya John Bosho?”

“Kusema kweli Anita alikuwa ni mtu msiri sana ingawa alikuwa ni rafiki yangu mkubwa. Na mambo mengine hakuniambia, hasa yanayohusu yeye binafsi.”

“Je, wakati wa uhai wake alikuwa na maadui wangapi, au aligombana na nani?”

“Anita aliishi vizuri sana na watu . hivyo sidhani kama alikuwa na maadui…” Getruda akamaliza huku akiuficha ukweli mwingine, ukizingatia hata yeye alichangia kifo cha Anita kwa kushirikiana kimapenzi na John Bosho. Lakini hayo hakuyasema!

Ni hatari tupu!

“Sawa Getruda, nashukuru sana kwa msaada wako wa maelezo mazuri uliyonipa. Kwa kiasi fulani yatanisaidia katika upelelezi wangu. Basi, twende nikurudishe nyumbani,” Kachero Inspekta Malik akamaliza huku akinyanyuka.

“Sawa,” Getruda akasema huku naye akinyanyuka. Halafu wote wakatoka nje na kupanda gari la Malik. Safari ya kumrudisha nyumbani kwake, mtaa wa Moshi, Ilala, ikaendelea.

Hatimaye baada ya nusu saa, Kachero Inspekta Malik alimfikisha Getruda nyumbani kwake, na yeye akageuza, akiwa amepanga kurudi nyumbani kwake, Shariff Shamba. Lakini wakati huo njaa ilikuwa inamuuma sana, ukizingatia alikuwa hajala kitu chochote tokea palipopambazuka kutokana na hekaheka zile zinamwandama. Siku zote anapoamua kufanya kazi, kamwe suala la chakula huwa analiweka kando kwanza!

Hata hivyo wazo la kwenda nyumbani kwake aliliacha, hivyo akaamua kuingia katika hoteli Ubena  Resort, iliyoko eneo la Amana, Ilala, ili kujipatia chakula cha mchana. Ni hoteli nzuri inayotoa huduma nzuri ya chakula, hivyo baada ya kuingia na kukaa, akamwagiza mhudumu ampelekee chakula, wali kwa mchuzi na kuku wa kukaanga na bia moja aina ya Safari. Kwa vile huduma ilikuwa ni ya kuridhisha, mhudumu hakukawia kumpelekea kile chakula. Akaendelea kula taratibu, lakini kwa tahadhari ya hali ya juu.

Ukweli ni kwamba, ilimbidi Malik ajilinde hasa ukizingatia hakujua adui yake alikuwa wapi, na upande gani! Hivyo akawa anatupa macho yake pande zote za hoteli hiyo bila mtu yeyote kumgundua, kwa vile yalikuwa macho ya kipelelezi. Watu wote waliokuwa wanaingia katika hoteli ile mchana huo, walionekana ni watu wa kawaida tu.

Watu waliokuwa wanakwenda kula chakula hapo, aliwaona ni watu wa kawaida kabisa, kwa mujibu wa yeye alivyoweza kuwachunguza kwa kutumia uzoefu wake. Ni mara nyingi mtu anapokuwa adui yako ni lazima angekusaka huku akiwa na wasiwasi kidogo punde anapokuona kwa kugonganisha macho yenu. Sasa kati ya watu wote wale, hakukuwa na kitu hicho. Kila mmoja alikuwa na hamsini zake!

********

GARI moja aina ya Toyota Corolla inayotoa huduma za teksi, ilisimamishwa nje ya Ubena Resort Hotel, kando ya Barabara ya Uhuru, eneo la Amana, Ilala. Baada ya kusimama, mlango wa nyuma ukafunguliwa, kisha akashuka mwanadada mmoja, mrembo wa nguvu, ambapo baada ya kushuka, alimlipa dereva fedha, na yeye akavuta hatua kuingia ndani ya hoteli hiyo.

Ni muda mrefu ulikuwa haujapita tokea Kachero Inspekta Malik ameingia ndani ya hoteli hiyo na kuendela kula chakula. Ndipo alipoaingia mwanadada huyo, ambaye alikuwa na sifa zote za uzuri. Zaidi ya uzuri wake, pia, alionekana ana maringo, kwani alikuwa akitembea kwa mwendo wa Twiga.

Kwa muda huo, mwanadada huyo alikuwa amevalia gauni la rangi ya pinki, fupi, lililoishia mapajani, na viatu vilivyofanana na lile gauni alilovaa, kwapani alikuwa ametundika mkoba mdogo, na moja kwa moja akaelekea kwenye meza ile aliyokuwa amekaa Malik. Baada ya kuifikia akavuta kiti kimoja na kukaa upande wa pili wa meza, na pia akaiweka simu yake  hapo juu ya meza.

Harufu ya mafuta ya uzuri, ambayo hayakuleta kero puani, yalienea kote na kutoa burudani ya pekee, halafu baada ya kukaa, akauweka ule mkoba wake mezani na kuirekebisha ile nguo yake fupi iliyoacha wazi mapaja yake meupe yaliyonona!

“Habari yako kaka…” mwanadada yule akamsalimia Malik.

“Nzuri tu dada…” Kachero Inspekta Malik akaitikia huku akimwangalia kwa makini na kukubali ni kweli alikuwa mzuri na mrembo anayejipenda.

“Samahani kaka, nimejikalia hapa, sijui kuna mtu mwingine?” Akamuuliza.

“Unaweza kukaa tu, hakuna mtu,” Malik akamwambia huku akimshangaa! Ni kwanini akae pale, na siyo sehemu nyingine ndani ya hoteli ile!

“Nashukuru…”

“Du, imekuwa vizuri…utanisaidia kula, kwani chakula kingi hiki…” Kachero Inspekta Malik akamwambia kwa kumwonyesha ukarimu.

“Nashukuru kaka’angu…nimeshaagiza chakula…” akajibu kwa sauti nyororo.

“Muda gani, wakati umekuja sasa hivi tu? Tafadhali…”

“Ndiyo, hapa hotelini nafahamika sana. Basi, wanaponiona huwa wanajua oda yangu.”

“Aisee…kumbe ni mtu maalum.”

“Ni kama hivyo kaka…”

Baada ya muda mfupi, mwanadada huyo alihudumiwa chakula chake, ndizi kwa nyama, na bia moja aina ya  Castle ya baridi. Akaendelea kula taratibu. Pia, Malik naye akaendelea kula huku mawazo yakiwa mbali sana, hasa kuhusu mwanadada yule aliyekuwa pale, kwani ni mara nyingi alikuwa akijiepusha sana kumwamini mwanamke, hasa anapokuwa katika pilikapilika zake za kazi nzito ya upelelezi.

Kuna wasiwasi kuwa, wanawake wengi huwa wanatumiwa na majambazi, wakitumika kama chambo kutokana na uzuri wao. Kachero Inspekta Malik akaukumbuka usemi ambao aliwahi kuambiwa na babu yake miaka mingi. Ni maneno machache, ambayo yalikuwa na ujumbe mzito uliosema:

 “…Mjukuu wangu, hivi sasa unakuwa mtu mzima. Kumbuka kwamba wanawake ni viumbe dhaifu, ingawa ni mama zetu waliotuzaa. Unaweza ukamkuta mwanamke mzuri, mfano wa Malaika; mwaenye sauti nzuri, nyororo na maneno mengi ya kuvutia. Lakini mara nyingine jihadhari na mwanamke huyo, kwa wakati mwingine anaweza kuwa na ulimi wenye sumu kali, inayoweza kukudhuru mara moja, ingawa siyo wote! Yakupasa kujihadhari!”

Ndiyo. Kachero Inspekta Malik aliyakumbuka yale maneno punde tu alipokuwa amekaa sambamba na mwanadada huyo mwenye uzuri wa aina yake. Na wakati wakiendelea kula chakula, kimwana huyo ambaye walikuwa bado hawajafahamiana, alikohoa kidogo kusafisha koo. Halafu akanywa maji yaliyokuwa kwenye bilauri na kumwangalia Malik kwa macho malegevu! Mtego huo! Akawaza!

“Samahani kaka…” mwanadada huyo akamwambia 

“Bila samahani…” kachero Inspekta Malik akamwambia..

“Imekuwa kama bahati tumejikua tumekaa wote…ningependa tufahamiane, ikiwezekana jina lako, mahali unapopatikana na namba yako ya simu ya mkononi….” mwanadada huyo akaendelea kumwambia huku ameshika simu yake akiwa tayari kuingiza namba!

Mbona haraka hivyo? Malik akajiuliza!

“Mh!” Kachero Inspekta Malik akaguna. Akabaki ameshangaa sana juu ya mwanadada huyo mrembo kutaka kujua jina lake, kiundani zaidi, wakati walikuwa hawajafahamiana! Hakika alishindwa kutoa jibu!

“Usiwa na wasiwasi…” mwanadada hyo akaendelea kumwambia na kuongeza. “Nimetokea kukupeda tu, ndiyo maana nikapenda kukaa na wewe. Unajua wewe ni kijana mtanashati uliyeumbika kiume. Lakini naomba usinielewe vibaya labda ukafikiri mimi ni malaya!”

“Mungu wangu!” Malik akajisemea moyoni mwake! Hakumwelewa kabisa!

“Upendo wangu kwako, ndio uliosababisha yote haya…” akaendelea kurindima. “Na pia nafahamu wazi kuwa utamaduni wetu ni vigumu mwanamke kumweleza mwanaume kuwa unampenda, zaidi ya kumwonyesha kwa vitendo…”

“Huyu mwanamke vipi?” Kachero Inspekta Malik akaendelea kujiuliza!

Hata hamu ya chakula ikamwisha!

“Hata hivyo…” akaendelea mwanadada yule. “Uzalendo umenishinda mtoto wa kike…ndiyo maana nimekuomba usinielewe vibaya kaka, kwani sisi watu tuliotembea kidogo na kukutana na watu wengi, tumeshaivua aibu!”

“Umeshamaliza?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza!

“Ndiyo…mimi nimemaliza. Nakusubiri tu wewe mtoto wa kiume!” Mwanadada yule akasema huku akijiamini sana!

Kachero Inspekta Malik akawa na wasiwasi bado! Isije ikawa mwanadada huyo ni mtego wa majambazi, ukizingatia tokea jana alikuwa akiandamwa na kukoswakoswa na risasi ndani ya Kimicho Bar Buguruni, hivyo kwa kujihami akamwambia:

“Unasikia dada…nimekuelewa sana. Hebu tufahamiane kwanza…wewe ni nani, jina lako, na unatika wapi, nafikiri huo ndiyo utaratibu.”

“Ni kweli usemayo kakaangu…” mwanadada akasema huku akirembua macho yake makubwa mazuri na yenye mvuto.

“Ok, unaitwa nani?”

“Kwa jina naitwa, Helen Fataki….”

“Vizuri sana. Ni jina zuri lenye mvuto, pia ni jina linalonikumbusha mbali sana!”

“Ni kweli ee, basi nashukuru sana kwa kunisifia kaka…ni wachache sana hufanya hivyo.”

“Ni wajibu wangu kukusifia Helen Fataki.”

“Basi, tuendelee…” Helen Fataki akasema na kuendelea. “Mimi ni mfanyabiashara ninayeishi hapa jijini Dar es Salaam. Nakukumbusha tena kwamba nahitaji namba yako ya simu, kwani  najua tatizo unalolifuatilia, ambalo kwa namna moja ama nyingine ninaweza kukusaidia kulitatua. Kumbuka kwamba  mimi ni raia mwema!” Helen Fataki akamaliza kusema.

“Tatizo linalonikabili?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza.

“Ndiyo, usiwe kama mtoto mdogo, mimi naelewa kila kitu, ndiyo maana nikakwambia mimi ni raia mwema, unanipata?”

“Vizuri sana Helen, nimekuelewa….”

“Nashukuru kama umenielewa.”

Kachero Inspekta Malik  akamkubalia Helen baada ya kumsoma na kuona kwamba hakuwa na matatizo, na pia ni mtu ambaye alikuwa anajua kuwa yeye ni kachero ingawa hakuwa na namba zake za simu, ambazo ndizo zilikuwa kitu muhimu sana kwa upande wake. Hivyo akampa jina lake, namba zake za simu ya mkononi, na pia, Helen akampatia za kwake. Baada ya pale wakaagana kwa ahadi ya kuwasiliana zaidi kwa simu za mkononi, kila mmoja akaondoka.

Kachero Inspekta Malik alielekea nyumbani kwake, Shariff Shamba, Ilala, huku akiwa na mawazo ya kujihami na adui zake waliojaribu kuzuia kazi yake aliyokuwa ameianza. Akaahidi kupambana nao kufa na kupona! Ni kiapo cha Ushindi!

********          

MAWAZO mengi sana yalikuwa yamemtawala Getruda, mara baada ya kushushwa kwenye gari na Kachero Inspekta Malik, walipokuwa wametoka kwenye  Kituo cha Polisi Buguruni, katika mahojiano, alilekea nyumbani kwake kwa mwendo wa taratibu akiwaza jinsi Malik alivyoweza kugundua mapema kwamba walikuwa na uhusiano na marehemu Anita.

Ukweli ni kwamba chanzo cha matatizo yote yale, yalikuwa yamesababishwa na yeye  mwenyewe, mara baada ya kumgeuka rafiki yake, Anita na kumchuka mchumba wake, John Bosho, na kushirikiana naye katika vitendo vya ngono. Na huko kukamfanya naye amgande kama Luba, mpaka yalipotokea mauaji hayo ya kumziba mdomo!

Baada ya kufika nyumbani kwake alikopanga chumba, alimkuta yule msichana mdogo aliyekuwa anashona nguo pale barazani kwa cherahani, ambapo alimsabahi na kuanza kuingia ndani kwa hatua za kinyonge, lakini msichana yule akamwambia:

“Habari za kanisani dada Getu…”

“Nzuri tu Salma…za hapa..”

“Hapa ni nzuri, lakini kuna mgeni wako alikuja hapa na kukuulizia…”

“Mgeni wa aina gani? Mwanaume au mwanamke?”

“Ni mwanaume, ambaye alikuja na gari ambalo alilisimamisha palee!”

“Ameacha ujumbe?”

“Hakuacha…hata hivyo nilimwambia kwamba umekwenda Kanisani, na yeye akasema kuwa anakufuata hukohuko, je, hujamwona?”

“Ah, basi tu,” Getruda akamwambia, halafu akaingia ndani, kwani alikuwa ameshaonana na Kachero Inspekta Malik, ambaye mpaka muda ule hakuwa na hamu naye! Ni mtu ambaye aliona kwamba anataka kumwangamiza kabisa kama akiigundua ile siri nzito ya kifo cha Anita!

Baada ya kuingia chumbani mwake, huku akiwa amesimama, Getruda akatoa simu yake ndani ya mkoba wake. Halafu akakaa kwenye egemeo la sofa, akiwa na nia ya kumpigia John Bosho. Ni juu ya kumjulisha mambo yalivyokuwa yanaendelea tokea walivyoachana juzi nyumbani kwake, Ukonga, alipokwenda kumtembelea baada ya kumwitakujadili hatima ya penzi lao.

Akapiga simu ile upande wa pili ukasema:

“Haloo…Getruda mpenzi…”

“Oh, vipi mpenzi, hujambo?”

“Mimi sijambo…sijui wewe!”

“Hata mimi sijambo kiasi…nipe habari…”

“Oh, amekuja!”

“Amekuja nani?”

“Askari mpelelezi.”

“Mpelelezi yupi Getruda?”

“Anajiita Malik Mkoba.”

“Mh, Inspekta Malik Mkoba?”

“Ndiye huyohuyo!”

“Unasema amekuja hapo nyumbani?”

“Ndiyo…amekuja hapa nyumbani na kunikosa, halafu akanifuata Kanisani na kuanza kunihoji kuhusu wewe, kama nakufahamu.”

“Ni nani aliyemweleza?”

“Ameelekezwa na mama mwenye nyumba aliyokuwa anaishi Anita kule Tabata…”

“Aisee…” John Bosho akasema. “Kumbe yule mama ni mtu mshenzi sana!”

“Usiseme hivyo John, yule mama amehojiwa tu. Lakini si unajua polisi walivyo?”

“Sasa baada ya kukuhoji ukamwambia nini kuhusu mimi?”

“Ilinibidi nimwambie…” Getruda akasema na kuendelea. “Sikuwa na jinsi, kwani alivyokuja hapa alikuwa na habari kamili, pamoja na picha zetu wote. Wewe, mimi na marehemu Anita!”

“Mama yangu! Amezipata wapi?”

“Bila shaka amezichukua chumbani kwa Anita baada ya kufanya upekuzi.”

“Mh!” Akaguna John. “ Ulimweleza juu yangu?”

“Basi, ndiyo hivyo John. Nilimwelewa, lakini sikumwambia kwamba wewe ndiye muuaji. Nimemtambulisha kama mfanyabiashara mkubwa.”

“Oh, vizuri sana…sasa unanipa ushauri gani?”

“Nilikuwa nakufahamisha tu, ili ujihami!”

“Kujihami ni muhimu sana. Hivyo basi, kuanzia sasa, tena leo hii, fanya hima uje hapa nyumbani kwangu Ukonga, ili ujifiche. Kwa mimi ninavyowajua polisi, anaweza akarudi tena kukupeleleza ili kutaka sifa!”

“Sawa, nafungasha nguo zangu. Nitakuja huko muda siyo mrefu, kwani nimeshaanza kuingiwa na wasiwasi…”

“Na ukitoka hapo usimuage mtu yeyote kuwa unaelekea wapi! Iwe siri yako! Tafadhali zingatia!”

“Sawa, nitazingatia…”

“Ok, bai…”

Wakamaliza kuwasiliana.

Kuanzia muda ule Getruda hakupoteza muda, akaanza kukusanya nguo zake muhimu za kubadili, ambazo alizitia ndani ya begi dogo. Pia, akachukua vikorombwezo vingine vingi ambavyo aliona vingemsaidia katika safari yake ile ya kuyakimbia makazi yake pasipo kupenda! Baada ya kumaliza kukusanya aliyoona vinamfaa, akaamua kujipumzisha kwenye kochi kubwa akingali bado anasumbuliwa na mawazo.

Ni mawazo ambayo yalimfanya hata asisikie njaa kutokana na kasheshe lile lililoanza kufukuta kichinichini. Ama kweli pale ndipo alipoamini kuwa mkono wa dola ni mrefu, usioweza kukwepeka kamwe! Kwa mbali akawa anaendelea kuujutia ule uamuzi wake wa kukubali kurubuniwa na John Bosho, kwa ajili ya fedha! Hata hivyo kuwaza sana halikuwa suluhisho la kutatua tatizo lake. La muhimu ilikuwa ni jinsi ya kupanga kuepukana nalo kwa gharama yoyote!

        ********

ILIPOTIMU saa kumi na moja za jioni, Getruda akaamua kuodoka pale nyumbani kwake kuelekea Ukonga. Ingawa John alimwambia asiage mtu yeyote, lakini hakufanya hivyo, aliwaaga wapangaji wenzake na kuwadanganya kwamba alikuwa anakwenda Sinza kwa shangazi yake. Hata hivyo, hakuna hata mtu mmoja aliyemhoji zaidi ya kumtakia safari njema. Getruda akakodi teksi iliyokuwa inapita katika mtaa ule wa Moshi, na kumwambia dereva ampeleke Ukonga.

Safari ikaendelea kwa mwendo wa wastani. Dereva akaendelea kupangua gea na kukanyaga mafuta hadi walipofika Ukonga Mombasa. Nusu iliyobaki akaamua kutembea kwa miguu, kuelekea nyumbani kwa John Bosho, kwa kukatiza pembezoni mwa Kambi ya Askari wa Kutuliza Ghasia, na kutokeza relini ilipo nyumba inayomilikiwa na John Bosho.

Baada ya kufika  kwenye makazi ya John Bosho, Getruda aliingia kama mwenyeji, mara baada ya kuruhusiwa na mlinzi wa kimasai aliyekuwa analinda hapo getini. Alipoingia ndani, alimkuta John Bosho akiwa amekaa sebuleni katika sofa za gharama akiangalia runinga. Na kama ilivyo ada mbele yake kwenye meza ndogo, ulikuwepo mzinga wa Konyagi aliokuwa anakunywa taratibu kuisukuma wikiendi.

“Oh, karibu sana Getu…” John Bosho akasema huku akinyanyuka kumpokea lile begi dogo. “Karibu…”

“Ahsante, nimekaribia…” Getruda akasema huku akikaa kwenye sofa, na pengine kumkazia macho John. “Safari gani ya kupewa pole?”

“Ni lazima nikupe pole kwa sababu ni safari ambayo ulikuwa hujaipangilia…”

“Ahsante…nimepoa…”

John Bosho na Getruda walikaa pale sebuleni huku wakiongea hili na lile, hatimaye John akatoa wazo kuwa siku ile ya Jumapili watoke kidogo nje ya nyumbani, ili wakale chakula cha usiku na pia vinywaji. Getruda ambaye kwa muda mwingi alikuwa ni mtu wa kukubali tu, hakupinga wazo lile, akakubali kwenda kule alipoamua kwenda . Hivyo basi, wakatoka nje wakiwa kama wapenzi wawili huku wameshikana mikono, wakapanda ndani ya gari na kuodoka eneo hilo huku wakimwacha yule mlinzi wa kimasai akilinda eneo la nyumba.

“Huyu mlinzi wa kimasai mwisho wake wa kazi ni leo…simtaki tena!” John Bosho akamwambia Getruda.

“Kwa nini humtaki?” Getruda akahoji.

“Nimemshtukia…hawezi kutunza siri punde atakapohojiwa na polisi…”

“Kwa hivyo umempata mwingine?”

“Ndiyo. Nimempata kutoka kwenye kampuni ya ulinzi ya binafsi, ambao nimeshaandikishiana nao mkataba. Ataanza kazi kesho, na huyu namlipa haki yake aende sehemu nyingine!”

“Ni sawa kama umeamua hivyo…” Getruda akamuunga mkono.

“Ni uamuzi wa busara!” John akamaliza kusema huku akiongeza mwendo wa gari wakiifuata Barabara ya Pugu, kuelekea Gongo la mboto.

John Bosho aliamua kwenda kuburudika katika sehemu tulivu ya Mangi Villa Bar, ikiwa ni sehemu iliyotulia sana na pia burudani ya muziki wa Zilipendwa ulipatikana. Kama kawaida Getruda alikubaliana naye hadi walipofika, akaliegesha gari sehemu ya maegesho palipokuwa na magari mengine. Halafu wakashuka na kwenda kukaa kwemye sehemu nzuri iliyokuwa nje yenye upepo.

Baada ya kukaa, vyakula navinywaji na kuendelea kula na kunywa, na pia wakiendelea na maongezi yao mengi yakiwepo ya yeye John kutaka kumwoa Getruda, ili aje kuwa mke wake atakayemzalia watoto. Hata hivyo pamoja na kuimbiwa kawimbo hako ka mapenzi, Getruda alikuwa mbali sana kimawazo dhidi ya mtu huyo katili!

Ni hadi ilipotimu saa tano za usiku, waliamua kuondoka hapo Mangi Villa Bar, kurudi nyumbani wakiwa wamechangamka vya kutosha. Muda wote huo John Bosho alikuwa na hamu kimapenzi na Getruda, bila kuwazia ule unyama alioutenda kwa rafiki yake, Anita, na isitoshe hata wiki moja ilikuwa haijaisha!

*********       

JUMATATU asubuhi kunako majira ya saa moja na nusu, ilimkuta Kachero Inspekta Malik alikuwa ofisini kwake akichapa kazi, ukizingatia alikuwa na mafaili kadhaa ya kuyashughulikia. Alikuwa amepanga kwamba achape kazi mpaka saa tisa za alasiri, halafu ndiyo aende nyumbani kwa John Bosho, Ukonga, akaendelee na upelelezi wake aliouanza.

Mawazo yakiwa yamezama ndani ya faili moja, mara simu yake ya mkononi iliyokuwa kando ya meza ikaita. Akaichukua na kuangalia namba za mpigaji, ambazo zilionyesha ni za mwanadada Helen Fataki, ambaye walikuwa wamekutana naye jana yake na hatimaye kupeana namba za simu zao za mkononi.

“Haloo…Helen…Malik hapa…” Kachero Inspekta Malik akamwitikia.

“Ndiyo mimi Helen Fataki naongea…vipi hali…”

“Hali nzuri, habari za tokea jana.”

“Habari ni nzuri.”

“Nashukuru sana kwa kunikumbuka kwa simu asubuhi hii Helen…” Malik akamwambia.

“Nami nashukuru. Samahani kwa usumbufu, najua uko bize sana.”

“Ni kweli Helen. Si unajua kazi zilivyotutinga? Nimeelewa si mchezo!”

“Ok, sasa kuna la maana nataka kukueleza. Hivyo naomba jioni tukutane sehemu gani kwa maongezi zaidi?”

“Naomba upange wewe sehemu ya kukutana Helen…” Malik akamwambia.

“Tukutane Sarova Pub, hapo Buguruni…”

“Sarova Pub iliyoko jirani na Kimicho Bar?”

“Ndiyo.”

“Kwa nini umeamua tukutane hapo?”

“Ni sehemu ambayo kazi yetu inaanzia hapo. Nataka tukutane, ili nikupe michapo juu ya kazi unayoifuatilia. Ninarudia kuwa ni muhimu!” Helen Fataki akasisitiza!

“Muda gani?”

“Saa moja za usiku…samahani kwa usumbufu…”

“Bila samahani Helen…nitafika…”

Baada ya kumaliza kuwasiliana, Kachero Inspekta Malik akaendelea kuchapa kazi, ambapo kwa siku ile nzima aliamua kushinda ofisini hadi ilipotimu saa tisa na nusu, ndipo alipomaliza kazi na kufunga ofisi. Kama alivyokuwa amepanga, akapanda gari na kuelekea Ukonga, nyumbani kwa John Bosho kufuatilia nyendo zake ukizingatia alikuwa bado hajamfahamu. Kwa vile Getruda alishamwelekeza nyumbani kwake, basi akajua asingepotea, ataifuata ramani iliyoko kichwani mwake!

Ili asishtukiwe, kachero Inspekta Malik alilipaki gari lake eneo maarufu la Ukonga Mombasa, ambayo ni sehemu yenye pilikapilika nyingi za watu. Halafu akachepuka kwa miguu na kukatiza vichochoro hadi alipotokeza upande wa pili sehemu ya relini kama alivyokuwa ameelekezwa. Baada ya kutokea eneo lile, akaanza kuchunguza nyumba ya John, ambayo hakupata shida kuiona ikiwa imezungukwa na ukuta madhubuti, na mbele kukiwa na geti kubwa la chuma.

Akaamua kuiendea ile nyumba kana kwamba alikuwa mwenyeji na getini akamkuta mlinzi wa kampuni ya binafsi akiwa amesimama kwa ukakamavu na makini kwa lindo lake. Mlinzi huyo ndiye yule aliyekuwa amewekwa siku ile, mara baada ya John kuamua kumwachisha kazi yule mlinzi wa kimasai aliyekuwa mwanzo, kwa kile alichokiita kutomwamini kujibu maswali ya polisi walioanza kumfuatilia.

Kwa wakati huo, mlinzi huyo wa kampuni binafsi alikuwa amevalia sare zake za rangi ya bluu na michirizi ya njano. Akawa anamwangalia Malik alivyokuwa anamwendea pale aliposimama.

“Habari za kazi!” Kachero Inspekta Malik akamsalimia baada ya kumfikia.

“Nzuri tu…nikusaidie…” mlinzi yule akaitikia huku akimkagua Malik, kuanzia juu hadi chini, ukizingatia masharti aliyokuwa amepewa na John Bosho. Ni kujihadhari na watu waliokuwa wanafika pale kumuulizia!

“Nisaidie ndugu yangu. Naulizia kwamba hapa ni nyumbani kwa mfanyabiashara, John Bosho?” Kachero Inspekta Malik akamuulizia huku amemkazia macho yake ya kipolisi, ambayo mlinzi aliyakwepa!

“Hukukosea…ndiyo penyewe!” Mlinzi akasema.

“Sijui nimekuta?”

“Ndiyo…umemkuta…”

“Basi, nina shida naye…”

“Una ahadi naye?”

“Sina ahadi naye,” Kachero Inspekta Malik akamwambia. “Ninataka kumuona tu, wala sikuwa na miadi…”

“Aisee…” mlinzi yule akasema huku akionyesha kama vile anasita. Hakuwa tayari kumruhusu kwa jinsi alivyoelekezwa na John Bosho.

“Kwani kuna masharti ya kumwona?”

“Ndivyo alivyoamua bosi mwenyewe!”

“Mjulishe bosi wako! Mweleze kwamba kuna mgeni anataka kuonana naye. Kuna jambo la muhimu.”

“Sawa,” mlinzi yule akasema huku akiona ilikuwa ni adha imeanza!

Mlinzi akachukua simu yake ya mkononi na kubonyeza namba kumpigia John Bosho aliyekuwa ndani. Simu ikaanza kuita na mlinzi kuanza kuisikiliza huku ameyakodoa macho yake makubwa kwa Malik. Upande wa pili wa simu, John akamwuliza kwa hasira kidogo!

“Unasemaje?”

“Kuna mgeni bosi!”

“Mgeni? Mwanaume au mwanamke?”

“Mwanaume…”

“Umemuuliza jina lake?”

“Hapana…sijamuuliza bosi.”

“Ok, mruhusu aingie…”

“Sawa bosi…” mlinzi yule alikasema huku akiendelea kumwangalia Malik, ambaye alikuwa ameshayagundua yale maongezi waliyokuwa wanaongea! Halafu akamwambia.

 “Amesema uingie…”

“Ina maana kuna masharti ya kumwona?”

“Ndivyo alivyopanga yeye mwenyewe…na isitoshe mimi nimeanza kazi leo!” Mlinzi yule akasema huku amechukia!

Hata hivyo Kachero Inspekta Malik hakumsemesha tena, isipokuwa aliamua kuingia ndani kwa kupenya katika mlango mdogo uliokuwa pale getini, na kutokeza ndani ya nyumba ile ya kifahari iliyokuwa na bustani nzuri na ya kupendeza. Baada ya kuingia tu, akamwona Getruda akiwa amesimama nje ya kibaraza cha nyumba, na baada ya kumwona Malik akashtuka na kujikuta akisema kwa sauti ya kujilazimisha:

“Oh, karibu Inspekta Malik…”

“Ahsante sana…” Kachero Inspekta Malik akaitika na kushangaa kumkuta Getruda katika nyumba ile, wakati ilikuwa ni ya John Bosho, aliyekuwa mchumba wa marehemu Anita! Ambaye ni rafiki yake mkubwa Getruda!

“Ooohps!” Getruda akavuta pumzi ndefu na kuzishusha kwa nguvu!

“Vipi Getruda…mbona uko hapa?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza baada ya kumkuta pale, kwani hakutegemea!

“Kwani vipi?” Getruda naye akamuuliza

“Nauliza hivyo kwa sababu hapa ni nyumbani kwa shemeji yako. Isitoshe rafiki yako Anita amefariki, au sivyo?”

“Nimekuja kumsalimia shemeji yangu John, kwani kuna ubaya wowote?”

“Hakuna ubaya,” Kachero Inspekta Malik akasema kwa kumtoa wasiwasi Getruda. Hata hivyo akagundua kuwa amemsaliti mwenzake kwa kuanzisha uhusiano usiofaa, hususan wa kimapenzi na John.

“Vipi, John nimemkuta?”

“Umemkuta, yuko ndani…”

“Vizuri sana…imekuwa bahati sana…”

“Bahati gani?” Getruda akamuuliza.

“Kumkuta, kwani ni mtu muhimu sana kwa wakati huu!”

“Karibu…utamkuta tu, kajaa tele ndani.”

Kachero Inspekta Malik na Getruda wakaingia ndani huku Getruda ametangulia, na Malik akimfuata nyuma. Baada ya kuingia pale sebuleni, wakamkuta John amejaa tele amekaa kwenye sofa, na alipomwona Malik, akanyanyuka na kujifanya kumchangamkia kwa kumkaribisha kwa ukarimu.

“Oh, karibu mgeni…karibu sana…”

“Ahsante…nimekaribia…” Malik akasema huku akijiandaa kukaa kwenye sofa dogo.

Kachero Inspekta Malik akakaa kwenye sofa lile dogo, moja kati ya yale matatu ya thamani yaliyokuwa katika sebule ile kubwa iliyosheheni samani.

“Karibu na ujisikie uko nyumbani…” John Bosho akaendelea kumwambia Malik.

“Ahsante, na nimeshakaribia…” Kachero Inspekta Malik akasema huku akiangaza macho yake pande zote za sebule ile nadhifu.

Ukimya mfupi ukatawala kwa muda pale ndani, baina ya watu wale, Kachero Inspekta Malik, John Bosho na Getruda, kila mmoja akitegea atakayeanza mazungumzo!

********

TOKEA mwanzo John Bosho  alishagundua kuwa aliyefika pale nyumbani kwake, Ukonga, alikuwa ni Kachero Inspekta Malik Mkoba, aliyekuwa anafuatilia kadhia ile ya mauaji ya Anita, aliyemuua yeye mwenyewe. Ndipo alipomwambia Getruda akampokee kule nje, ingawa yeye Getruda hakujua kama ni Malik, zaidi ya mgeni wa kawaida tu, ambao huwa wanafika mara kwa mara kumtembelea. Kumbe haikuwa hivyo!

Basi, baada ya Getruda kutoka nje tu, ndipo yeye John alipoingia chumbani kwake, ambapo  alichukua bastola yake iliyokuwa imejaa risasi, halafu akaichomeka kiunoni upande wa nyuma, akaifunika na fulana aliyokuwa amevalia. Alipomaliza kuihifadhi, ndipo alipotoka pale chumbani na kurudi sebuleni alipokuwa amekaa mwanzo, na kuendelea kuangalia runinga huku amechukia kwa kile kitendo cha kufuatwafuatwa! Pia, akawa anamsubiri mgeni wake kwa hamu!

Wakati John Bosho akimkaribisha Malik, Getruda alibaki amesimama, akisubiri kumkarimu mgeni yule, japo kwa kinywaji anachopendelea. Na muda huohuo, John akamkabidhi Getruda kipande cha karatasi kilichokuwa na ujumbe mfupi uliosomeka hivi “Ingia chumbani, fungua droo, chukua ‘Sumu ya nyongo ya Mamba,’ mtayarishie mgeni juisi ya maembe. Tafadhali tekeleza!”

Baada ya kuuchukua ule ujumbe, Getruda aliondoka na kuelekea ndani chumbani alipoelekezwa kuwa kuna ile sumu kali, ili amtayarishie mgeni wao juisi.

“Ndiyo bwana, mimi naitwa Kachero Inspekta Malik Mkoba…nimetokea katika kituo cha Polisi, Buguruni,” Kachero Inspekta Malik akajitambulisha kwa John Bosho.

“Nashukuru kwa kukufahamu, karibu sana,” John Bosho akamwambia Malik.

“Samahani sana kwa kuingilia mapumziko yako ya jioni…”

“Bila samahani.”

“Natumaini kuwa wewe ni John Bosho, maana sikufahamu…”

“Naam, ndiyo mimi…”

“Ok, mimi nimekuja hapa kwako kwa ajili ya upelelezi wa kifo cha marehemu Anita, kwa vile nasikia alikuwa mchumba wako.”

“Ni kweli afande, Malik, kabla ya kifo chake, alikuwa ni mchumba wangu…”  John Bosho akasema huku akiwa na wasiwasi.

“Sasa ndugu John, kama Anita alikuwa ni mchumba wako wakati wa uhai wake, mbona kwenye msiba wake au siku za mazishi hukufika?”

Swali lile likawa gumu kwake. Akanyamaza kimya!

Halafu Malik akaendelea “…Yaani hukuonekana kabisa hata sura yako!”

“Ah, unajua…nili…kuwa sababu…” John Bosho akaendelea kujikanyaga.

“Narudia tena…hivi ina maana kweli Anita alikuwa mchumba wako, halafu wewe usiende kwenye msiba wala mazishi yake?” Kachero Inspekta Malik akaendelea kumhoji.

“Nilikuwa ‘Bize’ sana…hapana…unajua mimi nilisafiri…”  John akazidi kujichanganya! Hakika alikuwa amekumbana na maswali ya kikachero, ambayo hakujiandaa kuyajibu.

“Hivi John, unaweza kuwa ‘Bize’ mpaka ukashindwa kuhudhuria mazishi ya mchumba wako?”

“Mh,” John Bosho akajibu kwa kuguna.

“Enhe, hivi na huyu mwanadada aliyenipokea hapa ni nani kwako?” Kachero Inspekta Malik akaendelea kumuuliza swali jingine, ambalo lilikuwa ni mtego, kana kwamba alikuwa hamfahamu Getruda!

“Huyu ni mchumba wangu Getruda…” John Bosho akasema bila kuwa na wasiwasi wowote!

“Unasema ni mchumba wako?”

“Ndiyo, ni mchumba wangu mpya!” John Bosho akasema na kuongeza, “Vilevile alikuwa ni rafiki wa Anita.”

“Kwa hiyo huoni ubaya wowote kumwoa msichana huyu, wakati alikuwa rafiki wa mchumba wako, marehemu Anita?”

“Kwa hilo mimi sioni ubaya wowote. Isitoshe kila mmoja ana nafasi yake!” John Bosho akajibu kijivumi, huku amechukia! Hata hivyo akamezea, na ukimya ukatawala kwa muda kila mmoja akitafakari lake kichwani!

        *********

AKIWA katika hali ya sintofahamu, baada ya kuuchukua ule ujumbe kutoka kwa John Bosho, Getruda alikuwa ameshaondoka na kuelekea ndani chumbani alipoelekezwa kuwa kuna ile sumu kali, ili amtayarishie mgeni wao juisi. Na kweli alipoingia humo chumbani, alifungua droo na kuitoa ile sumu iliyokuwa katika hali ya unga mweusi ndani ya pakti maalum ya nailoni iliyofungwa madhubuti. Alipoichukua, akaenda nayo jikoni na kuichanganya katika juisi ya maembe iliyokuwa ndani ya friji.

Sumu hiyo alikuwa ameiweka ndani ya bilauri ya Kachero Inspekta Malik, na kuijaza juisi ndani yake. Alipomaliza kuiandaa akaipeleka mezani ikiwa ndani ya jagi la kioo, pamoja na bilauri tatu kubwa. Hakika ilikuwa ni juisi iliyotamanisha kuinywa, kiasi kwamba hakuna mtu yeyote ambaye angeacha kuitamani na kuacha kunywa. Ilikuwa ya mchanganyiko wa rangi ya njano iliyokolea.

Hivyo basi, Getruda alimmiminia Malik hiyo juisi na kumsogezea stuli iliyoundwa kwa kioo, ikiwa ni moja kati ya stuli nne zilizokuwa pale sebuleni pamoja na meza yake. Ile bilauri ya juisi akaiweka juu ya stuli hiyo kwa heshima ya kuvunja goti kwa kuinama kidogo, na kumwambia:

“Karibu juisi…”

“Ahsante sana…” Kachero Inspekta Malik akasema huku akiitamani ile juisi ya maembe kwa mwonekano wake.

“Karibu juisi ndugu, Malik…” John Bosho  akamwambia huku yeye akiichukua bilauri yake na kuanza kunywa taratibu ili kumwondoa wasiwasi!

“Ahsante sana,” kachero Inspekta Malik akasema na kuinyanyua ile bilauri kubwa tayari kwa kuinywa, na tayari alikuwa ameshaisogeza mdomoni!

Getruda aliyekuwa akimwangalia kwa makini, aliyafumba macho yake wakati Malik alipokuwa anaipeleka bilauri ile mdomoni mwake. Kwa vyovyote alijua kuwa muda wowote ule atakuwa mfu, kitu ambacho kilimwogopesha sana!

Lakini kabla Malik hajainywa ile juisi, simu yake ya mkononi iliita hapohapo! Halafu akaitoa mfukoni mwake na kuangalia namba za mpigaji, ambapo ilionyesha ni za Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi Buguruni , Mrakibu Mwanadamizi wa Polisi, Alfred Ganzo, ndiye aliyekuwa akimpigia muda ule. Hivyo Malik akataka kuirudisha ile bilauri mezani huku bado akiiangalia ile simu iliyokuwa inaita mkononi mwake!

Hata hivyo kwa bahati mbaya, bilauri ile iliteleza katika stuli ile ya kioo na kudondoka chini kwa kujipigiza kwenye sakafu ya tarazo, na bilauri ile ikavunjika na juisi yote kumwagika! Hakika ilikuwa ni bahati ilioje, kwani hakuwahi hata kuionja hata kidogo!

“Oh!” Kachero Inspekta Malik akaguna huku akiitazama ile bilauri iliyokuwa imevunjika.

“Ah, bahati mbaya!” John Bosho akasema huku akishangaa!

“Mungu wangu!” Getruda akaishia kusema hivyo!

“Ngoja niliisikilize simu…”  Kachero Inspekta Malik akasema. Hakujali, akanyanyuka na kujisogeza pembeni kabisa karibu na mlango wa kuelekea kwenye korido. Akaanza kuisikilize ile simu iliyokuwa bado inaita.

John Bosho na Getruda walibaki wanaangalia kwa mshangao na hamaki! Hawakujua kingetokea kitu kama kile, kwani walitegemea angeinywa ile juisi iliyoachanganywa na sumu ya nyongo ya Mamba! Afe, wakamzike shambani, mchezo kwisha!

“Afande…naomba maelekezo…” Kachero Inspekta Malik akasema kwa sauti ndogo.

“Malik uko wapi?”  Alfred Gonzo akamuuliza.

“Niko hapa Ukonga, afande…”

“Si unajua kwamba hatujaonana kabisa?”

“Ni kweli afande, hatujaonana…niko kwenye pilikapilika za upelelezi.”

“Unafuatilia lile tukio la mauaji siyo?”

“Ndiyo, afande!”

“Umefikia wapi mpaka muda huu?”  Alfred Ganzo akamuuliza na kuendelea. “Maana Mkuu wa  Upelelezi Kanda Maalum, anaulizia…”

“Afande, ninaendelea vizuri, lakini siwezi kukuelezea kwenye simu…”

“Kwa hivyo?”

“Nakuletea taarifa…sijui utakuwepo ofisini?”

“Niende wapi na mimi nasumbuliwa? Njoo nakusubiri…”

 “Sawa afande, nakuja kukupa taarifa za upelelezi wangu..”

“Ok, nakushukuru…”

Baada ya kumaliza kuwasiliana na mkuu wake,  Kachero Inspekta Malik aliwageukia John na Getruda waliokuwa bado wanaagaliana, kisha akamwambia kwa sauti ndogo:

“Jamani mimi nashukuru kwa karibu yenu, lakini nahitajika ofisini mara moja. Lakini nitarudi baadaye…”

“Oh, ngoja basi nikumiminie juisi nyingine…” Getruda akamwambia baada ya kuona mpango wao haujakaamilika!

“Nashukuru sana…nitakunywa siku nyingine!” Kachero Inspekta Malik akasema huku akiona kwamba alikuwa anapoteza muda, ukizingatia alikuwa anasubiriwa na mkuu wake wa kazi!

Kachero Inspekta Malik akatoka kwa hatua za haraka huku akisindikizwa na John Bosho, huku nyuma wakifuatiwa na Getruda hadi walipofika nje ya geti. Malik akachanganya hatua kuelekea eneo la Ukonga Mombasa, alipokuwa ameliacha gari lake, wenyewe wakarudi ndani huku wameghadhibika!

Kachero Inspekta  alipoondoka pale nyumbani kwa John Bosho, wala hakuwa na habari kwamba alikuwa ametiliwa sumu kwenye juisi ili afe! Hakuwa na wasiwasi kuwa John angeweza kumdhuru!

Alijiamini sana!

      ********

WOTE wawili, John Bosho na Getruda waliporurudi ndani, yeye John alifura kwa hasira na kubaki akizunguka pale sebuleni kama mtu aliyechanganyikiwa. Ina maana windo lake limefanikiwa kumponyoka? Tena ndani ya himaya yake? Hakutegemea kabisa!

“Mshenzi sana huyu kachero! Atanitibulia mipango yangu!” John Bosho akasema kwa hasira!

“Ukweli ni kwamba ana bahati sana!” Akaongeza Getruda.

“Sikubali!” John akasema kwa hasira!

“Hukubali nini?” Getruda akamuuliza.

“Yaani aniponyoke hivihivi?”

“Sasa unatakaje?”

“Mimi namfuata kummaliza!” John Bosho akasema huku akiipapasa bastola yake!

“Unataka kufanya nini?” Getruda akamuuliza John aliyekuwa anaanza kutoka.

“Nitamtwanga risasi! Anatufuata sana mtu huyu… yaani tunamwangalia atuharibie?”

“Usifanye hivyo John, yule ni polisi, usije ukazua mengine!”

“Sasa tufanyeje?”

“Nakwambia utaharibu kila kitu, kama nilivyokwambia huyo ni polisi, halafu umuue hadharani? Si Jeshi zima la Polisi litahamia hapa nyumbani kwako? Hapana!”

“Oh, nitafanya nini sasa? Shenzi sana!” John Bosho akaendelea kusema huku akijipiga katika paji la uso!

“Panga mpango mwingine mzuri!”

“Ok, ngoja nitapanga mpango mwingine kabambe na vijana wangu wa kazi. Tena nitawataarifu usiku wa leo, tukutane katika maskani yetu, Machimbo ya Mawe! Baada ya kukutana huko, tutajua la kufanya!” John Bosho akasema huku akirudi pale sebuleni na kukaa kwenye sofa!

Ama kweli alikuwa amechanganyikiwa!

“Hilo ni jambo la maana…” akamaliza kusema Getruda, ambaye naye alikaa kwenye sofa.

Hakika walikuwa wamechanganyikiwa!

John Bosho akaona kuwa mipango yake inaendelea kwenda mrama. Na cha zaidi kilichomuumiza, ni juu ya yule mganga wao, Mzee Chiloto Bandua, wa Chamazi, ambaye alimpatia dawa ya kumfanya asiweze kukamatwa, au kujulikana kama ndiye aliyemuua Anita! Mbona sasa imekuwa vile?

“Vipi John, mbona hivi?” Getruda akamuuliza baada ya kuona akiendelea kuwaza!

“Aisee…ni lazima niwaze!”

“Punguza mawazo…”

“Unajua kuna kitu kimoja kinanitatiza. Ilikuwa ni siri, lakini inabidi nikwambie…”

“Ni kitu gani hicho? Mbona sikuelewi!”

“Utanielewa tu,” John Bosho akamwambia na kuongeza. “Ngoja nikuambie ukweli wenyewe muda siyo mrefu!”

John Bosho na Getruda walikuwa bado wamekaa pale sebuleni, ikiwa ni baada ya Kachero Inspekta Malik kuondoka na kurudi kituoni. Wakati huo, Getruda alikuwa akisubiri kusimuliwa ile siri iliyokuwa inamsumbua John, baada ya kushindwa kwa jaribio la kumuua  kachero Inspekta Malik kwa sumu ya nyongo ya Mamba, iliyotiwa ndani ya juisi.

“Nisikilize kwa makini Getruda…” John Bosho akamwambia kwa msisitizo.

“Ndiyo nakusikiliza…” Getruda akasema huku akimwangalia na kumsikiliza kwa makini.

“Unajua baada ya mimi kumuua mchumba wangu, Anita, ilinibidi nijihami…”

“Ujihami kivipi?”

“Ili nisijulikane kama mimi ndiye niliyefanya mauaji hayo, niliamua kwenda kwa mganga mmoja  wa jadi, ambaye huwa anatusaidia katika shughuli zetu. Baada ya kumwendea akanipa masharti, ambayo niliyatekeleza. Lakini nashangaa mambo yamezidi kuwa magumu kiasi cha kuanza kuandamwa! Sasa sijui kama kanitapeli?”

“Kwani huyo mganga alikupa masharti gani?”

“Ni kumpelekea baadhi ya viungo vya mwili wa Anita!”

“Viungo vya mwili wa Anita?”

“Ndiyo manaake…”

“Ina maana ni nyie mlifukua kaburi lake usiku?” Getruda akauliza huku amefumba macho!

“Ndiyo sisi. Ni kama nilivyokueleza kwamba yalikuwa ni masharti magumu niliyopewa na mganga huyo anayejulikana kwa jina, mzee Chiloto. Lakini cha ajabu  ndicho hiki ninachoendelea kuona kuwa ni uongo mtupu! Amechukua fedha yangu bure mzee yule mshenzi!

“Oh, Mungu wangu!” Getruda akasema!

“Ndiyo hivyo Getruda. Sasa cha muhimu, mimi nimepanga kwamba nimwendee nyumbani kwake, ili anieleze ukweli wa jambo hili! Kabla mimi sijatiwa mbaroni, lazima na yeye awe kuzimu!” John Bosho akasema kwa msisitizo!

“Ina maana unataka kuua tena?”

“Ndiyo…lazima nimmalize!”

“Mungu wangu!”

“Hakuna cha kusema Mungu wangu! Jiandae tuondoke wote!”

“Unasema tuondoke wote?”

“Ndiyo! Habaki mtu hapa! Na baada ya kummaliza huyo mganga, ndiyo tunakwenda Machimbo ya Mawe, kukutana na vijana wangu. Ni katika kupanga mpango wa kummaliza Kachero Inspekta Malik!”

Getruda hakusema kitu chochote zaidi ya kubaki amechanganyikiwa! Alikuwa mbele ya muuaji!

Hakuwa na la kufanya!

********       

INGAWA kulikuwa na usumbufu wa foleni ya magari barabarani, Kachero Inspekta Malik hakukawia kufika kwenye Kituo cha Polisi Buguruni. Baada ya kufika, akaingia moja kwa moja katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo, ambaye alikuwa ni mtu mchapakazi na anayeijali kazi yake. Kwa bahati nzuri alimkuta amekaa akiendelea na kazi ya kuyapitia mafaili kadhaa.

“Karibu Malik…” Alfred Gonzo alimkaribisha Kachero Inspekta Malik, ambaye alivuta kiti na kukaa huku wanatazamana.

“Nimefika, afande…” Kachero Inspekta Malik akamwambia mkuu wake wa kazi.

“Karibu…na pole na kazi…”

“Ahsante, afande…”

“Nipe taarifa za kazi Malik…”  Alfred Gonzo akamwambia.

“Upelelezi wangu unaendelea vizuri afande. Unajua tokea mauaji yale yalipotokea, nimekuwa nimebanwa sana na upelelezi, hasa ukizingatia kifo chenyewe kilivyotingwa na utata mkubwa…” Kachero Inspekta Malik akaendelea kumwambia mkuu wake.

“Ni kweli, kifo hicho kina utata, kwani inaonyesha watu waliotenda kosa hilo wana kitu kingine zaidi ya hicho. Haiwezekani watu hao wakuwinde na wewe kiasi cha kutaka kukuangamiza, ndiyo maana Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum anataka kujua upelelezi huo umefikia wapi…” Alfre Gonzo akamwambia Malik.

“Kwa vile upelelezi huu nilishauanza, niko mbioni kuukamilisha kuanzia muda wowote ndani ya saa ishirini na nne afande!” Kachero Inspekta Malik akamwambia.

“Una uhakika na unachokisema?”

“Ni kweli afande, kama si usiku wa leo, basi ni kesho!”

“Basi, kama itakuwa ni hivyo, nakutakia heri, lakini kumbuka kila mara tuwasiliane ili niweze kukupatia msaada wa askari itakapobidi. Hivi sasa endelea pake yako kwanza kwa kile tunachokwepa kuweka wapeleleza zaidi ya mmoja, kwani tunaweza kuharibu kazi. Sisi tunasubiri wakati wa ukamataji tu!”

“Sawa afande, nitakujulisha kila hatua zinavyoendelea…” Kachero Inspekta Malik alimweleza mkuu wake juu ya upelelezi wake ulivyokuwa unakwenda tokea alivyouanza, na pia angemtia mbaroni muuaji wakati wowote!

Baada ya kumaliza kumpa taarifa Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, Kachero Inspekta Malik aliaga na kutoka. Wakati huo ilikuwa imetimu saa kumi na moja za jioni, hivyo akaona hakukuwa na haja ya kuelekea nyumbani kwake, Shariff Shamba, Ilala, bali aliamua kuelekea katika miadi yake na mwanadada Helen Fataki, walikopanga kukutana, Sarova Pub, majira ya sa kumi na mbili za jioni.

Kwa vile Pub ile haikuwa mbali sana, Kachero Inspekta Malik hakutumia muda mrefu kufika kwa gari lake, ambalo alilipaki sehemu nzuri iliyojificha ikiwa ni kwa usalama zaidi ukizingatia alishamtibua John Bosho baada ya kumfuata nyumbani kwake Ukonga, jioni ile. Kwa vyovyote alijua kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa John Bosho kumwekea watu wa kumwinda na kummaliza kabla hajawatia mbaroni.

Hivyo basi, kabla ya hajaendelea na safari yake, Malik akaangaza macho pande zote kuangalia kama kuna mtu yeyote anayemfuatilia, na roho yake ilikuwa nzito kwa kutomruhusu kuangalia ndani ya Kimicho Bar, iliyokuwa jirani na sehemu anapokwenda, ambapo alishambuliwa mara ya kwanza. Akaongeza mwendo na kupenya kwenye uchochoro mmoja kwa hadhari, na kutokeza upande wa pili ya mtaa, ambapo ndipo sehemu walipoahidiana kukutana na Helen.

 Baada ya kufika pale Sarova Pub, Malik aliangaza macho yake kabla ya kutafuta sehemu ya kukaa. Muda wote alikuwa makini sana kwa kila hatua alizokuwa anakwenda, masikio, pua na hisia zake zilikuwa wazi kwa kunusa hatari yoyote itakayotokea mbele yake! Hata hivyo akiwa mawazoni, akashtuka akishikwa bega lake kwa mkono laini!

 “Ni nani? Akajiuliza Malik huku akigeuka nyuma haraka sana kwa kutoa shambulizi kama ni adui. Macho yake yakakutana na mwanadada, Helen Fataki, mwanadada mrembo aliyekuwa anatabasamu!

“Oh, ni wewe Helen?”  Kachero Inspekta Malik!

“Ndiyo, ni mimi, Malik…” Helen Fataki akamwambia huku akitabasamu.

“Jihadhari Helen, siku nyingine unaweza ukaumia usipokuwa makini! Usije kwa kunivizia!” Kachero Inspekta Malik akamwambia kimasikhara!

“Kwa hivyo ulikuwa tayari kunimaliza?”

“Ni kitu kama hicho!

“Duh, pole sana…”

Wakasalimiana wakiwa bado wamesimama, na baada ya hapo wakatafuta sehemu ya kukaa kwa ajili ya maongezi yao muhimu. Lakini kwa kujihami, Helen akamwambia:

“Tusikae humu ndani.”

“Kwa nini?” Malik akamuuliza baada ya Helen kumwambia vile!

“Ni kwa ajili ya usalama zaidi!”

“Mbona sikuelewi?”

“Utanielewa tu…”

“Tukae wapi sasa?”

“Nifuate mimi…”

Kachero Inspekta Malik akamfuata Helen Fataki alipokuwa anaelekea. Wakapenya katika vichochoro vingine kadhaa vya eneo lile la Buguruni na kutokeza upande wa pili wa Pub ile. Sehemu ile kulikwa na baa nyingine tena, ambapo wanywaji wengi walikuwa wamekaa katika viti vilivyopangwa nje. Hakika Malik akashangaa kuwa mwanadada yule alikuwa amevifahamu vipi vchochoro vyote vile?

“Hapa ndiyo pazuri…panafaa kwa maongezi yetu bila bughudha zozote!”

“Mh, wewe ni kiboko!” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen Fataki huku akivuta kiti cha plastiki na kukaa, akifuatiwa na Helen.

“Kiboko kivipi?” Helan Fataki akamuuliza.

“Yaani unajua vichochoro vingi kama askari?”

“Ndiyo utambue kuwa mpaka sasa uko na mtu wa shughuli, si mchezo!” Helen akaendelea kumwambia Malik kwa msisitizo!

Baada ya kukaa tu, mhudumu, mwanadada mmoja akawaendea pale walipokuwa wamekaa. Akiwa amejiandaa, Helen akaagiza vinywaji, ambavyo kila mmoja alikuwa anatumia. Ni vinywaji ambavyo walipelekewa wakabaki wakiendelea kunywa taratibu. Sehemu ile waliyokuwa wamekaa, palikuwa na giza kiasi, lilifanya wasiwasi kuonekana kirahisi.

“Hapa sasa tunaweza kuongea mambo yetu!” Helen Fataki akamwambia Malik huku akimimina kinywaji chake kwenye glasi.

“Ni kweli, nimeitikia wito wako, naomba unipe michapo!” Kachero Inspekta Malik akamjibu huku akijiweka vizuri pale kwenye kiti walipokuwa amekaa. Helen Fataki akajiandaa kumwelezea!

********        

WAKATI Getruda akiendelea kuwaza juu ya kile alichokuwa ameelezwa na John Bosho, yeye John aliwapigia simu vijana wake wa kazi, Robi, Kessy, Chogolo, Muba na Shabani, wakutane Machimbo ya Mawe, baada ya saa tatu. Alipomaliza kuwataarifu, akaingia chumbani huku hasira zake zinaonekana wazi. Getruda naye akamfuata nyuma na kumkuta akifungua kabati la nguo na kuanza kutoa nguo maalum kwa ajili ya kazi hiyo!

 John Bosho akachukua fulana nyepesi iliyobana na suruali nyeusi ya Jeans na koti kubwa jeusi la ngozi. Vingine ni kofia kubwa ya pama, na miwani mieusi, lakini iliyoweza hata kuona hata gizani, na kisu aina ya Okapi. Pia, hakuacha kuchukua bastola kubwa, iliyokuwa na risasi za kutosha. Baada ya kumaliza kufanya maandalizi, akavalia zile nguo na kumfanya abadilike na kuwa mtu wa aina yake! Akatisha hata kumwangalia!

Wakati wote ule Getruda alikuwa akimwangalia John Bosho kwa hofu kubwa iliyokuwa imejengeka moyoni mwake. Na pale ndipo alipouhakikisha unyama wake, kiasi cha kujiona kama nusu mfu. Akajiona kama na yeye angeweza kugeukwa muda wowote, kama alivyofanywa rafiki yake mkubwa, Anita, ikiwa ni baada ya kuijua siri ya kifo chake!

 Makubwa!

“Getruda…” John Bosho akamwita kwa sauti ndogo.

“Bee…” Getruda akaitikia huku akimwangalia.

“Mbona umenyemeza kimya? Jiandae tuondoke, alah!” John Bosho akamwambia!

“Mimi niko tayari…” Getruda akamwambia huku akijiangalia.

“Yaani hivyo ulivyo? Chukua hili koti kubwa uvae!” John Bosho  akamwambia huku akimrushia koti moja kubwa, ambalo alilitoa ndani ya kabati. Getruda akalichukua na kulivaa!

Baada ya kuwa tayari, John Bosho na Getruda walitoka nje na kupanda lile gari aina ya Toyota Harrier, na safari ya kwenda Chamazi ikaanza huku wote wakiwa kimya ndani ya gari. Kila mmoja akiwa na mawazo yake, na hakuna aliyezungumza na mwenzake hadi walipofika Mbagala, kwa mganga wa jadi, mzee Chiloto Bandua. Hata hivyo ili wasijulikane, John akalipaki gari mbali na nyumba ya mganga yule.

“Tumeshafika!” John Bosho akamwambia Getruda ambaye alikuwa mbali kimawazo!

“Mh, tumeshafika?” Getruda akauliza.

“Ndiyo, tumeshafika…”

“Sasa kinachoendelea?”

“Tushuke tumfuate!”

“Haya…”

 John Bosho na Getruda walishuka kutoka garini, na kuiendea nyumba ya mganga huyo kwa mwendo wa wastani kama watu waliokuwa wanapita njia tu. Eneo zima lilikuwa limefunikwa kwa giza kiasi, lililomfurahisha John, kwani angeifanya kazi yake kwa wepesi zaidi na kumtia adabu mzee yule ambaye kwa muda ule alikuwa amehesabia kuwa alikuwa amemtapeli na kula fedha zake.

Baada ya kufika katika himaya yake,walimkuta mzee Chiloto Bandua amekaa nje ya kibaraza cha nyumba yake, kwenye kiti cha uvivu, na hakukuwa na wateja kwa muda ule. Alipowaona wageni wale, akawakaribisha ndani ya chumba cha kuhudumia wateja kilichokuwa upande wa pili wa nyumba yake kubwa. Lakini John alikataa na kumwambia wakutane faragha, kwani kuna maongezi muhimu. Hata hivyo mzee Chiloto alishtuka baada ya kuambiwa vile!

“Kwani vipi?” Mzee Chiloto Bandua akauliza!

“Leo hatukuja kwa tiba…nina shida nyingine!” John Bosho akamwambia.

“Oh!” Getruda akaguna kwa mbali!

“Shida gani usiku huu jamani?” Mzee Chiloto akaendelea kusema huku wasiwasi ukimzidi! Ule ugeni wa John Bosho ulimtia wasiwasi, hasa ukizingatia ile dawa aliyomtengenezea majuzi tu, ilikuwa haifanyi kazi!

“Ni shida ya kawaida tu mzee, mbona huwa unatibu hata usiku?” John Bosho akaendelea kumwambia.

“Lakini si umesema leo huhitaji matibabu?” Mzee Chiloto Bandua akaendelea kumuuliza!

“Wewe njoo tuongee, usiwe na wasiwasi…” John Bosho akamwambia kwa sauti ya upole iliyomridhisha Mzee Chiloto Bandua. Ndipo waliposogea kando nyuma ya nyumba yake kubwa.

“Haya jamani, ni shida gani?” Mzee Chiloto Bandua akawauliza John na Getruda waliokuwa mithili ya giza, kwa ajili ya zile nguo nyeusi walizokuwa wamevalia!

“Mzee Chiloto!” John Bosho  akaanza kumwambia.

“Nakusikiliza bwana mdogo…” Mzee Chiloto akamwambia huku akimwangalia kwa makini sana.

“Mimi nimekuja hapa kwa jambo moja tu!”

“Jambo gani hilo?”

“Mimi nilichojia hapa siyo kingine zaidi ya kutaka kujua kwamba ile dawa uliyonitengenezea ni ya kweli ama la!

“Kwani vipi?”

“Uliniambia kwamba unanitibia ili Polisi wasiweze  kunigundua kama ni mimi niliyehusika na mauaji ya mchumba wangu,” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Sasa hapa ninapoongea na wewe, ninaandamwa kishenzi!”

“Ina maana wanakufuata?” Mzee Chiloto Bandua akamuuliza kana kwamba hakumwelewa!

“Ndiyo jibu lake!” Akasisitiza John Bosho.

“Au ulivunja masharti?”

“Masharti gani uliyonipa?”

“Mh, makubwa!” Mzee Chiloto Bandua akasema huku akianza kuogopa! Alijua fika kuwa John ni jambazi, na kamwe jambazi hana rafiki!

“Ni makubwa kweli!” Akaongeza John Bosho na kuongeza. “Tena umenichimbisha kaburi la marehemu, kumbe usanii mtupu!”

“Aisee, sasa. Haidhuru, ngoja nakuja…” Mzee Chiloto akasema huku akitaka kuondoka ikiwa nia yake ni kukimbia!

“Unakwenda wapi?” John alimuuliza.

“Nakwenda kujisaidia…oh!”

“Jisaidie hapa hapa…leo mpaka kieleweke!”

“Yamekuwa hayo bwana mdogo?”

“Ndiyo, huendi popote!” John Bosho  akamwambia huku akimkamata kwa nguvu ili asiweze kumponyoka!

Halafu John Bosho akampiga ngumi moja ya nguvu, iliyompata kwenye taya lake, ambayo iliyomfanya Mzee Chiloto aanguke chini kwa kishindo! Akanusa ardhi na kusikia harufu yake!

“Ooohps! Mhn!” Mzee Chiloto Bandua akatoa mguno ulioambatana na maumivu!

“Nakuua!” John Bosho  akamwambia.

“Usiniue tafadhali!” Mzee Chiloto akasema kwa sauti huku amepiga magoti!

“Sasa kwa nini ulinidanganya?”

“Oh…oh…” Mzee Chiloto Bandua akaendelea kugugumia!

“Lazima niitoe roho yako! Nimeshachukia!” John Bosho akamwambia huku amemwekea bastola kichwani! Mzee Chiloto akaendelea kutweta kwa woga! Kifo si mchezo!

“Nisamehe bwana mdogo…”

“Rudisha fedha zangu!”

“Sina n’nshatumia…oooh!”

“Msamehe …naomba umsamehe John!” Getruda akamwambia.

“Wewe unamwonea huruma sivyo?”

“Msamehe tu…” akasisitiza Getruda huku akimwonea huruma mzee yule.

“Haya, toka hapa!” John Bosho  akamwambia Mzee Chiloto bandua huku akimsindikiza kwa teke la nguvu!

Mzee Chiloto akachomoka mbio mithili ya Paka mwizi aliyekurupushwa akidokoa nyama jikoni! Akapotea gizani na kuwaacha John na Getruda wakiumia mbavu!

“Bahati yake, twende zetu Machimbo ya Mawe!” John Bosho akamwambia Getruda huku akiichomeka bastola yake kiunoni.

Wote wawili wakaondoka kwa mwendo wa kawaida kuutoka mji wa mganga Chiloto, kuelekea kule walikoliacha gari lao. Hakuna aliyemsemesha mwenzake!

Ni mtafutano!

********   

HELEN Fataki alivuta pumzi ndefu na kuzishusha, punde tu baada ya kupiga funda moja la pombe yake na kuiweka glasi chini. Halafu akamwangalia Kachero Inspekta Malik takriban dakika moja hivi, kwani alikuwa ameamua kumtolea ukweli ili kurahisisha kazi yake ya upelelezi iliyokuwa inamkabili.

“Kwanza kabisa napenda kukujulisha kwamba sakata lote unalolifuatilia, mimi nalifahamu fika!” Helen Fataki akamwambia Malik!

“Ina maana hata mimi ulikuwa unanifahamu sivyo?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza huku akimwangalia kwa makini.

“Ndiyo. Mimi nakufahamu, na ndiyo maana nikakufuatilia ili nikusaidie juu ya huyo mtu hatari, John Bosho, na juu ya kifo cha mwanadada Anita. Narudia kusema kwamba ndiyo maana jana nikakufuata nikiwa na nia ya kukupa msaada. Hivyo basi,  mpaka sasa elewa hilo!”

“Aisee, basi naomba unipashe vizuri…” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen. Akaona ni mtu aliyempunguzia kazi! Ukweli hakutegemea kitu kama hicho!

“Kwanza kabisa, mimi nimefahamiana na John Bosho kwa muda mrefu sana, kwa upande wa mambo ya kibiashara. Lakini baada ya kugundua vitendo vyake viovu, ndipo nikaamua kuachana naye, ili asije akanipakazia…” Helen Fataki akamwambia, lakini hakugusia kuwa waliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi!

“Mlikuwa mnafanya biashara gani?”

“Ni biashara nyingi, lakini nyingine zilikuwa za haramu, ambazo nimeshaziacha…”

“Hizo achana nazo…hebu tuendelee…” Kachero Inspekta Malik  akamwambia huku akimsikiliza kwa makini.

“Basi, yeye John Bosho alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu Anita kwa muda mrefu, kiasi ambacho waliamua kuwa wachumba na kupanga kuoana. Lakini baadaye John akavutiwa na rafiki yake, Anita, aitwaye Getruda. Akatembea naye na kumfanya mpenzi wake. Mwishowe Anita akagundua na kuamua kuuvunja uhusiano kabisa, kiasi cha kuwa maadui kama Paka na Panya…” Helen akanyamaza kidogo huku akimwangalia Malik.

“Aisee, mbona habari hii inasisimua?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza Helen.

“Basi, kwa vile Anita alikuwa ameshazijua siri za John Bosho, kama ni jambazi, ndipo akaamua kumuua kwa stahili ya aina yake ya kumdunga sindano ya sumu ya nyongo ya Mamba, baada ya kumvizia bafuni wakati anaoga. Kwa hivyo tambua mpaka sasa muuaji ni John Bosho!”

“Mungu wangu!” Kachero Inspekta Malik akasema na kuendelea. “Sasa wewe ndiyo umenipa picha kamili. Yeye ndiye muuaji, na pia waliofukua lile kaburi na kuitoa maiti ya Anita. Lakini sidhani kama yuko peke yake!”

“Hayuko peke yake…” Helen akasema na kuendelea. “John Bosho anamiliki Kikosi cha Uhalifu akiwa na vijana wake kadhaa, ambao huwatuma kufanya uhalifu katika sehemu mbalimbali hapa nchini!”

“Unasema kweli?”

“Ni kweli, ni vijana hatari ambao wameshatenda maovu mengi sana, na pia wana maficho yao ya siri yaliyoko kule Ubungo Machimbo ya Mawe, ambapo wana bohari kubwa wanalolitumia kama sehemu yao ya kutendea uhalifu…” Helen akaendelea kumwambia na kubaki akimwangalia.

“Hata hivyo,” Helen akaendelea kusema. “Kuna habari njema kwamba usiku wa leo wamepanga kwenda kukutana kwa kikao cha faragha. Kwa hivyo mimi nimejitolea kukusaidia ikiwezekana kukupeleka kuwachunguza. Au unasemaje?”    

“Kama umeamua kunisaidia hakuna tatizo, mimi niko tayari. Baada ya kunipeleka huko, nitawasiliana na uongozi wa juu na taratibu za kuwakamata zitafuata mara moja!” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen.

“Naapa kukusaidia…ondoa shaka!” Helen akamwambia.

“Basi, nashukuru, na pia utakuwa umelisaidia Jeshi la Polisi ukiwa kama Raia mwema!”

“Ni jukumu letu sote, na kama wote tungefanya hivyo, hakika uhalifu ungepungua kama siyo kumalizika kabisa!”

“Ni kuupunguza tu, lakini uhalifu hauwezi kwisha…”

Wakati Kachero Inspekta Malik akiongea na Helen Fataki, mara wakaingia vijana wawili waliokuwa wameongozana. Vijana hao walikuwa na maumbile yaliyoshupaa na kuonyesha walikuwa ni watu wa mazoezi, na baada ya kuingia, wakatafuta sehemu ya kukaa, ambayo ilikuwa mbali kidogo na sehemu ile waliyokuwa wamekaa wao.

Mhudumu mmoja wa kike ambaye alionyesha kuwa anawafahamu, alipowaona akawaendea pale walipokuwa wamekaa. Wakamuagiza vinywaji na kuendelea kunywa taratibu. Hata hivyo, Malik  hakuwafahamu wala kuwatilia mashaka.

“Umewaona wale vijana?” Helen Fataki akamwambia Kachero Inspekta  Malik.

“Si wale waliokaa kule mwisho?” Akauliza Malik.

“Ndiyo wenyewe…” Helen akasema

“Nimewaona…” Kachero Inspekta Malik akamwambia huku akiendelea kuwaangalia ingawa hakuweza kuwaona vizuri kutokana na sehemu ile kuwa na giza.

“Basi, wale ni vijana wa John Bosho, ambao wanaojulikana kwa majina ya Robi na Kessy. Bila shaka wanakwenda kwenye maficho yao kama walivyopanga na bosi wao. Hapa bila wanapata vinywaji tu!” Helen Fataki akamwambia Malik

“Kama wanakwenda kwenye maficho yao, basi tutawafuatilia!” Kachero Inspekta Malik akasema na kuendelea. “Na itakuwa wananisaidia sana kuyafahamu maficho yao! Tutawafuatilia!”

“Hakuna shaka…leo kazi moja tu!”

“Mpaka kieleweke!”

Kachero Inspekta Malik akaendelea kujipa moyo!

      ********

NI kweli kwamba baada ya vijana, Robi na Kessy kuingia katika eneo lile la baa, hawakuwaona Kachero Inspekta Malik, wala Helen Fataki katika sehemu ile walipokuwa wamekaa, hasa ukizingatia palikuwa na giza kiasi, lililosababishwa na taa yenye mwanga wa kijani iliyokuwa inawaka. Walikuwa wameamua kupitia pale wakiwa safarini kuelekea Machimbo ya Mawe, baada ya kutaarifiwa na bosi wao, John Bosho.

John Bosho aliwajulisha wakati ule alipokuwa anakwenda nyumbani kwa mganga wa jadi, mzee Chiloto, akiongozana na Getruda.  Hivyo basi, vijana hao walielekea kule machimboni kiawamu, kwani hawakupenda kuongozana wote kwa kuhofia kujiingiza kwenye mtego wa Jeshi la Polisi, hasa ukizingatia hali ilikuwa imeshachafuka!

Ndipo, Robi na Kessy walipoamua kupitia kwanza katika baa ile, ili kupooza makoo yao. Kwa vile walikuwa bado vijana wabichi na wanaohusudu sana ulevi na wanawake, vijana hao walijihusisha sana na wale wahudumu muda wote waliokuwa pale, na pia kunywa pombe kwa pupa!

Kwa upande wa Kachero Inspekta Malik na Helen Fataki, walikuwa wakifuatilia nyendo za vijana wale, ambapo nao waliendelea kunywa huku mara nyingi wakiwasiliana kwa simu, kudhihirisha kuwa walikuwa na mipango mikubwa iliyokuwa inawakabili. Tuseme kwamba walikuwa hawatulii vitini, mara nyingi walikuwa wakinyanyuka na kuongea kwa simu, kudhihirisha kwamba hawakutaka mtu yeyote asikie yale mazungumzo yao.

Baada ya kutimu saa nne za usiku, wote walikuwa wameshapata nishai ya kutosha, hivyo wakanyanyuka vitini na kuamua kuondoka wakiwa wameongozana. Robin  na Kessy wakaelekea kwenye gari lao aina ya Toyota Mark 11 Grande, waliyofika nayo pale, ambalo lilikuwa katikati ya magari mengine.

Baada ya kupanda wakaondoka kuelekea Machimbo ya Mawe, dereva akiwa ni Robi, na Kessy akiwa amekaa upande wa kushoto. Wakaifuata Barabara ya Nelson Mandela kwa mwendo wa wastani, kama vile watu wasiokuwa na haraka yoyote, wakiwa wanaongea mambo yao huku muziki mororo ukitumbuiza ndani ya gari na kutakasa nafsi yao usiku ule.

 Tena, vijana hao walikuwa wakivuta sigara kwa pupa na kupuliza moshi ovyo. Kwa ujumla pale walipokuwa walikuwa wamekamilika ipasavyo, wakiwa wamechimbia bastola zao sehemu fulani, kiasi cha kuwafanya wajiamini kupita kiasi. Hawakutishika na chochote!

Mara simu ya mkononi ya Robi ikaita. Kwa haraka akaichukua kutoka katika mfuko wa kushoto na kuipachika sikioni.

Mkono mwingine wa kushoto Robi akawa anaendesha gari. Kessy naye akawa anamkodolea macho Robi, ili kujua kwamba ile simu ilikuwa inatoka kwa nani! Simu ilikuwa imetoka kwa bosi wao, John Bosho!

Na wakati huo ndiyo alikuwa anatokea Chamazi, kwa Mganga, mzee Chiloto!

“Bosi…Robi naongea…” Robi akaipokea.

“Mko wapi saa hizi?” John Bosho akauliza kwa sauti iliyojaa hasira!

“Ndiyo tunaelekea Machimbo ya Mawe bosi…”

“Mko wangapi?”

“Niko mimi na Kessy!”

“Je, wengine…Chogolo, Muba na Shabani…”

“Wameshatangulia bosi.”

“Ok, na mimi nakuja huko.”

“Sawa bosi…”

Wakakata simu baada ya mawasiliano.

“Ni nani? Au bosi?” Robi akamuuliza.

“Ndiyo…ni bosi. Salamu hizo mwanangu!”

“Anasemaje?”

“Anataka kujua tuko wapi! Na yeye yuko njiani anakuja!”

“Mh, basi leo kuna kazi…najua bosi atakuwa amechukia sana. Lakini ni kwanini alimwua Anita, kiasi cha kuleta usumbufu wote huu?”

“Ah, hata mimi sielewi. Yote ni mipango yake mwenyewe! We’ twende huko huko tukamsikilize!”

Robi akaendelea kuendesha gari, ambapo usiku ule magari yalikuwa machache sana barabarani kiasi cha kuwafanya wasipoteane!

********    

WALIENDELEA kuwaungia mkia. Kachero Inspekta Malik  na Helen Fataki waliendelea kuwafuatilia nyuma watu wale pasipo wao kugundua, hadi walipofika eneo la Tabata na kuendelea na safari mpaka Ubungo Riverside. Hapo Robi alipinda kulia na kuifuata barabara moja ya udongo, iliyokuwa inaelekea katika makazi ya watu eneo lile la Ubungo.

Ni eneo ambalo ndiyo kwanza nyumba mpya zilikuwa zinajengwa katika viwanja vilivyopimwa, na chache zikiwa zimeshakamilika na kuhamiwa. Basi, wakaifuata barabara hiyo, huku wakipanda na kushuka milima, hadi walipofika katika sehemu ya tambarare. Sehemu hiyo pia palikuwa na nyumba mpya zilizojengwa kwa mpangilio maalum.

Ili wasishtuke kama walikuwa wanafuatiliwa, Malik akazima taa zote za gari na kuendesha kwa uzoefu. Hatimaye wakafika katika eneo lililokuwa na nyumba chache, na miti mingi ya mikorosho. Ni eneo linaloitwa Machimbo ya Mawe, ambapo kipindi cha nyuma palikuwa panachimbwa mawe ya ujenzi, na kampuni moja ya ujenzi.

Vilevile palikuwa pamejengwa mabohari kadhaa ya kuhifadhia bidhaa, na mengine ni kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi, makatapila,vidampa vya kubebea mchanga, malori na mitambo mingine inayohusiana na shughuli za ujenzi kwa ujumla. Kwa mbele kama umbali wa mita hamsini hivi, palikuwa na uzio mkubwa wa seng’enge na waya, uliozunguka eneo lote ili kudhibiti watu wenye nia mbaya kuweza kuingia.

Kwa ndani ya uzio palikuwa na jengo kubwa lililiojengwa mjengo wa bohari, likiwa limezungukwa na miti kiasi cha kufanya lijifiche na kutawaliwa na giza kwa upande wa nje. Lakini kwa ndani palikuwa na taa chache zilizokuwa zinawaka kuzunguka hilo bohari, ambazo zilikuwa na mwanga hafifu usiofika mbali.

Gari walilokuwemo Robin na mwenzake, Kessy lilisimamishwa nje ya geti kubwaa la chuma, ambapo upande wa juu hapo nje, palikuwa na kibao kikubwa cha mbao, kilichoandikwa maandishi makubwa yaliyosomeka: ‘J.B.ENTERPISES LTD.’ Ni maandishi yaliyokuwa yanamulikwa na taa yenye mwanga mkali kiasi cha kufanya yasomeke kwa uwazi. Honi ikapigwa mara tatu hivi, halafu akatokea mlinzi mmoja aliyekuwa amevalia koti refu jeusi, na kifuani mwake amebeba bunduki aina ya Automatic Rifle.

Kabla ya kuwafungulia lile geti, mlinzi huyo akatoka hadi nje na kuwakagua kama walikuwa ni watu wao, au ni watu wengine wasiohusika. Baada ya kuhakikisha ni watu wao, akalifungua geti na wao wakaingia ndani na geti likafungwa kama mwanzo. Kama walivyokuwa wametaarifiwa mwanzo na John Bosho, vijana wote walikuwa wameshafika ndani ya lile bohari, wakimsubiri bosi wao, kwani wa mwisho kufika walikuwa ni Robi na Kessy.

Basi, vijana wote wakaingia ndani ya chumba maalum kilichokuwa ndani ya bohari lile, kumsubiri bosi wao kama alivyowaahidi wakutane. Wote wakajiandaa kupokea ujumbe mzito! Na siyo mwingine zaidi ya mapambano!

“Unaona pale waliposimamisha gari?” Helen Fataki akamwambia Kachero Inspekta Malik

“Ndiyo, naona…” Malik akasema.

“Ndipo penye bohari lenyewe, sasa tusubiri mpaka waingie na sisi tupitilize…”

“Sawa,” Kachero Inspekta Malik akasema huku akilisimamisha gari.

Baada ya lile gari walilokuwemo Robi na Kessy kuingia ndani ya uzio wa bohari, Kachero Inspekta Malik na Helen Fataki, waliokuwa ndani ya gari wakiwafuatilia vijana hao, wakapitiliza moja kwa moja ili wasije wakashtukiwa, ambapo Malik akasimamisha mbele kidogo, sehemu ambayo ilikuwa siyo rahisi kuonekana, kwani palikuwa na vichaka na miti midogo midogo iliyokuwa na kiza.

Wote wakashuka na kuanza kurudi walipotokea kwa miguu taratibu na kwa tahadhari ya hali ya juu, huku mkononi mwake, Malik  amekamata bastola yake imara, na redio ya mawasiliano (Radio Call)  ameipachika kiunoni katika mkanda wa suruali, na pia simu yake ikawa katika mfuko wa shati.Wakati wote huo, Helen alikuwa akimwelekeza jinsi yale maficho yao yalivyokuwa, ukizingatia yeye aliyafahamu yalivyo.

Baada ya kutembea kwa muda, wote wawili wakaamua kujificha kwenye kichaka kidogo kilichokuwa kando ya barabara, chini ya mti wa mkorosho. Ni sehemu ambayo haikuwa mbali sana na bohari lile walilokuwa wanaliendea, ni umbali wa mita mia hamsini hivi. Malik na Helen aliamua kujificha pale kwa sababu waliona mwanga wa taa za gari ukiwamulika kuelekea sehemu waliyokuwa wanaelekea.

Wakabanisha pale hadi gari lile lilipowapita kwa mwendo wa wastani, ambapo lilikuwa ni gari aina ya Toyota Harrier ya rangi ya fedha, ambayo ndani yake palikuwa na watu wawili, John Bosho na Getruda, na baada ya gari lile kuwapita, likaelekea moja kwa moja usawa wa geti la kuingilia mle ndani ya bohari.

Mlinzi yule wa mwanzo aliyekuwa pale getini karibu na kibanda cha ulinzi, akaenda kulifungua geti na kuliruhusu gari hilo kuingia ndani. Baada ya kuingia, gari hilo likaenda kupaki sehemu maalum ya kupaki magari iliyokuwa upande wa mbele ya bohari, na pia yalikuwepo magari mengine machache yanayowahusu wao waliokuwa wamefika kwa ajili ya kikao hicho.  John Bosho na Getruda wakashuka kutoka ndani ya gari na kuingia ndani ya bohari lile kwa mwendo wa haraka!

        *********

WAKIWA bado wamebanisha kichakani, Kachero Inspekta Malik na Helen Fataki, waliweza kuona jinsi gari lilivyoingia mle ndani, na kisha yule mlinzi alivyofunga geti kama mwanzo, halafu akarudi katika kibanda chake kilichokuwa karibu na geti, wala hakujua kama umbali wa mita chache tu, kulikuwa na watu waliokuwa na kiu ya kuwaingilia mle ndani!

“Umewaona?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza Helen.

“Ndiyo, imewaona,” Helen akasema na kuongeza. “Ni kama nilivyokwambia kuwa leo ni siku ya funga kazi, kwani wote wanakutana mle ndani kwa kikao maalum. Hivyo ni wakati muafaka wa kuwakamata!”

“Vizuri sana,” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen na kuendelea. “Sasa wewe nisubiri hapo, mimi nakwenda katika eneo lile kuchunguza zaidi. Halafu nitawasiliana na Kikosi Maalum cha Polisi!”

“Haya, mimi nakusubiri hapa…nakutakia kazi njema!” Helen Fataki akamwambia Malik huku akimpiga busu shavuni!

Kwa bahati nzuri siku ile Kachero Inspekta Malik alikuwa amevalia nguo za rangi nyeusi zilizoshabihiana na lile giza. Baada ya kutoka pale, akaikamata bastola yake vizuri kwa mkono wake wa kulia na kuanza kunyata ili miguu yake isiweze kutoa sauti na kuwafanya watu washtuke kwamba kulikuwa na adui. Hatimaye akaufikia ule uzio wa waya uliozunguka eneo zima la bohari.

Akiwa amechuchumaa chini, Kachero Inspekta Malik akauinua uso wake na kuchungulia mle ndani takriban dakika tatu hivi, lakini hakuweza kuona chochote zaidi ya giza la ukimya. Kwa kutumia nguvu, akaunyanyua ule waya uliotumika kama uzio kwa juu, kiasi kwamba aliweza kupata mwanya wa kuweza kuingia ndani ya uzio ule kwa kupenyeza kiwiliwili chake kizima.

Hatimaye baada ya kufanikiwa kuingia ndani ya uzio, akaanza kutembea kwa tahadhari kubwa kuelekea usawa wa jengo lile kwa upande wa nyuma, ambao ulikuwa na miti mingi. Kila alivyokuwa anatembea, Malik alikuwa akisikia sauti za watu, zikionyesha wazi kwamba zilikuwa zinatokea sehemu aliyokuwepo yeye. Hivyo akaruka na kujificha nyuma ya tanki moja la kuhifadhia maji, lililokuwa karibu na kufanya wasiweze kumwona.

Hata hivyo baada ya kusimama kwa muda, sauti zile zikatoweka na akapata fursa ya kuliendea lile jengo la bohari ambalo halikuwa mbali sana, na pia akijikinga na vivuli vya miti ile iliyozunguka eneo lote.  Hatua kadhaa kabla ya kulifikia hilo jengo, Malik akasikia vishindo kikikimbilia sehemu hiuyo aliyokuwa amesimama yeye! Ni kitu gani tena?

Hamad! Malik akawaona mbwa wawili wakubwa mithili ya beberu, wakimwendea kimya kimya bila kubweka, kitu ambacho alikuwa hajakitegemea. Ni Mbwa ambao walikuwa wamepata mafunzo maalum ya kushambulia bila kupiga kelele, basi, akagundua kuwa hawakuweka ulinzi upande wa nyuma! Hata hivyo hakupaniki, akasimama tayari kwa kuwakabili, kwani alijua kama angekimbia tu, wangemshambulia kwa nyuma! Mbwa hao nao wakasimama wakimsubiri akimbie tu, wamrukie na kumng’ata!

Kwa vile bastola yake ilikuwa na kiwambo cha kuzuia mvumo, akakaza mkono na kufyetua risasi mbili kuelekea walipo Mbwa wale, ambao kwa pamoja waliruka juu na kisha kutua chini kwa kishindo wakiwa maiti. Kitendo kile kilikuwa cha haraka sana, na pia hakuzubaa, akajiondoa huku akikimbia kidogo kuelekea upande wa nyuma wa bohari,ambalo lilikuwa limejengwa kama mabohari mengine ya kawaida tu, lakini upande wa kushoto palikuwa na vyumba  vilivyotumika kama ofisi, pamoja na ukumbi mdogo wa mikutano.

Ni chumba ambacho Kachero Inspekta Malik alihisi walikuwepo wale watu waliokuwa wanaongea. Kwa bahati nzuri sehemu ile aliyobanisha ukutani, palikuwa na dirisha kubwa lililokuwa na vioo. Akajiinua kidogo na kuchungulia kule ndani! Baada ya kuchungulia, aliweza kuona vizuri watu wote waliokuwa mle ndani, ambao ni John Bosho mwenyewe, aliyekuwa amekaa mbele yao pamoja na Getruda.

Halafu walifuata vijana wale, Robi, Kessy, Shabani, Muba na Chogo. Wote walikuwa wamekaa kwenye viti wakionyesha kuwa na kikao maalum cha siri baada ya mipango yao kuharibika! Hivyo Malik akawa anawasikiliza jinsi walivyokuwa wanapanga mikakati yao. Ndani ya chumba hicho, John Bosho alikohoa kidogo ili kusafisha koo lake, halafu akawatizama vijana wake huku amekunja sura kwa hasira alizokuwa nazo, ambao wote waliweza kuzitambua kwa jinsi walivyomzoea bosi wao. Hasa mipango aliyopanga inakwenda mrama!

“Tumekutana hapa tena usiku huu!” John Bosho akawaambia.

“Ndiyo bosi…” wakasema.

“Ni matumaini yangu kuwa nyote hamjambo!” John Bosho akaendelea kuwaambia!

“Sisi hatujambo bosi!” Wote wakasema!

“Jamani…nimeona niwaite huku kwa ajili ya kikao hiki cha dharura usiku huu,” John Bosho akasema ba kuendelea. “Kwa upande wangu naona mambo siyo mazuri, yanazidi kuwa mabaya mara baada ya kumuua mchumba wangu,!”

Wakaendelea kumsikiliza!

“Na hata kama ningemwacha hai Anita, asingesita kunichoma kwa Polisi kuwa alikuwa anaishi na Mchumba Jambazi! Cha msingi ninachotaka kuongelea ni kuhusu huyu mtu wa pili, Kachero wa Polisi, Inspekta Malik. Ananifuatilia kwa kasi sana, kiasi kwamba ameshapafahamu hata nyumbani kwangu, Ukonga, na mbaya zaidi ameshajua kuwa mimi ndiye muuaji wa mchumba wangu!”

“Mh, ni hatari!” Robi akasema

“Aisee?” Kessy akaongeza kusema!

“Basi, jioni ya leo amekuja nyumbani, Ukonga, na kuanza kunihoji maswali mengi, ambayo kwa kiasi fulani yaliniingiza mtegoni!”

“Mh!” Robi akaguna!

“Mungu wangu!” Kessy akadakia!

“Aisee?” Muba naye akasema kwa kuonyesha mshangao!”

“Tumejaribu kwa hali na mali kummaliza, lakini tumeshindwa, ikiwa ni kumtilia ile sumu kali ya nyongo ya Mamba kwenye kinywaji, lakini akafanikiwa kukwepa! Ina maana tumemshindwa mtu huyo mmoja kiasi cha kuweza kutuchanganya namba hii? Eti jamani!”

Baada ya kutoa maelezo yale, John Bosho akabaki anawaangalia huku kando yake akiwepo Getruda, aliyekuwa akijiona kama mtu aliyekuwa ndotoni. Hakutegemea kwa usiku ule kuwa katikati ya kundi la majambazi, waliokuwa wanajadili kutoa uhai wa binadamu! Na vijana, Robi, Kessy, Muba, Shabani na Chogo, wakawa wanaangaliana kwa zamu. Kwa ujumla walikuwa wamemwelewa!

“Bosi, tumekusikia vizuri…” Robi, kijana anayejiamini akasema na kuongeza. “Sisi hatujashindwa kazi!”

“Hamjashindwa? Sasa mnanipa ushsuri gani?”

“Cha muhimu ni kumsaka tena!” Robi akaongeza kwa msisitizo!

“Ni kweli bosi, tumsake tena!” Chogo naye akaunga mkono.

“Bosi, huyo Malik ni mtu mdogo sana. Tutamsaka usiku wa leo na kummaliza. Kesho asubuhi atahesabika ni marehemu. Na hata ikiwezekana tumchomee ndani ya nyumba yake baada ya kuimwagia mafuta ya Petroli!” Shabani akachangia!

“Vizuri sana…naona mna moyo. Nashukuru sana kwa kuniunga mkono katika wakatui huu mgumu. Kama mko tayari, nawasihi tuingie kazini mara moja na kuhakikisha tunamsaka mtu huyo katika sehemu yoyote atakayokuwa, labda awe mbinguni, ambapo tuna uhakika hatuwezi kufika!”

“Sawa, bosi!” Robi akasema.

“Hakuna shaka!” Akamaliza Muba!

“Ok, poteeni!”

********

MAMBO yalikuwa magumu kwa upande wa Kachero Inspekta Malik, ambaye alikuwa ameamua kujitosa na kuingia ndani ya ngome ya maadui, ikiwa ni baada ya kuyasikia yale mazungumzo waliyokuwa wanaongea, ambayo yalimtisha. Ni pale ilipotolewa adhabu ya kifo dhidi yake, ambayo ilitakiwa ikamilike baada ya saa ishirini na nne.

Hivyo basi, Kachero Inspekta Malik hakuendelea kukaa pale kando ya dirisha lile alilokuwa amejibanza, bali alijiondoa kwa mwendo wa haraka huku akijikwepesha kwenye vivuli vya miti, na kufanikiwa kutoka nje ya uzio ule kama alivyoingia. Baada ya kutoka, akatembea huku ameinama hadi alipofika katika kichaka kingine na kubanisha ndani yake.

Hakika ilikuwa ni sehemu nzuri ambayo siyo rahisi kuonekana na adui. Akiwa ndani ya kichaka hicho, Malik akatoa simu yake ya mkononi na kumpigia Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, ili amweleze hali halisi ilivyo.

“Nakupata Inspekta Malik…nipe taarifa…” upande wa pili  Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo akasema.

“Napenda kukujulisha kuwa bado niko kazini…”

“Uko wapi muda huu?”

“Niko hapa Ubungo Machimbo ya Mawe…”

“Nipe taarifa za hapo, je, kuna mafanikio?”

“Ndiyo afande, nimeigundua ngome ya wahusika tunaowatafuta. Hivi sasa wako ndani ya bohari wakipanga mipango yao, hivyo ni wakati muafaka wa kuwavamia na kuwatia mbaroni…”

“Kazi nzuri sana…hebu nipe ramani ya kufika hapo!”

“Fuata Barabara ya Nelson Mandele mpaka Ubungo Riverside. Halafu unapinda kushoto kuifuata barabara ya udongo moja kwa moja hadi kwenye mabohari ya kampuni ya ujenzi ya zamani….ni hapo…”

“Sawa, basi subiri hapo hapo…tunaandaa Kikosi Maalum cha askari, na tunakuja muda huu!”

“Sawa, afande…nawasubiri…”

Baada ya kumaliza kuwasiliana na Mkuu wa Upelelezi, Kachero Inspekta Malik akajiondoa ndani ya kichaka kile, na kuelekea pale alipokuwa amejificha mwanadada Helen Fataki. Akamkuta akiwa amejikunja na kujikunyata akipambana na mbu wengi waliokuwa wakisherehekea damu yake, ikiwa ni tafrija isiyo rasmi!

“Helen…” Kachero Inspekta Malik akamwita.

“Bee…” Helen Fataki akaitikia.

“Nimefanikiwa kufika eneo lile na kuwasikiliza mazungumzo yao waliyokuwa wanaongea, ambapo wana mkakati wa kunisaka mimi usiku wa leo na kuhakikisha kuwa wananimaliza kwa kunichomea ndani ya nyumba yangu. Hivyo nimewajulisha polisi ambao wako njiani wanakuja, hivyo basi, wewe nenda ndani ya gari ukanisubiri, kazi hiyo tuachie sisi polisi wenyewe!” Malik akamwambia Helen Fataki.

“Hakuna wasiwasi…utanikuta baada ya kazi!” Helen Fataki Fataki akasema huku akiondoka kwa mwendo wa kuinama na kunyata hadi lilipokuwa lile gari. Akaufungua mlango wa nyuma na kuingia, kisha akajilaza kwenye kiti. Kwa kiasi fulani akajisikia raha ilioje kwa kulisaidia Jeshi la Polisi akiwa raia mwema!

Kachero Inspekta Malik naye akajiondoa eneo lile kwa hatua za haraka, na kuelekea mwanzoni mwa barabara inayoelekea sehemu ile yenye mabohari, ili aweze kuwapa maelekezo Mkuu wa Upelelezi na wale askari polisi aliokuwa wanaelekea pale kutoa msaada. Baada ya kufika akabanisha kwenye kona iliyokuwa na miti ya mikorosho iliyofungamana na kufanya kuwe giza.

Baada ya dakika ishirini hivi, magari mawili, moja aina ya Land Rover 110 Deffender, na jingine Toyota Land Cruiser, yaliwasili eneo lile la Ubungo Machimbo ya Mawe, akiwemo Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo, pamoja na timu ya askari polisi maalum waliokuwa na silaha, bunduki aina ya Sub Machine Gun zilizosheheni risasi.

Askari polisi wale walishuka harakaharaka tayari kukabiliana na majambazi wale, huku wakiwa na kiongozi wao, Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo, ambaye naye alishuka haraka akiwa na bastola yake mkononi. Hakika walikuwa wamejiandaa vya kutosha, na hawakutaka kufanya makosa ya aina yoyote na kuwapoteza majambazi yale hatari. Baada ya kushuka tu, akampa maelekezo Malik kuwapanga askari wale, kila mmoja akae katika sehemu yake ili kulizunguka bohari pande zote!

*********    

JOHN Bosho na vijana wake bado walikuwa mle ndani ya bohari, wakimalizia kupanga mikakati yao bila kujua kwamba wamezingirwa na Kikosi Maalum cha Askari wa Jeshi la Polisi, waliokuwa na kiu kubwa ya kuwakamata. Kwa ujumla eneo lote lilikuwa kimya kabisa ukizingatia nyumba za wenyeji zilikuwa mbali kidogo na sehemu hiyo iliyokuwa maalum kwa ajili ya mabohari tu.

Hata hivyo yule mlinzi aliyejulikana kwa jina la Boaz, aliyekuwa pale getini tokea mwanzo, alishtuka baada ya kusikia michakacho ya miguu alipokuwa ndani ya kibanda chake. Akatoka nje na kuanza kuchunguza kwa makini na kuhisi hali ya hatari baada ya kuona vivuli vya askari wale waliokuwa wanajipanga kulizunguka bohari taratibu na kwa mpangilio maalum.

Mlinzi huyo akatupa macho yake pande zote, kisha akachomoka mbio kwa kutoka ndani ya kibanda chake, halafu akakimbilia ndani ya chumba cha mikutano huku ameinama wasiweze kumwona. Baada ya kuingia ndani ya chumba kile cha mikutano, akawakuta John Bosho na vijana wake ndiyo kwanza wanataka kutoka nje kwenda kutekeleza kazi yao!

“Wewe vipi?” John Bosho akamuuliza mlinzi yule baada ya kumwona akitweta!

“Hatari bosi!” Mlinzi huyo akasema huku akiendelea kuhema kwa nguvu!

“Hatari ya nini?” John Bosho akamuuliza.

“Tumevamiwa bosi!”

“Tumevamiwa na nani?”

“Nahisi watakuwa ni polisi…”

“Una uhakika na unachokisema?” John Bosho akamuuliza huku wasiwasi ukianza kumwingia! Akasimama!

“Ndiyo…nimewaona!”

“Oh, kazi ipo! Jamani jiandaeni kwa vita!” John Bosho akawaambia watu wake!

“Ni sawa bosi!” Robi akasema huku akijiandaa kuchukua silaha yake.

“Kumekucha!” Kessy akadakia naye akijiandaa.

“Oh, Mungu wangu!” Getruda akasema huku mikono yake ameiweka kichwani!

“Getu…usijali sana. Tupo pamoja na wala hakuna mtu yeyote wa kukutia hata kidole cha macho! Nitapambana nao!” John Bosho akamwambia huku akimshika mkono.

“Ni hatari jamani! Oh!” Getruda akaendelea kusema kwa hofu kubwa!

Vijana wote wakachukua silaha zao na kila mmoja akaruka kuchukua nafasi yake, tayari kukabiliana na askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa wameshajiandaa kule nje ya bohari!

Ni kizaazaa!

*********     

UPANDE wa nje wa bohari lile, walikuwepo, Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, na Kachero Inspekta Malik, ambao walikuwa wanawaangalia askari walivyokuwa wanajipanga kulizunguka bohari zima na kuiacha sehemu ile ya getini tu. Gonzo akamwambia Malik atoe amri ya kujisalimisha kwa majambazi yale yaliyokuwa yamejichimbia ndani!

Kachero Inspekta Malik ambaye alikuwa ameshika bastola yake mkononi, akachomoa kile kiwambo cha kuzuia sauti, halafu akafyetua risasi mbili angani na kupasua ule ukimya uliokuwa umetawala eneo lile katika usiku ule! Kisha akatoa amri kali!

“Wote mlioko ndani ya bohari, mko chini ya ulinzi! Jisalimisheni na mtoke huku mikono ikiwa juu!”

Ukatawala ukimya!

Hakuna mtu yeyote  aliyejitokeza kujisalimisha ndani ya bohari lile! Ilikuwa ni wakati huo vijana wa John Bosho walipokuwa wanachukua nafasi za kujificha. John Bosho na Getruda wakabanisha pembeni kabisa kwenye upenyo wa makabati yaliyokuwa mle ndani, wakati huo John akiwa amekamata bastola yake imara mkononi! Getruda alikuwa akitetemeka ovyo!

“Usihofu Getruda…” John Bosho akaendelea kumpa moyo!

“Oh, John umeniponza…” Getruda akamwambia.

“Poa…usijali wala usiwe na wasiwasi…” John Bosho akaendelea kusema huku akiangaza macho yake pande zote.

“Nisijali wakati nje kuna polisi?”

“Polisi hawatuwezi!”

“Hapana…jisalimishe…”

“Usiwe mwoga…yaani kirahisi namna hiyo?”

“Sasa tufanyeje?”

“Tutapambana nao!”?

“Oh, Mungu wangu!”

“Hakuna jinsi Getruda…” John Bosho akaendelea kusema huku uso wake kaukunja!

Milio mingine ya risasi ikasikika kule nje!

Askari polisi wakafyetua risasi kuelekea ndani ya bohari lile kiasi cha kutoboa mabati juu.Vijana wa John Bosho wakazidi kuchanganyikiwa na kujiweka tayari kwa mapambano ya kuokoa roho zao! Hata hivyo hawakupenda kushindwa kirahisi, kwani nao wakaanza kufyetua risasi kuelekea nje walipokuwa wamesimama wale askari polisi, ambao nao hawakukawia kujibu mapigo kwa kuanza kuwamiminia risasi kwa mpangilio maalum, ambao siyo kwa nia ya kuwaua bali waishiwe risasi na kujisalimishe!

Milio ya risasi na moshi wa baruti ikaenea eneo lote na kuchafua hali ya hewa! Ukweli ni kwamba waliona njia ya kuokoka ikiwa finyu sana, kwani baada ya muda wakaishiwa risasi walizokuwa nazo na hawakuwa na za akiba. Hapo ndipo askari polisi walipowasubiri kwa hamu wajisalimishe!

“Sasa jamani, ndiyo tumeishiwa risasi, sijui tufanyeje?” Robi akawaambia wenzake!

“Mh, ngoma nzito!” Muba akasema huku ameegemea ukuta.

“Hapa tutumie akili tu ili tuweze kuwatoka polisi hawa!” Shabani akasema huku akichungulia dirishani, ambapo aliweza kuwaona wale askari walivyokuwa wamejipanga kule nje baada ya kugundua wameishiwa risasi!

“Mimi najiondoa, siwezi kukamatwa kikuku!” Kijana, Boaz, mlinzi yule aliyekimbilia mle ndani mwanzo, akasema. Halafu akachomoka mbio huku ameinama chinichini kuelekea kwenye uchochoro mmoja uliokuwa na giza lililosababishwa na miti iliyokuwa imezunguka. Huku nyuma akafuatiwa na mvua za risasi zilizokuwa zinapigwa na wale askari polisi!

“Mamaa!” Boaz akasema huku akiruka juu! Risasi zote zilimpata kichwani na sehemu nyingine mwilini, zikamrusha mbali na kumfanya afe ndani ya ule uchochoro uliokuwa na giza!

Vijana wengine, Robi, Kessy, Chogolo, Muba na Shabani, wakaamua kutoka mbio kila mmoja na uelekeo wake. Hata hivyo wale askari waliokuwa imara, wakafyetua risasi mfululizo ambazo nyingi zilizowajeruhi na kuwaacha wakigaragara chini kwa maumivu makali na damu nyingi kuwatoka. Ndani ya bohari wakabaki John Bosho  na Getruda wakiwa wamebanisha katika sehemu ileile ya mwanzo wakiuona mwisho wao.

Ukweli ni kwamba, John Bosho na Getruda hawakuwa na njia nyingine ya kuweza kupambana na askari wale waliokuwa wamewazingira kote, ukizingatia vijana wake wote walikuwa wamejeruhiwa. Hivyo John akawa anajilaumu kwa upumbavu wa kumuua mchumba wake, Anita, kwa suala la mapenzi tu, ambalo lingeweza kuepukika kama angenyamaza!

“Oh, nimekwama jamani!” John Bosho akamwambia Getruda!

“Hakuna jinsi, ni kweli umekwama! jisalimishe tu!” Getruda akamwambia kwa kumsisitiza!

“Lakini kirahisi namna hiyo?” John Bosho akamuuliza.

“Wewe ulitakaje?’

“Hapana…” John Bosho akasema huku amemata bastola yake iliyokuwa imejaa risasi. Ni bastola iliyokuwa ina uwezo wa kubeba risasi kumi na mbili, ambao ni chache sana katika mapambano na askari waliokuwa na silaha kubwa kama bunduki.

Baada ya kuiandaa bastola yake, ndipo alipomkamata Getruda na kumwambia. “Nataka kucheza mchezo, mimi Komandoo!”

“Mchezo gani?” Getruda akamuuliza kwa hofu, kwani hakuelewa  John Bosho alikuwa amepanga kumtumia kama ngao, ili aweze kuwakwepa polisi, ambao wangesita kumpiga risasi kwa kuhofia kumdhuru Getruda asiyekuwa na hatia!

“Watatuua John!” Getruda akamwambia!

“Usiogope! Twende!” Akazidi kutoa amri!

John Bosho akabaki akivuta pumzi na kupanga jinsi ya kuwatoka polisi!

“Tafadhali tokeni nje na mjisalimishe!” Kule nje Kachero Inspekta Malik akaendelea kutoa amri kwao, ambao walikuwa wamebaki wao wawili.

Basi, kitendo bila kuchelewa, John Bosho akamsukuma Getruda mpaka kule nje huku amemkamata kwa nguvu akimtumia kama ngao! Halafu wakatoka naye mbio huku akijaribu kukwepa kwa kujibanza na vivuli vya miti iliyokuwa pale nje. Askari wakaugundua ule ujanja alioutumia. Askari wakajua kwamba John hakuwa na ujanja, hivyo wakamsubiri kwanza ili wapate wasaa mzuri wa kumkamata!

“Hafiki mbali!” Kachero Inspekta Malik akasema. “Nyie mzungukieni kwa mbele, na mimi namfuata kwa nyuma! Nitakapotoa amri tumdhibiti!”

“Sawa afande!” Askari wakasema huku wakimwangalia John Bosho alivyokuwa anakwenda huku akigeuka nyuma ya mti!

Askari polisi waliokuwa mbele yake, wakamfyetulia risasi na kumpa amri ya kusimama.

“Mungu wangu!” John Bosho akachanganyikiwa!

Akamwachia Getruda aliyekuwa kama ngao!

Bunduki za askari pamoja na bastola ya Inspekta Malik zikamwelekea!

Sasa ampige nani? Akashindwa!

“Angusha silaha yako!” Kachero Inspekta Malik akamwambia huku amemlenga kwa bastola yake!

“Sina ujanja!” John Bosho akasema. Halafu akaidondosha bastola yake chini na kunyoosha mikono yake juu!

“Shenzi sana! Umetusumbua sana!” Akasema askari mmoja!

“Mfunge pingu haraka!” Akaongeza askari mwigine!

Askari wakamzingira na kumlaza chini huku wakimfunga pingu baada ya kumpekua tayari kwa kumpeleka kwenye Kituo cha Polisi kwa hatua zaidi. Halafu wale majeruhi wengine, vijana wa John pamoja na maiti ya mlinzi wakachukuliwa kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Baada ya Getruda kuachiwa na John Bosho aliyekuwa akimtumia kama ngao, akabaki amechanganyikiwa na kujiona kama mtu aliyekuwa ndotoni. Milio ya risasi ilikuwa imemchanganya sana kitu ambacho alikuwa hajawahi kukumbana nacho! Kwa haraka Getruda akamkimbilia Mkuu wa Upelelezi,  Mrakibu Mwanamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, aliyekuwa karibu naye ikiwa ni katika kujiokoa!

“Oh, nisaidie!”

“Tulia…”  Alfred Gonzo akamwambia.

“Mimi sihusiki….majambazi ni hao!” Getruda akasema huku akitetemeka ovyo!

“Sasa ni nani kwako?”

“Ni mpenzi wa John Bosho…”

“Hukujua kama ni jambazi?”

“Sikujua!”

“Basi, tutaongozana wote mpaka kwenye Kituo cha Polisi Buguruni, na utakuwa shahidi muhimu!”  Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo akamwambia Getruda aliyekuwa bado anatetemeka!

“Sawa…” akasema Getruda huku akiyafikicha macho yake katika kiza kile.

“Panda garini…”

“Sawa…” Getruda akasema huku akijiandaa kupanda kwenye gari la polisi.

Hatimaye askari polisi wakamchukua Getruda aliyekuwa bado anatetemeka ovyo na hata haja ndogo kumtoka bila kipingamizi. Wakampakiza kwenye gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser  tayari kwa kumpeleke kituoni kwa hatua zaidi za mahojiano ya kina katika kuupata ukweli. Hakika hakuamini kama alikuwa amepona katika sakata lile baada ya kushuhudia wenzake wakisambaratishwa! Akawa anajuta ni kwanini alikuwa akishirikiana na John Bosho mtu aliyekuwa jambazi!

Kachero Inspekta  Malik akapanga askari wengine waliokuwa na magwanda, kwa ajili ya kulinda eneo lile la tukio, ili kesho yake liweze kufanyiwa uchunguzi. Kisha baada ya kuhakikisha kila kitu kimekwenda vizuri, na Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo wameshatangulia na wale watuhumiwa, Malik akajiondoa kwa hatua ndefu kuliendea gari lake, ambalo alikuwa ameliacha  huku mwanadada Helen akiwa ndani yake. Ni Helen Fataki aliyempa mpango mzima wa kuweza kuwapata watu wale, na sehemu walipokuwa wamejichimbia.

Baada ya kulifikia gari, akaufungua mlango wa upande wa dereva; akapokewa na harufu ya mafuta mazuri aliyokuwa amejipulizia Helen Fataki, ambaye muda huo alikuwa amejitandaza kwenye kiti huku akitoa tabasamu zito!

Tabasamu la ushindi!

“Twe’zetu,” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen huku akiufunga mlango wa gari na kuingia.

“Oh, pole sana…” Helen Fataki akasema huku akijiweka vizuri pale kwenye kiti cha gari.

 “Sijapoa bado…” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen Fataki huku akitabasamu.

“Vipi tena?”

“Hujanielewa tu?”

“Oh, nimekuelewa…basi subiri tufike nyumbani…”

“Poa, ama kweli kila kazi na dawa, kutokana na uchovu wa wiki nzima, ambayo umenisaidia kuhitimisha na kuwapata wabaya wetu!”

“Lilikuwa ni jukumu langu kukusaidia kama raia mwema…” Helen Fataki akamaliza kusema huku akiziweka nywele zake vizuri. 

Kacherio Inspekta Malik akalitia gari moto na kuondoka katika eneo lile la Ubungo Machimbo ya Mawe. Na eneo hilo likabaki tulivu tena baada ya pilikapilika zile za mapambano kumalizika. Hapo walibakia baadhi ya askari polisi waliopangwa kulinda eneo hilo la tukio, lililokuwa limezungushiwa utepe wa rangi ya njano ili ushahidi usiharibiwe na wananchi waliofika kushuhudia.

Mwisho

Author: admin

2 thoughts on “Muuaji asakwe

Comments are closed.