
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ametoa wito kwa watumiaji wa Kiswahili kuitazama lugha hii kwa jicho la fursa.
Naibu huyo waziri ambaye pia ni alikuwa mwanamuziki wa Bongo Fleva hapa nchini, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kuwa wepesi kung’amua kila upenyo kwa lugha hiyo na kuhakikisha inawafaidisha kwa kuwa inatambuliwa, inathaminiwa na kuaminiwa duniani.
Mwinjuma ambaye ni maarufu kwa jina la Mwana FA ametoa wito huo juzi Agosti 9, 2023 jijini Mwanza alipofungua Kongamano la sita la Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (Chalufakita).
Amesisitiza kuwa ni wakati wa kila mtumiaji na mtaalamu wa Kiswahili kuweka bidii ya kubuni namna ya kunufaika na Kiswahili. Kwa wale wenye kuandika vitabu vyenye maarifa ya ngazi mbalimbali wafanye hivyo na wenye uwezo wa kubuni na kuandaa kazi mbalimbali za kitamaduni wafanye hivyo pia.
Mwinjuma ameongeza kuwa ni muhimu kwa Waswahili kuweka bidii katika kujifunza na kutumia mifumo, nyenzo na majukwaa ya kidijiti katika kuandaa, kutangaza na kuuza kazi au mazao ya Kiswahili.
Maoni Mapya