Mwanafunzi Antonio raia wa Italia aishukuru Kampuni ya MCL

Nabil Mahamudu na Loveness John

Dar es Salaam. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anayesoma Shahada ya Umahiri katika Kiswahili, Antonio Onorati ameishukuru Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kupitia gazeti lake la Mwananchi na Tovuti ya Swahilihub kuchapisha makala yake iliyomwezesha kufahamika na kupata ajira.

Mwanafunzi huyo aliyesoma Kiswahili kuanzia shahada ya awali akiwa nchini Italia, Chuo Kikuu Cha Loriental mjini Napoli, Italia amepata kazi katika ubalozi wa Italia nchini Tanzania baada ya habari zake kusambaa mtandaoni.

Awali, katika mahojiano na Mwananchi aliyofanya hivi karibuni, Onorat alisema kilichomsukuma kusoma Kiswahili ni kutokana na raghba yake ya kujifunza utamaduni wa jamii mbalimbali.

“Nimekuja leo kwa mara nyingine nikiwa nimerudi kushukuru, mahojiano tuliyofanya mtandao wa Mwananchi Digital na habari kuchapishwa gazetini yamenisaidia kujulikana na kupewa kazi ubalozini,” amesema Onorat.

Aliongeza kuwa, “Ofisi ya balozi walishangazwa na uzungumzaji wangu wa Kiswahili hivyo walipenda nifanye kazi pale, kadhalika walishangaa mimi kuonekana katika mtandao wa Mwananchi kwa sababu ni chombo kinachoaminika katika utaoaji wa habari.”

“Naishukuru sana Mwananchi kwa kunifungulia fursa ya ajira, na ilikuwa tarehe 2 Septemba nirudi kwetu Italia ila kutokana nimepata kazi nitabaki hapa Tanzania,” amesema Onorat.

 Akizungumza kwa niaba ya MCL, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Joseph Damas amesema amefurahi kupata mrejesho na kumpongeza mwanafunzi huyo kufanya kazi kwa bidii.

 “Sisi Mwananchi kaulimbiu yetu kama inavyosema Tunaliwezesha Taifa, hivyo tunafurahi kusikia umepata fursa ya ajira. Hayo ni malengo ya Mwananchi Communications katika kuliwezesha Taifa pasipo kubagua mtu kwa hali yoyote ile iwe utaifa, kabila, hadhi na tabaka lolote,” amesema Damas.

Author: Gadi Solomon