Mwanasiasa Louis Rwagasore alivyofanikiwa kuwaunganisha Warundi kupitia lugha zao

Na Antonio Onorati

Sote tumepoteza fursa nyingi za kujua historia za mashujaa au viogozi hodari kwa sababu tunasoma sehemu moja ya historia tukisahau umuhimu wa michango ya watu wa nchi mbalimbali.

 Mfano mkubwa ni ule wa Louis Rwagasore kutoka Burundi, mtu ambaye anaweza kutufundisha mambo mengi kwa kupitia maisha yake.

Watu wachache wanajua historia ya mwanasiasa huyo ambaye aliishi wakati wa ukoloni na alithubutu kukabili utawala wa kikoloni kwa ajili ya uhuru wa nchi yake.

Louis Rwagasore alizaliwa mwaka 1932 mjini Gitega, alikuwa mtoto wa Mfalme wa Burundi, Mwambutsa Mbangiricenge, kutoka ukoo wa “Baganwa”, hawa walikuwa watu muhimu wa makao ya mfalme, walijulikana pia kama “watoto wa ngoma” na wote walikuwa na mhenga maarufu aliyeitwa Ntare Rushatsi, mfalme wa kwanza wa Burundi.

Louis Rwagasore alizaliwa mwaka 1932 mjini Gitega, alikuwa mtoto wa Mfalme wa Burundi, Mwambutsa Mbangiricenge.

Rwagasore alisoma kwenye shule ya kikoloni ya Astrida (Butare) nchini Rwanda na alimaliza masomo yake Ulaya nchini Ubelgiji.

Licha ya hali yake ya “ungwana” kuanzia wakati wa masomo yake alijitahidi sana katika kuboresha maarifa yake kuhusu namna mbalimbali ya kuwa na siasa nzuri ya kujenga taifa jipya la Burundi ya leo.

Kwa sababu ya uwezo wake alifanya kazi kwenye sehemu ya utawala wa kikoloni iitwayo  Centre administratif du Pays (CAP) tafsiri yake Utawala wa taifa, lakini baada ya muda aliacha kazi hii kwa sababu ya usumbufu wa wakurugenzi wa kikoloni.

Alianzisha chama cha kupigania uhuru wa Burundi, kiitwacho  Union pour le Progrès national (UPRONA) tafsiri yake Chama cha Umoja wa Maendeleo ya Kitaifa, na vyama vya ushirika vya kienyeji kwa ajili ya kupigania haki za wakulima na wananchi wote.  

Aidha Rwagasore alijenga urafiki wa kweli na Waswahili walioishi mjini Bujumbura  kwenye mtaa wa Buyenzi, alifanya hivyo kwa kuwa alijua kwamba nguvu ya utawala wa kikoloni ilitegemea na mbinu moja, yaani wakoloni walitawala kwa kupitia mgawanyiko, ndio maana alitafuta fursa nzuri kwa kupata mahusiano mazuri na watu wa Buyenzi ambao walikuwa wafanyabiashara hodari.   

Kama historia ilivyomwelezea Mwalimu Julius Nyerere, pia Rwagasore alitaka kuunganisha Wabarundi wote na kuendeleza mahusiano na watu wa Ulaya katika hali ya usawa.

Katika maoni yake hakuwa na nafasi ya ubaguzi au ukabila, nchini Burundi hamna makabila lakini yapo makundi manne ya watu: Waganwa, Wahutu, Watutsi na Watwa.

Wakoloni waliyaona kama makabila mbalimbali na walianza kufundisha mtazamo wao huu shuleni  hususani kwenye shule za wamisionari. Lakini kwa Rwagasore, Waburundi wote alichukulia ni kabila moja hamna utofauti yoyote, wanaongea lugha ile ile, na utamaduni pia ni uleule, kwa hiyo alichukia maneno ya ubaguzi wa wakoloni.

Baada ya kuanzisha harakati za ukombozi Rwagasore alipata matatizo mengi na alijaribu kuwasiliana na vyama vingine nje ya Burundi ambavyo vilipinga ukoloni ili aweze kupata msaada kutoka nchi zingine kama Misri. Mwanasiasa huyu hodari alikuwa na kipaji kikubwa na watu wengi wanatambua hilo.

Tunaweza kufupisha mtazamo wake kwenye vipengele viwili:
mosi, alitaka kujenga umoja wa taifa lake na kuwalinda waburundi na hatari kubwa ya ukabila na migawanyiko mbalimbali ambao ilitishia wakati ujao wa watu wake.
Pili, alitambua kwamba kwenye kila lengo la maendeleo ya nchi, kitu muhimu sana ni uchumi.

 Alijitahidi  kwa kutengeneza vyama vya ushirika kwa ajili ya maendeleo ya watu wote. Alifahamu kwamba hamna uhuru wa kweli bila uchumi mzuri. Kwa sababu ya jitihada zake kwa ajili ya Burundi aliuawa  Oktoba 13, 1961. Lakini mpaka leo anaonwa kama mfano mkubwa kwa sababu ya mchango wake katika historia ya Burundi hausahauliki, lakini pia kwa sababu ya akili yake na mbinu yake nzuri ya siasa, kiongozi kama huyu ni kiongozi bora ambaye anastahili kukumbukwa.

Antonio Onorati ni mwanafunzi raia wa Italia anayesoma Shahada ya Umahiri ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwanafunzi huyo amekuwa akiandika makala mbalimbali katika kujifunza zaidi lugha ya Kiswahili.

Author: Gadi Solomon