Mzee Mbwana ‘kamusi inayotembea’ aliyebaki na historia ya Lamu

NA KALUME KAZUNGU

Ufupisho: WELEDI wake na ufahamu wa ndani na nje kuihusu historia ya Lamu, jamii ya Wabajuni na maendeleo yao umewashinda hata maprofesa wenye hadhi ya juu nchini na duniani kote.

Upekee huu umemfanya Mzee Mohamed Mbwana Shee kutafutwa na wengi, aghalabu hata wale wasomi wa kimataifa, ilmradi awafichulie bayana historia ya Lamu na jamii ya Waswahili Wabajuni.

Ni kutokana na ukwasi huo wa historia kuihusu jamii yake na eneo lake la Lamu ambapo wengi, wakiwemo wenyeji, wageni na watalii wanamuona Mzee Mohamed Mbwana Shee kuwa sawasawa na ‘Kamusi Inayotembea’.

Ikumbukwe kuwa kamusi ni kitabu cha maneno yaliyopangwa kwa utaratibu wa alfabeti au mwingine na kutolewa maana na maelezo mengine.

Kwa mzee Mbwana aidha, wengi waliozungumza naye bila shaka wamemkubali kuwa  ni ‘Kamusi ya Lamu’ kwani maelezo yake kuihusu Lamu na jamii yake kwa ujumla ameyapanga vyema kama kamusi yenyewe.

Mzee Mbwana ni mzawa wa Kijiji cha Mvundeni, kata ya Mkokoni, Tarafa ya Kiunga, Lamu Mashariki.

Alizaliwa mwaka 1955, akiwa kifungua mimba katika familia ya watoto wanne wa mzee Mbwana Shee Rufai ambaye ni mkazi kindakindaki wa Mtaa wa Uwani, kijijini Mvundeni, tarafa iyo hiyo ya Kiunga, Lamu Mashariki.

Mbwana kwa sasa akiwa ana umri wa miaka 68, anasema yeye hakukanyaga darasani kusomea elimu ya kidunia.

Anasema alipofikisha umri wa miaka mitatu, wazazi wake walianza kumsomesha elimu ya dini kwa wingi, akihudhuria madrassa yaliyokuwa yakiongozwa na viongozi mashuhuri wa dini ya Kiislamu wa Lamu, akiwemo Sheikh Abdullahi Nassir.

Anasema katu hangeweza kuhudhuria masomo ya kidunia kwani wazazi wake walishikilia kuwa hayakuendana na mafunzo ya dini na yalipotosha.

Suala la eneo lao la Mvundeni na Kiunga kutokana na hali ya usalama lilichangia mzee Mbwana kukosa elimu ya ulimwengu au ya msingi kwani alijipata akiwa mkimbizi wa ndani kwa ndani (IDP) na jamii yake wakati akiwa miaka 9 pekee.

 Ni wakati akisomea madrasa akiwa na umri mdogo, ambapo walimu wake waligundua kipaji cha Mbwana cha kushika kile anachofundishwa vyema.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Mzee Mbwana anaeleza kwamba kunasa sauti na kuzirekodi akilini kama tepu ni kipaji alichokirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Anasema historia nyingi alizoelezewa na mababu na wazazi wake katika enzi za udogo wake ndizo ambazo hadi wa leo anazikumbuka kama vile alielezewa jana.

Anasema kilichosababisha yeye kuwa na utajiri mwingi wa historia kuihusu Lamu na jamii ya Wabajuni ni jinsi alivyopendelea kutumia muda wake mwingi, akikaa mabarazani na wazee na kupewa hadithi za jadi.

Anasema tofauti na vijana wengi wa zamani na wa sasa kupendelea kujiunga kwenye makundi ya watu wa umri sawa, yeye alikuwa muda wake mwingi akiutumia kusikiliza na kufuata wosia wa wazee na kuhudhuria vikao vyao vingi kiasi cha kumfanya kuwa katibu wa baraza la wazee wa kijiji chao kwa wakati huo licha ya umri wake mdogo.

“Nashukuru wazee wangu kwa kunilea na kunikuza katika mazingira ya kidini. Mimi sijakanyaga darasani eti kusomea elimu ya msingi au yoyote ile ya ulimwengu. Cha kutia moyo ni kwamba ufahamu wa historia nilionao kuihusu Lamu na jamii ya Wabajuni ni nadra kuupata kwenye mabuku. Nilifuata wosia ya wazee wetu wa zamani na kubahatika kuwa wa pekee katika kunasa na kukumbuka historia hizo hadi leo,” akasema Bw Mbwana.

Mbali na kuwa mjuzi wa historia, Mzee Mbwana pia anatambuliwa kwa kuwa mwanaharakati mkongwe zaidi anayepigania haki za jamii ya Wabajuni, hasa kuhusiana na ardhi na umiliki wake.

Yeye ni Mwenyekiti wa Muungano wa Shungwaya Welfare Association, ambao umekita mizizi katika kutetea maslahi ya jamii ya Wabajuni Lamu.

Muungano huo unaonekana au kuzingatiwa kuwa ‘Mama wa Wabajuni.’

Mbwana anasema kilichomchochea kuendeleza harakati za kuitetea jamii ya Wabajuni ni Mbunge wa kwanza wa Lamu kwenye Bunge la Afrika Mashariki-LEGCO la mwaka 1958, Bw Juma Bhalo, ambaye mbali na uongozi, yeye pia alikuwa mpiganiaji wa haki za jamii, hasa Wabajuni.

“Nilikuwa nikifuatilia kwa karibu harakati za Mbunge Juma Bhalo. Yeye uanaharakati wake haukuwa wa kibinafsi bali wa kuitetea jamii na Kenya kwa jumla. Nikaungana naye na wengineo nchini katika kupigania mabadiliko nchini, hasa wakati wa enzi ya Rais mstaafu, hayati, Daniel Toroitich Arap Moi. Hadi sasa mimi ni mwanaharakati, mambo yangu hasa yakihusu masuala ya ardhi kwa jamii ya Wabajuni ambao ndio wenye uhalisia wa Lamu,” akasema Mbwana.

Kinachomtia wasiwasi ni jinsi wazee wengi wa umri wake Lamu walivyokosa kutilia maanani historia za Lamu na jamii ya eneo hilo kwa jumla.

Ni kutokana na hilo ambapo Mbwana anahisi huenda vizazi vijavyo vikakosa kujua au kutambua chimbuko lao kwani hakuna wa kuwapokeza utajiri huo wa ufahamu ili kuwezesha pia kupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Anaisihi jamii ya Lamu kukumbatia wosia wake na kuutilia maanani ili historia ya eneo na jamii ya Lamu isiangamie.

“Ni masikitiko yangu kwamba wazee wenzangu ambao ni  rika hawafahamu lolote kuhusu historia ya Lamu na jamii ya hapa. Utapata wale tuliopowa mikoba hiyo na wazee wetu waliidharau na kuifuta kabisa akilini. Ndiyo sababu wengi wananijia mimi pekee kunitaka niwasaidia kuitambua Lamu na chimbuko lake. Hii ina maana kuwa ikiwa nitaondoka duniani leo, basi historia kuihusu Lamu itapotea. Ni vyema vijana wajitokeze kuipenda na kuishika historia ya Lamu ili kuweza kuipitisha kutoka kizazi hadi kizazi,” akasema Mbwana.

Mmoja wa wasomi wa Lamu, Abdallah Bakari anasisitiza haja ya jamii ya Lamu kumuenzi mzee Mbwana kwa kuhakikisha historia yake haipotei bure bali inanakiliwa kupitia maandishi na kuhifadhiwa kwa kizazi kijacho.

“Huyu mzee ni kweli kabisa kwamba ni kamusi inayotembea. Yeye atakueleza chochote kile ukitakacho kuihusu Lamu na jamii yetu ya Kibajuni bila kutapatapa. Atakufahamisha mpaka tarehe akina nani wakakifanya enzi hizo. Tusimdharau mwanahistoria na mwanaharakati wetu Mbwana. Ni kiungo muhimu kwa historia na maendeleo ya Lamu,” akasema Bw Bakari.

Kwa sasa juhudizinaendelea kuunda kitabu rasmi kumhusu mzee Mbwana na historia ya Lamu ambacho kinafadhiliwa na Msomi na Mhadhiri mmoja wa chuo kutoka nchini Sweden.

“Ni matumaini yangu kwamba hicho kitabu cha historia ya Wabajuni Lamu kitatumiwa vyema na jamii yangu kuielimisha jamii na watoto wetu kuhusu masuala yetu ya kijamii,” akasema Mbwana.

Mwandishi wa Makala ni wa Gazeti la Taifa Leo.

Author: Gadi Solomon