Nahau za Kiswahili na maana zake

Amani Njoka, Swahili Hub

Tunaendelea na kazi yetu ya kukuelemisha na kukuhabarisha kuhusu lugha ya Kiswahili. Hapa chini ni baadhi ya nahau ambazo tunazitumia sana katika mazungumzo ya kila siku na wakati mwingine tunafahamu maana zake au hatufahamu.

 1. Achia ngazi: jiuzulu nafasi uliyokuwepo, kata tamaa, acha kazi.
 2. Kata maini: umiza kwa maneno, tia hofu, mwambie mtu habari ya kusikitisha au kuhuzunisha.
 3. Ingia mkenge: potea njia, nenda mahali ambapo hukuwa takiwa kwenda. Danganyika kwa uongo au ulaghai wa mtu.
 4. Kula bata: Fanya starehe, furahia jambo kwa kuburudika.
 5. Toka kimasomaso: shinda kwa ajili ya wengi, fanya lililokuwa linasubiriwa. Furahisha.
 6. Vunja moyo: katisha tamaa kwa maneno, mwambie mtu maneno ya kukosesha motisha
 7. Ng’ata sikio: nong’oneza, mwambie mtu siri.
 8. Ona kijicho: kuwa na wivu dhidi ya mtu mtu au kitu.
 9. Pita kushoto: achana na mambo yasiyokuhusu, ondoka mahali fulani usipotakiwa kuwepo.
 10. Uso mkavu: sio na haya, mtu asiye na aibu wala uoga
 11. Lima barua: fukuza kazi kwa maandishi, taka mtu atoe maelezo kwa kuandika
 12. Kula bakora: adhibiwa kwa kuchapwa
 13. Bwaga manyanga: kubali kushindwa, kata tamaa, shindwa kuendelea kufanya jambo fulani.
 14. Liwa kichwa: ondolewa kwenye kinyang’anyiro, futwa kwenye orodha ya wagombea
 15. Funga kazi: maliza kufanya jambo, kamilisha jukumu fulani ulilokuwa umalifanya, kamilisha upelelezi.
 16. Funga virago: beba mizigo na uondoke mahali.
 17. Mlango wa nyuma: toa rushwa, hongo. tumia njia isiyo sahihi kupata jambo/ kitu mathali kazi.
 18. Pata shavu:pewa nafasi, upendeleo au fursa na mtu.

REJELEO

Sallah, H. D. (2017). Nahau za Kikwetu. Dar es Salaam: APE Network.

Author: Gadi Solomon