Mapenzi yamenishika, kichwa na kiwiliwili,
Moyo unanizunguka, nikuwazapo rijali,
Ninaandika haraka, nikiwaza mara mbili,
Usiku hivi silali, mpenzi nakukumbuka.
Saa zimekwenda hasa, mwenzako eti sijali,
Simu ninaipapasa, niliyoiweka mbali,
Laiti ungenigusa, mapigo katika mwili,
Ungejawa na maswali, moyo unavyotikisa.
Ai mapenzi hasara, ama ni kitu cha ghali,
Mfano nina harara, mwenzako silali kweli,
Yananipa ufukara, nisile hata ugali,
Nilipo hapa mahali, sio mbali nitagura.
Basi ulale unono, uote tupo wawili,
Tumeshikana mikono, twendavyo Kila mahali,
Ja wayo na kisigino, ya watu hatuyajali,
Lala, ulale rijali, hapa ndipo maagano.
Mtunzi Filieda Sanga
Mama B
Mabibo Dsm
0753738704
Maoni Mapya