Neno ‘baadhi’ lisitumiwe kurejelea kitu kimoja miongoni mwa vingi

NINADHANI vyombo vya habari vilikuwa vikiarifu jinsi baadhi ya maofisa wa kaunti nchini Kenya walivyotumia mgawo wa fedha za kaunti kwa safari za ughaibuni.

Mwanahabari fulani alisema hivi: Kakamega (sikumbuki iwapo ndiyo kaunti aliyoirejelea) ni baadhi ya kaunti iliyotumia takriban….

Tazama jinsi neno ‘baadhi’ lilivyotumika na kitenzi katika hali ya umoja. Hata kama kitenzi hicho kingekuwa katika hali ya wingi, sentensi isingekuwa sahihi kisarufi. Kabla ya kuifafanua hoja hii, ni muhimu kufafanua maana ya dhana ‘baadhi’.

Dhana yenyewe hurejelea sehemu ya vitu au watu. Halipaswi kutumiwa kurejelea kitu kimoja ambacho kinadhaniwa kuwakilisha vitu vingi katika orodha.

Hivyo ndivyo kosa hilo linavyodhihirika katika sentensi tuliyoitaja katika utangulizi wa makala. Neno baadhi hutumiwa wakati mzungumzaji anataja mifano michache kati ya mifano mingi katika orodha.

Kwa mfano: Kakamega, Bungoma na Machakos ni baadhi ya kaunti zilizotumia takriban…. Ni kosa pia kudhani kuwa kufuatisha ‘Kakamega’ na kitenzi katika hali ya wingi kutasaidia katika kulitatua kosa tulilolitaja.

Yaani, Kakamega isichukuliwe kuwakilisha kaunti nyingine ambazo hazijitokezi katika mazungumzo. Kwa hivyo, mzungumzaji hapaswi kusema:*Kakamega ni baadhi ya kaunti zilizotumia takriban…. Ifahamike kwamba si lazima vitu vinavyofafanuliwa kwa kutumia neno ‘baadhi’ vije mwanzoni.

Inawezekana neno hilo kutangulizwa kisha kufuatiwa na mifano rejelewa. Tazama sentensi ifuatayo: Baadhi ya kaunti zilizotumia takriban….ni Kakamega, Bungoma na Machakos. Ni kosa kuikamilisha sentensi tuliyoitaja hapa kwa ‘miongoni mwa nyingine’ kwa kuwa dhana hii ya pili tayari imekumbatiwa katika ‘baadhi’.

Makala na NA ENOCK NYARIKI wa Taifa Leo.

Author: Gadi Solomon