Nikiacha mke


Heri niweke bayana, kabula ya siku yake,
Kwa haya nayo yaona, hawa tuitao wake,
Nao siwezi patana, hata sanda mnivike,
Siku nikiacha mke siwezi kuoa tena.

Nasema sioi tena, muyashikao mshike,
Tabu ninazo ziona, kwa hawa waleo wake,
Ngozi wanavyo zichuna, haya wapi nimshike,
Siku nikiacha mke, siwezi kuoa tena.

Michoro imejazana, katika maungo yake,
Nani aliye mtona, nazipi gharama zake,
Nguo zao za kubana, shughuri kuvua kwake,
Siku nikiacha mke, siwezi kuoa tena.

Simoni wa kulingana, Aisha mfano wake,
Mke wakukwita bwana, rabeka umuitike,
Hakuna tena hakuna, sitaki nihangaike,
Siku nikiacha mke, siwezi kuoa tena.

Wakujitia mapana, mtaani asifike,
Hawachoki kusutana, na vibwebwe wajivike,
Hatuwezi kuwezana, Mkanya nifahamike,
Siku nikiacha mke, siwezi kuoa tena.

Kwenye kigoma mchana, nyonga aisukesuke,
Kila mtu anaona, na wengine wa mshike,
Na minywele ya kushona, kabeba kichwani mwake,
Siku nikiacha mke, siwezi kuoa tena.

Sioni wa kufanana, bi khadija nyendo zake,
Na hata mkikosana, msamaha autake,
Bure atakutukana, wewe si wahadhi yake,
Siku nikiacha mke, siwezi kuoa tena.

Na huyu tumeshibana, ngawa ana visa vyake,
Wengine navyo waona, bora huyu nimshike,
Talaka tukipeana, yabidi nipumzike,
Siku nikiacha mke, siwezi kuoa tena.

Natamatisha mungwana, penye kiza tumulike,
Maneno yangu supana, palokaza pafunguke,
Wafundeni wenu wana, kunga za ndoa washike,
Siku nikiacha mke, siwezi kuoa tena.

        MKANYAJI
    HAMIS AS KISAMVU
   kissamvujr@gmail.com
  0715311590/0734574747
  

Author: Gadi Solomon