Nyonda Zako

Naona ukiwa mbali, ndivyo nyonda hunizidi,

Aula kiwa wawili, hunipoza zisizidi,

Ninapokukosa kweli, la kutenda silitendi,

Nyonda zako kama keki, hazisubiri harusi.

Ninapokuwa mahali, nikiwaza hasa sudi,

Unanijia ahali, nikaiona akidi,

Vimeganda vivuli, vyetu vimetabaradi,

Nyonda zako kama keki, hazisubiri harusi.

Kama mahaba ni mali, katu sikosi nakidi,

Kuzikosa zako hali, kwa sekunde na vipindi,

Naliona la muhali, kuwa pamwe ni ahadi,

Nyonda zako kama keki, hazisubiri harusi.

Ramadhani Abdallah

Author: Gadi Solomon