PANYA ROAD- 1

Na Sosteness Isengwa

   UTANGULIZI

Bakari Mfaume (Beka) ni kijana mwenye umri wa miaka kumi na tisa aliyekuwa miongoni mwa vijana kadhaa waliokamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha kati (Central Police) jijini Dar es salaam, akihusishwa na mtandao maarufu wa uhalifu uliotikisa jiji hilo kwa muda mrefu uliofahamika kwa jina la Panya Road.

Mtandao huo uliohusisha vijana wengi wenye umri mdogo, ulishamiri kwa kasi na kushiriki matukio mengi ya unyang’anyi ambapo wafuasi wake walivamia kwa staili ya makundi makubwa mithili ya mbwa mwitu mawindoni wakipora mali na kujeruhi watu.

Vijana hao nunda walioshindikana na familia zao na jamii kwa ujumla hawakuwa watu wazuri hata kidogo, walikuwa ni wakora waliobobea kwenye matumizi  ya bangi na madawa ya kulevya na ikitokea ukaingia kwenye kumi na nane zao na kutoka salama baada ya kuporwa kila ulichonacho basi shukuru Mungu kwani walitumia kila aina ya silaha za jadi kama mapanga, marungu na visu katika kutekeleza uhalifu wao.

Hawakuwa na kanuni wala simile, wakikutia mkononi hata kama utawapa walichotaka bado watakujeruhi na kama ni mwanamke basi huweza hata kumbaka na kumwacha wakiwa wamemuharibu vibaya.

Amani ndani ya jiji ilipotea kwa muda mara baada ya kuibuka kwa genge hilo la uhalifu lililojumuisha vijana wadogo wa mtaani. Wakazi walishindwa kutembea nyakati za usiku kwa hofu ya kuvamiwa na vijana hao.

Giza lilipoingia na usiku kuwa mkubwa kila mmoja alijifungia nyumbani kwake kwa kuhofia kukumbana na Panya Road lakini hata huko majumbani nako hakukuwa salama sana kwani wakati mwingine walivamia na kuvunja makazi ya watu na kupora mali zao.

Jeshi la polisi lilijitahidi kadri ya uwezo wake kupambana na kundi hilo kwa muda mrefu na siku hiyo baada ya tukio kubwa na la aina yake lililosababisha umwagaji mkubwa wa damu, hatimaye walifanikiwa kuwakamata baadhi ya vinara wa kundi hilo na miongoni mwao alikuwa ni kijana Beka.

Kilichoibua maswali mengi na hali ya sintofahamu ni namna tukio la mwisho lililopelekea kukamatwa kwao lilivyokuwa, halikuwa tukio la kawaida kuweza kufanywa na vibaka wadogo kama hao, lilikuwa ni zaidi ya tukio la ujambazi lililohusisha matumizi ya silaha za moto na halikutokea katika mitaa iliyozoeleka kwa matukio yaliyofanywa na Panya road bali lilitokea maeneo waliyoishi watu wa kipato cha juu katika viunga vya jiji la Dar es salaam.Vijana hao walivamia nyumba ya mkurugenzi wa mashtaka(DPP) wakiwa na mtutu wa bunduki na kufanya mauaji yaliyozua taharuki mji mzima.

   SURA YA KWANZA

CHUMBA NAMBA NANE

Ilipata saa saba za mchana katika kituo cha polisi cha kati jijini Dar es salaam, magari matatu ya polisi (defender) yaliingia kwa kasi katika eneo la wazi la kituo hicho kikuu yakiwa yamesheheni askari warefu na wenye miili mikakamavu, waliovalia sare za kijani na kofia nyekundu kichwani huku wakiwa wamekamatia mitutu ya bunduki na kujifunga mabomu ya machozi viunoni mwao. Kwa jinsi magari hayo yalivyoingia kwa mikiki huku yakiliza ving’ora vyake kwa fujo ni dhahili iliashiria kuwepo kwa hali ya hatari.

Kabla hata hayajaegeshwa vizuri baadhi ya askari hao waliruka na kwenda kulizingira gari mojawapo na bunduki mikononi wakiwa wamejiweka tayari kwa lolote litakalotokea.

Mara akaonekana akishushwa mtu mmoja kutoka kwenye gari hilo akiwa amefungwa mnyororo uliounganisha pingu zilizofunga mikono na miguu yake.

Kwa jinsi alivyolindwa usingetia shaka kuwa mtu huyo alikuwa ni mhalifu hatari sana lakini cha kushangaza kwa mwonekano wake alionekana kuwa ni kijana mdogo sana kiumri licha ya umbo kubwa alilokuwa nao.

Alivalia suruali ya dengirizi nyeusi na juu alivaa kizibao kilichochanika vibaya, halikadhalika mwilini alikuwa na vidonda na alama nyingi za kama mtu aliyechapwa sana kwa fimbo au mjeredi, uso wake uliashiria kuchoka sana kiasi kwamba hata simama yake ilikuwa ya shida.

Baada ya kushushwa garini wale askari waliendelea kumzonga,  wakisimama kushoto na kulia, wengine mbele na wengine nyuma na kwa pamoja wakaanza kupiga hatua za haraka kuelekea ndani ya kituo na punde baada ya kuingia, mlango wa kituo ulifungwa na huduma zikasitishwa kwa muda.

Akiwa ndani alipelekwa moja kwa moja mpaka chumba namba nane, chumba kilichokuwa chini ya jengo la kituo hicho (underground) kilichotumika maalum kwa ajili ya kuwafanyia mahojiano watuhumiwa nguli wa matukio makubwa ya uhalifu nchini kama ya ugaidi, uhaini, ujambazi, unyang’anyi wa kutumia silaha na mauaji yanayoigusa jamii kwa namna moja ama nyingine.

Kiuhalisia chumba hicho kilikuwa na kiza totoro hali iliyolazimu kuwepo kwa taa kubwa zilizowashwa muda wote na kutoa mwanga mkali uliosaidia kulifukuza giza hilo, upande mmoja wa ukuta kulikuwa na kioo maalum kilichowezesha mtu aliyeko nje ya chumba kuona kinachoendelea ndani ilhali aliyeko ndani hakuweza kuona kinachoendelea nje na kwa wakati huo kulikuwa na jopo la wadau wenye nyadhfa kubwa ndani ya jeshi la polisi na wengine kutoka wizara ya mambo ya ndani wakiwa nje ya chumba hicho ili kufuatilia kitakachoendelea muda mchache ujao.

Zaidi ya hapo hakukuwa na kitu kingine ndani ya chumba hicho ukiacha meza moja pana na viti viwili vilivyowekwa kwa kutazamana.

Alipofikishwa alikalishwa kwenye kiti kimojawapo kisha askari waliomleta walitoka na kumwacha peke yake.

Alikaa mwenyewe kwa takribani dakika tano nzima akiangaza huku na kule asielewe kilichoendelea, ukimya mzito ulitawala kiasi cha kuanza kumtia hofu, mapigo ya moyo yalianza kumwenda kasi na kijasho chembamba kumtiririka, alitamani kupaza sauti yake ili kuhoji nini kitafuata lakini aliogopa na kuamua kubaki kimya kusubiria hatima yake.

Punde si punde mlango ulifunguliwa na kuingia mwanamke mmoja wa makamo aliyevalia sare nadhifu za polisi zenye nyota mbili na ngao mbili mabegani na kuashiria kwamba alikuwa na cheo kikubwa ndani ya jeshi la hilo.

Yule mtu aliyefungwa pingu alibaki akimtazama mwanamke huyo kwa kumtathmini kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa na kimo cha wastani, si mrefu na wala si mfupi, mweusi kiasi na alikuwa na mwili mkakamavu wa mazoezi uliomfanya aonekane tofauti na wanawake wengine.

Aliingia akiwa amekamekamatia jalada mkononi na kwenda kuketi kwenye kile kiti kingine kisha akaliweka jalada hilo mezani, juu ya jalada kulikuwa na maandishi makubwa yaliyosomeka ‘confidential’.

Pi akavua  kofia yake na kuiweka mezani na kuruhusu nywele zake zenye mvi chache alizosuka mtindo wa twende kilioni zionekane bayana.

Miongoni mwa askari wenzake alifahamika kwa jina la utani la ‘The mind reader’ ingawa jina lake halisi akianzia na cheo chake aliitwa SACP Dr Anastasia Buberwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa jeshi la polisi mwenye shahada ya uzamivu ya Saikolojia aliyoipatia nchi Ujerumani.

SACP Anastasia alikuwa askari polisi aliyefanya kazi na ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) kwa kuwafanyia mahojiano watuhumiwa  mbalimbali waliokamatwa wakihusishwa na matukio makubwa ya uhalifu na alikuwa mbobezi kwenye kitengo hicho akiwa na uzoefu wa miaka zaidi ya kumi na tano akiwasaili wahalifu waliotikisa nchi kabla ya kufikishwa mahakamani ambapo wengi wao waliishia gerezani baada ya kupatikana na hatia. Alikuwa na mbinu nyingi za kuhoji na alikuwa na uwezo mkubwa wa kusoma akili ya mtu na kuupata ukweli pale alipouhitaji.

“Bila shaka wewe ndio Bakari Mfaume aka Beka boy aka Snake boy, kijana maarufu kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa sasa?” SACP Anastasia alianzisha mazungumzo akiwa anafungua lile jalada na kulipitia juu juu.

“Naam ni mimi ila kuhusu hilo la umaarufu sina hakika kwakuwa nimetokea mahabusu hivyo sijui kinachoendelea huko uraiani”

Kijana aliyefungwa pingu alijibu huku naye akitupia macho ya kuibia kwenye lile jalada japo hakuweza kuona vizuri kilichoandikwa kutokana na upande alioketi na hata angefanikiwa kuona asingeambulia kitu kwa kuwa liliandikwa kwa lugha ya kingereza.

“Una miaka mingapi?” SACP Anastasia aliuliza sasa akifunika jalada hilo na kumtazama kijana huyo kwa umakini mkubwa.

“Kumi na tisa” kijana alijibu.

“Imewezekanaje kijana mdogo kama wewe kutekeleza mauaji ya watu sita akiwemo mkurugenzi wa mashtaka? Tena kwa silaha ya moto!” alihoji kwa mshangao.

“Siyo kweli mama….sijaua watu sita mimi…hii kesi nimepakaziwa….itakuwa kuna mtu aliyeua na kuamua kunisingizia”

Kijana alipaza sauti na kujitetea akionyesha dalili ya kuanza kuhamanika.

“Kwahiyo kama hujaua watu sita umeua wangapi? mmoja….wawili?”

“Sijaua hata mmoja….hata huyo mkurugenzi sijui wa nini…..sijamuua mimi….kweli kuna mtu alinihaidi milioni kumi kwa ajili ya uhai wake ingawa si mimi niyeshika silaha na kufyatua risasi” Kijana alijibu kwa mchecheto.

“Ni nani aliyekutuma kumuua mkurugenzi wa mashtaka?” Anastasia aliuliza.

“Mtu mmoja hivi anajiita Mshirika”

“Mshirika ndio jina lake halisi?”

“Hapana jina lake halisi silijui maana alijitambulisha kwangu kwa jina hilo…..ni yule ambaye polisi walikuja kunikamata nyumbani kwake  mara ya mwisho” kijana alijitahidi kutoa ufafanuzi.

“Sasa ilikuwaje hadi ukamuua na huyo Mshirika ambaye kumbe ndiye aliyekutuma kwenda kumuua mkurugenzi wa mashtaka na kukuhaidi donge nono la milioni kumi?”

“Hapana mama sijamuua mimi kwanini hutaki kuniamini…..”

“Tafadhali usiniite mama….mimi siyo mama yako….ukiniita afande inatosha!”

SACP Anastasia alimkatisha na kumwambia kwa upole ingawa alionekana kukereka na kitendo cha kijana huyo kumwita mama mara kadha wa kadha.

“Sawa afande….niwie radhi” Kijana alibadili kauli yake na kuomba msamaha.

“Unasema huyo unayemwita Mshirika ndio aliyekutuma kumuua mkurugenzi wa mashtaka, sasa iweje muda mchache kabla ya tukio alipiga simu polisi kuomba msaada akidai kuwa kuna mtu amevamia nyumbani kwake na kumuua dereva na mlinzi wake, na  baada ya polisi kufika nyumbani kwake kweli walikuta wote wakiwa wameuawa  kwa kupigwa risasi huku nawe ukiwepo eneo la tukio pamoja na silaha iliyotumika kutekeleza mauaji hayo, silaha ambayo uliiba siku uliyomuua mkurugenzi wa mashtaka?”

SACP Anastasia alizidi kumbana maswali akidadavua kwa undani zaidi kuhusiana na mazingira halisi ya tukio hilo.

“Ni kweli ile bastola niliiba lakini siyo mimi niliyemuua Mshirika na wapambe wake…..mimi ni kibaka wa mtaani tu….wala sina jeuri ya kushika bunduki na kupanga mauaji kama haya!”

Kijana alikazana kushikilia msimamo wake huku machozi yakimrengarenga.

“Unasemaje si wewe uliyeua wakati silaha iliyotumika kufanya mauaji ilikutwa na alama  za vidole vyako na kama haitoshi risasi zilizokutwa kwenye miili ya marehemu ndio risasi zilizotoka kwenye silaha hiyo!”

“Kweli afande nakuapia si mimi niliyemuua Mshirika na wala siyo mimi niliyepanga mauaji ya huyo mkurugenzi”

“Hukupanga mauaji ya mkurugenzi lakini ulimuua?”

“Hapana sikumuua”

“Ila ulishiriki mauaji yake?”

“Ndio nilishiriki ila siyo mimi niyempiga risasi”

“Ila uliishika bastola iliyotumika kumuua?”

“Ndi….ndio”

“Na baada ya mauaji yake uliiba bastola hiyo?”

“Ndio”

“Na ni kweli ulikutwa na polisi nyumbani kwa Mshirika ukiwa na bastola uliyoiiba huku yeye, dereva wake na mlinzi wakiwa wameuawa kwa bastola hiyo?”

“Ndio ila sijawaua mimi afande….Hakyamungu! siyo mimi….. tafadhali naomba uniamini…..kwanza hata sijui nilifikaje mule ndani!”

SACP Anastasia alinyamaza kimya akitafakari kwa muda maelezo machache aliyopewa, kwa uzoefu alionao alitambua kuwa ni kweli kijana huyo asingekuwa na jeuri ya kutekeleza mauaji yote hayo bila ya kuwepo mtu nyuma yake. Japo hilo halikumwepusha na hatia.

Alishusha pumzi ndefu na kutazama chini huku akitikisa kichwa kwa masikitiko kabla ya kunyanyua tena uso wake na kumtazama kijana huyo kwa dakika nzima bila ya kuzungumza  lolote.

“Kijana unatakiwa unieleze kinagaubaga kilichotokea….ni kweli kuwa haya matukio hayawezi kufanywa na kibaka kama wewe pasipo uwepo wa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kuratibu uhalifu wa kiwango hiki….this look like an organized crime, sasa kwa faida yako ni bora uniambie kila kitu la sivyo kwa mujibu wa kifungu 197 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 ya mwaka 2002 hukumu ya kifo itakuhusu na nisingependa kuona uhai wa kijana mdogo kama wewe ukikatishwa hivihivi wakati wahusika wakuu wa haya mauaji wakiendelea kupeta mtaani”

Alifungua kinywa chake na kumtahadhalisha huku akijiweka sawa pale kwenye kiti kabla ya kuendelea na mahojiano.

Kijana aliposikia hivyo alishindwa kujizuia na machozi kuanza kumtiririka kwa kujua sasa alielekea kunyongwa hadi kufa kwa kesi ya mauaji kwani kwa ushahidi uliokuwepo dhidi yake hata angekuwa yeye ingemuwia vigumu kuamini maelezo yake.

***************

USIKU WA SHAMBULIO

“Oyaa mwanangu huku ulipotuleta siyo kabisa….pamekaa kishua sana! Hivi una uhakika na huu mchongo kweli? Tusije kufa kifo cha mende maana mjengo kama huu hauwezi kosa mlinzi mwenye chuma!”

Faki maarufu kama Pengo alimuuliza Beka wakiwa wamejibanza kwenye kichaka  kilichokuwa mbele ya jumba moja kubwa na la kifahari lililokuwa maeneo ya kitajiri, mitaa ya Mbweni.

“Tulia kichaa wangu!  Unakuwaje mwoga mtoto wa kiume! nimeambiwa huyu mzee leo anarudi home na mkoba wenye milioni ishirini cash……za dili alilopiga mchana ofisini kwake, tukizipata hizo hela tutakuwa tumetoboa kimaisha na ndio itakuwa mwisho wa kukaba watu uswahili na kupora simu na hela za madafu”

Beka alijibu kwa sauti ya chini macho yote yakiwa mbele ya geti jeusi la jumba hilo.

Ilipata saa sita kasoro za usiku, ulikuwa ni usiku tulivu kabisa katika maeneo hayo yaliyopo pembezoni mwa bahari ya Hindi, upepo mwanana kutoka baharini ulipuliza na kutoa ubaridi fulani hivi uliolipoteza kabisa lile joto la Dar es salaam lenye kukera.

Wakaazi  karibia wote walishajifungia majumbani mwao katika mitaa hiyo ambayo nyumba zilijengwa kisasa kwa kuachana mbali mbali huku kila moja ikiwa na uzio na geti kama unavyojua tena maeneo ya uzunguni kila mtu na kwake, hakuna kuombana chumvi kama kule kwetu  pangu pakavu tia mchuzi.

Usiku huo wenyeji wa maeneo hayo walikuwa wamejipumzisha kwenye milki zao bila ya kuwa na habari ya kwamba mitaa yao ilipata ugeni usio rasmi uliokuja kwa nia ovu.

Beka na vijana wenzake takribani tisa wa kundi maarufu lililotikisa jiji kwa muda lililojulikana kama Panya road, walikuwa wamejibanza nje ya nyumba mojawapo wakisubiri kutekeleza uhalifu wao.

Hao walikuwa ni baadhi tu  kwani hawakuweza kufika wote kutokana na mazingira kutoruhusu kwani kundi hilo lilikuwa na vijana zaidi ya mia kutoka vitongoji mbalimbali vya jiji.

Siku hiyo walikuwa mbali na maeneo yao ya kujidai maana walishazoea kukaba na kupora anga za uswahilini kama Mabibo, Tandika, Manzese, Mbagala na kwingineko lakini siku hiyo walikuwa ushuani na hilo liliwatia hofu kidogo kwasababu hawakuwa na uhakika na usalama wao hasa ukizingatia kuwa nyumba nyingi za huko zililindwa na walinzi wenye silaha za moto, mbwa wakali na fensi za umeme.

Beka ndiye aliyewashawishi wenzake kuja hapo baada ya kuwahakikishia kuwa alipewa taarifa ya kwamba usiku huo mmiliki wa nyumba hiyo angerudi kwake na mamilioni ya pesa na wakati huo alikuwa njiani akirejea.

“Tukifanikiwa kuupata huo mzigo lazima tuvimbe sana kitaa….mitungi jumlisha totoz kwa sana!”

Alizungumza kijana mwingine huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa msokoto wa bangi na kiberiti, aliuweka mdomoni na kutaka kuuwasha ili kutoa nishai kidogo, hata hivyo Beka hakutaka kumpa nafasi hiyo, aliuchomoa kutoka mdomoni mwake na kuutupa chini kisha akaukanyaga na kuusiliba kwa guu lake la kushoto.

“Una akili sawa sawa wewe bwege! Unajua kabisa harufu ya mmea ni kali…..ukiwasha hapa itasambaa na kufanya tushtukiwe kwa urahisi….unataka kutukamatisha au? hebu acha ujinga mi sina mpango wa kurudi jela hivi karibuni” alimfokea kwa ukali na kumfanya kijana huyo anywee kwa nidhamu ya woga.

Beka aliheshimika kama kiongozi mmojawapo wa Panya road na heshima hiyo hakuipata kirahisi, ilimgharimu miaka iliyohusisha matukio mengi hatarishi yaliyomfanya alichungulie kaburi huku akiingia na kutoka gerezani mara kadha wa kadha. Mtaani heshima haikuwa ikitolewa bure bali ilitafutwa na ili uipate ilikuwa aidha uwe na hela ama uwe mbabe.

“Poa basi kausha Snake boy ila hakukuwa na haja ya kuiharibu hiyo dawa, nimeinunua kwa pesa ndefu sana….ni yenyewe hiyo….ya Chuga siyo famba!”

Kijana huyo aitwaye Cholo, swahiba mkubwa wa Pengo alijibu kwa upole akimtupia lawama kwa kitendo cha kuukanyaga msokoto wake.

“Vunga mwanangu.….tukipata hela zetu utanunua  shamba zima la bangi uvute mwenyewe hata heka nzima ikibidi”

Pengo naye alidakia na kumpooza Cholo huku akimpiga piga mgongoni na kuwafanya wenzake waangue kicheko cha chinichini.

Wakati stori za hapa na pale zikiendelea, mara kwa mbali wakaona gari aina ya Toyota Prado likija kuelekea usawa wa nyumba iliyokuwa mbele yao, wote wakanyamaza kimya na kubonyea kichakani huku wakijiweka tayari kwa kitakachofuata.

Pengo akaingiza mkono ndani ya koti lake refu jeusi alilovaa na kuchomoa bunduki aina ya SMG na kuikamatia kwa mikono yake miwili, kwa namna alivyokuwa ameishika alionekana bayana kupatwa na kitete kilichoashiria kwamba hakuwa mzoefu wa kutumia silaha za moto, si unajua tena vibaka wa mitaani walishazoea visu na mapanga na silaha zingine ndogo ndogo.

“Kumbuka maelekezo niliyokupa…..usiue mtu asiyehusika! ni mtu mmoja tu anayestahili kufa usiku wa leo naye ni bosi mwenye hela zetu na si mwingine”

Beka alisisitiza baada kumwona Pengo ametoa silaha hiyo.

“Kausha! Najua ninachokifanya”

Pengo alijibu kwa kujiamini kulikotokana na  kujilazimisha.

Punde si punde lile gari liliwasili mbele ya geti la nyumba ile na liliposimama tu, dereva alipiga honi mbili tatu nadhani kwa lengo la kutaka afunguliwe ili aingize gari ndani.

Haikuchukua muda wakashuhudia geti likifunguliwa na mlinzi mmoja aliyekuwa amevalia sare za bluu akiwa amening’iniza bunduki begani.

Alipofungua geti hilo mpaka mwisho ndipo lile gari likaingia uani na wakati anajiandaa kulifunga, ghafla bin vuu Beka na kundi lake walikurupuka kutoka mafichoni na kutimua mbio kuelekea getini.

Mlinzi alijikuta akipigwa na bumbuazi maana hakuelewa kundi hilo la vijana waliokuwa wakimjia kwa kasi ya kuogopesha tena kimya kimya walitokea wapi na walikuwa na nia gani.

Alitunduwaa kwa muda na akili ilipomrudia na kutaka kufunga geti harakaharaka, tayari alikuwa amechelewa kwani vijana hao walishamfikia na ile kutahamaki watatu kati yao walimpamia na kumwangusha chini wakati wengine waliingia uani na kuwahi kutoboa matairi yote manne ya gari kwa kutumia visu vikali walivyokuwa navyo.

Wakiwa pale chini mlinzi alijitahidi kujinasua lakini haikuwa rahisi kwani alishadhibitiwa kisawasawa, licha ya kwamba alikuwa na mwili mkubwa ila vijana hao wadogo walishamzidi nguvu na alipotaka kutumia ubavu aliokuwa nao kuchukua bunduki yake ikawa ndio kosa kubwa alilofanya kwani mmoja wa vijana hao alichomoa kisu ghafla na kumchoma nacho hovyo sehemu mbalimbali  hasa kifuani na shingoni.

Damu nyingi zikiruka mithili ya bomba na mlinzi huyo akaanza kupaparika kwa kihoro, alijaribu kupiga kelele ili kuomba msaada lakini sauti haikutoka na kuishia kukoroma tu kwa maumivu makali aliyoyapata na kuikamatia shingo yake iliyokuwa na majeraha makubwa ya visu.

ITAENDELEA…

0657 241821

Author: Gadi Solomon