PANYA ROAD-2

Na Sosteness Isengwa

0657 241821

Damu nyingi zikiruka mithili ya bomba na mlinzi huyo akaanza kupaparika kwa kihoro, alijaribu kupiga kelele ili kuomba msaada lakini sauti haikutoka na kuishia kukoroma tu kwa maumivu makali aliyoyapata na kuikamatia shingo yake iliyokuwa na majeraha makubwa ya visu.

Kwa hofu ya kuonwa na wapita njia wakamburuta hadi ndani na kufunga geti.

Kitendo hicho kilionekana kumshtua mno Beka, hakutarajia kabisa kama hali hiyo ingejitokeza mapema kiasi hicho, alianza kuona dalili ya mambo kwenda tofauti na mipango yake.

Aliduwaa kwa sekunde kadhaa akimshangaa yule mlinzi alivyokuwa anatapatapa pale chini  kabla ya kutulia tuli na kuashiria kuwa ameshakata roho katikati ya dimbwi kubwa la damu.

Alipogeuka na kutazama lile gari aliona wenzake wengine wameshalizingira huku Pengo akiwa amesimama mbele huku ule mtutu wa bunduki akiwa ameuelekeza kwenye kioo na mkanda wa risasi ukining’inia tayari kwa matumizi.

Alipoona hivyo naye haraka akaenda na kusimama pembeni yake na kupitia  kioo cha mbele cha gari hilo alimwona dereva akiwa ameketi nyuma ya usukani akiwakodolea macho kwa taharuki kubwa, halikadhalika siti ya nyuma alikuwepo mtu mwingine ambaye hapana shaka ndio alikuwa bosi mwenyewe ingawa hakuweza kumwona vizuri kutokana na kiza.

Siyo siri dereva wa gari hilo alishikwa na woga mkubwa mno na Pengo aliligundua hilo hivyo alimpa ishara ya kumtaka asijaribu kuleta ujuaji wowote ule utakaomgharimu huku akiwa bado amemwelekezea mtutu wa bunduki, dereva alionekana kutii hilo kwani alinyanyua mikono yake kama ishara ya kujisalimisha.

Kwa utulivu wa hali ya juu Beka akampa ishara ya kumtaka afungue mlango wa gari, dereva alitaka kufungua kweli lakini yule mtu aliyekaa siti ya nyuma alimshika begani na kumwambia maneno ambayo hawakuweza kuyasikia lakini hapana shaka alimzuia kufanya hivyo.

Kitendo hicho kilionekana kumchukiza mno Pengo, alitoka pale mbele akifuatiwa na Beka na kuelekea mlango wa nyuma wa gari hilo, upande aliokuwa ameketi yule bosi na kuanza kugonga gonga kioo taratibu kwa kutumia vidole vyake kama ishara ya kumtaka afungue lakini  bosi huyo bado aliendelea kukaidi.

Ghadhabu zikazidi kumpanda Pengo na ghafla akanza kupiga kile kioo kwa nguvu kwa kutumia kitako cha bunduki huku matusi ya nguoni yakimtoka.

“Si unajifanya jeuri wewe…..sasa ngoja nikuonyesha kuwa mimi ni jeuri zaidi yako!”

Alibwata kwa jazba huku akizidi kukishambulia kile kioo mfululizo mithili ya mtu aliyepagawa jambo lililosababisha wale wenzake nao wapandwe na mzuka na kuanza kupiga mbinja na kelele wakishangilia kitendo hicho.

Sasa halikuwa tukio la kimya kimya tena kwani hapana shaka kelele zao ziliweza kupaa na hata kuwafikia watu waliokuwa ndani ya nyumba hilo.

“Vunja….mtoe nje….mtoe tumshughulikie….mtoe atupe chetu!”

Ilisikika sauti kutoka miongoni mwao na kupelekea wengine nao wazidi kushangilia na kupayuka hovyo huku lugha chafu zikitawala.

Kufumba na kufumbua kioo kilivunjika na kusambaratika hovyo huku vipande vyake vimwagikia ndani ya gari na vingine nje na sasa Pengo akajikuta akiwa ana kwa ana na mtu aliyekaa siti ya nyuma ya gari hilo, hata hivyo katika hali ya kushangaza sura yake ilibadilika ghafla kutoka kwenye hali ya ghadhabu na kujiamini kwingi na kusawajika na kuwa mpole, macho yakiwa yamemtoka mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango.

Punde baada ya kioo kuvunjika macho yake yalikutana na mdomo wa bastola iliyoelekezwa katikati ya paji la uso wake, wakati huo bunduki aliyoishikilia alikuwa bado ameigeuza upande wa kitako chake na hakuwa na uhakika kama angekuwa na kasi ya kuwahi kuigeuza kabla mtu huyo hajamfyatulia risasi.

“Leo mmeingia choo cha kike chokoraa wakubwa nyinyi! Sasa kwa usalama wako weka hiyo bunduki chini taratibu kabla sijaufumua ubongo wako kwa risasi”

Alibwata akiwa amemkazia macho Pengo aliyekuwa amenyorodoka mithili ya kuku mwenye mdondo. Kimya kilitanda ghafla, wale wenzake waliokuwa wakibwatuka hovyo wote walibaki wametunduwaa wasiwasi ukiwa umewajaa, wakionekana kutotarajia kabisa kama mhanga wao angeweza kujihami kwa bastola na kuonyesha uanaume kiasi hicho.

“Pengo….weka silaha chini….usithubutu kufanya ujinga wowote…”

Beka alimsihi mwenzake kwa sauti iliyotoka kwa kigugumizi kilichotokana na woga mkubwa alioupata hasa ukizingatia alikuwa amesimama nyuma yake kwa umbali mdogo wa kama mita moja na ushee tu, kwahiyo ina maana kama huyo mtu angefyatua risasi basi baada ya Pengo angefuata yeye.

Hata hivyo Pengo alionekana kuwiwa vigumu kutii agizo alilopewa kwani bado aliendelea kuikamatia ile bunduki, ingawa alijitahidi kujikaza kisabuni ili kuonyesha kwamba hakuna alichohofia lakini kijasho chembamba kilichoanza kumtiririka licha ya ubaridi uliokuwepo kilimuumbua na kuashiria hofu iliyotanda ndani yake.

“Usijifanye shujaa bwana mdogo! weka silaha chini….nitakuua….sitanii!”

Mtu huyo alisisitiza huku akiikoki bastola yake aina ya Raging bull 454 tayari kwa matumizi. Bastola hiyo ni miongoni mwa silaha hatari sana duniani zenye uwezo wa kasi hadi kufikia mita 580 kwa sekunde na hutumika zaidi kuwindia wanyama pori ila usiku huo mdomo wake ulikuwa mbele ya kichwa cha kijana chakaramu Pengo.

Hata hivyo bado alikuwa mbishi kusalimu amri, alijua akiweka silaha chini ndio itakuwa mwisho wa mpango wao na kila kitu kingeharibika, hakutaka hilo litokee kwake na kuonekana dhaifu mbele ya wenzake waliokuwa wakimtazama kwa macho ya matumaini.

“Mtaa haujanilea hivyo…..siwezi kukubali kushindwa kirahisi…..aidha uniue au niku….”

Pengo aliongea kwa sauti iliyotoka kwa kujitutumua na kabla ya kumalizia sentensi yake ghafla ulisikika mlio mkubwa sana wa risasi iliyotoka na kupita katikati ya paji la uso wake na kuufumua ubongo wake huku damu nyingi zikiruka hadi kumfikia Beka aliyekuwa amesimama nyuma yake.

Lilikuwa ni tendo la kushtukiza na kuogopesha mno, Beka alimshudia Pengo akianguka chini mbele ya macho yake kukata roho papo hapo bila hata ya kuomba walau kikombe cha maji. Alibaki amezubaa akimtazama pale chini alipoangukia akiwa na tundu la risasi iliyopita kwenye paji la uso wake na kutokea kisogoni huku damu iliyochanganyika na ubongo ikitapakaa hovyo kiasi cha kumfanya ajihisi kizunguzungu na kichefuchefu na kutamani kutapika. 

Yule mtu alipoona Pengo amekuwa jeuri aliamua kumpiga risasi moja tu iliyouondoa uhai wake, sauti ya mlio wa risasi kutoka kwenye bastola yake ulikuwa mkubwa mno na bila shaka uliweza kusafiri umbali hata kilomita kadhaa kutoka eneo hilo.

Mara baada ya risasi kufyatuliwa, sauti za wanawake wakilia kwa kihoro zilisikika kutoka ndani ya nyumba hiyo, bila shaka sauti hizo zilitoka kwa wanafamilia walioishi humo waliokumbwa na hofu kuu pindi waliposikia mlio wa risasi kutokea kwenye ua wa nyumba yao.

Baada ya kufyatua risasi yule mtu alishuka haraka kutoka ndani ya gari na kuivutia kwake bunduki ya Pengo iliyokuwa imeanguka chini kando ya mwili wake, aliivuta kwa kutumia mguu wake wa kuume na kuikanyaga huku bastola yake akiwa ameielekeza kwa Beka ambaye sasa ndio alikuwa amesimama mbele yake.

Alikuwa ni mtu wa makamo mwenye umri wa miaka hamsini ya mwanzoni, mrefu, mweusi na mnene wa wastani, alikuwa amenyoa upara huku kidevuni akiwa amechonga ndevu zake mtindo wa O na alivaa miwani ya macho, kwa ujumla alionekana kuwa mtu makini mwenye heshima zake.

“Mmefanya kosa kubwa sana kuvamia nyumbani kwangu…..kuhatarisha usalama wa familia yangu….leo mtakiona cha mtema kuni wanahizaya nyinyi!”

Aliongea kwa hasira akiwa amemkazia macho Beka aliyekuwa ametahayari isivyo kawaida akiwa ameganda mithili ya sanamu la Bismaki, mwili wote ulimfa ganzi na si yeye tu hata wale wenzake nao walibaki wameshikwa na bumbuazi wasijue la kufanya.

“Mika hebu shuka upesi uokote hii bunduki tuwaweke wote chini ya ulinzi….hakuna atakayeondoka hapa mpaka polisi watakapofika!”

Alizungumza kwa kujiamini na kumpa maagizo dereva wake aliyekuwa bado amejikunyata ndani ya gari woga ukiwa umemtawala akionekana kuzidiwa ujasiri na bosi wake ambaye hadi wakati huo hakuwa hata na chembe ya hofu licha ya kuua mtu muda mchache uliopita.

“Mika hebu shuka kwenye gari ebo! Acha ulelemama…..nikikufata huko nitakutandika makofi!” 

Alifoka kwa sauti baada ya kuona dereva anakawia kushuka huku akigeuza shingo kumwangalia na hilo ndio lilikuwa kosa kubwa kwake kwani alipogeuka tu ghafla alichomoka kijana mmoja ambaye haikujulikana wapi alipotokea na kumjia kwa kasi akiwa amenyanyua juu mkono wake uliokuwa umeshikilia kipande cha nondo. Aliposikia vishindo vya hatua za mtu akimjia akageuka tena haraka kuangalia vishindo vilipotokea huku mkono wenye bastola akiuelekeza huko lakini kwa bahati mbaya alikuwa ameshachelewa kwani kijana huyo alishamfikia na kwa nguvu zake zote aliupiga kwa nondo mkono wake ulioshikilia bastola mpaka ukalia KAAAH!

“Yalaaaah….mko….no…..wanguuuu!”

Alipiga yowe kwa sauti kubwa kutokana na maumivu makali aliyoyapata na kujikuta akiachia bastola bila kupenda na kuufumbata mkono wake uliokuwa ukining’inia baada ya kuvunjika vibaya, japo alikuwa mtu mzima aliyekula chumvi kiasi lakini kwa uchungu aliousikia alilia mithili ya mtoto mdogo.

Aliyempiga na nondo alikuwa ni Cholo, swahiba wa Pengo…..marehemu, aliyehaidiwa shamba la bangi iwapo misheni hiyo isingeenda kombo. Punde tu ile bastola ilipogusa ardhini aliwahi kuiokota kisha akarudi nyuma hatua kadhaa akiwa amemwelekezea mtu huyo na bila hata ya kujishauri alianza kufyatua risasi, kwa kuwa hakuwa mzoefu wa kutumia silaha za moto alifyatua hovyo hovyo jambo lililosababisha wenzake wainame chini kwa hofu ya kuuawa.

Alipiga risasi takribani nne mfululizo kisha akaibwaga bastola chini huku akitetemeka mwili mzima mawenge yakiwa yamemjaa.

Ukimya wa kuogofya ulitawala tena kila mmoja akihofia nafsi yake ila ukimya huo haukudumu sana baada ya kukatishwa na sauti za watu kutokea ndani ya nyumba hiyo wakipiga mayowe na kulia kwa uchungu ijapokuwa hakuna aliyediriki kutoka nje.

Beka alinyanyua kichwa chake taratibu na alipopeleka macho kuangalia alipokuwa yule mtu alimwona amelala chini akiwa anavuja damu nyingi sehemu za kifuani na tumboni na kwa namna alivyokuwa ametulia ni dhahili alishafariki dunia.

Damu ilitapakaa kila mahali na harufu yake ilitawala ndani ya jumba hilo la kifahari, maiti tatu zililala chini katikati ya madimbwi ya damu, roho ya umauti ilishika hatamu usiku huo tulivu, ilikuwa ni mithili ya jahanamu ndogo iliyoshuka duniani kwa muda.

Ni kweli Beka alishashiriki matukio mengi ya uharifu, alishaiba, alishapora, alishakaba, alishapiga na kujeruhi lakini hakuwahi kuua. Japo aliwahi kushuhudia mauaji yakifanyika mbele yake mara kadha wa kadha lakini si kama idadi ya siku hiyo.

Wakiwa bado katika hali ya kuhamanika, kwa mbali mlio wa king’ora cha gari la polisi ulisikika na hapo ndipo kila mmoja akakurupuka na kutafuta pa kutokea ili  asiangukie mikononi mwa vyombo vya dola. Hakuna aliyekuwa na wazo la zile milioni ishirini tena maana walijua shughuli imeshaharibika.

Wakati wenzake wakipigana vikumbo wanguwangu kuelekea nje, Beka yeye akaona hapana! Haiwezekani kushiriki umwagaji damu wa kiasi hicho harafu aondoke mikono mitupu pasi na kutimiza lengo lililowaleta hapo, upesi akakimbilia kwenye lile gari na kuingia ndani yake kupitia mlango wa nyuma uliokuwa wazi na kuanza kuangaza angaza, alimwona yule dereva akiwa bado ameketi vilevile kwenye kiti chake akiwa anatetemeka huku akiangua kilio cha chinichini, kwa jinsi alivyokuwa ameshikwa na hofu nina hakika haja zote alikuwa amezimalizia pale.

Hakuwa na muda wa kujihusisha naye, alipotupa macho huku na kule aliona mkoba mweusi ukiwa pembeni yake, aliunyakua haraka kisha akafungua zipu na kuchungulia kilichomo na alipojiridhisha akaufunga na kushuka nao ndani ya gari, aliposhuka tu jicho lake lilitua kwenye ile bastola ya yule mtu ambaye kwa sasa ni marehemu ikiwa imeanguka chini, bila kujiuliza mara mbili aliiokota na kuisweka kibindoni kisha naye akatoka mbio kuelekea nje. Wakati huo mlio wa kile king’ora ulizidi kusogea jambo lililoashiria kuwa polisi walikaribia kufika eneo la tukio.

Alipofika nje alikuta wenzake wameshatawanyika na hakujua wamekimbilia wapi hivyo naye akashika njia kuelekea barabara kuu ya Bagamoyo ili akatafute usafiri utakaomtoa mitaa hiyo haraka iwezekanavyo na kwa bahati mbaya upande alioelekea ndiko ving’ora viliposikika vikitokea na hilo lilimwogopesha sana lakini ilikuwa lazima apite huko kusudi aweze kufika stendi.

Alikimbia kwa mwendo wa wastani wenye tahadhali kubwa huku akigeuka nyuma kila wakati ili kuhakikisha hakuna mtu anayemfuata, akiwa njiani alivua shati lake lililokuwa limetapakaa damu na kulitumia kupangusa uso wake ambao nao ulirukiwa na damu ya mshkaji wake Pengo wakati alipochabangwa risasi, alipomaliza akalifinyanga na kulirusha kando kwenye kichaka kilichokuwa pembeni na kuendelea kukimbia akibakiwa na fulana nyekundu aliyokuwa ameivaa kwa ndani. Mpaka wakati huo hakupishana na mtu yoyote yule njiani, hapana shaka kila mtu alijifungia ndani kwa hofu baada ya milio ya risasi kurindima.

Kiza kinene kilitanda ingawa mwanga wa mbalamwezi na taa za nyumba zilizokuwa kando ya barabara ya vumbi aliyokuwa akipita zilimsaidia kuona alipoelekea.

Baada ya kukimbia umbali wa kama mita mia mbili hivi kwa mbali aliona mwanga wa taa ya king’ora cha gari kutokea mbele yake hivyo akasimama na kuangaza macho akitafuta pa kujificha, haraka alitoka njiani na kwenda kujibanza upenuni mwa ukuta wa nyumba moja iliyokuwa pembezoni. Punde si punde magari mawili ya polisi (defender) yaliyosheheni askari polisi wenye mitutu ya bunduki yalimpita kwa kasi kubwa yakiwa yamewasha mwanga mkali wa taa huku yakitimua vumbi kubwa nyuma yake.

Defender hizo zilipompita alitoka alipojificha na kuanza kutembea kwa hatua za haraka haraka kwasababu alihofia endapo angeendelea kukimbia huenda angeshtukiwa kwa urahisi. Siyo siri mapigo ya moyo yalimwenda mrama na alipatwa na kimuhemuhe cha hali ya juu baada ya kushuhudia kundi hilo la askari likielekea eneo la tukio. Wakati wote huo ule mkoba mweusi alikuwa ameuning’iniza begani na alikuwa makini nao kweli kweli.

Haikumchukua muda mrefu aliwasili barabarani, maeneo ya kituo cha daladala na kukuta watu wachache wakisubiri usafiri wa kuelekea mjini na kwa bahati yake ile anafika tu kituoni hapo, daladala aina ya Coaster iliyotokea Bagamoyo ilisimama kituoni na abiria wote waliokuwa hapo akiwemo yeye walipanda.

Daladala ilipoondoka ndio kidogo akajisikia  ahueni ijapokuwa alikaa kimagutumagutu akiwa hana imani kabisa na usalama wake, alijitahidi mno kujiweka katika hali ya kawaida maana kila aliyemtazama alihisi kama vile alijua alichotoka kufanya mda mchache uliopita.

Daladala iliendelea kuchapa mwendo na kwa kuwa ilikuwa usiku sana ilisimama kwa nadra vituoni kupakia abiria mmoja mmoja kwani asilimia kubwa ya wakazi wa Dar es salaam nyakati hizo walikuwa wameshapumzika.

Walipofika maeneo ya Tegeta walisimama na baadhi ya abiria walishuka huku wengine wakipanda kabla ya safari kuendelea. Muda mchache tu walipotoka maeneo hayo utingo alianza kukusanya nauli kwa abiria mmoja baada ya mwingine akianzia mbele kabisa, Beka alikuwa amekaa siti ya katikati.

Alipokaribia alipokuwa amekaa, aliingiza mkono kwenye mfuko wa suruali yake na kutoa noti ya shilingi elfu mbili tayari kwa kumkabidhi utingo huyo lakini cha kustaajabisha alipomfikia alimruka na kuendelea kukusanya nauli kwa abiria aliyefuata.

Kitendo hicho kilimshangaza kidogo na kudhani pengine alipitiwa hivyo ikabidi amshtue kwa kumgusa na kumnyooshea mkono uliokuwa umekamatia ile noti lakini hata hivyo utingo hakuipokea na badala yake alimwambia kauli iliyozidi kumduwaza.

“Tayari ushalipiwa na mwenzio pale mbele”

“Mwenzangu! Mwenzangu yupi tena?”

Beka alihoji huku akiangaza huku na kule ndani ya daladala kuona kama kuna mtu aliyemfahamu lakini hakuwepo hata mmoja.

“Aisee maswali mengi ya nini! Umelipiwa na yule pale aliyekaa karibia na mlango amevaa kofia nyeusi….au unataka kulipa mara mbili?” Utingo alimjibu akiwa anaendelea kukusanya nauli kwa abiria wengine waliosalia.

Ile hofu iliyokuwa imepungua  ikarejea upya na mara hii kwa kiwango cha hali ya juu kwasababu hakujua mtu huyo aliyemlipia nauli ni nani na alimfahamu vipi! Alijaribu kumtazama kwa makini lakini hakuweza kumwona vizuri kwasababu alikuwa amempa mgongo. Akabaki amejawa na maswali mengi kichwani yaliyokosa majibu na kwakuwa daladala ilikuwa katikati ya mwendo ikabidi atulie ingawa mapigo ya moyo yalimuenda mbio kama vile alitoka kushiriki marathon na hali alikuwa ameketi.

Akiwa katika hali ya sintofahamu mara yule abiria aliyekuwa amekaa pembeni yake alimpa taarifa utingo kuwa anashuka kituo kinachofuta kisha akaamka na kusogea mlangoni na baada ya muda mfupi daladala ilisimama kituoni na abiria huyo akashuka na safari ikaendelea.

Author: Gadi Solomon