Profesa Senkoro kutoa mada mhadhara kumuenzi Ken Waribora

Wapenzi wa Kiswahili nchini Kenya wanajipanga kuandaa mhadhara wa kwanza wa umma kumuenzi marehemu Prof Ken Walibora, aliyefariki Aprili 2020 katika ajali ya barabarani jijini Nairobi.

Prof Walibora alikuwa msomi, mwanahabari na mwandishi wa vitabu aliyesifika nchini Kenya na duniani kote kutokana na mchango wake mkubwa katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili.

Mhadhara huo umeratibiwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Kibabii Aprili 10, 2024, kulingana na taarifa iliyotolewa na Kituo cha Taaluma za Lugha na Utamaduni cha chuo hicho (KITALU).

Mhadhara huo umepangiwa kufanyika kati ya saa nne asubuhi hadi saa saba mchana.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumanne, Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kibabii Prof Odeo Isaac Ipara, alisema kuwa tayari kuna kamati inayoendeleza mipango ya maandalizi ya mhadhara huo.

“Ndipo tumeanza mipango ya maandalizi ya mhadhara huo. Tutatoa maelezo kamili kuhusu hali ya matayarisho kuanzia wiki ijayo,” akasema Prof Ipara.

Mtoa mada mkuu atakuwa ni Profesa F.E.M Senkoro, aliye Profesa Mstaafu wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wadau mbalimbali wa Kiswahili nchini wamekuwa wakizishinikiza taasisi tofauti kuweka mikakati ya kumkumbuka Prof Walibora, kutokana mchango mkubwa aliotoa katika kuipa utambuzi Kenya duniani kupitia uandishi wa kipekee wa vitabu.

IMEANDALIWA NA WANDERI KAMAU WA TAIFA LEO

Author: Gadi Solomon