Raia wa kigeni wapambana kujifunza Kiswahili Tanzania

Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Kutokana na mwamko kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali kutaka kujifunza lugha ya Kiswahili, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) linaendelea na kozi za Kiswahili cha mawasiliano kwa wageni zinazofundishwa kwa muda mfupi.
Mwalimu wa Kiswahili kwa wageni, Wema Msigwa amesema kuwa watu mbalimbali wamekuwa wakifika katika ofisi za baraza hilo kwa ajili ya hitaji la kujifunza lugha ya Kiswahili.

Amesema kazi ya kufundisha wageni inahitaji umahiri wa kutumia stadi na mbinu mbalimbali za kufundishia wageni.

“Si kila mwalimu wa Kiswahili anaweza kufundisha Kiswahili kwa wageni,” amesitiza Msingwa.
Msigwa amewakaribisha wataalamu wa lugha wanaopenda kufundisha wageni kufika BAKITA ili kupatiwa mafunzo ya kuimarisha stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza tarehe 20/11/2023.

Mmoja wa wanafunzi ambaye ni raia wa Denmark anayesoma kozi za Kiswahili Bakita, Avemaria amesema amejifunza Kiswahili kwa muda wa miezi mitatu na sasa anaweza kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika vizuri kwa lugha ya Kiswahili.

Author: Gadi Solomon