Rais Magufuli afariki dunia

Na Mwandishi Wetu

Ni huzuni kwa Watanzania. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amefariki dunia.

Akitangaza taarifa ya msiba huo, Makamu wa Rais Mama Samia Hassan Suluhu alisema Rais Magufuli amefariki kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam.

Alisema alilazwa Machi 06, 2021 katika Hospitali ya Jakaya Kikwete na kuruhusiwa Machi 7 na kuendelea na majukumu yake.

“Machi 14 alijisikia vibaya na akarudi Hospitali ya Mzena ambapo aliendelea na matibabu hadi umauti unamkuta, nchi yetu itakuwa na maombolezo ya siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti,” Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametoa pole kwa Serikali ya Tanzania na familia ya marehemu na Watanzania wote kwa kuondokewa na Rais Dk John Magufuli, huku akisema serikali yake itakuwa bega kwa bega katika wakati huu mgumu.

Rais Uhuru Kenyatta amesema Rais Magufuli alikuwa kiongozi wa Afrika mwenye maono.

“Nimempoteza rafiki, mwenzangu na mshirika wa karibu,” alisema Rais Uhuru Kenyatta.

Kufuatia msiba huo Kenya imetangaza siku 7 za maombolezo kitaifa.

Rais Magufuli atakumbukwa na Watanzania wote kwa jinsi alivyokipigania Kiswahili Afrika na duniani kwa ujumla ili kiheshimike kama lugha zingine kubwa.

Author: Gadi Solomon