Rais Magufuli ampongeza Jaji kwa kutumia Kiswahili

Amani Njoka, Swahili Hub

Dodoma: Rais John Magufuli amesisitiza matumizi wa lugha ya Kiswahili katika uandishi wa nyaraka mbalimbali katika uga wa mahakama na sheria huku akisisitiza kwamba kwa kufanya hivyo kutaonesha uzalendo halisi.

Ameyasema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Sheria ambapo Mahakama ya Tanzania inatimiza miaka 100 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1921.

Katika maadhimisho hayo Rais Magufuli alifurahishwa na hatua ya Jaji Zephania Gareba wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kuandika moja ya hukumu alizowahi kuzitoa kwa lugha ya Kiswahili.

“Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Jaji Gareba wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Musoma kwa kutumia Kiswahili katika kutoa hukumu kwenye kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi….”

Rais Magufuli amesisitiza kuwa matumizi ya Kiswahili katika mahakama si dhambi na kwamba tunapaswa kuonesha kwamba tumekuwa huru na tunamuenzi Baba wa Taifa ambaye ndiye mwanzilishi wa lugha ya Kiswahili na kuyaunganisha makabila zaidi ya 120.

Kwa sababu ya uzalendo aliuonesha Jaji Gareba aliamua kuandika hukumu kwa Kiswahili bila woga dhidi ya miiko ya kimahakama na kwamba amekuwa shujaa wa Kiswahili. Tayari Rais amemteua Jaji Gareba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa uzalendo aliuonesha.

Author: Gadi Solomon