Rais Magufuli atunukiwa nishani kwa kuendeleza Kiswahili

Amani Njoka, Swahili Hub

Dodoma. Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Baraza la Kiswahili la Zanzibar limemteua Rais John Magufuli kuwa mtunukiwa wa Nishani ya Juu ya Shaaban Robert.

Hayo yamesema na Mwenyekiti wa Badi ya Bakita, Dk Samweli Method alipokuwa akitoa hotuba katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili jijini Dodoma.

Katika kilele cha maadhimisho hayo yaliyoanza Januari, 19, 2020 na kumalizika leo tarehe 20 Januari, iliazimiwa kuwa Rais Magufuli atunikiwe nishani ya heshima kutokana na mchango mkubwa wa serikali yake na katika kukiendeleza Kiswahili kwa kufanya marekebisho ya sheria ya Kiswahili yaliyoliweza Baraza la Kiswahili la Taifa Bakita kufanya kazi kwa ufanisi.

“Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza), Idara za Kiswahili za Vyuo mbalimbali vilivyoshiriki leo, vyama vya Kiswahili pamoja na mashirikisho yamemteua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli awe mtunukiwa wa nishani ya juu kabisa ya Shaaban Robert katika maadhimisho haya”. Alisema

Dk Method alisema, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli iliwezesha upatikanaji wa kanuni za uendeshaji wa Bakita mwaka 2019. Matumizi ya Kiswahili pamoja na msisitizo wake kwa serikali katika kukipa kipaumbele Kiswahili ni miongoni mwa mengi ambayo Rais ameyafanya kuhusu Kiswahili.

“Sifa nyingine iliyofanya wadau waone ipo haja ya kumpa Rais tuzo hiyo ni pamoja na mchango aliutoa mwezi Mei, 2019 ambapo alifanya ziara katika nchi mbalimbali za kusini mwa Afrika zikiwamo Zimbabwe na Namibia. Katika nchi hizo Rais alikinadi Kiswahili na kuwaahidi wakuu wa nchi hizo kutoa waalimu wa kufundisha Kiswahili katika nchi zao ambapomjuhudi hizo zimezaa matunda,” aliongeza

“Vilevile ilani ya CCM ya mwaka 2020/25 ambayo Rais Magufuli anasimamia utekelezaji wake, imetoa msisitizo katika maendeleo ya Kiswahili hasa katika ibara ya mbalimbali. Uchambuzi uliofanyika kwa kuangalia ilani za vyama vingine, ilionekana ilani hii ndiyo iliyoweka msisitizo wa juu kabisa katika maendeleo ya Kiswahili na miongoni mwa masuala yaliyotajwa ni pamoja na kuendeleza diplomasia ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.”

Mbali na masuala yalioelezwa katika ilani ya CCM, juhudi za Rais Magufuli zimefungua milango na fursa kwa waalimu wa Kiswahili katika nchi alizozitembelea. Pia, tajiriba yake katika utumizi wa Kiswahili majukwaani huku akiibua msamiati mpya mathalani ‘tumbua majipu’ ambao una maana ya kumuondoa kiongozi katika wadhifa kutokana na kutoridhika na utendaji wake. Kutokana na hilo, msemo huo umepata maana nyingine tofauti na ile iliyozoeleka.

Sambamba na Rais Magufuli, taasisi na mashirika mbalimbali yalitunukiwa tuzo kama ishara ya kutambua mchango wao katika kukidumisha Kiswahili. Miongoni mwa taasisi na mashirika hayo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dawasa, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) Mwananchi Communications kupitia gazeti la Mwananchi, TCRA kwa uchache.

Tuzo nyingine ya mtunzi bora wa vitabu ilienda kwa mwandishi nguli wa vitabu vya Isimu ya Kiswahili vyuo vikuu, David Massamba kwa mchango wake wa upatikanaji wa vitabu vya Kiswahili kwa wanafunzi wa vyuo.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilipata tuzo kwa mchango wake mkubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili kwa kufanya tafiti, uandishi wa machapisho, ufundishaji na utahini wa wataalamu wa Kiswahili kwa muda mrefu.

Pia kulitolewa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vyema katika mitihani yao kwa upande wa somo la Kiswahili. Wanafunzi walifanya vizuri katika mtihani ya kidato cha Pili mwaka 2019 Tanzania Bara ni Timoth Mujuni (Marian Boys, Pwani) na Raiyan Diwani Mohammed kutoka Zanzibar.

Kidato cha Nne mwaka 2019 kutoka Tanzania Bara ni Peter A. Muhindi (Shule ya Sekondari Lulenge, Kagera) na kidato cha Sita ni Ignas Ludonya (Shule ya Sekondari Kasulu, Kigoma).

Author: Gadi Solomon