Rais Samia apongeza Bunge la Kenya kutumia lugha ya Kiswahili

Gadi Solomon, Mwananchi

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelipongeza Bunge la Kenya kwa kuazimia kutumia Kiswahili ndani ya Bunge.

Rais Samia ameyasema hayo Jumatano Mei 5, 2021 wakati akilihutubia Bunge la Kenya kwenye ziara ya kikazi siku mbili nchini humo.

“Tulifurahishwa zaidi na uamuzi wenu wa kuanza kutumia lugha ya Kiswahili ndani ya Bunge. Na ndicho kinachonifanya mimi nisikilize Bunge la Kenya. Nainjoy kile Kiswahili kile. Kiswahili chenu kinavionjo vingi kuna vionjo vyake ambavyo peke yake ni burudani tosha kusikiliza,” alisema Rais Samia.

Amesema anapenda kusikiliza Bunge la Kenya kwa sababu yanayojadiliwa mle pia nasi Watanzania yatuhusu.

“Mimi binafsi huwa napenda kusikiliza Bunge la Kenya, tunafanya hivyo kwa kuwa yanayojadiliwa humu nasi yanatuhusu. Niseme tu kuwa Bunge la Seneti la Kenya na Bunge la Taifa la Kenya linatusisimua kwa mengi,” alisema Rais Samia

Aliongeza; “Nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Naibu Spika anavyoshindwa kutaja namba za miaka kwa Kiswahili. Lakini inafurahisha mlishatunga kanuni za Bunge za Kiswahili na mkamualika Mheshimiwa Job Ndugai (Spika wa Bunge la Tanzania) kuja kuzindua kanuni zile tar 31.9.2019. Hii inatia moyo kuwa tupo pamoja na kweli mnataka kutumia Kiswahili lakini hatua kwa hatua.”

Author: Gadi Solomon