Rais Samia: Mchakato Kiswahili kuwa lugha rasmi Sadc uharakishwe

na Juma Issihaka, Mwananchi


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaka mchakato wa kukipitisha rasmi Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha nne za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uharakishwe.
Kiswahili kilipendekezwa kuwa miongoni mwa lugha za SADC Agosti 14, 2019 katika mkutano wa Baraza la mawaziri la Jumuiya hiyo, chini ya Mwenyekiti Profesa Palamagamba Kabudi.
Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano huo wa mwaka 2019, Profesa Kabudi, ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema Kiswahili kuwa lugha ya nne ya SADC ni moja ya mapendekezo yaliyofanywa na baraza hilo.
Hata hivyo, katika mkutano wakuu wa nchi chini ya mwenyekiti wa wakati huo wa SADC, Dk John Magufuli, Kiswahili kilipitishwa kuwa lugha ya nne ya jumuiya hiyo.
Jana Alhamisi, Rais Samia alishiriki mkutano wa 42 wa wakuu wa nchi za SADC uliofanyika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kusisitiza mchakati wa Kiswahili kuwa lugha ya nne ya jumuiya hiyi uharakishwe.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, Rais Samia alizitaka nchi wanachama kuzingatia uwiano wa jinsia katika ngazi za maamuzi, akibainisha kuwa Tanzania imejitahidi katika hilo. ” Nafasi hizo za uongozi serikalini na bungeni nchini Tanzania ni pamoja na Waziri wa Ulinzi (Dk Stergomena Tax), Mambo ya nje (Liberatha Mulamula), Uwekezaji (Dk Ashatu Kijaji),
Utalii ( Dk Pindi Chana) na nafasi ya Spika wa Bunge (Dk Tulia Ackson),” alisema
Katika hatua nyingine, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa usalama wa chakula kwa nchi wanachama , huku akiyataka mataifa hayo kuwekeza kwenye uchumi wa buluu.
Jana Alhamisi Rais Samia alifanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini humo na kuzungumza na mwenyeji wake, Rais Felix Tshisekedi.

Author: Gadi Solomon