Rais Samia atangaza vivutio Tanzania kupitia filamu ya ‘Royal Tour’

Dar es Salaam. Baada ya kusubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua filamu ya ‘Royal Tour’ yenye lengo la kutangaza duniani vivutio vya utalii na uwekezaji vinavyopatikana hapa nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan alianza kurekodi filamu hiyo Agosti 29, 2021 kwa lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii.

Wakati akirekodi filamu hiyo pamoja na mwongozaji maarufu wa filamu, Peter Greenberg, Rais Samia alitembelea na kuonyesha kwa wageni vivutio mbalimbali vya utalii, uwekezaji, sanaa na utamaduni vilivyopo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas ameandika katika ukurasa wake wa Facebook akieleza kwamba filamu hiyo itaonyeshwa kwa nyakati mbalimbali mwaka mzima kuanzia Aprili 18 mwaka huu.

“Baadhi ya TV za Marekani zitakazoonesha filamu ya ‘Royal Tour’ kwa nyakati mbalimbali kwa mwaka mzima kuanzia Aprili 18, 2022, zilianza kutangaza ratiba zao.

“Hapa kituo cha Channel 11 (WTTW) cha mjini Chicago Illinois, moja ya vituo vikubwa katika mfumo wa utangazaji kwa umma (pbs) kilifungua mlango live Aprili 18. Kituo hiki kinaangaliwa na zaidi ya watu milioni 3.5. Orodha nyingine inakuja,” ameandika Dk Abbas.

Katika mkutano wake na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, Rais Samia alimweleza kuwa, Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji na utalii na kwamba amekwenda kuzindua filamu hiyo Marekani akiamini itaufikia ulimwengu.

“Nikiwa hapa Marekani, nitazindua kipindi cha ‘Royal Tour’, kipindi hiki kinalenga kuonyesha fursa za utalii na uwekezaji zinazopatikana Tanzania.

“Kuchaguliwa kwa Marekani kuwa sehemu ya kuzindulia, hakukuja kwa ajali, tulifanya hivyo tukitambua hapa ni mahali ambako wapenzi wa burudani na starehe wanapatikana, hiyo inafanya kuwa jukwaa sahihi la kuonyesha kipindi hiki duniani kote,” alisema Rais Samia.

Author: Gadi Solomon