Rais Samia atunukiwa shahada ya Uzamivu

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametunukiwa udaktari wa heshima (PhD) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mkuu huyo wa nchi ametunukiwa udaktari huo Jumatano Novemba 30, 2022 na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jakaya Kikwete katika mahafali ya 52 ya chuo hicho yaliyofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Kwa mamlaka niliyokabidhiwa, ninakutunuku digree ya heshima ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hongera sana” amesema Kikwete akimtunuku Rais Samia udaktari huo wa heshima.

Baada ya kutunukiwa udaktari huo, Rais Samia ameshukuru huku akibainisha kuwa alijaribu kuitafuta shahada hiyo lakini muda haukumpa nafasi.

“Suala la kupewa tuzo hii nimelipokea kwa unyenyekevu mkubwa. Lakini nilijiuliza maswali kadhaa sababu huko nyuma nilijaribu kuitafuta shahada hii lakini muda haukunipa nafasi,” amesema Rais Samia

Januari 27, 2022 wakati wa mahojiano maalumu yaliyorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) yaliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia alibainisha alijaribu kufanya Shahada ya Uzamivu lakini kutokana na majukumu mengi ameshindwa huku akisema ataimalizia baadaye.

Mkuu huyo wa nchi ambaye siku hiyo alikuwa anaadhimisha kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa, alieleza mambo mbalimbali tangu alipozaliwa mpaka kuwa Rais huku katika safari yake ya elimu akisema ameishia kwenye shahada ya uzamili (masters) akibainisha kuwa alikuwa na matarajio ya kufanya PhD lakini majukumu yamezidi.“Nilijaribu kufanya PhD lakini ukweli ni kwamba pilika ni nyingi nimeshindwa, sijui niseme nimeshindwa au nitaimalizia baadaye, sijui. Labda nitaimalizia baadaye” alisema Rais Samia.

Pia katika mahafali hayo mtayarishaji wa kipindi cha Lulu za Kiswahili kinachoruka katika Shirika la habari Tanzania (Tbc), Victor Eliya ametunukiwa shahada ya uzamivu (PhD).

Author: Gadi Solomon