Serikali kuchapisha miswada ya washindi Tuzo ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Nyerere

Mwandishi Wetu, Swahili Hub

Dar es Salaam. Serikali itagharamia uchapishaji wa miswaada ya washindi wa kwanza Tuzo ya Taifa ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Nyerere na kuvisambaza vitabu hivyo kwenye shule na maktaba zote nchi nzima.

Hayo yameelezwa wakati wa utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu msimu wa pili hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa The Super Mome, Masaki Aprili 13, 2024.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda, alielezea sababu ya tuzo hizo kupewa jina la Mwalimu Nyerere, akisema hatua hiyo imefanyika kumuheshimisha kiongozi huyo aliyejulikana kwa kupenda kwake kusoma na kuandika.

“Mwalimu Nyerere alikuwa na mahaba na vitabu. Alivisoma na alivichambua na zaidi, alivitafsiri na aliviandika,” amesema Profesa Mkenda na kuongeza

“Tunajua pia alitafsiri pia kitabu cha mwanafalsa wa Kigiriki, Plato, ambacho tunatumaini tutakiona, tutazungumza na familia yake.”

Tanzania huadhimisha Aprili 13 siku ya kuzaliwa Mwalimu Julius Nyerere na kumuenzi kwa kutoa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.

Akizungumza katika halfa hiyo, mgeni rasmi Profesa Abdulrazak Gurnah alisema uandishi bunifu una umuhimu kwa taifa na dunia kwa ujumla kwani hutumika kuhifadhi historia, uchumi, siasa na utamaduni wa watu wenyewe ambayo yote husaidia kujenga jamii thabiti kimtazamo na kitabia.

Amesema maandiko hayo huelimisha kuburudisha na kuliwaza kulingana na nyakati tofauti ambazo jamii inapitia.

 Gurnah pia moja ya kazi zake bunifu ni Riwaya ya Paraise ambayo imetafsiriwa kwa Kiswahili na Ida Hajivayanis na kuitwa Peponi.

Katika tukio hilo burudani na matukio mbalimbali yaliweza kunogesha tuzo hizo ambapo mgeni rasmi alikuwa ni mshindi wa Tuzo ya Nobel wa mwaka 2021 kwa upande wa fasihi ambaye ni Profesa Gurnah.

Awali, jumla ya washindi 30 walitangazwa wakati wa halfa hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo maofisa waandamizi wa serikali, mabalozi na wanaotoka katika tasnia ya uandishi nchini.

 Pia kumi wakiwa ni waandishi bunifu kwenye tangu ya riwaya, kumi wakiwa washairi na kumi wakiwa ni waandishi wa hadithi za watoto.

Hafla hiyo ilianza kwa wahudhuriaji wake kutangaziwa washindi kumi mpaka saba kutoka kwa kila tanzu ambao wote walitambuliwa na kupewa vyeti vya ushiriki wao.

Washindi wa nafasi ya tatu kutoka kwa kila tanzu walijishindia vyeti na Sh5 milioni na kwa washindi wa pili walijipatia Sh7 milioni.

Washindi wa kwanza walikuwa ni Laura Kiswaka upande wa Riwaya, Blandina Lucas upande wa hadithi za watoto na Mohamed Juma upande wa Ushairi ambao walizawadiwa vyeti, ngao Sh10 milioni kila mmoja.

Author: Gadi Solomon