Serikali kushirikiana na sekta binafsi kutangaza lugha ya Kiswahili

Elizabeth Edward, Mwananchi

Dar es Salaam.Serikali imejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji mpango wa kuitangaza lugha ya kiswahili na kuifanya kuwa fursa ya kibiashara.

Hayo yameelezwa leo na mlezi wa mradi wa kufundisha na kujifunza lugha ya kiswahili kwa kutumia lugha za asili Profesa Palamagamba Kabudi.

Kabudi aliyepokea kijiti cha ulezi leo kutoka kwa Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi amesema mpango wa serikali ni kuifanya lugha hiyo kuwa fursa ya kibiashara.

Amesema mbali na kuwa lugha ya sayansi na tenkonolojia, kiswahili ni lugha ya diplomasia ya uchumi hivyo ni muhimu kuhakikisha sekta binafsi inashiriki katika kuhakikisha wanaona ni kwa namna gani wataiingiza lugha hiyo kwenye biashara.

“Tunataka tukitumie kiswahili kama fursa ya ajira, wenye kuzalisha bidhaa zinazohusu lugha hii basi wafanye hivyo na shughuli nyingine zinazohusisha biashara ndiyo maana katika hili tunawahitaji sekta binafsi.

Sekta binafsi inayo mchango mkubwa, zipo bidhaa mbalimbali zinazoweza kutengenezwa na viwanda zote hizo zikawekewa lugha ya kiswahili, nafikiria kukutana na Taasisi ya Sekta binafsi tuzungumza nao kuhusu nafasi yao,” amesema.

Akizungumzia mradi huo profesa Kabudi amesema ulianza rasmi Februari 2020 chini ya Mzee Mwinyi na unahusisha vyuo vikuu 20 vya mataifa mbalimbali duniani.

Kwa upande wake Mwinyi amesema ni faraja kwake kumuachia kazi ya ulezi mtu anayemfahamu kuwa amebobea kwenye lugha ya kiswahili.

“Nataka mkiendeleze kiswahili, kile kiswahili fahasa msibanange kiswahili. Naamini wewe ni kijana na una nguvu basi kazi hii utaifanya vyema,” amesema Mwinyi.

Author: Gadi Solomon