Serikali: Ndoto ya Kiswahili kutumika Afrika yatimia

Gadi Solomon na Pelagia Daniel

Dar es Salaam. Dunia inapoelekea Siku ya Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili kesho Julai 7, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na mabaraza ya Kiswahili Bakita na Bakiza vyama vya Kiswahili,wadau wa utamaduni na wadau wa Kiswahili  imeandaa

 imeandaa mdahalo wenye mada kuhusu mchango wa Kiswahili na Ukombozi wa Bara la Afrika leo Alhamisi.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema ndoto za Kiswahili kutumika katika Afrika zimekamilika baada ya lugha hiyo kupewa hadhi ya kimataifa.

Waziri Mchengerwa amesema hayo wakati akizungumza kwenye mdahalo wa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatayofanyika kesho kwenye  Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNIC).

Amesema lugha ya Kiswahili sasa inatumika katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii na afya.

“Kiswahili ni lugha ambayo imechelewa kuanza kutumika ipasavyo kwa sababu ndiyo lugha ya ukombozi iliyotumika kumuondoa mkoloni,” amesema Waziri Mchengerwa.

Amesema kwa kuwa Kiswahili imekuwa lugha ya kidunia, ni vyema kuitumia ipasavyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Waziri huyo amesema kama Kiswahili kiliweza kutukomboa katika mikono ya ukoloni sasa lugha hii ndiyo nyezo muhimu kwa ajili ya kutukomboa kiuchumi.

Awali, waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume walikuwa na ndoto kuwa Kiswahili kiwe lugha ya Afrika jambo ambalo walilianza kwa kuhimiza nchi zingine zitumie Kiswahili.

Waziri mchengerwa ameagiza historia ya nchi kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu walioandika kwa lugha za kigeni yapo mambo mengi waliyapotosha. Pia ameliomba Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) kutumia jitihada nufaishi kukibidhaisha Kiswahili kimataifa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdrahman Kinana amesema lugha ya Kiswahili iliwezesha mapambano ya ukombozi katika kutafuta uhuru kusini mwa Afrika.

Amesema licha ya kuwapo kwa majeshi kwa nchi zilizokuwa zikitafuta ukombozi wao lakini lugha ya Kiswahili ndiyo ilikuwa kichocheo kwa sababu walitumia lugha hiyo ili kuwasiliana.

“Wanajeshi kwa nchi nyingi za Afrika zilizokuwa zikipambania ukombozi walitumia lugha ya Kiswahili kufundisha mikakati na mipango yao,” amesema Kinana.

Amewaomba Watanzania kuchangamkia fursa za Kiswahili ili kukuza uchumi wa nchi. Kinana ametumia nafasi hiyo kumpongeza baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa kinara wa kukipaisha Kiswahili katika kipindi chake chote cha kupigania uhuru na uongozi.

Author: Gadi Solomon