Serikali yaagiza kazi za fasihi kuhakikiwa Bakita, Bakiza


Kongamano hilo lilidumu kwa siku tano lilishirikisha wadau mbalimbali wa kiswahili kutoka ndani na nje ya nchi likiwa na kauli mbiu, Tasnia ya Habari na Fursa za Ubidhaishaji Kiswahili Duniani.

Saddam Sadick, Mwananchi


Mbeya. Watunzi, Waandishi na Wahariri wa vitabu wametakiwa kuwasilisha kazi zao Baraza la Kiswahili nchini (Bakita) au Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza) kabla ya kusambaza bidhaa zao ili kuhakikiwa matumizi sahihi ya lugha.

Akizungumza Machi 22,2024 katika hitimisho la Kongamano la nne la Idhaa za Kiswahili Duniani, Naibu Waziri Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema ili kuhakikisha lugha ya kiswahili inakua na kuenea duniani lazima kada hiyo iwasilishe kazi zao katika mabaraza hao kuhakikiwa.

Amesema kutokana na ushindani unaoonekana katika lugha hiyo ambayo imeanza kutumika Afrika, inahitajika juhudi binafsi ili kuibidhaisha bidhaa hiyo kiuchumi.

“Hatuwezi kubidhaisha Kiswahili kwa lugha mbovu, hivyo watunzi, waandishi na wahariri wa vitabu wapeleke kazi zao Bakita au Bakiza ili kuhakikiwa kujua matumizi ya lugha sanifu” amesema Mwinjuma.

Naibu huyo amewataka waandishi wa habari kushiriki kikamilifu kuhamasisha lugha ya kiswahili kupitia kalamu na vyombo vya habari na kutafuta fursa za kiuchumi kupitia bidhaa hiyo.

“Lazima tuipongeze serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kazi aliyoifanya kuitangaza Afrika hadi kutumika kwenye shughuli mbalimbali, hii ni fursa kiuchumi tusiwaachie wengine kunufaika nayo,” amesema Mbunge huyo wa Muheza mkoani Tanga.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema katika kongamano hilo wamepokea mapendekezo kadhaa kwa washiriki na wataenda kuyafanyia kazi, huku akitaja maazimio.

Pia amesema upo mkakati wa kubidhaisha lugha hiyo ulioanza mwaka 2022 hadi 2032 ikiwamo ushiriki wa balozi zote za Tanzania kufungua vituo vya lugha hiyo.

“Mchakato wa ajira kwa waandishi wa habari kwenye vyombo vya habari haswa utangazaji, matangazo kwa lugha ya alama kwa lugha ya kiswahili na vipindi vya watoto kwa lugha ya kiswahili,” amesema na kuongeza.

“Tunashukuru balozi zote tayari zikefungua vituo vya lugha ya kiswahili ikiwamo Sudan. Mauritania, Nigeria, Zimbabwe, Ufaransa, Korea na Aboudhahab,” amesema Consolata.

Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Beatrice Mwampamba amesema kutokana na kiswahili kusambaa duniani inawapa chachu kutumia lugha hiyo kuibidhaisha kiuchumi.

“Tunapokuwa kwenye kazi zetu lazima tuzingatie matumizi ya lugha sahihi na kuondokana na mazoea lakini kutumia kiswahili kwa manufaa haswa kiuchumi, ” amesema Beatrice ambaye ni mtangazaji wa Redio Must ya jijini Mbeya.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Author: Gadi Solomon