Serikali yaanza kutekeleza maagizo saba ya Makamu wa Rais

Gadi Solomon, Mwananchi
gsolomon@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imeagiza kuanza utekelezaji wa kisheria na kikanuni kuhusu maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.

Tamko hilo limetolewa ljumaa ikiwa ni hatua ya kuanza utekelezaji wa maagizo saba yaliyotolewa na Makamu wa Rais ili kuendana na kasi ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili duniani.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa ametoa maagizo hayo huku akizionya taasisi na kampuni ambazo zitapuuza zichukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na kanuni za Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).

Akizungumza kwa niaba ya Waziri huyo, Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolota Mushi, amesema maagizo kama hayo yalianza kutolewa mwaka 1967 na viongozi mbalimbali akiwamo Mzee Mfaume Kawawa.

Amesema maagizo hayo yanayotakiwa kuanza kutekelezwa kuanzia sasa ni nyaraka za idara na idara au taasisi na taasisi kuanza kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili.
“Iwapo taasisi iliyopo inaendeshwa na watu wanaotumia lugha za kigeni, inatakiwa nyaraka zake kuwa pia na tafsiri ya Kiswahili,” amesema Waziri Mchengerwa.

Amesema maeneo mengine ambayo utekelezaji wake unapaswa kuanza mara moja ni pamoja na mabango ya matangazo yote yaliyopo barabarani kuwa katika lugha ya Kiswahili, maelezo ya bidhaa zote zinazozalishwa viwandani, maelezo ya dawa zinazozalishwa viwandani, majina ya baarabara yote yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili na Kiswahili sanifu.

Lengo la kuandika kwa Kiswahili amesema ni kumsaidia mwananchi ili asije akadhurika au kupata athari hasi kutokana na kutoelewa maelezo yaliyotolewa.

Hata hivyo amesema serikali haijazuia maelezo kuandikwa kwa lugha yoyote ya kigeni lakini kila mzalishaji anatakiwa kutambua lugha ya Kiswahili kwanza.

“Baraza la Kiswahili limeshirikishwa na linashirikiana na mamlaka husika kuhikisha Kiswahili sanifu na fasaha kinatumika katika nyaraka za kisheria ambazo zimeanza kutafsiriwa,” amefafanua Waziri Mchengerwa.

Akizungumza kuhusu kutandawaa kwa lugha ya Kiswahili, Katibu Mtendaji, Mushi amesema Kamusi ya Kiingereza ya Oxford katika toleo lake jipya limeingiza maneno 200 ya lugha ya Kiswahili.

Mushi amesema hii ni mara ya pili kwa waandaaji wa kamusi hiyo kuingiza misamiati ya Kiswahili na kuitolea ufafanuzi kwa lugha ya Kiingereza ambapo hapo awali waliweka misamiati mitano pekee.
“Miongoni mwa maneno yaliyoingizwa kwenye kamusi hiyo, ni Chipsi yai, singeli, mamantilie, jembe, daladala, chapo, kolabo,” amesema Mushi.

Author: Gadi Solomon