
Gadi Solomon, Swahili Hub
Dar es Salaam. Serikali imewatadharisha wananchi, taasisi na mashirika yanayohitaji huduma ya tafsiri na ukalimani kuacha kuwatumia watu wa mitaani wasiotambulika na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).
Akizungumza juzi Jumamosi Oktoba 7, 2023 wakati wa mkutano na mawakala wa Bakita, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Dk Resani Mnata amesema kutokana na Kiswahili kuchukua taswira ya kimataifa, amewataka wananchi, taasisi na kampuni mbalimbali kuwatumia wakalimani na watafsiri waliosajiliwa na Bakita.
Amesema watu hao wanaotoa huduma hizo mitaani bila kufuata utaratibu wajue wanavunja sheria na kanuni hivyo wanapaswa kusajiliwa mara moja.
“Huko mtaani kuna watu hawana taaluma na hawatambuliki na baraza wanafanya ukalimani na tasfiri jambo ambalo linaweza kuleta taswira mbaya kwa nchi iwapo watakuwa wamekosea,” amesema Dk Mnata.
Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema jukumu la baraza hilo ni kuhakikisha linasaidia wananchi, mashirika na taasisi mbalimbali wapate huduma ya ukalimani na tafsiri kutoka kwa watu wenye utaalamu.
Amesema Baraza hilo limeweka utaratibu wa kuwapima wakalimani na watafsiri kutoka lugha mbalimbali na kutoa ithibati kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Mushi amesisitiza kwamba kwa kiwango cha kimataifa ambacho Kiswahili kimefikia sasa, ipo haja ya kusimamia kikamilifu eneo hilo.
“Tuwaalike wananchi na mashirika mbalimbali kuwasiliana na baraza iwapo wanahitaji wakalimani na watafsiri kutoka lugha yoyote, tunao mawakala ambao tunafanya nao kazi kwa ukaribu wa lugha mbalimbali, hii itawasaidia wanaohitaji huduma hiyo kuepuka upotoshaji,” amesisitiza Mushi.
Baraza hilo limeanzisha utaratibu wa mafunzo kwa wakalimani ili kuwatahini na kutoa ithibati ya kufanya kazi hiyo kwa utaalamu.
Maoni Mapya