Sheria 450 kuwa kwa Kiswahili Desemba mwaka huu

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza kuzitafsiri sheria kuu 450 zilizotungwa kwa lugha ya Kiingereza ili ziwe kwa lugha ya Kiswahili kuanzia mwishoni mwa mwaka huu.

Mwandishi Mkuu wa Sheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Onorius Njole alisema hayo mwishoni mwa wiki mjini Morogoro katika Mkutano wa  Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo.

Alisema kuanzia sasa sheria zitakazotungwa bungeni zitakuwa kwa lugha ya Kiswahili.

Njole alisema mchakato wa kuzitafsiri sheria zilizopo zilizotungwa kwa Kiingereza unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

Alisema baada ya kukamilika kwa sheria hizo kuu, kazi itakayofuata ni kuzitafsiri sheria ndogo 30,000 zilizotungwa na taasisi, mamlaka za serikali na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

“Pale itakapotakiwa sheria hizo zitumike kwa Kiingereza katika sehemu mbalimbali kwa manufaa ya Taifa, zitatafsiriwa kutoka Kiswahili kwenda katika lugha hiyo ya Kiingereza,” alisema Njole.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Evaristo Longopa alisema katika kuhakikisha nchi inakuwa na mikataba yenye tija na inayowanufaisha wananchi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliweza kuipitia mikataba ya kitaifa na kimataifa 622 na hati za makubaliano 39.

                 (Chanzo Gazeti la HabariLeo  Jumatatu Aprili 12, 2021)

Author: Gadi Solomon