CHAMA cha Kiswahili katika shule ya upili ya St Albert The Great Siakago Boys kinadhamiria kuboresha matumizi ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na kupiga jeki shughuli za Idara ya Kiswahili.
Aidha, kinakusudia kuwapa wanafunzi majukwaa maridhawa ya kusoma magazeti na kukuza vipaji vyao katika sanaa na fani zinazofungamana na Kiswahili kama vile uigizaji, uanahabari, ulumbi, uandishi wa hadithi na utunzi wa mashairi.
Chama hiki ni kiungo muhimu cha Idara ya Kiswahili inayoongozwa kwa sasa na John Macharia Karori ambaye pia ni mlezi wa chama.
Wanachama hukutana kila Jumanne jioni kuzamia mada zinazowatatiza katika Kiswahili na kuratibu midahalo na mijadala mbalimbali kwa uelekezi wa viongozi wao – John Lucky Mdachi (Mwenyekiti), Abdumalik Hussein (Naibu Mwenyekiti), Ben Syanda (Katibu) na Fredrick Ogino (Mhazini).
Kwa mujibu wa Karori, kuwepo kwa chama hiki kumebadilisha mtazamo hasi miongoni mwa wanafunzi kuhusu somo la Kiswahili.
Chama kimepania pia kuhimiza wanafunzi kushiriki makongamano ya lugha huku wanachama wakichochewa kushiriki mashindano mbalimbali ya Kiswahili, hasa Uandishi wa Insha katika gazeti la Taifa Leo.
Chama pia kina mpango wa kuchapisha jarida la shule kwa lengo la kuzua mijadala ya kitaaluma na kuwapa wanafunzi fursa za kujieleza na kunoa vipaji vyao katika utunzi wa kazi bunilizi.
Mbali na kuzamia masuala ya utafiti, wanachama hukusanya habari za matukio mbalimbali shuleni, kuzihariri na kuziwasilisha katika gwaride. Wao pia hushiriki shughuli za kuhifadhi mazingira na utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii.
Maoni Mapya