Siku ya Kiswahili Duniani: ni fursa au changamoto

Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Alhamisi tarehe 07.07. 2022.

Hatimaye baada ya ushawishi na juhudi za dhati kwa zaidi ya miongo saba,  tarehe 07 Julai imekuwa siku adhimu kwa Afrika na dunia kwa ujumla.

Naam! Ni zaidi ya miaka 70! Ikumbukwe kuwa mnamo miaka ya 1950 Umoja wa Mataifa ulianzisha kitengo cha Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa. Hili halikuja bure, kuna sababu kadhaa zilizopelekea hilo ambazo nitazieleza baadae.

Kipekee, siku hii imekuwa muhimu zaidi kwa Tanzania.

Umuhimu wa siku na  tarehe hii kwa Tanzania unakuja katika sura mbili, mosi hii ni tarehe ambayo Tanzania husherekea kilele cha Maadhimisho ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Saba Saba.

Lakini pili, nadhani wengi wetu hili huenda hatulifahamu ni kwamba tarehe 07 Julai, 1954 ni siku ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza rasmi kwamba ‘Kiswahili kitakuwa ndiyo nyenzo pekee na muhimu ya kufikia Uhuru.’

Kutokana na umuhimu huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)  katika kikao chake cha 41 lilipitisha Azimio namba 41C/62 kuitangaza siku ya tarehe 07.07 kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

Azimio hili la UNESCO, lilikuja baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  (UNGA) kupitisha Azimio Namba 71/328 la tarehe 11 Septemba, 2017 likielekeza kuwepo kwa siku Maalumu ya Kusheherekea lugha zake rasmi ili kuelezea historia   na utamaduni wa kugha hizo.

Hivyo Kiswahili kimechukuliwa kuwa ni lugha ya Afrika.

Je haya ni mafanikio au changamoto kwa Tanzania? Makala hii itaangazia hilo kwa kina.

MAFANIKIO YA JUMLA

Mosi, ni lazima tukubali kuwa kuwepo tu kwa siku hii ni mafanikio makubwa kwa Tanzania.

Kupitia Kiswahili Tanzania ina nafasi kubwa sana ya kuwa nchi kiongozi kiushawishi Afrika endapo kutakuwa na mikakati thabiti kutumia nafasi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya kufikia ajenda za kinchi.

Mtu anaweza kushangaa hili lakini tujiulize, Tanzania iliwezaje kuwa na ushawishi mkubwa miaka ile ya 1960-1980 ambapo ilifika wakati  katika vikao vya Umoja wa Mataifa nchi nyingine zote za Afrika zilikuwa zikisubiri kusikia nini kitasemwa kutoka Tanzania kabla viongozi wa nchi hizo hawajazungumza? Ni wazi kuwa Tanzania ilikuwa ushawishi wa hali ya juu. Umepotelea wapi? Na vipi tutaurudisha ushawishi huo?

Mafaniko ya Kiswahili yamepitia hatua kadhaa ambazo hatuna budi kuzitambua.

Harakati mbalimbali zilifanyika na zinaendelea kufanyika ili kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano barani Afrika kama ambavyo Muthwili na Kioko (2004) walivyobainisha:

Mwaka 1958 Baraza la Pili la Waandishi na Wachoraji Weusi lilipitisha Azimio la kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano kwa bara zima la Afrika. Hili litatimia siku si nyingi ingawa kunahitajika juhudi za dhati na utashi.

Pendekezo la kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi Afrika  liliwasilishwa na Mawaziri wa Afrika wa Utamaduni wakati wa Mkutano wa OAU uliofanyika Port Louis, Mauritius mwaka 1986 (Indakwa, 1978).

Chagizo lilifanyika pia katika Muendelezo wa Tamasha la Kwanza la Kuhanikiza Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya Afrika uliofanyika Zanzibar (Taasisi ya Utafiti ya Afrika ya Mashariki, Lugha za asili na Lugha za taifa za Afrika, 1986).

Sambamba na juhudi hizo, viongozi wa nchi za Afrika walikutana katika Mkutano wa Kilele (Summit) mwezi Julai 2002 jijini Durban, Afrika ya Kusini na kutangaza kwa pamoja kuwa Kiswahili ni moja ya lugha rasmi za kiutendaji za Jumuiya ya Umoja wa Afrika (Sasa Umoja wa Afrika) (Jumuiya ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Uchumi ya Afrika, mwaka 2000, ibara ya 25, ukurasa wa tano).

Hatimaye mnamo  tarehe 25 Mei, 2021 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, aliongoza kikao cha mabalozi wa Afrika katika kusheherekea siku ya Umoja wa Afrika ambapo Waziri Mulamula alieleza kuwa lugha ya Kiswahili imepitishwa rasmi kutumika kama lugha ya mawasiliano katika mikutano rasmi ya Umoja wa Afrika.

Kukubalika kwa Kiswahili  kama lugha ya Mawasiliano katika Mikutano Rasmi ya Umoja wa Afrika kunaonesha wazi kuwa  kuanzia mwanzoni mwa karne ya 21 lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa sana.

Uamuzi Umoja wa Afrika kuipitisha lugha ya Kiswahili umetokana na kutambua utimilifu wa lugha ya Kiswahili, lakini pia historia yake katika ujenzi wa amani na hivyo kuipa nafasi kupenya katika korido za Umoja wa Mataifa.

Katika muendelezo huo, tukumbuke pia kuwa mwezi Machi mwaka huu 2021 Tanzania iliomba Kiswahili kitumike pia katika kuendeshea mikutano ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi za SADC ili kukifanya kuwa lugha rasmi ya kuendeshea mikutano ya SADC.

Hili lilifuatia mapendekezo ya Kamati Maalumu iliyopitisha mapendekezo hayo mwezi Agosti, 2019 katika mkutano wa Kilele wa SADC uliofanyika Dar es Salaam.

Kutokana na mafanikio hayo, Kiswahili ni fursa adhimu kwa serikali, wafanyabiashara,wajasiriamali na wananchi wa kawaida katika kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika kiuchumi, kisiasa na kijamii Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa nini naamini hivi?

Kwa sababu mwaka 2013 wakati Umoja wa Afrika ukitimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963 nchi za Afrika zilikuja na mpango wa maendeleo wa Afrika ujulikanao kama Ajenda 2063 ambayo inalenga kuliunganisha bara la Afrika katika nyanja zote: kijamii, kisiasa, kisayansi, kiuchumi, kibiashara na kiutamaduni.

Kutokana na mpango huu mkakati wa Afrika 2063 na utumikaji wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano utainufaisha sana Tanzania kuweza kuyafikia malengo yake ya kisera.

Ni wazi kuwa Kingereza ambacho  bado kinaonekana kama lugha ya kikoloni hakiwezi kuinufaisha Tanzania kufikia malengo yake ya kisera. Na  wala si kifaransa ambacho nchi pekee zinazongumza ni zile za kaskazini na Magharibi sambamba na DRC, Burundi na Rwanda. Kichina ambacho ndiyo kwanza kinaanza kufundishwa Afrika hakiwezi kabisa kuwa lugha yetu ya mawasiliano.

Kwa kutazama changamoto ya lugha nyingine tunaona kuwa ni wazi kuwa Kiswahili pekee ambacho kinaweza kutumika kuziunganisha nchi za Afrika na hili litainufaisha sana Tanzania kuongeza ushawishi katika maamuzi ya kisera na ya  kimkakati ya Umoja wa Afrika.

Katika kuthibitsha hilo, Adebayo na wenzake katika kitabu chao Marginality and Crisis cha mwaka 2010  (2010:62) waliandika:

Kiswahili kimetambuliwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) kama lugha yenye kuleta umoja katika nyanja za maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kielimu, kisayansi na kiteknolojia. Hivyo ni wazi kama Tanzania itatumia fursa ya Kiswahili itafikia baadhi ya malengo yake na kuongeza ushawishi katika siasa za Kimataifa na Diplomasia na kuleta Ukombozi wa kweli Afrika kama ninavyofafanua hapa chini:

KIDIPLOMASIA

Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa na kongwe duniani ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uhusiano wa kidiplomasia kabla na baada ya Uhuru wa bara letu la Afrika.

Haya yamewekwa wazi na Adebayo na wenzake walipoeleza kuhusu mchango wa Kiswahili katika mahusiano, na ninawanukuu:

“Kihistoria, Kiswahili imekuwa lugha ya mawasiliano kwa jamii ya mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki tangu karne ya Kumi na nne. Ni lugha ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu milioni mia moja ishirini katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. (Adebayo na wenzake, 2010:64). Kwa sasa lugha hii inazungumzwa na watu zaidi ya milioni mia mbili duniani.

Kiswahili ni lugha inayozungumzwa katika mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Afrika ya Kusini. Hivyo ni lugha inayozungumzwa na mataifa mengi Afrika.

Kidiplomasia ukuaji wa ushirikiano kati ya ukanda wa Afrika Mashariki na Mashariki ya Mbali pamoja na Mashariki ya Kati ulitegemea ukuaji wa Kiswahili.

Hivyo basi, Kiswahili kimetumika kama kiungo kati ya wafanyabiashara wa nje na wa ndani kukuza Diplomasia ya Uchumi.

UKOMBOZI

Kwa upande mwingine lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya ukombozi wa bara la Afrika.

Kiswahili ndiyo lugha iliyotumiwa na chama cha TANU kuwaunganisha na kufanikisha ukombozi na uhuru wa Tanganyika.

Kiswahili kilikuwa pia lugha ya ukombozi na kilitumika kama nyenzo ya mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1964.

Kiswahili ndiyo lugha iliyoziunganisha Tanganyika na Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964.

Lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya ukombozi wa nchi za Kusini na Kaskazini  mwa Afrika.

Mashujaa wa FRELIMO,PAC,ANC,MPLA, POLISARIO na ZANU-PF walipokea mafunzo yao na msaada wa ukombozi kwa mchango wa Kiswahili kama lugha iliyowaunganisha.

Hivyo basi katika hatua za awali za utekelezaji wa sera ya kwanza ya mambo ya nje lugha ya Kiswahili ilikuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wake, hususan kwenye eneo la ukombozi.

Mbali na hayo Kiswahili kilitumika pia kama lugha ya Ukombozi  wa bara zima la Afrika huku Tanzania ikiwa ndiyo kitovu cha harakati hizo chini ya Kamati ya Ukombozi iliyoongozwa na Hatayi Brigedia Jenerali Hashim Mbita.

Hili lilielezwa kwa kina na Khatib (2004) akielezea uwezo wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya ukombozi wa waafrika.

Khatib alieleza kwa mawanda mapana namna nasaba ya Abushiri ilivyoweza kutumia Kiswahili kupambana na uvamizi wa waarabu katika karne ya Kumi na Saba.

Kwa umuhimu wa kipekee, Kiswahili kilitumika pia  kama lugha ya ukombozi katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Afrika ya Kusini (wakati wa ubaguzi wa rangi), Uganda, Rwanda, Burundi, Afrika ya Kati na Kongo.

UTAFITI

Kiswahili pia kinatumika kama lugha ya utafiti katika vyuo vikuu mbalimbali vya Afrika, Ulaya, Asia, na Marekani.

Kutokana na nafasi hiyo ya Kiswahili taasisi mbalimbali za kimataifa husaidia tafiti katika elimu ya Kiswahili.

Hizi ni miongoni mwa sababu zilizofanya Sekretarieti ya Umoja wa Afrika (AU) kukichagua Kiswahili kama lugha yake rasmi ya kazi (Adebayo na wenzake, 2010:65).

Tunapozungumzia utaifa na demokrasia leo hii katika Afrika tunapaswa kufahamu kuwa msingi wake ni lugha ya Kiswahili.

Katika kuthibitisha hili Muthwii na Kioko (2004) wameandika:

Lugha ni chombo muhimu katika kuhanikiza utaifa.

Kwa msingi huo Kiswahili kina umuhimu mkubwa katika kuanzishwa kwa demokrasia ya kweli na usawa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.

MAFANIKIO MAHUSUSI

Ongezeko la matumizi ya Kiswahili katika nchi mbalimbali za Afrika na duniani kwa ujumla kunatoa ishara ya kukua na kuimarika kwa lugha hii.

Ushawishi wa Kiswahili katika majeshi ya Rwanda, Burundi, Uganda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kunaonesha ni jinsi ambavyo Kiswahili kinabeba ujumbe wa amani.

Zipo sababu kadhaa zinazoashiria mafanikio haya ya kukua kwa Kiswahili zikiwemo nchi ya Afrika ya Kusini kuanza kukitumia Kiswahili katika mitaala ya shule zake nchini humo katika ngazi mbalimbali.

Kujiunga kwa nchi za Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kunaifanya lugha ya Kiswahili kuwa na nafasi kubwa ya ushawishi Afrika.

Mbali na hilo, kuwepo kwa idhaa za Kiswahili za Mataifa kama Ufaransa (RFI), Marekani (VoA Kiswahili), Uingereza (BBC Kiswahili), Ujerumani (DW Kiswahili), China (CRI), Japan (Redio Japan Kiswahili) sambamba na redio ya Umoja wa Mataifa (UN) inayorusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili.

Mbali na nchi hizo na UN nchi ya Urusi ina vyuo vikuu vutatu vinavyofundisha Kiswahili.

Tukiwa kwenye Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika ambao ni mpango mkakati wa kulibadii bara la Afrika katika miaka hamsini ijayo na kuleta maendeleo endelevu kuna haja ya kujenga misingi imara ya kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya kupeleka ushawishi kwenye utendaji wa Umoja wa Afrika.

Bara la Afrika linaongozwa na Dira isemayo Afrika iliyofungamana, yenye maendeleo na amani inayoendeshwa na wananchi wake na inayowakilisha kani isiyosimama katika nyanja za kimataifa. Kumbe kuna haja ya kuathiri wananchi wengi wa nchi za Afrika watumie Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Tunaanzia wapi? Hilo ndilo suala la msingi lakini naamini kupo pa kuanzia. Tunahitaji kuanza na haya:

KISWAHILI KIWE NYENZO YA KUFIKIA MALENGO YA NCHI

Kama nilivyosema awali kuwa Kiswahili kinaweza kutumika kama nyenzo ya ushawishi ambayo kwa lugha ya Kingereza huitwa soft power yaani  nguvu isiyo ya shuruti, ni kwa vipi?

Joseph Nye ameifafanua nguvu hii isiyo na shuruti kwa kusema kwa lugha ya Kingereza kama ifuatavyo:

‘Soft power is the ability to set the agenda in world politics through persuasion, enticing and attracting others through the force of one’s beliefs, values and ideas, and not through military or economic coercion’ (Nye, 1990:176).

Kwa tafsiri yangu; Nguvu isiyo na shuruti ni uwezo wa kujenga ajenda/hoja katika siasa za dunia kupitia ushawishi na kuwavutia wengine kupitia nguvu ya imani ya mtu, misingi na mawazo, na si kupitia majeshi au vikwazo kiuchumi.

Kwa mantiki hiyo   tunaweza kushawishi nchi za Afrika zote zikatumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano katika nchi zao kama Tanzania itakuwa na mkakati madhubuti wa kuitumia lugha hii kufikia malengo.

Kama Tanzania iliweza   kujenga hoja za kufanya kuwepo na mabadiliko ya ibara ya 25 ya Sheria ya Kimamlaka ya Afrika (African Union Constitutive Act)  kulikopelekea kuondolewa kwa maneno ‘working languages’ na kuwekwa maneno ‘official languages’ kama ilivyoelekeza ibara ya 11 sheria ndogo ya mabadiliko kwenye Mkataba wa Kimamlaka wa Afrika yaani Protocol on Amendments to the Constitutive Act of the African Union basi Tanzania inaweza kujipanga kuifanya lugha ya Kiswahili iwe lugha ya kila taifa la Afrika.

Kwa kuanzia, Tanzania inaweza kuanzia kwa mabalozi waliopo nchini wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Serikali inaweza kuandaa utaratibu wa kuhakikisha mabalozi wote wa nchi za kigeni wanapatiwa mafunzo ya Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia (CFR) kilicho chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mtu anaweza kuuliza kwa nini Chuo cha Diplomasia?

Kwa sababu Chuo cha Diplomasia si Chuo tu bali ni Kituo chenye hadhi ya kibalozi kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1986 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu Upendeleo na Kinga za Mabalozi kama ilivyotoholewa kutoka kwenye Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 na ule wa 1963 inayohusu Mahusiano ya Kidiplomasia na Kikonseli. Hivyo Chuo hicho kinakidhi kufundisha lugha ya Kiswahili kwa mabalozi kwa sababu ya kuwa na hadhi ya kibalozi.

Pili Chuo cha Diplomasia (CFR) ni sehemu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika inayotambuliwa na Umoja wa Afrika kwa sababu kabla ya Makubaliano ya Nchi za Msumbiji na Tanzania mnamo tarehe 13 Januari 1978 awali kilitumika kama Taasisi ya Elimu ya Juu ya wapigania Ukombozi wa Kusini mwa Afrika hivyo kwa hadhi na historia ni sehemu muhimu na nzuri ya kuwafundisha mabalozi Kiswahili.

Mbali na hilo, Tanzania inahitaji kujenga vituo vya kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi mkakati kama Nigeria, Misri, Senegal, DRC na Afrika Kusini, vituo hivi vitasaidia kueneza na kusambaza Kiswahili katika nchi hizo na jirani.

Balozi zote za Tanzania  zinaweza kuwekewa kiunganishi (link) maalumu kwa wageni kujifunza Kiswahili katika  tovuti za Balozi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuwavutia wageni kukijua Kiswahili.

Lingine la kufanyika ni kuwa na Tamasha kubwa Kiswahili Afrika ambalo  litakuwa likifanyika hapa Tanzania kila tarehe 7 Julai.

Hili linawezekana kwa sababu tayari Umoja wa Afrika umeazimia kujenga Kituo Kikuu cha Urithi wa Ukombozi Afrika hivyo kupitia hiki kituo tunaweza kupenyeza ushawishi wetu kukifanya Kiswahili lugha ya waafrika wote.

Sambamba na hilo, kufuatia uwepo wa ujenzi wa Kituo hicho cha Urithi wa Ukombozi, Tanzania inaweza kujenga kituo cha Utafiti (Research Centre) ambacho licha ya kufanya utafiti wa masuala mbalimbali ya kisera Afrika, kituo hicho kitakuwa kikifanya utafiti wa lugha mbalimbali za Afrika ili kuipa lugha ya Kiswahili misamiati mingi zaidi kutoka katika lugha hizo na hivyo kuongeza ushawishi zaidi na kuifanya lugha hii ikubalike Afrika nzima.

Ninaamini ili kufikia dira ya Afrika 2063 lugha ya Kiswahili ndiyo kiunganishi pekee ambacho ni fahari ya waafrika.

Ni moja ya vielelezo vya kujitawala. Aidha kwa kiasi kikubwa ni lugha ya maendeleo ya mwafrika.

Hivyo basi mikakati madhubuti inahitajika kukifanya Kiswahili kitumike Afrika nzima nasi kama nchi tunufaike kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ndimi:

Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse)

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp)

Author: Gadi Solomon