Somo la Kiswahili lang’ara darasa la saba

Na Aurea Simtowe

Wakati Baraza la Mitihani la taifa (Necta) likitangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022 leo, Kiingereza ndiyo somo lililoonekana kuwa somo gumu kwa wanafunzi wengi tofauti na somo la Kiswahili ambalo limeng’ara kwa ufaulu.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa leo Desemba Mosi na Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Almasi yanaonyesha kuwa asilimia 67.71 ya watahiniwa wote katika mtihani huo walipata daraja D katika somo la kiingereza.

Matokeo hayo ya kumaliza elimu ya msingi yametangwa leo jijini hapa ikiwa ni baada ya watahiniwa 1,384,186 kukaa katika chumba cha mtihani Oktoba 5 na 6 mwaka huu.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa 912,708 walipata ufaulu wa daraja hilo huku wengine 39,086 wakipata daraja E (Utepe mwekundu wa daraja la I) ambao ni sawa na asilimia 2.90.

“Katika somo la English language jumla ya watahiniwa 59,990 wamepata daraja A (utepe wa kijani daraja la kwanza), watahiniwa 56,569 wamepata daraja B (utepe wa kijai daraja la II) na watahiniwa 279,580 wamepata daraja C.

Hiyo ni tofauti na somo la Kiswahili ambapo ni asilimia 7.74 pekee ya watahiniwa ndiyo waliopata daraja D na asilimia 2.76 wakipata daraja E katika somo hilo.

Watahiniwa wengi katika somo hili walikuwapo katika daraja B, ambapo 552,404 walikuwa katika kiwango hicho cha ufaulu ikiwa ni sawa na asilimia 40.92, watahiniwa 403,825 sawa na asilimia 29.96 walipata daraja A katika somo hilo.

“Katika Kiswahili watahiniwa 250,194 sawa na asilimia 18.56 wakipata daraja C.”

Idadi ya wanafunzi waliofaulu kwa daraja A hadi C katika somo hilo ni 396,139 ambayo ni sawa na asilimia 43.4 ya wanafunzi wote waliopata daraja D.

Matokeo hayo yamepata maoni ya wadau mbalimbali wa elimu miongoni mwao ni mwandishi wa vitabu, Richard Mabala aliyesema

“Nadhani umefika wakati wa kubadili lugha ya kujifunzia kuwa Kiswahili na kuwepo na vyuo vya kufundisha lugha za kigeni kama Kiingereza, kireno, Kifaransa, bila hivyo tutakuwa wanafunzi wenye shahada ila hajiamini, hawana ujuzi wa kutosha kwa sababu walisoma kwa kukariri.

Author: Gadi Solomon