Tanzania, Afrika Kusini zapendekeza AU kukitambua Kiswahili

Mwandishi Wetu

Tanzania pia imeuomba Umoja wa Afrika kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la Afrika kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa wapigania uhuru ikizingatiwa kuwa kaulimbiu ni ‘Sanaa, Utamaduni na Urithi’.

Ombi hilo limewasilishwa na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa katika Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia mtandao na kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli.

“Tumeuomba Umoja wa Afrika kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la Afrika kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa wapigania uhuru ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni sanaa, utamaduni na urithi,” Amesema Profesa Kabudi.

Akiufunga Mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi amesisitiza kuwa umoja, mshikamano na amani katika bara la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakayoliwezesha bara hilo kuendelea kiuchumi ili kuendana na rasilimali ilizonazo.

“Umoja, mshikamano na amani katika bara la letu la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakatuwezesha sisi kuendelea kiuchumi ili kuendana na rasilimali tulizonazo kwa maslahi yetu mapana,” Amesema Rais Tshisekedi

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umejadili mambo mbalimbali ikiwemo uundaji wa Kamati mpya ya uongozi wa Umoja wa Afrika (the AU Bureau of Assembly) kwa mwaka 2021, uzinduzi wa Kaulimbiu ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2021 inayohusu “Sanaa, Tamaduni na Urithi katika kufikia azma ya Afrika Tuitakayo”

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitumia fursa hiyo kueleza utayari wake kuendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na Nchi Wanachama wa Umoja huo katika kutekeleza jitihada zinazolenga kuiwezesha Afrika kujitegemea.

Author: Gadi Solomon