Tanzania yatajwa kitovu cha lugha ya Kiswahili duniani

Juma Isihaka, Mwananchi

Dar es Salaam. Pamoja na Tanzania kuwa kitovu cha lugha ya Kiswahili, Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Abdulrahman Kinana amesema Watanzania si wafaidikaji wakubwa wa lugha hiyo duniani.

Kinana ameyasema hayo leo Juilai 6, 2022 katika hafla ya siku ya mchango wa Kiswahili katika ukombozi wa bara la Afrika.

“Watanzania tunajivunia kuwa sisi tunajimwambafai sisi ndiyo kitovu cha Kiswahili, lakini kwa bahati mbaya sisi sio wafaidikaji wakubwa wa Kiswahili duniani,” amesema.

Amesema kwa sasa takriban mataifa 14 duniani huzungumza rasmi lugha hiyo, huku mapato yanayotokana na Kiswahili ni Dola za Marekani 1.3 bilioni.

“Sasa jiulize sisi Watanzania katika hizo tunapata kiasi gani. Mapato hayo yanatokana na wanafunzi, wakufunzi, wakalimani na redio na televisheni zinazozungumza Kiswahili,” amesema.

Hata hivyo, Kinana amesema idadi kubwa ya wakufunzi wa Kiswahili duniani hutokea Kenya, wakati Tanzania wakitoka wachache.

Taasisi 72 duniani, amesema hufundisha lugha hiyo wakati Vyuo Vikuu 112 Marekani hufundisha Kiswahili.

“Katika Vyuo vikuu maarufu duniani, Chuo cha Havard, Stamford na vingine vinafundisha lugha ya Kiswahili, sijafanya utafiti kujua je huko wanaofundisha lugha hiyo ni watu kutoka Tanzania au vipi,” amesema.

Amefafanua kuwa hata wakalimani wa Kiswahili wanaotoka Tanzania hawafiki 80, akisisitiza kuwa, “waasisi wa Kiswahili ni sisi lakini tusiofaidika na Kiswahili ni sisi sasa kuna kazi kubwa ya kufanywa”.

Ameeleza kuwa watu milioni 500 huzungumza lugha ya Kiswahili duniani.

chanzo: Mwananchi

Author: Gadi Solomon