Tanzania kuadhimisha Siku ya Kiswahili siku saba mfululizo

Siku ya Kiswahili kuadhimishwa siku saba mfululizo Dar Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO) lilitangaza kuwa kila ifikapo Julai 7 ya kila mwaka dunia itaadhimisha siku ya Kiswahili.

Nasra Abdallah,Mwananchi

nabdallah@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ikiwa kwa mara ya kwanza dunia inatarajia kuadhimisha siku ya Kiswahili, Tanzania katika kuipa heshima siku hiyo, itaiadhimisha kwa siku saba mfululizo.

Novemba mwaka jana Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza kuwa kila ifikapo Julai 7 ya kila mwaka dunia itaadhimisha siku ya kiswahili na hivyo kufanya lugha hiyo kuwa ya kwanza kutoka Afrika kutambulika duniani.

Akizungumza  leo Jumatano Juni 29, 2022 katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema mkoa wake umechaguliwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kitaifa ambapo wataadhimisha kwa siku saba mfululizo kwa kufanya shughuli mbalimbali.

“Katika kutekeleza hilo Wizara ya Utamaduni, Sanaa  na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi yangu tumeandaa tamasha kubwa la kitaifa la utamaduni litakaloanza Julai Mosi hadi 7,2022 ambalo  litakufunguliwa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, Julai 2 na siku ya kilele mgeni rasmi anatarajiwa kuwa  Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Makalla.

Pamoja na mambo mengine, amesema  tamasha hilo litawaleta pamoja marais wastaafu wa bara la Afrika watakaoeleza namna Kiswahili kilivyochangia ukombozi wa bara la Afrika ambapo mpaka sasa waliothibitisha kuja ni pamoja na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano na Rais mstaafu wa Namibia, Sam Nujoma.

Wakati kuhusu shughuli zitakazofanyika, Makalla amesema ni pamoja na maonesho ya burudani za Taarabu asilia na kisasa, ngoma za asili, vyakula vya asili na matembezi ya utamaduni ambayo haya yatafanyika viwanja vya Uhuru, mkoani humo.

Aidha Pia amesema kuwa Julai 3, mwaka huu kutakuwa na maonesho ya taarabu za asilia na kisasa yatakayofanyika fukwe za Coco Beach huku mgeni rasmi  akitarajiwa kuwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson.

Aliwataja wasanii watakaopamba usiku huo kuwa ni pamoja na Hadija Kopa, Isha Mashauzi, Patricia Hilary, Mzee Yusuphu, vikundi toka Safina Modern Taarabu,  First Class, Wana Nakshi Nakshi, Fahari Zamani, Nasi Ikhwan Anafaa  na vikundi vya muziki kutoka nchi za Burundi, Kenya na Visiwa vya Comoro.

Kaulimbiu ya tamasha hilo ni “Utamaduni wetu, fahari yetu, tujiandae kuhesabiwa na kazi iendelee,”

Mwisho.

Author: Gadi Solomon