Tanzania yaja na mikakati ya kukuza Kiswahili na kuzitumia fursa kiuchumi

Saddam Sadick, Mwananchi

Mbeya. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha inakuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili duniani ikiwamo kuagiza balozi zote za Tanzania kuweka vituo vya lugha hiyo ughaibuni.

Akizungumza jijini Mbeya Jumatatu Machi 18, 2024 wakati wa kufungua Kongamano la Nne la Idhaa za Kiswahili Duniani, Majaliwa amesema Serikali inaandaa mkakati wa kitaifa katika kuifanya lugha hiyo kuwa fursa kiuchumi.

Amesema hadi sasa watanzania waishio nje ya nchi ‘Diaspora’ tayari wamepata elimu hiyo ikiwa ni kuongeza wigo wa ajira kwa Watanzania na kuwataka wananchi kujipanga vizuri ili kutotopoteza fursa hiyo kwa wenye uhitaji.

“Zipo Balozi ambazo zimefungua vituo vya lugha ya Kiswahili kama Korea, Colombia, Italia, Zimbabwe na Ufaransa na nilifurahia nilipofika shule moja ya Korea kuongea na Wakorea ambao waliongea Kiswahili na wengine wamejipa majina ya Kiswahili ikiwamo Zuhura, Tausi, Joseph na Adam,” amesema na kuongeza

“Kwa maana hiyo lazima tujipange vizuri vinginevyo ajira zitatutoka na kwenda kwa wenye mapenzi ya lugha hii, serikali inaandaa mkakati wa kitaifa kufanya lugha hii kuwa fursa kiuchumi kwa kuibidhaisha,” amesema Majaliwa.

Waziri huyo ameongeza kuwa kwa sasa lugha hiyo imepiga hatua kubwa ambapo awali ilikuwa ikiunganisha mataifa ya Afrika Mashariki, lakini kwa sasa imeanza kufika hadi ukanda wa SADC ambapo huko watu wanaozungumza Kiswahili.

Amesema katika kuenzi kazi ya viongozi wa awamu ya kwanza walioshawishi lugha hiyo, lazima Kiswahili kitumike bila kuchanganywa katika matukio yoyote ikiwamo bungeni.

“Katika kukuza lugha hii eneo la wanahabari linahitaji kuboreshwa na ni muhimu sasa kutoa muongozo ili kuondoa zile lugha binafsi, wizara tafuta mkakati wa kutoa mafunzo kwa vijana kuondokana na kupotosha lugha hii kwa kuzingatia matumizi ya sarufi,” amesema Waziri huyo.

Pia Kiongozi huyo ametoa maelekezo kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kushirikiana na wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo na ile ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar kutafsiri lugha inayokuwapo kwenye vifaa vya dawa.

Ameitaka pia Wizara ya Elimu na Sayansi kuandaa na kuimarisha mafunzo kwa kuandaa wataalamu wa kuweza kutafsiri lugha ili kutoa wigo kwa Watanzania kupata ajira.

“Bakita na Bakiza tekelezeni mpango wa mafunzo kwa wahariri, waandishi wa vitabu, nyaraka zote za Serikali ziwe katika lugha ya Kiswahili sawa na matukio yote na kama kutakuwapo mtu kutoka nje haelewi Kiswahili asaidiwe kwa vifaa maalumu au mkalimani,” amesema Waziri.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid amesema wizara yake kwa kushirikiana na waziri Dk Damas Ndumbaro watahakikisha wanaitangaza lugha hiyo na kuziletea kipato nchi hizo na kwamba Kiswahili kinadumisha tamaduni zetu.

“Tunashirikiana na Dk Ndumbaro tutashirikiana kwa kutekeleza maelekezo ya viongozi kuhakikisha tunaitangaza lugha hii kwa manufaa ikiwamo pato la nchi zetu” amesema Tabia.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Consolata Mushi amesema lengo la kongamano hilo ni kuangalia matumizi ya lugha, maudhui katika uandishi na utangazaji.

“Katika hitimisho la kongamano hili tutapokea mawazo, ushauri na mapendekezo ya washiriki na kisha Baraza kuyafanyia kazi ikiwamo makosa yanayofanywa na vyombo vya habari,” amesema Mushi.

Mapema akitoa taarifa ya Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera amesema Mbeya ni sehemu yenye fursa nyingi za kiutalii ikiwamo Ziwa Ngosi, Hifadhi ya Taifa Ruaha, Ziwa Nyasa na maporomoko ya maji.

“Hili kongamano ni fursa kwa mkoa wetu kutangaza vivutio kwani hata wale nyani wa aibu, lakini ni mkoa ambao una maeneo mengi na rafiki kwa uwekezaji kwa mtu yeyote,” amesema Homera.

Author: Gadi Solomon