
Ufupi: Dk Khatib ni mkongwe wa siasa aliyetumikia CCM na Serikali katika nafasi kadhaa za uwaziri
Noor Shija, Mwananchi
Dodoma. Mkongwe wa siasa nchini Dk Muhammed Seif Khatib (70), amefariki dunia Jumatatu Februari tarehe 15 asubuhi mjini Unguja.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Mkurugenzi wa Maelezo Zanzibar, Dk Juma Mohammed.
“Ni kweli amefariki asubuhi kwa mujibu wa taarifa za mwanawe na mwili wake uko kwenye Hospitali ya Al Rahma,” amesema Dk Mohammed baada ya kuulizwa kuhusu taarifa zilizokuwa zikisambaa kwamba amefariki dunia.

Taarifa zaidi zimesema Dk Khatib anatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne saa nne asubuhi huko Mpendae, Unguja.
Dk Khatib ni mwanasiasa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Uzini, Unguja na amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM na nafasi kadhaa uwaziri kama vile Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.
Atakumbukwa kwa utaalamu wake wa lugha ya Kiswahili ambapo hadi anafariki dunia ni Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza). Pia, ni mwanafunzi wa kwanza kupata shahada ya uzamivu (PhD) ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) tangu mwaka 1978 hadi 1983. Na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuanzia mwaka 1978 hadi 2002.
Dk Khatib atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika fasihi ya Kiswahili kwa utunzi wake uliotukuka. Miongoni mwa kazi zake zitakazobaki kama alama isiyofutika ni diwani za Wasakatonge na Fungate ya Uhuru.
Maoni Mapya