Tusipuuze lugha mama zimechangia maneno mengi ya Kiswahili

Jicho la Kiswahili leo limeangazia umuhimu wa lugha mama au lugha za asili kwa maendeleo ya kijamii, uchumi barani Afrika. Shirika la Umoja wa Mataifa la  Elimu, Sayansi na Utamaduni limetenga siku ya lugha mama Kila tarehe 21 Februari kila mwakakuadhimisha siku ya lugha mama duniani.

Wiki iliyopita barani Afrika ilitengwa juma lote kwa ajili ya kuadhimisha lugha mama za Kiafrika na kilele chake kilikuwa ni tarehe 28 Februari, 2024.

Unapozungumzia lugha mama kila mtu huenda ana lugha yake ya asili, kwa Watanzania ukizungumza lugha mama zinaweza kuwa lugha za makabila na wapo watu wengine ukisema lugha mama inaweza kwake ikawa ni Kiswahili. Kwa hiyo lugha mama wakati mwingine inategemea na mazingira.

Kwa Afrika lugha mama tunalenga lugha zetu za asili ambako ni chimbuko la wazazi au koo zetu. Mwaka huu  kaulimbiu kwa upande wa Afrika inasema ‘Kuziwesha  lugha za Kiafrika kwa elimu bora  na biashara huru kwa Afrika tunayoitaka.’

Tunavyo vyombo mahususi ambavyo vimepewa jukumu la kusimamia lugha za Kiafrika katika Umoja wa Afrika kinafahamika The African Academy of Languages (Acalan) ambacho kinafanya kazi na mabaraza ya Kiswahili katika nchi zote wanachama, pamoja na vyuo vikuu vya serikali ili kuhakikisha kinatimiza malengo yake ya kuhimiza matumizi ya lugha za Kiafrika.

Upande wa Tanzania, tuna makabila takriban 120 ambayo tunaweza kusema ndiyo chimbuko la lugha mama kwa Watanzania walio wengi. Licha ya juhudi kubwa za viongozi wa Taifa letu kuhimiza matumizi ya Kiswahili, bado lugha za asili zimeendelea katika nyenzo muhimu kwa mawasiliano miongoni mwa jamii.

Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ukabila nia yake njema ilikuwa ni kudumisha amani, upendo na mshikamao miongoni mwa Watanzania na hiyo ndiyo sasa inawatofautisha na majirani zao wanaowazunguka kwa kuwafanya kuishi kwa umoja, bila kujali tofauti zao za makabila wala rangi.

Tunayo mifano kutoka lugha zetu za makabila kuchangia maneno mengi ya asili katika lugha ya Kiswahili. Mfano neno Ng’atuka kutoka Kablia la Wazanaki. Limeingia kwenye kamusi zetu na kuwa neno rasmi.

Kuna dhana potofu zimeendelea kujengeka miongoni mwa jamii kuwa lugha za asili zinajenga ukabila.

Vilevile mfumo wa maisha ya kisasa unaleta changamoto za kukuza lugha za asili pamoja na kudumisha mila na desturi nzuri za makali mbalimbali.

Pia, mwingiliano wa jamii, kukua kwa miji, maisha ya kuhamahama na kukua kwa mfumo wa elimu ni miongoni mwa mambo yanayodidimiza maendeleo ya lugha za asili

Kwa mujibu wa Unesco lugha za asili ni utambulisho wa makabila mbalimbali na zina umuhimu mkubwa katika jamii.

Bado upo umuhimu kuendelea kuwarithisha watoto lugha mama kwa sababu zimebeba utambulisho wao katika mila na desturi.

Tangu Kiswahili kitambuliwe na Unesco na kupitishwa kuwa lugha itakayotambulisha bara la Afrika kutokana na kuwa na wazungumzaji wengi, bado kinakabiliwa na changamoto kwa sababu ya kuonekana kwamba ni asili ya watu wa Afrika Mashariki, hivyo mataifa mengine yakitaka lugha zao ndizo zipewe nafasi kuwa lugha za Afrika.

Lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha ya Afrika ni kutokana na kuwa na wazungumzaji wengi duniani ambao wanakadiriwa sasa kufikia milioni 500.

Mathalani kwa hapa nchini Tanzania tunayo Makumbusho ya Taifa ambayo yamekuwa yakihifadhi uasili, historia ya lugha za makabila takribani 120 hapa nchini.

Hata hivyo kutokana na maendeleo ya teknolojia ipo haja ya kuwa na maktaba ya mtandao ambayo inahifadhi historia ya makabila yote 120, vyema kila kabila kuingiza taarifa zao ili watoto wao waweze kusoma na kujifunza mamabo mbalimbali ya lugha mama zao.

Author: Gadi Solomon