Tutumie Kiswahili kufundishia

Profesa Raymond Mosha

Gazeti hili mara kadhaa limekuwa na mjadala kuhusu kutumia Kiswahili au Kiingereza kufundishia shuleni na vyuoni.

Wapo wanaosema kwamba tuendelee kutumia Kiingereza, kwa sababu hatuna msamiati wa kutosha wa Kiswahili katika kufundishia.

Wanaongeza kwamba Kiingereza ni lugha kubwa duniani hivyo tuendelee kuitumia. Wanadai kwamba wahitimu wetu hawatamudu soko la ajira nje ikiwa wamejifunza kwa Kiswahili. Hizo ni baadhi ya sababu zinazotelewa.

Wapo pia wanaotetea matumizi ya Kiswahili kufundishia wakisema kwamba wanafunzi wetu wataelewa masomo vizuri zaidi tukitumia Kiswahili.

Katika toleo la tarehe 27 Aprili mwaka huu, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faraja Kristomus, alionyesha kwamba wanafunzi waliofaulu mtihani wa kidato cha nne vizuri mwaka 2019 ni wale waliofaulu vizuri Kiingereza katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2015.

Ufaulu mzuri hapa una maana ya daraja la kwanza hadi la tatu, yaani asilimia 35.1 ya wahitimu wote. Ufaulu usioridhisha ni daraja la nne na sifuri, ambao ni asilimia 64.9 ya wahitimu wote. Advertisement

Binafsi si mwepesi wa kuona kwamba tunatoa elimu bora tunapotambua kwamba asilimia 64.9 ya wahitimu wetu wamepata daraja la tatu na sifuri.

Mwandishi huyu anahitimisha akisema kwamba wanafunzi wa darasa la saba wanaokuwa na ufaulu mdogo katika Kiingereza wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kupata ufaulu mdogo katika mtihani wa kidato cha nne.

Kama hivyo ndivyo, ni wazi kwamba wanafunzi wanaopata ufaulu mdogo kidato cha nne, wangefanya vizuri zaidi ikiwa wangejifunza kwa Kiswahili.

Napenda kuongeza hapa sababu zinazonifanya niamini kwamba tunaweza kutumia Kiswahili kama Lugha ya kufundishia kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.

Kwanza, Kiswahili ni lugha yetu ya Kiafrika. Ni tunu yetu, ni utamaduni wetu hata kama watoto wa vijijini wanaongea lugha nyingine za kikabila.

Ukweli ni kwamba asilimia kubwa sana ya watoto wa Tanzania wanaongea Kiswahili na wakifundishwa vizuri watajua Kiswahili vizuri zaidi. Ni jambo la msingi sana tujivunie lugha yetu bila kudharau lugha nyingine kama Kiingereza.

Pili, tunatambua kwamba mwanafunzi anapojifunza kwa Kiingereza atajaribu sana kukariri na kukumbuka anachofundishwa, zaidi kuliko kuelewa anachofundishwa.

Ni vizuri tutambue kwamba katika kuishi na kujifunza kuna hisia za akilini na moyoni ambazo hazitafsiriwi katika lugha yo yote. Hisia haina lugha, lakini mwanafunzi atakaribia sana kuelewa na kueleza hisia hizo katika lugha anayotumia kila siku

Wanasayansi na wabunifu wa maarifa mbalimbali huanza na hisia, ambayo mwanzoni haielezeki katika lugha. Huyu mbunifu akijaribu kuiweka katika maneno atatumia lugha ya mama yake, ambayo kwetu ni Kiswahili.

Kwa maneno mengine, tukitumia Kiswahili kufundishia tutawapa wanafunzi wetu fursa zaidi za ubunifu na uvumbuzi wa maarifa mbalimbali. Rafiki yangu mmoja kutoka taifa moja la Ulaya alinieleza kuwa tukiendelea kutumia Kiingereza hatutasogea kamwe katika maendeleo ya maana kama mataifa mengine.

Tuangalie mahali pengine duniani. Hakuna taifa lililoendelea hata moja linalotumia lugha ya kigeni kufundishia. Wajapani wanatumia lugha yao. Angalia wanavyotingisha dunia kwa uvumbuzi wa magari, vyombo vya muziki, kamera na kadhalika. Tuangalie China, India, Ulaya, Malaysia, Marekani, Amerika Kusini, Urusi na nchi nyingine; wanafundishia kwa lugha zao.

Kinachotakiwa sasa ni sisi tuamue kwa dhati kutumia Kiswahili kufundishia. Hatutakurupuka, la hasha. Tukishaamua, tutaanza kujipanga kwa miaka kadhaa. Tutayarishe mitalaa yetu vizuri, tutayarishe vitabu, na tutayarishe walimu kwa lengo hilo.

Sambamba na hayo, tutayarishe msamiati wa kutosha katika kila somo. Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) liingie kazini pamoja na wataalamu wetu wa sayansi na masomo mengine ili kubuni misamiati ya masomo mbalimbali. Misamiati hii itaendelea kukua kama vile lugha ikuavyo na kubadilika.

Nimezungumza na walimu na wahadhiri kadhaa, karibu wote wanasema inawezekana kutumia Kiswahili, lakini tujipange vizuri.

Kuanzia shule za msingi watoto wasome vitabu vya Kiswahili, wasomo hadithi, wasome fasihi na kadhalika ili kunoa hisia zao na ubunifu wao katika kufikiri. Jambo la msingi ni kuamua.

Wakati huohuo, tuendelee kufundisha Kiingereza kama somo, na tulifundishe vizuri. Walimu wa Kiingereza watayarishwe vizuri kama vile walimu wa Kiswahili. Ikiwezekana tufundishe pia Kichina, Kiarabu, Kifaransa na lugha nyingine.

Profesa Raymond Mosha anapatikana kwa namba (255) 769-417-886; (255) 783-417-886. www.rsgmosha.com Advertisement

Author: Gadi Solomon