Tuzo ya Kiswahili Safal-Cornell Fasihi ya Afrika kutolewa Dar es Salaam

Gadi Solomon, Mwananchi

[email protected]

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la utoaji Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika kutoka Kampuni ya Mabati ya Alaf ambayo ni tawi la Kampuni ya Safari Investments Mauritius Limited kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Corenll Marekani.

Tuzo za mwaka huu jumla ya Watanzania watano wameingia kwenye kinyang’anyoro katika vipengele vya riwaya na ushairi wakiwania jumla ya zawadi ambazo ni takribani Sh34,800,000.

Shughuli ya utoaji tuzo hiyo itafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City keshokutwa Jumatano Janurai 25, 2023 kuanzia saa 3 asubuhi.

Tuzo hiyo inayofadhiliwa na Safal Group, kupitia matawi yake ya Mabati Rolling Mills Kenya, Alaf LTD Tanzania, Kituo cha Taaluma za Afrika katika Chuo Kikuu cha Cornell Marekani na Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o imekuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya fasihi ya Afrika kutokana na kuwezesha uchapishaji wa miswada inayoshinda.

Majaji waliosoma na kuiteua miswada ya mashindano hayo walikuwa ni Profesa F.E.M.K Senkoro ambaye alikuwa mwenyekiti wa majaji mwaka huu. Pia alikuwepo Dk Magdaline Nakhumicha wa Chuo Kikuu cha Moi na Dk Hamisi Babusa wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Wanaoshindana kwenye vipengele vya tuzo hizo ni utanzu wa Riwaya; Ahmad Simba (Tanzania), Isaac Ndolo (Kenya) na Ditto Daudi (Tanzania).

Kipengele kingine ni Utanzu wa ushairi Lenard Mtesigwa (Tanzania), Salum Makamba (Tanzania) na Ally Bakari (Tanzania).

Mshindi wa kipengele cha Riwaya na Ushairi kila mmmoja atajinyakulia Dola 5,000 huku mshindi wa pili katika utanzu wowote ataondoka na Dola 2,500.

Taarifa ilitotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa ALAF LTD, Ashish Mistry ilieleza kuwa, mbali na zawadi hizo, miswada iliyochapishwa na East African Education Publishers, Kenya na Mkuki na Nyota Publishers Tanzania na miswada ya mashairi itakayoshinda itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na African Poetry Book Fund.

Author: Gadi Solomon